MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Thursday, August 16, 2012

MAREKANI YAENDELEZA MAUAJI SOMALIA

MOGADISHU
Ndege za kigaidi zisizo na rubani za Marekani zimeendelea kufanya mauaji ya watu katika nchi ya Waislamu ya Somalia iliyopo Afrika.
Watu wasiopungua saba wameauwa na wengine kumi na saba wamejeruhiwa katika mashambulizi ya jana Jumatano yaliyofanywa na ndege hizo kwenye mji wa JOWHAR nje kidogo ya mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.
Hadi sasa hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu hasara nyingine zilizosababishwa na mashambulizi hayo ya kinyama.
Mbali na nchini Somalia, Marekani imekuwa ikitumia ndege zisizotumia rubani kufanya mashambulizi ya kigaidi katika nchi za Afghanistan, Pakistan, Yemen na imewahi kutumia pia ndege hizo nchini Libya.
Marekani inadai kuwa inashambulia wanamgambo wa AL-QAEDA na AS-SHABBAB, lakini wananchi wa kawaida ndio wahanga wakuu wa mashambulizi ya ndege hizo za kigaidi.

MAELFU WAKIMBIA MAKAZI YAO

KINSHASA
MAPIGANO ya miezi mitano sasa kati ya waasi wa kundi la M23 na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya KONGO yamewalazimisha zaidi ya watu nusu milioni kukimbia makazi yao huko mashariki mwa nchi hiyo.
Ripoti zinasema kuwa raia wengi wa maeneo ya Kivu Kaskazini yenye utajiri mkubwa wa madini wamelazimika kukimbia makazi yao baada ya kujikuta katikati ya machafuko na mapigano ya kundi la M23 na Jeshi la serikali ya Kinshasa.
Maafa hayo yanaendelea kuwapata raia wa kawaida wa KONGO licha ya kuwepo maelfu ya askari wa Umoja wa Mataifa waliopelekwa nchini humo kwa ajili ya kulinda amani.
Mamia ya wakimbizi hao wa KONGO wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani za RWANDA, BURUNDI na UGANDA huku Serikali ya KONGO ikitoa shutuma kali kwa nchi ya RWANDA na UGANDA kwa kuwaunga mkono waasi wa kundi la M23.
Waasi wa M23 walijitenga na jeshi la serikali ya Kinshasa wakidai kuwa serikali haijatekeleza vipengele vya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini MACHI 23, 2009.

HRW YAINGILIA KATI WAISLAAM KUKAMATWA ETHIPEA

ADDISABABA
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeitaka serikali ya Ethiopia kuwaachia huru viongozi 17 wa Kiislamu waliokamatwa katika maandamano ya amani yaliyofanyika nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na hilo la Kutetea Haki za Binadamu imesema serikali ya Ethiopia inapaswa kuwaachia huru viongozi hao 17 wa Kiislamu waliotiwa nguvuni wakati askari wa usalama wa Ethiopea walipowakandamiza kinyama wapinzani Waislamu mjini Addis Ababa.
Watu hao walitiwa nguvuni katika maandamano makubwa ya amani yaliyofanywa na Waislamu mwezi jana kupinga uingiliaji usio wa kisheria wa serikali katika masuala ya Waislamu.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesisitiza kuwa mahabusu hao wanakabiliana na hali mbaya na wanashikiliwa bila ya kujulishwa makosa yao au kuwa na wakili.
Waislamu wanaunda zaidi ya asilimia 30 ya jamii ya watu milioni 83 ya Ethiopia.

TRA WAPATA SCANNER MPYA TANGA

TANGA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Tawi la Tanga imepata mashine mpya ya kisasa yenye uwezo wa kutambua bidhaa zilizohifadhiwa ndani ya makontena (Scarner) na kuiwezesha mamlaka hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi na haraka.
Meneja wa Mamlaka hiyo Mkoani Tanga Nyonge Mahanyu, amesema mashine hiyo itakuwa mkombozi kwa wafanyabiashara wa mkoa huo kwa kuwa itaondosha kero za wafanyabiashara kucheleweshewa shehena zao katika Bandari ya Tanga.
Mahanyu amesema awali wafanyabiashara wa Tanga walikuwa wakilalamikia kucheleweshwa kwa ukaguzi wa mizigo yao bandarini hapo jambo lililokuwa likitishia uhai wa bandari kongwe ya mkoa wa Tanga.
Amesema baada ya ujio wa mashine hiyo utaweka mvuto kwa wafanyabiashara wengi kwa kuwa wataweza kushusha shehena zao kwa wakati na bila ya usumbufu.
Mahanyu amefafanua kuwa mashine hiyo ina uwezo wa kukagua kontena moja kwa dakika tatu tu jambo ambalo litaiwezesha TRA kukagua makontena mengi ndani ya muda mfupi na hivyo kukusanya kodi nyingi tofauti na ilivyo sasa.
Kwa upande wake mtaalamu wa Scana Mhandisi Julias Joseph, amesema mashine hiyo ambayo ina uwezo mkubwa wa kukagua na kutambua shehena zilizomo ndani ya makontena itakuwa kimbilio la wafanyabiashara kushusha bidhaa zao katika bandari ya Tanga.
Kutokuwapo kwa ufanisi katika utoaji wa huduma katika Bandari ya mkoa wa Tanga kumesababisha wafanyabiashara wengi nchini kuikimbia bandari hiyo na kuamua kushushia mizigo yao katika bandari za Mombasa, Zanzibar na Dar es Salaaa.

HATARINI 'KUTOGRADUATE'

ZANZIBAR
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimesema wanafunzi wote wanaomaliza masomo yao na ambao hawatakamilisha malipo ya ada hadi Agosti 22 mwaka huu hawataruhusiwa kufanya mitihani yao ya muhula wa pili kwa mwaka 2011/2012.
SUZA inatarajia kuanza mitihani yake ya muhula wa pili ya kufunga mwaka wasomo kuanzia Agosti 22 mwaka huu chuoni hapo.
Onyo hilo limetolewa na Makamu Mkuu wa SUZA Professa Idriss Ahmad Rai mbele ya waandishi wa habari muda mfupi baada ya kikao cha pamoja kati ya uongozi wa chuo na serikali ya wanafunzi kwenye Makao Makuu ya chuo hicho Vuga, mjini Unguja.
Profesa Rai amesema onyo hilo halitawahusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili ambao wameruhusiwa kufanya mitihani baada ya kujaza mkataba maalum baina ya mwanafunzi binafsi na chuo.
Profesa Rai amesema mkataba huo utawalazimisha wanafunzi hao kulipa malimbikizo ya ada wanayodaiwa kabla ya kuanza muhula mpya wa masomo unaotarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu na kwamba watakaoshindwa kulipa hawataruhusiwa kuanza masomo katika muhula huo.
Hata hivyo amesema wanafunzi watakaoshindwa kuanza mitihani Agosti 22 mwaka watapewa nafasi ya kufanya mitihani wakati wa mitihani ya marejeo (supplementary examination) lakini kwa upande wao utakuwa ndio mtihani wa kawaida iwapo watakamilisha malipo ya madeni yao.
Professa Rai amesema SUZA imeamua kufanya uwamuzi huo mzito kutokana na wanafunzi wengi kushindwa kulipa ada zao na hivi sasa wanawadai kiasi cha shilingi 270 milioni.
Amesema lengo la chuo siyo kuwakomoa wanafunzi lakini ni njia ya kuhakikisha wanapata fedha ambazo ni muhimu katika kukiendeleza chuo hicho pamoja na ruzuku inayotolewa na Serikali.
Ameongeza kuwa wanaelewa ugumu wa maisha unaowakabili wanafunzi wengi hasa katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani na kuelekea sikukuu ya IDD-EL-FITRI lakini alidai hakuna njia ya mkato ya kupata mapato ya kuendesha chuo hicho.

NGALAWA AWAASA WAISLAAM


TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga Chiku Ngallawa, amewataka Waislamu katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mfungo wa Ramadhani kuhakikisha mafunzo wanayoyapata kutoka kwa Mashekh wao wanayaendeleza hata baada ya mfungo wa mwezi mtukufu.
Ngallawa ameyasema hayo katika futari iliyoandaliwa na Bank ya CRDB tawi la Tanga.
Ngallawa amesema tabia ya upendo na kuoneana huruma katika jamii iliyojengeka miongoni mwa waislaam kipindi hiki cha Ramadhani ni dalili za kuyapokea mafunzo mbalimbali yanayotolewa na Masheikh.
Kwa upande wake Meneja wa huduma kwa wateja wa CRDB Makao Makuu, Godwin Semunyu, amesema kwa kuzingatia utukufu wa mwezi wa Ramadhani ndio mana wamekuwa na utaratibu wa kufuturisha lengo likiwa ni kuleta umoja na mshikamano katika jamii.
Semunyu amesema CRDB itaendelea kuwa karibu na Waislamu hasa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani na kutoa misaada kadiri ya uwezo wake kwa kuwkufanya hivyo ni faida kubwa kwa jamii na beki hiyo.