MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Tuesday, June 16, 2009

Regia Mtema: Ni mlemavu wa viungo, si wa kufanya kazi



Salim Said
“MIMI ni mlemavu wa kimaumbile wala si mlemavu katika kazi, lakini kuna watu ni wazima kimaumbile, lakini ni walemavu kwenye kazi,” hivi ndivyo anavyoanza Regia Mtema katika mazungumzo yake na Mwananchi.

Mtema msichana ambaye ni Afisa Mafunzo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Kurugenzi ya Organaizesheni, anasema ulemavu wake haumzuii wala kumpunguzia uwezo wake wa kufanya kazi.

Kielimu Mtema ni muhitimu wa Shahada ya kwanza katika Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua) kwenye fani ya Sayansi ya Uchumi na Lishe.

Anasema, amejipatia elimu yake ya Msingi katika shule ya msingi Mchikichini Ilala kuanzia mwaka 1989 hadi 1995, huku elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne akiipatia katika shule ya Sekondari ya Forodhani kuanzia mwaka 1996 hadi 1999 zote za jijini Dar es Salaam.

Mtema anasema, alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Benjamin Mkapa katika Mchepuo wa Kemia, Biolojia na Lishe (CBN) mwaka 2000, lakini aliomba uhamisho ili kwenda shule ya sekondari ya wasichana ya bweni Machame Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, kwa kuwa kutokana na hali yake alishachoka kusoma shule za kwenda na kurudi.

“Nilianza kuvutiwa na siasa tangu sekondari, lakini nilishindwa kujiunga na chama chochote cha siasa, kwa sababu sekondari za zamani zilikuwa hazina masuala ya siasa tofauti na sasa, ambapo matawi ya vyama yapo hata katika shule hizo,” anasema Mtema.

Anasema, akiwa Machame alivutiwa na Chadema, baada ya kutembelewa na Mwenyekiti wa sasa wa Chadema Freeman Mbowe alipokwenda kuwatembelea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2000, wakati huo akiwa ni mgombea ubunge wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro.

“Nilivutika sana na Chadema nilipokutana na Mbowe alipokuja shuleni kwetu kuomba kura mwaka 2000 akiwa ni mgombea ubunge, alinivutia sana na sera za chama chake, ingawa sikujiunga na chama kwa wakati huo, tena alishinda,” anasema Mtema.

Baada ya kuhitimu kidato cha tano na sita Mtema anasema, alijiunga na chuo cha kilimo Sua, kuanzia mwaka 2003 hadi 2006 ambapo alifanya, fani ya Sayansi ya Uchumi na Lishe na huko ndiko alikopata uamuzi wa kujiunga na siasa rasmi yani chama cha Chadema.

“Nilijiunga na Chadema nikiwa Sua mwaka 2005 kufuatia vuguvugu la kisiasa vyuoni,” anasema Mtema.

Anasema, baada ya kukamilisha masomo yake chuoni hapo, mwaka 2007 aliamua kujiunga na Chadema Makao Makuu akiwa ni Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana na Wanawake, iliyokuwa ikiongozwa na Mkurugenzi wake John Mnyika.

Anasema akiwa katika nafasi hiyo, alipata uzoefu kwa kujifunza mambo mingi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii huku akipata msaada mkubwa wa mafunzo na maelekezo ya kazi kutoka kwa Mnyika.

“Awali nilipofika makao makuu kuna wengine walidhani kama sitaweza kufanya kazi na wengine waliona nitaweza, lakini kwa ushirikiano na wenzangu nimefanikiwa sana,” anasema.

Mtema anafafanua kwamba, baada ya mabadiliko ya uongozi ndani ya kurugenzi mbalimbali za chama chao Januari mwaka huu, aliteuliwa kuwa Afisa Mafunzo katika Kurugenzi ya Oganaizesheni na Mafunzo ya Chadema.

“Hii ni sababu na ushahidi tosha kwamba kazi zangu zinakubalika kwa kuwa kama hazikubaliki nisingeteuliwa katika nafasi hii hata siku moja,” anajisifia Mtema.

Anasema, ameamua kujiunga na siasa na kuacha kazi nyingine za kuajiriwa, kwa sababu anaamini kuwa, katika siasa ni rahisi kwa mtu kutoa maoni yake na kusikilizwa pamoja na kufanyiwa kazi kwa haraka.

“Mimi ni mlemavu, lakini nyuma yangu kuna walemavu wengi, ambao hawajapata elimu kwa sababu mbalimbali zikiwamo mitazamo potofu ya jamii, juu ya watu wenye ulemavu, na kama huna elimu huwezi kuajiriwa, hivyo niliamini kuwa ipo siku moja nipata nafasi ya kuwasaidia japo kufikisha kero zao serikalini,” anasema Mtema na kusisitiza:

“Nilitaka kuja kuwasaidia wenzangu, kwa sababu kwenye siasa ndio mambo yote yanakofanyika. Utungwaji wa sera, sheria, usimamizi na marekebisho yake yanafanyika katika siasa, nilipenda na mimi niwe miongoni mwa watunga sera, sheria na hata warekebishaji.”

Akizungumzia changamoto kazini Mtema anasema, kwanza alipata ugumu kutoka katika familia yake kwa sababu hawakuwa tayari mtoto wao ajiunge na kazi ya siasa kutokana na imani waliyonayo kwamba, siasa ni fujo, vurugu na mchezo mchafu.

“Hofu yao kubwa ilikuwa ni kupoteza maadili kwa sababu wanaona siasa labda ni uhuni na ni kazi isiyo na heshma. Lakini nilitumia ujanja bila ya wao kujua,” anasema na kutoa mfano wa ujanja aliyotumia:

“Kwa mfano, baba yangu mzazi alijuwa kuwa mimi ni mwanasiasa wa Chadema Makao makuu baada ya miezi miwili, licha ya kuwa nilikuwa nalala nyumbani mwake, nakula chakula chake na nilikuwa napanda gari baadhi ya wakati kwa fedha yake, alikuwa ananiona natoka asubuhi narudi jioni, tena alijua kupitia mtu mwingine sio mimi.”

Anasema, baada ya kuja walisikitika sana, lakini ilibidi wakubali matokeo na mpaka leo hawaridhiki mimi kuwa mwanasiasa na hii inatokana na tafsiri mbaya ya siasa katika jamii kuwa ni fujo, mikiki mikiki na uovu.

Mtema anasimulia kuwa, kwa upande wa changamoto kazini, “Nilipoonekana kuwa ni mlemavu maswali yalikuja ataweza kweli? na wengine walikuwa wanaongea pembeni, na kunihukumu kuwa siwezi tu, lakini baadhi waliona naweza kina Mnyika na nimefanya nao kazi vizuri sana.”

Anasema, kwa wale walimuamini na kumkubali kuwa anaweza, wamethibitisha kwa sababu ndani ya muda wake Chadema ameweza kufanya kazi vizuri, tena wakati mwingine kuliko hata wale waliowazima na wakamilifu wa kimaumbile.

“Ulemavu wangu ni wa kimaumbile tu lakini si katika kazi,” anasema Mtema.

Anasema, baadhi ya wakati akipanda Jukwaani kabla ya kuhutubia umati wa watu katika mkutano, huwa anashangiliwa sana jambo ambalo anasema humpa maswali mingi bila ya majibu, iwapo kelele hizo ni za kukubalika kwake au la.

Mtema anasena amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kazi ya siasa hasa akiwa makao makuu ya Chadema na kwamba matarajio yake kwa sasa ni kugombania nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Baraza la Vijana la Chadema katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

“Nikifanikiwa kushinda nitakuwa nitatengeneza historia kwa sababu nitakuwa msichana na mlemavu wa kwanza Tanzania kuwa katibu mkuu wa baraza la vijana katika vyama vyote,” anasema Mtema.

Sambamba na hilo, Mtema anasema anatarajia kujitupa Jimboni kugombea ubunge katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kama Mwenyezi Mungu atamueka hai na mzima.

“Kwa mwaka 2010 ni ngumu kuingia jimboni, lakini matarajio yangu ni kuijtupa huko katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa sababu jamii bado haijawakubali ipasavyo walemavu, wanawake na vijana lakini natarajia ikifika muda huo, mwamko utakuwa wa kutosha katika jamii kuhusu sisi,” anasema.

Mbali na kuwa Afisa Mafunzo wa Chadema Mtema ni Mkurugenzi wa Vijana na Michezo katika Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata).

Mlowe: Chagueni viongozi, msichague wafadhili

Salim Said
VITA dhidi ya adui ufisadi inaendelea kushika kasi nchini, ambapo watu wengi sasa kwa nafasi zao mmoja mmoja au kupitia jumuiya na madaraka yao wanaamua kuchukua nafasi na hatua.

Hii ni kwa sababu watu wameanza kuelewa kuhusu ubaya na hasara ya ufisadi nchini katika nyanja tofauti za maisha ya jamii, kiuchumi, kisiasa na hata kijamii.

Baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi Taifa, Mikoa, Wilaya hadi Kata, baadhi ya viongozi waliochaguliwa wameonekana kuingia madarakani wakiwa na nia nzuri ya kupambana na ufisadi kwa maslahi ya taifa.

Bononi Mlowe ni Mwenyekiti mpya wa jumuiya ya wazazi kata ya Mabibo jijini Dar es Salaam, anasema kwa muda mrefu watoto wa kitanzania wamekuwa wakikosa ada ya shule na hata vyuo, vitabu vya kusomea na maabara za uhakika na miundombinu mingine ya kielimu kwa sababu ya ufisadi uliokithiri nchini.

Anasema Watanzania wanazidi kuzama katika dimbwi la umasikini na ufukara kwa sababu ya baadhi baadhi ya viongozi kujifanya wafadhili badala ya kuwa viongozi na kuwatumikia wananchi waliowachagua.

“Pengo la walionacho na wasiokuwanacho linazidi kukua siku hadi siku si kwa sababu nyingine bali baadhi ya viongozi ndani ya vyama na serikali kuwa sio waaminifu katika kulinda rasilimali za umma,” anasema Bononi.

Ili kuondokana na tatizo hilo, Bononi anawashauri wapiga kura wote nchini katika chaguzi za ndani ya vyama na zile za kitaifa za viongozi wa serikali, kuwa makini na kutokubali kabisa kumchagua mgombea yeyote kwa sababu ya kugawa fedha wapigakura.

“Tujiepushe na tuwajue wale wote wanaokuja kwetu kuomba kura kwa kigezo cha kugawa fedha kwa wananchi au wanachama wenzao, hao si viongozi bali ni wafadhili na wafanyabiashara,” anasema Bononi na kusisitiza:

“Sitegemei hata kidogo baada ya watoto wetu kukosa ada, baada ya miundombinu yetu kuzidi kuwa mibovu na baada ya mama wajawazito na watato wachanga kupoteza maisha kwa sababu ya ufisadi, halafu mtanzania akakubali kurubuniwa kwa fedha mbuzi, ili atoe kura yake, iwe ndani ya chama au nje ya chama.”

Anasema, ikiwa mtanzania yeyote atakubali kurubuniwa kwa fedha au mchele katika kampeni za uchaguzi ajue kuwa anatengeneza mazingira ya mtoto wake kukosa ada, matibabu na hata miundombinu bora ya kusomea.

Anasema, watanzania wamekuwa wakichagua viongozi kwa miaka mingi, lakini viongozi hao hawawajali wapiga kura wao na badala yake wanaamua kutajirisha matumbo yao.
“Kwa muda mrefu tunaumizwa na viongozi kama hawa sasa imefika wakati wa kuhakikisha kuwa tunaondokana na tatizo la viongozi wafadhili, badala yake tupate viongozi watoa huduma,” anasema Bononi.

Anasema, viongozi wengi wamekuwa wakiingia madarakani wakiwa masikini wasio na kitu, lakini muda mfupi baada ya kuingia madarakani wanaibuka na kuwa matajiri wakubwa nchini na kuanza kutoa misaada kwa watu mbalimbali bila wao kuhoji fedha hizo zimetoka wapi.

“Lazima tuhoji, mtu tulikuwa naye, baadhi ya wakati tumesoma darasa moja kwa nini baada ya muda mfupi kuingia madarakani awe tajiri mkubwa, hivi huu uongozi ni dhamana au biashara,” anahoji Bononi.

Anawataka wananchi kuwakataa wagombea wa vyama vyote vinavyojaribu kuomba kura kwa kutanguliza fedha, kwa sababu kiongozi wa namna hiyo hawezi kuwajali wapiga kura wake, bali kwanza atataka kujilipa fedha zake alizotumia wakati wa kuomba kura.

Bononi anafafanua, tatizo la uporaji wa mali za umma na za chama kwa baadhi ya viongozi linatokana na tamaa kubwa ya mali waliyonayo pamoja na ukosefu wa kazi nyingine za kujitegemea kwa ajili ya kujipatia kipato.

“Uongozi wa kisiasa ni huduma kwa maana kuwahudumia wananchi, lakini watu wengi wanashindwa kuelewa, jambo ambalo huibadilisha huduma hiyo na kuifanya kuwa kazi ya kutafutia fedha au biashara, watu wa namna hii ni hatari na hawatufai,” anasema Bononi.

Anasema, katika awamu yake ya miaka mitano, atahakikisha kuwa anawashawishi viongozi wa jumuiya hiyo kutafuta kazi nyingine kwa ajili ya kujipatia fedha na kuifanya kazi ya uongozi kuwa huduma badala ya biashara.“Wakipata kazi nyingine ya kutafutia fedha watakuwa waaminifu katika mali za chama na ada za watoto wetu, hii itatusaidia kunyanyua maendeleo na kuimarika kwa jamii,” anasema Bononi.

Anasema, lengo la ushawishi huo ni kuhakikisha kuwa wanapata viongozi bora watakaoipeleka mbele jamii ya watanzania na sio bora viongzi watakaoendelea kuididimiza na kuidumaza jamii ya watanzania.

“Tunataka kila mtu ajue kuwa uongozi ni dhamana ya kuwahudumia wananchi na sio kuanza kumaliza ada za watoto na fedha za maendeleo kwa kuifanya dhamana hiyo kuwa ajira,” anasema Bononi.

Anasema, tatizo la ufisadi si tu la kata yake bali ni kitaifa ambapo kumalizika kwake kunahitaji mchango wa kila mtanzania bila ya kujali rangi, dini, itikadi au kabila.

Bononi anasema, atahakikisha kuwa wanaendesha semina za elimu ya uraia kwa viongozi ili kuhakikisha wanawajenga kiuzalendo kwa ajili ya kuwafanya kuwa askari wazuri wa kulinda rasilimali za Umma.

Changamoto kubwa ambayo anaiona iko mbele yake Bononi anasema, watu ambao wanatumia dhamana ya uongozi kama biashara wamejipanga vizuri, wako imara, wana fedha na ni hatari lakini anasema kwa kushirikiana na wananchi inawezekana kuwang’oa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Makete mkoani Iringa Hawa Ng’humbi anasema, kukithiri kwa vitendo vya wizi wa rasilimali wa umma ni matokeo ya kuporomoka kwa maadili miongoni mwa watanzania.

Anasema, ni hatari kubwa kwa kuwa kadiri siku zinavyoenda na ndivyo maadili ya vijana wa kitanzania ambao ndio watakuwa viongozi wa baadaye yanavyozidi kuporomoka.

“Watanzania hasa wazazi tuna kazi na jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa tunajenga na kurudisha maadili mema kwa vijana wetu ili waje waikoe nchi yetu siku za baadaye,” anasema Ng’humbi ambaye pia ni mlezi mkuu wa jumuiya ya wazazi ya CCM kata ya Mabibo.

Ng’humbi anakiri kuimarika kwa vyama vya upinzani nchini jambo ambalo kila chama kinahitaji kuingia madarakani kwa kutumia mbinu na mikakati mbalimbali vilivyojiwekea.