MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, June 17, 2009

Karibu katika maisha mapya ya Tanzania


Mama mongella akikaribishwa mara baaada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu J. K. Nyerere jijini Dar es Salaam.

TGNP waisifu bajeti ya Serikali

Salim Said
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeisifia bajeti ya serikali ya mwaka 2009/10 kwa kuwa imelenga kukuza pato la ndani na kupunguza utegemezi kwa wahisani na misaada ya nje.


Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao huo, Usu Mallya katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyoandaliwa na timu ya wataalamu wa jinsia na maendeleo katika semina ya wiki moja.

Mallya alisema, bajeti hiyo imewekeza fedha nyingi katika sekta mmuhimu za kijamii na kiuchumi zikiwamo za elimu, kilimo, miundombinu na maji.

“Tumefurahishwa sana na bajeti ya mwaka kwa kutenga fedha nyingi katika vipaumbele muhimu vya kijamii na kiuchumi, japokuwa kuna ukosefu wa taarifa za kuhakikisha fedha hizo zinawafaidisha walengwa,” alisema Mallya na kuongeza:

“Hususan makundi ya watu yanayotengwa na kukandamizwa kimaendeleo ambao ni pamoja na wanawake, waathirika wa virusi vya ukimwi na watu wenye ulemavu.”

Alisema wanakubaliana na mpango wa serikali wa kupunguza matumizi ya fedha za umma kwa katika gharama za safari, semina, makongamano na ununuzi wa magari ya kifahari.

“Japokuwa hii si mara ya kwanza kwa serikali kupitisha maamuzi kama haya, lakini swali la kujiulza hapa ni vipio kuhusu ukubwa wa serikali kuu yenye mawaziri 26,” alisema Mallya.

Alisema, TGNP inaunga mkono juhudi za serikali katika kujinasua na athari za mtikisiko wa kiuchumi duniani, kwa kuongeza uzalishaji wa chakula cha ziada na kuimarisha miundombinu na mawasiliano ili kuweza kuhimili ushindani wa soko la kikanda na kidunia.

“Ni ulinzi wa aina gani ambao serikali imeuweka katika kulinda ajira za watanzania, soko la mazao ya Tanzania na viwanda vidogo na vya kati ambavyo vimeathirika mitaji yao kutokana na mtikisiko wa kiuchumi,” alihoji Mallya.

Alisema, serikali za magharibi zilibaini athari za mitikisiko huo mapema na kuanza kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na hali hiyo katika sekta za uchumi na fedha.

Hata hivyo Mallya alisema, fedha nyingi zinahitajika ili kufikia malengo ya milenia ya usawa wa kijinsia kwa asilimia 50 kwa 50 kati ya wanaume na wanawake, katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Aliitaka serikali kuimarisha wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuongeza kodi kwa makampuni na watu wenye kipato cha juu.

Alitahadharisha kuwa, mzigo wa kuimarisha wigo wa kukusanya mapato ya ndani usiangushwe kwa viwanda vidogo, vya kati, wajasiriamali pamoja na watu masikini pekee nchini.

“Ikizingatiwa kupanda kwa gharama za maisha na kuanguka kwa thamani ya shilingi, mshahara wenye kodi ya asilimia 30, lazima ipande kutoka Sh720,000 hadi Sh1,000,000 au zaidi na wale wa mstari wa chini lazima ipande kutoka Sh100,000 hadi Sh150,000 ili kutoa nafuu kwa watu wenye kipato cha chini,” alisema Malya na kuongeza.

Je, itakuwa bajeti ya Kilimo Kwanza


Salim Said
‘LEO ni siku ya Bajeti’, Zaidi ya Watanzania 40 milioni nchini kote wanaelekeza macho, masikio na hisia zao Mji Mkuu wa Tanzania Dodoma, ambako Waziri wa Fedha na Uchumi Mustapha Mkulo anasimama Bungeni kuisoma bajeti ya serikali kwa mwaka 2009/10.

Kila Mtanzania awe wa mjini au kijijini kuanzia mwanafunzi au mwalimu, mkulima au mfanyakazi, tajiri au masikini, mfugaji au mvuvi na hata mchimbaji madini au mfanyabiashara ana hamu na shauku ya kutaka kujua, iwapo bajeti hiyo itamkwamua kiuchumi, kijamii na kisiasa au itazidi kumdidimiza.

Aidha, mwelekeo huo wa bajeti ya 2009/10, unaonyesha serikali inatarajia kukusanya Sh9.5 trilioni ikilinganishwa na Sh7.3 trilioni za mwaka 2008/09, ambapo pato la ndani litachangia Sh5.1 trilioni, misaada na mikopo ya nje Sh3.2 trilioni na Sh1.2 trilioni zitatoka katika mapato mengine, huku matumizi ya kawaida yakitarajiwa kuwa Sh6.7 trilioni na maendeleo Sh2.8 trilioni.

Mtanzania wa kila rika na daraja ana hamu ya kujua ni mambo gani ambayo yamepewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka huu, je ni masuala Mtambuka (cross cutting issues) au sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Bajeti ya mwaka 2008/2009 ilitoa kipau mbele katika sekta nne kubwa ambazo ni elimu, miundombinu, kilimo na afya, swali ni je, bajeti ya mwaka huu ni sekta gani, zitapewa kipaumbele na kuongezewa gawiwo au fungu la fedha?

Wakati waziri Mkulo anasimama bungeni leo kwa muda wa masaa kadhaa kusoma kurasa, aya na maelfu ya maneno ya maelezo ya bajeti hiyo, jamii ya kitanzani inakabiliwa na changamoto kubwa ya athari ya mtikisiko wa kiuchumi unaoendelea kuikabili dunia.

Upepo unaonesha, bajeti ya mwaka huu inaakisi wazi kuwa, vipaumbele vitatu vya kwanza ni elimu sh1.7 trilioni 2009/10 kutoka sh1.4 mwaka jana, miundombinu sh1.0 trilioni mwaka huu kutoka sh973.3 bilioni mwaka Jana na kilimo iliyoongezewa fungu kutoka sh513 bilioni 2008/09 hadi sh666.9 bilioni 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 30.

Vipaumbele vingine ni afya sh963.0 bilioni kutoka sh910.8 bilioni mwaka jana, maji sh 347.3 bilioni mwaka huu kutoka sh231.6 mwaka jana na nishati.

Waziri Mkulo anasema, bajeti ya 2009/10 ni ya kilimo kwa kuwa mkazo utawekwa katika kuhakikisha serikali inaimarisha sekta ya hiyo, baada ya kuathirika mno na mtikisiko wa kiuchumi duniani, ikiwa na sura ya sekta mama ya kiuchumi na kijamii.

“Kwa Tanzania madhara ya mikisiko huo yamejitokeza katika kilimo, ambapo wauzaji wa mazao ya pamba, kahawa, katani, korosho na maua wameathirika kutokana na kuanguka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia,” anasema Mkulo.

“Lakini serikali tayari imeanza kuinusuru nchi hasa sekta ya kilimo kutokana na athari za kuadimika kwa chakula duniani zilizochochewa na mtikisiko huo pamoja na hali mbaya ya hewa.”

Anasema, licha ya fungu la kilimo kuzidiwa na sekta nyingine mbili yani elimu na miundombinu, lakini mkazo mkubwa utawekwa katika kilimo kwa upekee, ili kuhakikisha mabadiliko yanapatikana katika sekta hiyo.

“Kauli mbiu ya bajeti ya 2009/10 ni ‘Kilimo Kwanza’ ambapo serikali itaweka mkazo katika kupanua na kuboresha kilimo kwa mapana yake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mbolea, madawa, mbegu bora, zana za kilimo, huduma za ugani na mikopo nafuu kwa ajili ya kilimo,” anasema Mkulo.

Waziri Mkulo anasisitiza, “katika bajeti ya 2009/10 serikali itahakikisha kupanua miradi ya kilimo cha umwagiliaji, lengo ikiwa ni kuwahikikishia watanzania upatikanaji wa chakula cha kutosha na kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao ya biashara.”

Anasema, serikali pia katika bajeti hiyo, itaongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP) na mikakati ya kukabilaina na athari za kuporomoka kwa uchumi wa dunia, hususan katika sekta ya kilimo.

Ili kuthibitisha nia ya dhati ya serikali katika kuimarisha sekta ya Kilimo Mkulo anasema, “kwa mwaka huu wa bajeti wataongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo, hususan katika sekta ya kilimo kwa kuanzisha benki ya Kilimo na ya Wanawake ili kuongeza uzalisaji wa mazao ya chakula.”

Kabla ya Mkulo kusema haya, serikali ilishaanza kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha inaboresha sekta ya kilimo nchini, ambapo Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda alipiga marufuku uendeshaji wa semina, warsha na makongamano na ununuzi wa magari ya kifahari ya serikali, ili kupunguza matumizi mabaya ya fedha za umma.

Badala yake anataka fedha hizo zitumike katika kununulia matrekta na kuyasambaza katika maeneo muhimu ya kilimo nchini, ili kuimarisha sekta hiyo na kuwaondoa wakulima katika kilimo cha jembe la mkono na kuwapeleka katika kilimo cha biashara.

Pinda anasema atahakikisha, analibeba ipasavyo suala la kuleta mageuzi katika kilimo kwa kuhakikisha upatikanaji wa matrekta kwa wakulima na kusisitiza, wizara na idara nyingine za serikali hazina budi kuimba wimbo mmoja wa ‘Kilimo Kwanza’, hadi yapatikane mageuzi katika sekta hiyo.

Pamoja na hayo ya Pinda, Rais Jakaya Kikwete naye aliitangaza baadhi ya mikoa kuwa ni maeneo muhimu kwa kilimo ambayo ni pamoja kuutangaza mkoa wa Morogoro kuwa ghala la taifa la chakula.

Aidha, Rais Kikwete anasema taifa limepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu nchini ambapo wamefanikiwa kujenga shule ya sekondari katika kila kata na nyengine zikiwa na shule zaidi ya moja na ndio mana mkazo sasa ukawekwa katika kilimo.

Lakini baadhi ya wabunge nao wanazipokeaje juhudi hizi za serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula na upanuzi na uimarishaji wa sekta ya kilimo chini ya mwevuli wa kauli mbiu ya ‘Kilimo Kwanza’?

Omar Saddiq mbunge wa Mvomero (CCM) anahoji namna serikali inavyoyafanyia kazi maeneo ya vipaumbele vya bajeti, akidai hadi sasa kila mwaka serikali inatangaza vipau mbele, lakini hajaridhika na namna vinavyofanyiwa kazi.

“Taifa haliwezi kujinasua hata kidogo kiuchumi na kijamii bila ya viwanda, hivyo serikali inatakiwa kuandaa mkakati maalum wa kuanzisha, kufufua na kuboresha viwanda vya ndani,” anasema Saddiq na kusisitiza:

“Haya matarakimu ya serikali imetenga fedha kiasi gani hayana maana kwa mwananchi wa kawaida na wala hana habari nayo, anachohitaji ni kupata maisha bora. Mkazo wa ajira katika sehemu nyeti za kilimo, elimu, afya na miundombinu lazima uwekwe.”

Monica Mbega (CCM) kwa upande wake analia na watoa mikopo wanavyowakandamiza na kuwazidishia umasikini wakopaji wadogowadogo kwa kuwatoza kiwango kikubwa cha riba na kuhoji.

“Je wataalamu wetu wa Wizara ya Fedha na Uchumi pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wanafanya nini ili kuhakikisha watu wengi wanapata mikopo tena kwa riba na masharti nafuu kwa ajili ya kuongeza shughuli za kilimo kama sekta ya kiuchumi nchini.”

Anafafanua, Wizara ya Fedha na Uchumi na Wizara ya Kilimo na Mifugo ni wizara zinazotegemeana sana, lakini hajui ni kwa kiwango gani zinashirikiana, ili kuhakikisha vocha za mbolea zinawafikia wakulima kwa wakati.

“Naomba wizara hizi zishirikiane kwa karibu ili kuhakikisha vocha za mbolea zinawafikia wananchi mapema mwezi Agosti, ili mvua za vuli zikianza zikute tayari mbolea imemfikia mkulima,” anaomba Mbega.

Naye, Devotha Likokola viti maalum (CCM) anasema, duniani kote Benki Kuu zinasimamia shughuli za Makbwela (microfinance), lakini anahoji BoT inafanya kazi gani?

Dk. Mreru Omar mbunge wa Morogoro Mjini (CCM) anasema, Rufiji na Morogoro ni maeneo muhimu kwa kilimo na kwamba yanaweza kuliokoa taifa kwa muda mfupi.

“Hatutaki mbolea sisi, tunachohitaji ni vitendea kazi, ukituletea mbolea unaharibu rasilimali. Sisi tuletee matrekta, mbegu bora na wataalamu na ndio mana rais Kikwete, akautangaza mkoa wetu wa Morogoro kuwa ghala la taifa la chakula, anasema Dk. Mzeru.

Juma Siraju Kaboyonga mbunge wa Tabora Mjini (CCM) anasema,“Tukubali tusikubali lakini riba katika mabenki na taasisi za fedha nchini ni tatizo na kikwazo kwa maeneleo ya kilimo. Sisi tukiweka fedha benki riba yake ni asilimia 3, lakini ukikopa ni asilimia 18 hadi 20.”

Anashauri, “Tuache kutumia fedha za umma katika kusafirisha warembo na timu za mpira nje ya nchi kwa gharama kubwa, badala yake tupeleke fedha hizo katika kilimo.”

Kaboyonga anaonesha hofu yake kuhusu kauli mbiu ya ‘Kilimo Kwanza’ akisema, “Hiyo ni misemo tu ya kisiasa, lakini kinachohitajika ni utendaji na ufanisi.”

“Zimepita nyingi kama hizo ikiwa ni pamoja na ‘Kilimo ni uti wa Mgongo, Siasa ni Kilimo, Kilimo ni Sekta Kiongozi na sasa Kilimo kwanza’. Tunahitaji uwezeshwaji na ufanisi wala si misemo ya kisiasa.”

Mkulo: Pato la taifa litaanguka hadi 2011

Salim Said
WAKATI ukuaji wa uchumi katika mataifa ya Ulaya na Marekani ni wa kukimbia, ule wa nchi za Afrika unazidi kudorora kwa kurudi nyuma hatua kadhaa badala ya kusonga mbele.

Haya yanathibitishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi Mustapha Mkulo katika ripoti yake ya kurasa 26, kuhusu ‘Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2008 na Malengo ya Uchumi Katika Kipindi cha Muda wa Kati (2009/2010 hadi 2011/2012)’.

Waziri Mkulo anathibitisha katika ripoti hiyo, kuanguka kwa pato la taifa kulikosababishwa na kuyumba na kutikisika kwa uchumi wa dunia kuanzia Marekani, Ulaya hadi Afrika.


Awali, kabla ya Mkulo kukiri kuanguka kwa uchumi wa taifa, wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kiuchumi, walidokeza anguko hilo wakiwamo, Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini Esther Mkwizu.

Wachambuzi hao walisema, mtikisiko wa kiuchumi unaoendelea kuikumba dunia una sura ya herufi ‘L’ ikiwa na maana kwamba, uchumi utaanguka hadi chini na utakaa kwa muda wa miaka mitatu hadi mitano ndipo utanyanyuka na kutengamaa.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, hiyo inasababishwa na benki na kampuni kubwa za kimataifa kuanza kufilisika, huku shughuli za kiuchumi zikizidi kuanguka licha ya benki hizo, kushusha riba hadi asilimia 0.0.

Maneno haya ya profesa Lipumba na Mkwizu yanathibitishwa na waziri Mkulo kwa kusema, pato la taifa kwa mwaka 2009 litaanguka kwa asilimia 2.4 ambapo ukuaji wake utakuwa ni asilimia 5.0 ikilinganishwa na asilimia 7.4 mwaka 2008 na asilimia 7.1 mwaka 2007.

Mkulo anasema, ukuaji huo wa pato la taifa mwaka 2008, ulichangiwa zaidi na kuongezeka kwa viwango vya ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika sekta ya kilimo, uvuvi na huduma.

Anasema, ukuaji wa viwango vya juu vya pato la taifa mwaka 2008 ulijionesha katika shughuli ndogo ndogo za kiuchumi za mawasiliano asilimia 20.5, fedha 11.9 na ujenzi asilimia 10.5.

“Hata hivyo kiwango cha ukuaji katika shughuli za kiuchumi za viwanda na ujenzi kilipungua kidogo ikilinganishwa na mwaka juzi,” anasema Mkulo.

Kwa mujibu wa Mkulo, pato la taifa si tu kuwa litaanguka kwa mwaka 2009, bali litaendelea kudorora katika kipindi chote cha muda wa kati ambapo mwaka 2010 ukuaji ni asilimia 5.7 na kwamba pato hilo litatengamaa mwaka 2011/2012 kwa kufikia kiwango cha asilimia 7.5.

“Ili kukabiliana na hali hiyo, serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kukuza pato la taifa na kupunguza umasikini na kwa kuzingatia hilo hatua zinachukuliwa kuboresha mazingira ya kuziwezesha sekta hizo kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi,” anasema Mkulo.

Anasema, serikali ina mpango wa kukamilisha sera ya ubia kati ya sekta ya Umma na Binafsi (PPP Policy) ili kuharakisha maendeleo ya sekta binafsi na kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini nchini.

Anasema, pia serikali itaongeza ufanisi katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma, biashara, kilimo, uwekezaji na kupunguza matumizi ya serikali yasiyo ya lazima katika mapato yake.

Mkulo ansema, serikali kwa kuzingatia chanzo cha mtikisiko huo, Benki Kuu (BoT) imeanzisha utaratibu wa uangalizi na usimamizi wa taasisi za fedha kila siku, ili kubaini matatizo yatakayojitokeza na kuchukua hatua za haraka.

“Kwa kupunguza makali na kuhimili shinikizo la mtikisiko huo hususan katika kuwalinda wananchi walio kwenye hatari kubwa zaidi, Serikali inalinda ajira, hasa katika shughuli zitakazokumbwa na ukwasi kutokana na kupungua kwa utashi wa bidhaa na huduma wanazotoa,” anasema Mkulo.

Anasisitiza, ili kuinusuru nchi kutokana na athari za kuadimika kwa chakula, serikali inaongeza kasi katika kilimo, kulinda programu muhimu za kijamii na uwekezaji kwa maendeleo ya nchi.

Huku pato la taifa likiporomoka kwa asilimia 2.4 kwa mwaka 2009, nchi inakabiliwa na matatizo ya mfumko wa bei, kushuka kwa thamani ya sarafu mambo ambayo, serikali inasema haina uwezo wa kuyadhibiti kwa madai kuwa ni ya kimfumo na yanategemea zaidi nguvu ya uchumi wa soko.


Waziri Mkulo, anasema tatizo la kushuka kwa thamani ya sarafu halizuiliki kwa sababu ni la kimfumo na linasababishwa na mfumuko wa bei za bidhaa muhimu na upatikanaji wa fedha za kigeni, ambao ni wa msimu. “Mheshimiwa Mwenyekiti tutake tusitake, tatizo la kupanda na kushuka kwa sarafu ya Tanzania lipo na serikali haiwezi kulizuia kwa sababu ni la kimfumo,” anasema Mkulo.

Anafafanua, kinachofanywa na serikali kukabiliana na tatizo hilo ni kuangalia iwapo mzunguko wa shilingi ya Tanzania unaendana na uchumi wa soko au vinginevyo.

“Kama mzunguko ni mbaya tunaweza kuingilia na kurekebisha lakini, kama unaendana na uchumi wa soko, hatuwezi kuingilia hata kidogo,” anasisitiza Mkulo.

Mkulo anathibitisha, “Upatikanaji wa fedha za kigeni nchini kuwa ni wa msimu hususan wa mavuno kuanzia Juni hadi Disemba ya kila mwaka, lakini pia tukiweza kudhibiti mfumko wa bei za bidhaa muhimu tunaweza kudhibiti thamani ya Shilingi yetu.”

Kwa mujibu wa Mkulo, thamani ya Shilingi ya Tanzania imeshuka hadi kufikia wastani wa Sh280.30 kwa Dola ya Marekani Desemba mwaka jana ikilinganishwa na Sh1,132.09 Desemba 2007.
Anasema, mfumko wa bei kwa mwaka 2008, ulikua kwa asilimia 10.3 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2007, ambapo kiwango cha chini cha kasi ya mfumko huo 2008, ilikuwa Januari kilipopanda kwa asilimia 8.6 na kiwango cha juu asilimia 13.5 Disemba mwaka huohuo. “Lengo letu la ukuaji wa mfumko lilikuwa asilimia 5.0 Juni 2008, lakini halikufikiwa kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji hasa baada ya kupanda kwa bei ya nishati hususan mafuta na umeme,” anasema Mkulo na kuongeza:

“Hadi April 2009, mfumko ulifikia asilimia 12.0 kutokana na hali hiyo, ambapo awali lengo la mfumko huo lilitarajiwa liwe chini ya asilimia 7.5 ifikapo Juni 2009, lakini sasa tunatarajia asilimia 11.0 ya mfumko.”

Mkulo anasema, ili kuhakikisha wanarudisha utengamano wa pato la taifa serikali itakabiliana na mtikisiko wa uchumi duniani, kuongeza uwekezaji katika maeneo ya mwingiliano wa kisekta hususan kilimo, miundombinu, uzalishaji viwandani na nishati ikiwa ni pamoja na kuhimiza ushirika wa sekta binafsi katika maeneo hayo.

“Serikali itaongeza upatikanaji wa mikopo hasa kwa sekta ya kilimo kwa kuwa na benki ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula,” anasema Mkulo.

Anasema, serikali itaongeza na kuboresha mapato ya ndani ili kugharamia sehemu kubwa ya matumizi ya serikali, kuimarisha usimamizi katika matumizi ya fedha za umma na kuendelea kulinda mafanikio yaliyopatikana.

“Serikali itaendelea kulinda na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta za kijamii na kuboresha utoaji wa huduma ili kuongeza wigo wa ukusanyaji na ukuzaji wa pato la taifa,” anasema.

Anasema, serikali pia itaongeza na kuboresha mipango ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kuongeza ajira pamoja na kupima ardhi ya vijijini ili wamiliki waweze kutumia hati zao kupatia mikopo.