MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Monday, June 1, 2009

TFDA kubadili maduka 9,000 ya dawa baridi kuwa ya dawa muhimu

Salim Said

MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), imesema inatarajia kubadilisha maduka 9,000 ya dawa baridi kuwa ya dawa muhimu (ADDO) hadi kufikia mwaka 2010 nchini kote.

Pamoja na lengo hilo, hadi sasa mamlaka hiyo tayari imeboresha na kubadilisha maduka 1200 ya dawa baridi na kuwa ya dawa muhimu katika mikoa minne ya Tanzania.

Kaimu Mkurugenzi wa Dawa na Vipodozi wa TFDA Hiiti Sillo aliiambia Mwananchi mwisho wa wiki iliyopita, kwamba pamoja na kuwaagiza wamiliki wa maduka ya dawa baridi kuyaboresha maduka yao ili yawe ya dawa muhimu, pia wanatoa mafunzo ya bure kwa watoa huduma wa maduka hayo, na kuwatunuku vyeti.

“Kwanza tunawaagiza wamiliki waboreshe maduka yao ya dawa baridi ili tuwapatie leseni za maduka ya dawa muhimu, wakikataa tunayafungia,” alisema Sillo.

Sillo alizungumza na Mwananchi Kibaha mkoani Pwani, mara baada ya kuwatunuku vyeti wahitimu 486 vya kuhitimu mafunzo ya siku 35 ya kutoa huduma katika maduka ya dawa muhimu.

“Tunashukuru leo tumewakabidhi vyeti wahitimu hawa ambao asilimia 99 ni wanawake na wameweza kushona unifomu za kutoa huduma za dawa zenye nembo ya TFDA,” alisema Sillo.

Alisema, TFDA kwa sasa imefanikiwa kubadilisha maduka ya dawa baridi 1200 na kuwa ya dawa muhimu, katika mikoa minne ambapo lengo ni kufikia mikoa 10 hadi mwisho wa mwaka huu.

Sillo aliitaja mikoa hiyo, ni Ruvuma, Morogoro, Rukwa, Mtwara, Pwani, Lindi, Mbeya, Tanga, Kigoma na Singida.

“Tumewafundisha utaalamu wa kutunza na kuhifadhi dawa, mawasiliano na wagonjwa, namna ya kutoa dozi na hasara zake ikiwa haitokamilishwa au ikizidishwa,” alisema Sillo.

Alisema, mafunzo hayo yalifadhiliwa kwa ushirikiano wa TFDA na Mfuko wa dunia wa kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua kikuu (Global Fund), Shirika la Misaada la Denmark (Danida), Serikali ya Tanzania na washiriki wenyewe.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dk Eligreta Mzava alisema mafunzo hayo, yatausaidia mkoa wa Pwani kuondokana na tatizo la vioski vya dawa baridi.

Dk. Mzava, alisema, TFDA imewasaidia kuondokana na ‘vioski’ vya madawa kwa kuwapatia mafunzo ya ufamasia watoa huduma katika maduka ya dawa mkoani mwake.

“Mafunzo haya kwa watoa huduma katika maduka ya dawa mkoani mwetu yatatusaidia kuondokana na tatizo la watoa huduma wasio na taaluma ya ufamasia na pia itatusaidia kuondokana na ‘vioski’ vya madawa,” alisema Dk Mzava na kuongeza:

“Kwa muda mrefu tulikuwa hatuna maduka ya dawa bali tulikuwa na ‘vioski’ vya madawa, lakini baada ya mafunzo haya tunashukuru na tunaamini sasa tutapunguza kama si kumaliza kabisa tatizo hilo.”

Lize Mwampasha, ambaye ni mmoja wa wahitimu alisema, mafunzo hayo yatawasaidia wao kuaminika katika jamii, kwa sababu walikuwa wanapata matatizo ya kutotambulika na kuaminika kama wao ni watoa huduma za dawa.

“Mtu anakuja anakuuliza we umesomea, unajaribu kumuelewesha, lakini ni kazi kweli mpaka akuelewe. Hivi sasa akija ananikuta na nguo za kiuguzi zenye nembo ya TFDA na cheti ninacho basi, itasaidia kuniamini,” alisema Mwampasha.