MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Sunday, February 21, 2010

PYUZA: WATANZANIA WENGI WANAKULA UBWABWA KWA PUA'

WALI
Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro (KATC) wilayani Moshi Adam Pyuza akitoa maelezo kwa waandishi wa habari hivi karibuni. picha na Salim Said.

Salim Said
MOJA ya kilio kikubwa cha wakulima wa Tanzania ni kukosekana kwa soko la uhakika la ajili ya kuuza mazao yao baada ya suluba ya kipindi chote cha kilimo.

Ili kukabiliana na tatizo au kilio hicho, serikali ilianzisha mfumo wa stakabadhi ghalani kama njia ya kuwakwamua wakulima wa mazao ya biashara lakini, licha ya nia hiyo nzuri, mfumo huo umekuwa ukipata upinzani mkubwa kutoka kwa wakulima katika baadhi ya maeneo.

Mfumo huo umeingia kwa kasi katika mikoa na wilaya zote za kanda ya kusini ya Tanzania, wakulima hutakiwa kuweka mazao yao ghalani na kupatiwa mkopo wa fedha za kujikimu, hadi hapo mazao yao yatakapouzwa na kulipwa.

Lakini kwa kanda nyingine za Tanzania, mfumo huo haujafika, wakulima wengi wanahangaika kupata soko la mazao yao, jambo ambalo husababisha kuchelewa kuanza na kumaliza kwa msimu mpya wa kilimo au kupata ugumu wa maisha kwa kukosa fedha za kujikimu.

Mathalan, katika Mkoa wa Kilimanjaro, kuna wakulima wanaozalisha kwa wingi mpunga, mahindi, alizeti na hata maharagwe kwa ajili ya chakula na biashara.

Lakini kama ilivyo katika kanda nyingine za kilimo, wakulima wa hao nao wanakabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa soko la uhakika la kuuzia mazao yao hasa mpunga.

Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro (KATC), Adam Pyuza anasema kuna sababu nyingi za wakulima wa mkoa huo hasa Wilaya ya Moshi kukosa soko la uhakika la mazao yao hususan mpunga ambao unazalishwa kwa wingi katika Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika ukanda wa Moshi Chini.

Anasema sababu kubwa ya kukosa soko la uhakika wa mpunga wao ni asilimia kubwa ya Watanzania kula ubwabwa (wali), kwa kutumia pua badala ya mdomo na ulimi, kwa maana wanapenda ubwabwa unaonukia.

“Asilimia kubwa ya Watanzania wanakula ubwabwa kwa pua badala ya mdomo. Ikiwa mchele wako haunukii, basi ujue kwa walaji wa Tanzania haununuliki, kwani soko kuu la mpunga linalotegemewa na wakulima nchini kote ni jiji la Dar es Salaam,” anasema Pyuza na kuongeza:

“Sifa kuu ya mchele unaolimwa katika Mkoa wa Kilimanjaro ni kwamba haunukii na hiyo ni sababu kuu ya mpunga wa wakulima wa Moshi kukosa soko, hivyo kuishia kukaa ghalani hadi hapo mpunga unapoadimika na wao ndipo hupata fursa ya kuuza.”

Anasema kutokana na sababu hiyo, wafanyabiashara wengi wakati wa mavuno hukimbilia sehemu za Mbeya, Kyela na Morogoro kuchukua mpunga na kupeleka sokoni Dar es Salaam, kwa sababu mipunga ya huko inanukia sana.
Anasema baada ya wafanyabiashara kuhakikisha kuwa wamemaliza mpunga katika maeneo hayo ndipo huamua kwenda Moshi na ambako hulazimisha kuuziwa mpunga kwa bei ya chini kabisa.

Anasema kuwa licha ya kuwa mpunga wa Moshi haunukii lakini una sifa ya kubwa ya kuvimba unapopikwa na hivyo kuufanya uwe na baraka kwa watumiaji.

Anasema kutokana na hali hiyo mchele wa Moshi hutumiwa zaidi katika hoteli, migahawa, shule za bweni na vyuo na hata kwa mama lishe kwa sababu unavimba.

“Wajanja wote wa mahoteli ya Moshi na wilaya jirani utawakuta wanautumia sana mpunga wa Moshi Chini kwa sababu wanachotaka wao ni kutengeneza faida na siyo harufu nzuri ya ubwabwa kwa kumridhisha mteja,” anasema Pyuza.
Anafafanua kuwa licha ya kupendwa na wenyeji, kutokana na ladha yake nzuri mchele wa Moshi umekuwa ukipendwa na majirani wa Tanzania hasa Kenya... “Utakuta mchele wa Moshi unauzwa sana Kenya kuliko hata Tanzania, kwa sababu Wakenya wanajua uchumi na hawaangalii sana harufu ya mchele bali cha msingi kwao ni kama una ladha nzuri na unavimba kulisha familia kubwa?”

Anasema ikiwa wakulima wa Moshi watategemea soko la ndani, basi lazima wasubiri hadi ule wa mikoa ya Mbeya na Morogoro utakapomalizika... “Kwa maana hiyo mchele wa Moshi misimu yote huuzwa mwisho kabisa.”
Anasema sifa nyingine ya mchele wa Moshi ni kutokuwa na mawe kwa kuwa unaandaliwa kwa kutumia vifaa vya kisasa vinavyotengenezwa na wahandisi wa KATC. Pyuza anasema bei ya gunia (aina ya lumbesa) moja ya mpunga wa Moshi huuzwa kwa Sh70,000 hadi Sh80,000.

Anasema mfumo wa stakabadhi ghalani haujafika Moshi kwa sababu chama cha ushirika hakijaimarika ipasavyo, kwa sababu mfumo huo huwa unasimamiwa na chama cha ushirika wa eneo husika.

Taarifa zinaonyesha kwamba Moshi kupitia mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji unaofadhiliwa na serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Jica inazalisha mchele kwa wingi tangu mwaka 1994. Katika mradi huo hekta 1,100 zinatumika kuzalishia mpunga na kila hekta ina uwezo wa kuzalisha tani 6.5 hadi nane.

Pyuza anasema chuo chake kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kupitia Shirika la Jica, kipo katika mchakato wa kusambaza mbegu mpya ya mpunga kwa Bara la Afrika (Nerica series), ambazo zimeshafanyiwa utafiti na majaribio na kujiridhisha kuwa ni bora na mchele wake unanukia vizuri na unafaa kwa soko la Tanzania.
Wakulima wanalalamika kwamba kukosekana kwa soko kumekuwa na athari kubwa kwao kwani wakati mwingine hukosa fedha za fedha kukodisha mashamba, kulimia, kulipia maji ya mradi na hata kununulia pembejeo.
“Kwa kweli kukosekana kwa soko la uhakika kunatupa changamoto kubwa sisi wakulima, kwa sababu baadhi ya wakati hata misimu inachelewa kuanza kwa sababu ya kukosa fedha za kuendeleza kilimo, kutokana na mazao yetu kukaa ndani tu,” anasema mkulima kiongozi, Hanfred Msuya.

“Kuna mchezo mchafu ambao tunafanyiwa na wachuuzi wa mpunga. Sisi huwa tunapima debe sita kwa kilo 80 katika gunia, lakini wao hulazimisha kujaza viroba viwili vya kilo gramu 50 ambavyo huwa wanakuja navyo, ukijaza utakuta gunia lina kilo 95 au 100.”

Lower Moshi: Tulianza Kilimo Kwanza tangu 1994

Salim Said
MWAKA jana, Rais Jakaya Kikwete alizindua kampeni ya kitaifa ya kuboresha kilimo nchini, iliyobatizwa jina la Kilimo Kwanza ikiwa na lengo la kuweka fungu kubwa la fedha kuhudumia sekta hiyo.

Fungu hilo ni kwa ajili ya kuwaandaa wataalamu wa kilimo na kununulia pembejeo ambazo ni matrekta, mbolea, dawa na zana nyingine za kilimo kwa kutumia teknolojia nyepesi na za bei nafuu.

Lakini wakulima wa kilimo cha umwagiliaji Moshi Chini (Lower Moshi) mkoani Kilimanjaro wanasema Kilimo Kwanza si jambo geni kwao kwani walishaanza kukitekeleza tangu mwaka 1994.

Kabla ya kuanza kilimo hicho, wakulima hao wa mpunga walipatiwa mafunzo katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro (KATC), ambacho awali kiliitwa Chuo cha Maendeleo ya Kilimo Kilimanjaro (KADC).

Mkuu wa chuo hicho, Adam Pyuza anasema: “Sisi watu wa Lower Moshi tumeanza kilimo kwanza kwa miaka mingi sasa. Tangu mwaka 1994! Serikali imechelewa sana kuliona hilo.”

Pyuza anasema wakulima wa ukanda wa Lower Moshi wameanza kilimo kwanza baada ya wote kupatiwa elimu ya kilimo cha umwagiliaji kwa nadharia na vitendo kuanzia mwaka huo.

“Elimu hii ya kilimo cha umwagiliaji inatolewa kupitia Ushirikiano wa Kitaalamu katika Kusaidia Mfumo wa Utoaji Huduma katika Kilimo cha Umwagiliaji (TC-SDIA) au kwa lugha ya kawaida mpango huu tunauita ‘Tanrice’ ambao unafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Misaada Japan (Jica).”

“Wakulima tuliowapatia mafunzo wameweza kuanzisha skimu bora za kilimo cha mpunga na kupata mafanikio makubwa kwa kulima kidogo na kuzalisha zaidi. Kabla ya mradi huu, watu wa ukanda wa Lower Moshi walikuwa hata kula yao kwa mwaka ni tabu.”

“Lakini kwa sasa wakulima wameweza kuimarisha mashamba yao na hata wakulima ambao awali walikuwa hawalimi mpunga wameacha kilimo chao cha ndizi na kuingia katika mpunga baada ya kuona wenzao wamepata mafanikio makubwa.”

“Hata wale wa vijiji vya jirani ambao hawakutaka kuingia katika mradi, sasa wote wamekuja na wanalima mpunga baada ya kuona wenzao wana uhakika wa chakula kwa mwaka mzima, wanasomesha watoto wao vizuri, wanauza ziada, wamejenga nyumba nzuri za kuishi na hata maisha yao yamebadilika.”

“Faida ya kwanza ni uhakika wa chakula, kukuza kipato cha wakulima kwa kuuza kwa sababu kama unavyojua mpunga ni chakula kikuu cha pili nchini, lakini pia mpunga unaweza kulimwa nchini kote katika maeneo ya mabonde na hata ya miinuko,” anasema Pyuza.

Anasema teknolojia ya uzalishaji mpunga ipo karibu nao katika chuo cha KATC pamoja na uhakika wa kupata mbegu bora kupitia utafiti wa Jica. Kadhalika, anasema utayari wa serikali ya sasa kusaidia miradi ya kilimo hicho ni mkubwa na kwamba hayo yote yatasaidia kuongeza uzalishaji wa mpunga.

Mratibu wa Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji Moshi Chini, Mhandisi Hatib Jengo anasema kilimo cha mpunga kwa njia ya kisasa kinatoa tija kubwa kwa mkulima.

Anasema mradi huo umetengewa hekta 2,300 za ardhi na kati ya hizo, hekta 1,200 ni kwa ajili ya kilimo cha mazao mchanganyiko na hekta 1,100 ni kwa ajili ya kilimo cha mpunga. Anasema kuna hekta nyingine zaidi ya 1,000 zinazohudumiwa na mradi ingawa mwanzo hazikuwamo.

“Mradi huu unategemea maji kutoka katika vyanzo vya Njoro na Rau, maji ambayo yanapitia katika mabanio (gates) mawili makuu ya Mabogini na Rau,” anasema Mhandisi Jengo.

Anasema kwa sasa wakulima wanatumia mbegu aina ya aero 54 na 65 ambazo sifa yake kubwa ni kwamba mchele wake haunukii lakini, unavimba hivyo kupendwa zaidi katika familia kubwa, shule za bweni, hoteli na hata vyuo.
Anasema mradi huo umeleta mapinduzi makubwa ya kilimo katika ukanda huo, ukiachilia mbali kuimarika na kuboreka kwa maisha ya wakulima hao lakini, hata baadhi ya watu waliokuwa hawalimi mpunga sasa wanalima baada ya kuona mafanikio ya wenzao.

“Kabla ya mradi huu, wakulima wa Lower Moshi walikuwa hawana uwezo hata wa kunua nyama lakini kwa sasa watumishi wakifika sehemu za kuuzia nyama wakulima wameshamaliza. Hata katika elimu, sasa tuna shule tano za sekondari ambazo, hazikuwapo kabla ya mradi huu,” anasema Mhandisi Jengo.

Anasema mavuno yamepanda kutoka tani mbili hadi tatu kwa hekta kabla ya mradi na kufikia tani sita na nusu hadi nane kwa hekta moja baada ya mradi.

Jengo anasema kuwa pamoja na mafanikio yote hayo, mradi wao unakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinahatarisha maisha yake. Kubwa ni uharibifu wa miundombinu unaosababishwa na kuibuka kwa biashara ya chuma chakavu. Baadhi ya wananchi wasio waaminifu wanaiba mabanio ya mifereji ya maji, bomba na vifaa vingine vya mifereji.

“Tabia hiyo imekuwa ikiugharimu mradi mamilioni ya shilingi. Hivi sasa wanahitaji fedha kutoka serikali kuu na halmashauri ili kukarabati miundombinu hiyo.”

Anasema ili kudhibiti uharibifu huo wameanzisha mpango wa ulinzi shirikishi kati yao, wakulima na Chama cha Wakulima wa Kilimo cha Umwagiliaji Moshi Chini (Lomia).

Changamoto nyingine ni kutofautiana kwa ratiba ya upandaji wa mpunga, jambo ambalo linasababisha matatizo katika ugawaji wa maji... “Kwa sasa kwa kushirikiana na Lomia na Chama cha Wakulima wa Mpunga Moshi (Chawampu) tunatoa elimu ili tuwe na ratiba moja ya upandaji wa mpunga na hata uvunaji kwa lengo la kurahisisha ugawaji wa maji.”

Anasema Lomia inajumuisha vijiji saba vya wakulima ambavyo baadhi vimo katika mradi na vingine havimo lakini vinalima kilimo cha mpunga kwa njia ya umwagiliaji na vinategemea maji hayo hayo ya mradi. Anavitaja vijiji hivyo kuwa ni Kaloleni, Madokamnoni, Mabogini, Rau, Njoro, Oria na Chekereni.

Pia kuna uhaba mkubwa wa maji. Baadhi ya misimu hulazimika kuacha baadhi ya hekta za ardhi kwa kuwa maji hayawezi kuhudumia hekta zote 2,300 za mradi na zile ambazo hazimo katika mradi kwa pamoja.

“Kutokana na hali hiyo baadhi ya wakati misimu huchelewa kuanza au kumalizika. Kwa kawaida sisi tuna misimu mitatu kwa mwaka, wa kwanza huanzia Januari hadi Mei, wa pili Mei hadi Septemba na wa mwisho Septemba hadi Januari,” anasema Jengo.

Katika jitihada za kutatua tatizo hilo, mwaka 1995 ulifanyika upembuzi yakinifu uliofadhiliwa na Jica ili mradi huo uchukue maji ya mita za ujazo tisa kwa sekunde wakati wa masika na kubiki mita tano kwa sekunde wakati wa kiangazi kutoka Mto Kikuletwa.

Lakini wizara husika wakati huo ilikataa na badala yake ikapendekeza kutoa mita za ujazo 3.5 za maji kwa sekunde.
“Kwa hiyo ikashindikana, kwa sababu gharama ya kuyachukua maji hayo ilikuwa ni kubwa ikilinganishwa na kiwango cha maji yenyewe,” anasema Jengo.

Anasema changamoto nyingine ni uhaba wa matrekta. Mradi huo ulipata matrekta 30 kutoka Jica mwaka 1985 ambayo yalitumika hadi 1995 na kuharibika na baadaye kupata mengine 16 mwaka 1996 ambayo yamepigwa mnada pamoja na vifaa vingine mwaka jana bada ya ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

“Unajua Hazina ndiyo inapiga mnada kwa hiyo hata fedha za mnada huo huenda huko. Hatujui zimepatikana shilingi ngapi, lakini tumeiandikia barua Septemba mwaka jana kuomba fedha tununulie matrekta japo mawili.”

“Ingawa wakulima wetu wa Lower Moshi hawajawahi kutumia jembe la mkono katika mradi huu, lakini kwa sasa tunategemea matrekta manne na power-tellers nne za kukodi kutoka Chawampu.”

Jingo anasema hawajawahi kuvamiwa na magonjwa ya mazao hadi sasa katika ukanda huo, ingawa baadhi ya wakati hutokea wadudu waharibifu ikiwa ni pamoja na nzige, senene, kwelea kwelea na viwavijeshi vilivyotokea mwaka 1994.

HAYA KIMBIA: USAFIRI VIJIJINI

Kijana wa mashamba ya mpunga Leki Tatu, eneo la Usariver mkoani Arusha akiwa katika gari linalokokotwa na ng'ombe wanne likiwa na magunia ya mpunga kutoka katika mashamba ya kilimo cha umwagiliaji kwenda katika ghala hivi karibuni. Picha na Salim Said.

HIVI NDIVYO MBOLEA INAVYOMWAGWA



Mahamoud Pandu kutoka Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Kizimbani Zanzibar (KATC) akionyesha namna ya kumwaga mbolea aina ya Yurea katika mpunga kwenye mashamba ya Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro (KATC), wilayani Moshi hivi karibuni. Picha na Salim Said.

KILIMO KWANZA:

Baadhi ya wakulima wa Mtwango znz wakiwa katika shamba darasa kwenye Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro (KATC) kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro katika mafunzo maalum ya wiki mbili. picha na salim said