MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Thursday, July 2, 2009

Serikali imetelekeza mapendekezo ya Jaji Nyalali

Salim Said
WAKATI miaka 17 imepita tangu tume ya marehemu Jaji Francis Nyalali kutoa mapendekezo ya kuboresha demokrasia nchini mwaka 1991, wadau wa masuala ya kisiasa wamesema mapendekezo mengi ya tume hiyo hayajatekelezwa na serikali ya Tanzania.

Tume ya Jaji Nyalali iliyoundwa na rais mstaafu wa awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa madarakani mwaka 1991, ili kukusanya maoni ya watanzania kuhusu mfumo wa demokrasia nchini, ilipendekeza mambo kadhaa ya kutekelezwa kwa ajili ya kuboresha siasa za Tanzania.

Miongoni mwa mapendekezo hayo, ni pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, marekebisho ya katiba ya nchi, kuvipa meno vyombo vya bunge na baraza la wawakilishi la Zanzibar na kutoa uhuru kwa vyombo vya habari.

Mengine ni kuundwa kwa serikali tatu, kuanzishwa kwa nafasi ya mgombea binafsi, tume huru ya uchaguzi, kuwapo kwa kura uwiano, mwafaka wa kisiasa na kufutwa kwa sheria 40 nchini ambazo zilionekana kuwa zinaenda kinyume na haki za binadamu na utawala bora.

Wadau hao walisema hayo jana katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) Ubungo jijini Dar es Salaam, kujadili mafanikio ya utekelezwaji wa mapendekezo ya tume hiyo katika kuboresha demokrasia nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba alisema, kati ya mambo mengi yaliyopendekezwa na tume huru ya Jaji Nyalali ni pendekezo moja tu la kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ndilo lililotekelezwa kikamilifu, huku mengine yakiishia hewani.

“Tumefanikiwa jambo moja tu la kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa huku mengine yakiishia hewani, ndio mana tunatawaliwa na vurugu kubwa katika chaguzi zote zinazofanyika nchini mara kwa mara,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema, kitendo cha serikali ya Tanzania kuyatelekeza mapendekezo mengi ya tume ya marehemu jaji Nyalali, demokrasia ya Tanzania haikui kutokana na vyombo vingi vya demokrasia kukitumikia Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Swa tumeanzisha mfumo wa vyama vingi, lakini yale mambo yaliyopendekezwa kwa ajili ya kurutubisha na kuimarisha mfumo huo tumeyaacha, jambo hili litatuletea matatizo makubwa katika chaguzi zijazo iwapo hayatatekelezwa,” alisema profesa Lipumba.

Alisema, tume za uchaguzi, katiba ya nchi na sheria za nchi zilizopo si za kidemokrasia kwa kuwa, zitatumikia zaidi Chama tawala CCM badala ya kutumikia wananchi wote na demokrasia ya nchi.

Alifafanua, tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza kufutwa kwa sheria 40 nchini, ambazo zilionekana kuwa zinakandamiza haki za binadamu, lakini sheria hizo hadi sasa zinaendelea kutumika, huku serikali ikiongeza sheria nyingine za ukandamizaji.

“Tutayajadili kwa undani mambo haya, ili kuona ni kwa kiwango gani tumefanikiwa au kufeli, lakini kiufupi hatujafanikiwa kwani zile sheria 40 hazijafutwa na nyengine zimeongezwa ikiwamo ya ugaidi,” alisema profesa Lipumba.

Kwa upande wake mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Nape Nnauye aliitaka serikali kuhakikisha inayachukua na kuyafanyia kazi mawazo ya wadau, ili kuboresha demokrasia ya Tanzania.

Alikiri kuwepo kwa upungufu mwingi katika utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya Jaji Nyalali, lakini kwa kiasi fulani alisema serikali imejitahidi na kufanikiwa kuboresha demokrasia ya nchi.

“Ni kweli kuna upungufu katika utekelezaji wa mapendekezo ya jaji Nyalali, lakini pia lazima tukiri kuwa serikali kwa upande wake imejitahidi na yapo mafanikio makubwa tumepata katika demokrasia ya nchi yetu. Ila ni vyema serikali ikayaangalia mawazo ya wadau katika semina kama hizi na kuyafanyia kazi kuliko kuyaacha yakiishia hewani,” alisema Nnauye na kuongeza:

“Katika semina hii wadau watajadili tulikotoka kisiasa na kidemokrasia, tupo wapi na tunaelekea wapi, ili tuweze kujirekebisha pale tulipokosea na kujiimarisha tulipopatia.”

Naye Waziri wa Katiba na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Ramadhan Shaban alisema, nchi inakabiliwa na changamoto nyingi katika kuboresha demokrasia.

“Kwanza tunakabiliwa na changamoto ya kuondoa hofu ya wananchi kutoa maoni yao katika tume huru, kuzingatia amani na utulivu katika kufanya kazi za kisiasa na kuhakikisha kuwa vyombo vinavyohusika na utungaji wa sheria na kurekebisha katiba vinawapatia watanzania, sheria na katiba zinazokidhi haja na matakwa yao,” alisema Waziri Shaban na kuongeza:

“Pia tunapaswa kuhakikisha kuwa watendaji wetu wa serikali hawajishughulishi na shughuli za kisiasa, ili kuepusha migongano mikubwa ndani ya serikali na hivyo kuanguka kwa ufanisi wake katika kuwatumikia wananchi, kama chachu ya kuleta maendeleo.”

CUF wasema kauli Waziri Seif ni mfa maji

Salim Said
SIKU moja baada ya Waziri Mohammad Seif Khatib kudai bungeni, Maalim Seif Sharif aliyesababisha kufukuzwa kwa rais wa awamu ya pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, baadhi ya viongozi wa CUF wamesema waziri huyo, ameshindwa kujibu hoja iliyokuwa mbele yake.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alimfukuza Mzee Jumbe kwa tuhuma kwamba alikuwa na ajenda za siri za hatima ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwamba aliandaa ajenda ya kudai serikali tatu badala ya mbili zilizopo hivi sasa.

Akizungumza Bungeni mjini Dodoma juzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mohammed Seif Khatib alisema fitna za kishushu za Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) maalim Seif Sharif Hamad, zilisababisha Jumbe aondolewe madarakani.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, viongozi wa CUF walisema Wazir Khatib alitoa tuhuma hizo baada ya kushindwa kujibu hoja ya msingi iliyokuwa mezani.

Naibu katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Juma Duni Haji alisema baada ya kujibu hoja husika, Waziri Khatibu aliamua kusambaza fitina ambazo zinaweza kujenga chuki na uhasama katika jamii.

“Hoja iliyokuwepo mezani ni kero za Muungano ambazo zinasababishwa na mkataba wa muungano. Aliambiwa aipeleke hoja hiyo mezani ili ijadiliwe, lakini alishindwa kujibu hoja hiyo na ndio maana akaamua kutoa porojo na maneno ya mfa maji,” alisema Duni.

Duni ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa CUF alisema suala la kutimuliwa kwa Jumbe ni mfano mzuri wa kero za Muungano zinazolalamikiwa na Watanzania wengi.

“Ok, kama hivyo ndivyo, Jumbe alifukuzwa pekee, lakini maalim Seif alifukuzwa na wenzake saba, je alitiliwa fitna na nani,” alihoji Duni.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa CUF, Jussa Iismail Jussa, alisisitiza kuwa waziri Khatib alikwepa kujibu hoja ya msingi kuhusu kero za Muungano na kuamua kuingiza malumbano ya kisiasa katika hoja ya msingi ili kutimiza malengo yake.

“Waziri Khatib anataka kugombea urais Zanzibar na ndio mana anajipendekeza sana kwa viongozi wa CCM bara, kwa sababu Halmashauri Kuu ya CCM ndiyo inayochagua wagombea. Hivyo anawaheshimu na kuwatetea sana na kuwavunjia heshma wazanzibari ambao anataka kuwaongoza huku akidharau maslahi yao, lakini je atawaongoza vipi watu asiowaheshimu.

“Wazir Khatib anakwepa kujibu hoja ya msingi na kuingiza malumbano ya kisiasa katika hoja ya msingi yenye maslahi kwa Watanzania waliowengi ili kutimiza malengo yake,” alisema Jussa.

Naye Mbunge wa Wawi Kisiwani Pemba (CUF) Hamad Rashid Mohammed alisema anasikitika kuwa maalim Seif si mbunge, kwa sababu kama angekuwa mbunge angelidai ushahidi wa tuhuma zilizozungumzwa na Waziri Khatib.

“Lakini hata hivyo anaweza kutumia vyombo vingine vya kisheria na kikatiba kudai ushahidi wa tuhuma hizo,” alisema Mohammed.

Mohammed ambaye pia ni kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni alisema, kilichomfukuzisha Jumbe ni kudai serikali tatu jambo ambalo lilipingwa vikali na Itikadi, Sera, Ilani na msimamo wa CCM.

CUF yampuuza Lwakatare

Salim Said
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema kinaheshimu uamuzi wa aliyekuwa naibu wake katibu mkuu (bara), Wilfred Lwakatare kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuwa hii ni demokrasia.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Jengo la Shaaban Khamis Mloo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa CUF maalim Seif Sharif Hamad alisema uamuzi huo ni wa kidemokrasia na hawana kinyongo naye.
“Tunaheshimu uamuzi wa mheshimiwa Lwakatare kwa sababu ametumia demokrasia, lakini tunamkumbuka kwa sababu tulikuwanaye kwa zaidi ya miaka 10 ndani ya chama,” alisema Hamad.
Kuhusu tuhuma za Lwakatare kwamba baadhi ya viongozi wa CUF wamejaa majungu, unafiki na roho mbaya, Hamad alisema hiyo ni kazi ya mdomo ambayo ni nyumba ya maneno.
“Unajua ndugu zangu, Domo ni nyumba ya maneno, lakini Lwakatare tumekuwanaye kwa zaidi ya miaka 10 hapa kama naibu katibu mkuu. Je hakuyaona hayo majungu, unafiki na roho mbaya? Na kama aliyaona je alichukua hatua gani,” alihoji Hamad.
Alisema, kama amekaa miaka 10 ndani ya chama akiwa katika nafasi za juu kama mtendaji mkuu wa makao makuu ya CUF Buguruni halafu anasema mambo hayo baada ya kukosa cheo cha unaibu, ana wasiwasi naye.
“Ndugu waandishi kama Lwakatare amekaa ndani ya chama tena katika nafasi za juu kama mtendaji mkuu wa makao makuu ya CUF hapa hajaona majungu, fitna wala roho mbaya na ameyaona mambo hayo hivi sasa baada ya kukosa unaibu. Kwa kweli nina wasiwasi naye,” alisema Hamad.
Lwakatare alianza kwa kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya CUF baada ya kuangushwa katika nafasi ya unaibu katibu mkuu wa chama hicho na hatimaye kuukana uanachama wake na kuhamia Chadema.
Mbali na uamuzi huo, Lwakatare alituma taarifa katika vyombo vya habari za kuwatuhumu baadhi ya viongozi wa juu wa CUF kuwa walimuacha katika nafasi yake, kwa kusikiliza majungu na fitna za baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho.
Hadi sasa tayari Lwakatare ni mwanachama halali wa Chadema baada ya kukabidhiwa kadi ya uanachama hicho na Naibu Katibu Mkuu wake Dk. Wilbrod Slaa mjini Bukoba mapema wiki iliyopita.

Maalim Seif: Kujiuzulu Mwenyekiti ZEC hakutabadilisha lolote

Salim Said
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) maalim Seif Sharif Hamad amesema, kujiuzulu kwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jaji Omar Makungu hakutobadilisha chochote katika utendaji wa tume hiyo.

Jaji Makungu alitangaza uamuzi wa kujiuzulu nafasi yake ZEC wiki iliyopita ili kujipunguzia majukumu kwa kuwa alikuwa makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wakati huohuo ZEC.

Jaji Makungu aliliambia Gazeti hili kuwa, ameamua kujiuzulu kwa sababu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 unakaribia na hivyo hatoweza kuhudumu kwenye tume mbili za uchaguzi kwa wakati mmoja katika nafasi za juu.

“Ni kweli nimejiuzulu,” alithibitisha Jaji Makungu na kuongeza: “Nimejiuzulu kwa sababu tunaelekea katika uchaguzi mkuu kwa hivyo sitaweza kutumika kwenye NEC na ZEC kwa wakati mmoja.”

Kujiuzulu kwa Jaji Makungu, kumetafsiriwa kwa hisia tofauti na Katibu Mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad.

Akizungumza na Mwananchi Hamad alisema, kujiuzulu kwa jaji Makungu hakuwezi kubadilisha chochote katika mikakati ya ZEC kuikandamiza CUF na kuindalia mazingira mazuri ya ushindi CCM katika uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar.

“Ameondoka jaji Makungu, lakini hata huyo atakayechukua nafasi yake hatakuwa na tofauti kwa sababu anatoka CCM kama yeye na atateuliwa na Rais Amani Karume kama alivyoteliwa yeye,” alisema Hmad.

Alisema, ZEC inafanya kazi kwa kupata maelekezo kutoka kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na kwamba tume hiyo imekosa uhuru wa kuwatumikia wazanzibari.

Alifafanua, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kwa muda mrefu hayupo kazini kwa sababu anaumwa, hivyo kutokana na taarifa zilizopo visiwani humo Jaji Makungu amejiuzulu ili achaguliwe kuwa mwanasheria mkuu wa Zanzibar.

“Kutokana na taarifa tunazozisikia ni kwamba Jaji Makungu amejiuzulu ili aweze kutoa mwanya wa kuteuliwa kushika nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,” alisema Hamad na kuongeza:

“Lakini pia jaji Makungu alikuwa Makamu Mwenyekiti wa tume mbili za uchaguzi, ile ya Taifa (NEC) na ya Zanzibar (ZEC) kwa wakati mmoja, hivyo inawezekana amejiuzulu ili kujipunguzia majukumu.”