MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Sunday, October 24, 2010

HESLB, yachakachua majina ya waombaji wapya wa mikopo

* BAADHI WADAI HAWAONI MAJINA YAO, VYUO VYAO

Salim Said

HOFU na wasiwasi umetanda miongoni mwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini, baada ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), kutangaza orodha ya majina ya vyuo na waombaji waliofanikiwa kupata mikopo, huku majina ya baadhi ya vyuo na waombaji kutoonekana katika orodha hiyo.

Hofu hiyo imekuja kufuatia HESLB kutangaza majina ya baadhi ya vyuo na baadhi ya waombaji waliofanikiwa kupata mkopo huo, huku vyuo vingine na majina ya baadhi ya waombaji kutoonekana.

Taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa bodi hiyo, inasema waombaji na vyuo ambavyo majina yao hayapo katika orodha hiyo ya kwanza wanashauriwa kuwa wavumilivu, kwa kuwa kuna orodha nyingine ya majina ya vyuo na waombaji yanayotarajiwa kuchapishwa siku chache zijazo baada ya kumalizika kwa mchakato wa kupanga mikopo hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya HESLB waombaji hao wamegawanywa katika makundi mbalimbali na kwamba kundi lililochapishwa katika mtandao wake ni la waombaji 25,000 pekee kati ya zaidi ya 30,000 wanaotarajiwa kupata mkopo huo.

Kutokana na taarifa hiyo, zaidi ya waombaji 5,000 wa mikopo hiyo hawajatangazwa majina yao katika orodha hiyo ya kwanza, iliyopo katika mtandao wa HESLB, huku wakiwa na hofu kuwa ndio wamekosa mkopo.

Baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakipiga simu mara kwa mara katika chumba cha habari cha gazeti hili, wakilalamikia kutoona majina yao katika orodha hiyo iliyochapishwa katika mtandao wa HESLB.

Wakizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya waombaji ambayo majina yao na au ya vyuo vyao hayapo katika orodha hiyo, walisema hadi sasa wako njia panda.

“Kwa kweli sijajua kama nitasoma au sitasoma kwa sababu nilitegemea mkopo wa bodi ya mikopo ya serikali lakini nashangaa jina langu halipo katika orodha iliyowekwa katika mtandao wa bodi hiyo,”alisema Juma Omar ambaye ni mmoja kati ya walioomba mkopo.

Lakini Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa aliwatoa wasiwasi wanafunzi hao kwa kuwaeleza kuwa, majina ya vyuo na waombaji waliyochapishwa katika mtandao wa bodi hiyo ni baadhi tu na kwamba mchakato wa kuchanganua majina hayo bado unaendelea.

“Majina yaliyochapishwa ni baadhi tu ya vyuo na wale walioomba mkopo, mchakato unaendelea na mengine yatachapishwa hivi karibuni,”alisema Mwaisobwa.

Alifafanua kuwa, katika awamu hiyo ya kwanza zaidi ya majina ya waombaji 25,000 yamechapishwa na kwamba mengine yapo katika hatua za mwisho kuchapishwa.

Hata hivyo, Mwaisobwa alisema hakuweza kutaja idadi kamili ya jumla ya watu walioomba mkopo na waliofanikiwa mkopo kw mwaka huu wa masomo wa 2010/11.

“Unajua sina idadi kamili kwa sasa kwa sababu nipo nyumbani lakini nipigie kesho nikiwa ofisini itakupatia idadi kamili,”alisema.

Mkurugenzi huyo wa Habari alilaumu tabia ya baadhi ya waombaji wa mikopo ambao hawajaona majina yao katika orodha ya ‘Means Test’ ya bodi hiyo kutumia njia ya kupiga simu katika vyombo vya habari na kulalamika wakati sio chombo kinachoweza kutatua tatizo lao.

“Mimi nipo ofisini wazi kabisa kila siku, waje pale kama wana tatizo lolote. Sio kuanza kupiga simu katika vyombo vya habari, vitakusaidiaje kwani wao ndio wanatoa mkopo au wanafanya ‘Means Test,” alihoji Mwaisobwa.

Kwa mujibu wa majina yaliyochapishwa katika mtandao wa HESLB, kiwango cha mkopo kinatofautiana kwa wale waliofaulu kinatofautiana kutoka mwombaji mmoja hadi mwengine.

Tarrifa hiyo inaonyesha kuwa, wapo watakaopata mkopo wa asilimia 100 kwa daraja ‘A’ hadi wale wataopata mkopo wa asilimia 10 daraja ‘J’hadi asilimia 0 daraja ‘K’.

Kwa mujibu wa kalenda za vyuo vingi nchini, wanafunzi wanatakiwa kurudi vyuoni kuendelea au kuanza masomo kuazia Novemba 1 mwaka huu, ambapo kufika kwao vyuoni kunategemea sana kufanikiwa au kutangazwa kwa majina yao kwamba yamefanikiwa kupata mkopo.

Utaratibu wa kusoma elimu ya juu kwa njia ya fedha za mkopo kutoka serikalini, ulianza miaka mitano iliyopita baada ya serikali kufuta sera yake ya kutoa elimu ya juu bure sambamba na kuanzisha chombo cha kusimamia utaratibu wa kutoa na kurudisha mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Lakini mfumo huo umekuwa ukikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na malalamiko, migomo na aminoamano yasiyokwisha kutoka kwa wanafunzi wa taasisi mbalimbali za elimu ya juu, kuhusu mfumo mzima wa utoaji wa mikopo hiyo.

Orodha ya vyuo vilivyofanikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Bugando, Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam na Dodoma (CBE), Community Development Training Institute, College of Engineering and Technology, Chuo cha Elimu Zanzibar, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Institute of Accountancy Arusha, Taaisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IMF) na Institute of Medicine and Technology University.

Vyengine ni Institute of Rural Development Planning, Taasisi ya Ustawi wa Jamii, chuo kikuu cha Makumira, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya, chuo kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa, Moshi University College of Cooperatives and Business Studies, Chuo kikuu cha Mount Meru, chuo kikuu cha Tiba Muhimbili, chuo kikuu cha Waislaam Morogoro, chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Mwenge University College of Education na chuo kikuu cha Mzumbe.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo vyuo vingine ni National Institute of Transport, Ruaha University College, School of Journalism and Mass Communication, Sebastian Kolowa University College, St. Augustine University Tanzania matawi ya Mtwara na Mwanza, St. John’s University of Tanzania kampasi ya Dar es Salaam na Dodoma.

Vingine ni St. Joseph College of Engineering, Chuo Kikuu cha Serikali ya Zanzibar (Suza), Stephano Mosha Memorial University, chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUA), Tanzania Institute of Accountancy, Teofilo Kisanji University, chuo kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Iringa na KCMC, chuo kikuu cha Arusha, chuo kikuu cha Dar es Salaam na chuo kikuu cha Dodoma.