MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Friday, July 31, 2009

CUF: Masha, Mwema wawajibike kwa kujiuzulu

Salim Said
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimewataka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Laurence Masha na Mkuu Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema kujiuzulu mara moja kutokana na madai kwamba wameshindwa kudhibiti wimbi la ajali nchini.

Mwenyekiti wa CUF taifa Profesa Ibrahim Lipumba alisema jijini Dar es Salaam jana, ajali zinazoendelea kuikumba nchi zinatokana na utendaji mbovu wa wakuu hao pamoja na uzembe wa madereva.

Alisema ajali hizo zimekuwa zikisababisha upotevu wa nguvu kazi na rasilimali za taifa na kuongeza idadi kubwa ya watu wenye ulemavu.
Profesa Lipumba alisema, Waziri Masha na IGP Mwema, wamezidiwa nguvu na wauaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) pamoja na madereva wazembe, jambo linalosababisha kukuwa kwa uhalifu nchini.

“Kwa hivyo tunawataka waziri Masha na IGP Mwema wawajibike kwa kujiuzulu nyadhifa zao mara moja, ili kunusuru nchi na kuwapisha wengine watakaomudu na kulinda usalama wa raia na mali zao,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Pia serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inapaswa kuchukua hatua mahsusi za kubaini vyanzo vya ajali za zinazotokea mara kwa mara nchini, ili kuweza kuzidhibiti pamoja na kuangalia upya adhabu kwa wanaopatikana na makosa ya kusababisha ajali hizo”.

Wakati huohuo CUF imetoa salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa, familia na marafiki watu 27 waliokufa katika ajali ya Basi la Mohamed Trans, iliyotokea juzi baada ya basi hilo kugongana na lori la mizigo wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Basi hilo lililikuwa njiani kutoka Nairobi Kenya kuja Dar es Salaam Tanzania, liligongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa limebeba bia katika eneo hilo.

Profesa Lipumba alisema kwamba, “tumepokea habari za msiba huo kwa masikitiko makubwa na tunatoa salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na familia za marehemu wote, pia tunamuomba awalaze mahali pema, sambamba na kuwapa nafuu majeruhi wote”.

Alisema CUF inaamini kuwa ongezeko la ajali za barabarani nchini, linachangiwa kwa kiasi kikubwa na madereva wazembe na wanaokwenda mwendo wa kasi.

Alifafanua kuwa madereva hao wamekuwa na kiburi, dharu na kutowajali askari wa usalama barabarani kwa kile alichodai kuwa wanawahonga pindi wanapowakamata.

Alisema pia CUF inaamini kwamba ongezeko hilo la ajali linachangiwa kwa kiasi kikubwa na magari mabovu yasiyofanyiwa ukaguzi makini na kwamba uzembe huo unashamiri zaidi kutokana na chombo cha usalama barabarani kugubikwa na vitendo vya rushwa.

“Rushwa zinawajengea kiburi madereva na wamiliki wa magari kufanya watakavyo,” alisema Profesa Lipumba.

Aliitaka Idara ya Usalama barabarani kuwa makini na hali za magari yaingizwayo nchini ili nchi yetu isigeuzwe dampo la magari mabovu na kutahadharisha kwamba bila ya kufanya hivyo ajali zitaendelea kuiathiri nchi.

Wakulima Kigoma Kusini watishia kuishitaki serikali

Salim Said
WAKULIMA wa Kata tatu za Jimbo la Kigoma Kusini wanatarajia kuishitaki serikali katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora baada ya kuhamishwa katika makazi yao, bila kulipwa fidia.


Wakulima hao ni kutoka Kata za Nguruka, Mganza na Mtego wa Noti ambao walihamishwa na serikali ili mashamba yao, yatumike kwa ajili ya hifadhi ya mbuga za wanyama.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam jana, Mshauri wa wakulima hao David Kafulila alisema tayari wamepata ushauri wa kisheria kutoka kwa mwanasheria wao Tundu Lissu na kukubaliana kufungua kesi hiyo mwishoni mwa mwezi ujao.

“Tayari tumepata ushauri wa kisheria kutoka kwa mwanasheria wetu Tundu Lissu na ametushauri kufungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, tunatarajia kufanya hivyo mwishoni mwa Agosti,” alisema Kafulila.

Alisema wakati wa kuwahamisha wakulima hao, zaidi ya wakulima 500 waliamishwa na kuathirika baada ya mazao yao kufyekewa na nyumba kubomolewa bila ya kulipwa fidia.

“Kiutaratibu kabla ya kumuhamisha mtu katika eneo lake, unatakiwa kumpatia notisi ya miezi mitatu, kufanya uthamini wa hasara ya mali zake na kumlipa fidia, lakini hakuna hata moja lililofanywa na serikali kati ya haya,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kafulila alisema wanafanya mpango wa kupeleka bungeni malalamiko ya waliokuwa wafanyakazi wa Mgodi wa Chumvi wa Nyanza ili waweze kusaidiwa.

Alisema wafanyakazi hao zaidi ya 300 hawakulipwa mafao yao na kwamba wamekuwa wakifuatilia tangu mwaka 1998 bila mafanikio.

“Lakini hata walipofungua kesi mahakamani haikusikilizwa kwa sababu ilikuwa imepitwa na wakati.

“Kwa hiyo, tunawatumia wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuyafikisha bungeni malalamiko yao, ili wabunge waweze kuwasaidia kupata haki zao,” alisema.

Alisema endapo itashindikana kwa njia hiyo, watafanya mpango wa kuwakutanisha wazee zaidi ya 300 na Rais Jakaya Kikwete ili waweze kumueleza shida zao.

Migogoro ya ardhi na tatizo la wafanyakazi kucheleweshewa mafao nchini, limekuwa sugu na kusababisha kero kwa watu mbalimbali wanaodai haki zao.

Sera ya lugha ya Tanzania ni mbaya: profesa Mulokozi

Salim Said
MSOMI mashuhuri nchini na mtaalamu wa lugha ya Kiswahili Profesa Mugyabuso Mulokozi, amesema sera za lugha na elimu za Tanzania zina matatizo mingi na zinahitaji kuangaliwa upya.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii ofisini kwake jijini Dar es Salaam Profesa Mulokozim, alisema sera hizo zinawachanganya vijana wa kitanzania tangu ngazi ya elimu ya msingi.

Alisema, wakati wa uhuru Tanzania ilikuwa inafuata sera ya elimu na lugha za kikoloni ambapo zilibadilishwa baada ya uhuru na serikali ya awamu ya kwanza kuundwa chini ya uongozi wa baba wa taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Mwanzo tulikuwa tunatumia lugha na mitaala ya kikoloni katika shule zetu za msingi na hata sekondari, lakini tulipopata uhuru tulifanya mabadiliko na kuanza kutumia lugha na mtaala wetu ambao umetungwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA),” alisema Profesa Mulokozi.

Alisema, mabadiliko hayo hayakudumu sana ambapo hivi sasa tayari mwelekeo umebadilika na kwamba shule za Tanzania zimerudia lugha za kikolono na kufuata mtaala wa kikoloni yaani Cambridge.

“Sasa utakuta sera yetu ya lugha ina matatizo makubwa kwa sababu inamchanganya mwanafunzi. Zamani kiengereza kilikuwa kinafundishwa katika ngazi ya darasa la nne, lakini hivi sasa kinatumika kama njia ya kufundishia tena kuanzia shule za awali,” alisema Profesa Mulokozi na kuongeza:

“Mathalan herufi ‘A’ mwalimu wa Kiswahili akiingia darasani anamfundisha mwanafunzi kwa matamshi ya lugha hiyo na wa kiengereza naye anamfundisha kwa matamshi ya kiengereza, mwanafunzi huyu hata kuzungumza vizuri, kwa hiyo utakuta sera inawachanganya kwa kutumia lugha ya kigeni kuwa ya kufundishia.”

Alisema, matokeo yake ni kwa wanafunzi wa Tanzania kusoma kwa kukariri badala ya kusoma kwa kuelewa.

Aidha, alisema kuwepo kwa mitaala zaidi ya mmoja nchini kunarudisha nyuma ubora wa elimu ingawa ni mfumo wa utandawazi na biashara huria.

Alisema, baadhi ya shule nchini zinafuata mtaala wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) huku shule nyingine zikitumia mtaala wa kiengereza yaani Cambrije.

Mjadala wa lugha gani itumike kama njia ya kufundishia katika shule za msingi hadi vyuo vikuu umekuwapo kwa muda mrefu nchini huku wadau wa elimu wakigawika katika kambi mbili ambazo ni ile yawanaotaka Kiswahili na wanaotaka Kiengereza.

Tamwa: Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ni ufisadi

Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimewataka Watanzania kuupinga kwa nguvu zao zote Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF), unaotaka kuanzishwa na serikali kwa madai kuwa ni ufisadi.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya alisema uanzishwaji wa mfuko huo ni ufisadi.

Alisema Watanzania wanapaswa kupinga kwa nguvu zote kuanzishwa kwa mfuko huo, kwa sababu kutokana na hali ilivyo hivi sasa utatumiwa na wanasiasa mafisadi kufanikisha malengo yao binafsi ya kisiasa na kiuchumi, badala ya kuwezesha miradi ya maendeleo kwenye majimbo.

“Watanzania wanapaswa kuupinga kwa nguvu zao zote mfuko huu, kwa sababu ni ufisadi na utatumiwa na wanasiasa mafisadi kufanikisha malengo yao binafsi ya kisiasa na kiuchumi,” alisema Nkya.

Alisema wabunge wanaoshabikia mfuko huo, uanzishwe wanafahamu kuwa utawanufaisha wao zaidi kuliko wananchi kutokana na ukweli kwamba, hakuna juhudi zilizofanyika kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kufuatilia kwa makini matumizi ya fedha zao zitakazowekwa katika mfuko huo kwa shughuli za maendeleo ya majimbo yao.

“Kama lengo la serikali kuanzisha CDF ni kuondoa umaskini majimboni, kabla hata sheria ya kuanzishwa kwake kupitishwa na Bunge, serikali ingetenga bajeti mahususi kwa ajili ya vyombo vya habari kuelimisha wananchi umuhimu wa mfuko, ushiriki wao katika kuendesha kwa ufanisi na changamoto katika usimamizi wa fedha zao,” alisema Nkya.

Alisema Tamwa wanahoji sababu za serikali kufanya haraka kupeleka muswada wa kuanzisha CDF, bungeni kabla ya kuwashirikisha wananchi katika majimbo yote ambao ndio walengwa na wadau wakuu wa mfuko huo.

Aliihoji, serikali kuwa itawahakikishiaje wananchi kwamba fedha za CDF zitatumika kwa kutekeleza vipaumbele vya wananchi na hazitaibwa na wanasiasa mafisadi, endapo fedha za umma zimewahi kuibiwa katika vyombo nyeti ikiwa ni pamoja na Sh133 bilioni zilizoibwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania(BoT).

“Ni kwa nini serikali iharakishe kupeleka muswada wa CDF bungeni bila kujiridhisha kwanza kwamba wananchi, wametayarishwa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha fedha za umma zitakazopitia katika mfuko huo zinaendesha miradi majimboni kwa viwango na kwa wakati,”alihoji Nkya.

Aliihoji serikali iwapo haioni kuwa kuwashirikisha wabunge kusimamia mfuko wa CDF, ni kudhoofisha utawala bora na hivyo kuimarisha ufisadi, ambao ni kikwazo kikubwa cha haki na maendeleo ya wanyonge nchini.

“Tamwa tunaamini kuwa Tanzania ni moja ya nchi chache duniani ambazo zimeweka utaratibu mzuri wa kuwafikia wananchi kuanzia serikali kuu, halmashauri hadi ngazi za serikali za mitaa na kwamba kinachohitajika sasa ni kuondoa umaskini majimboni na si kuanzisha mfumo mpya,” alisema Nkya.

Alisema, lengo iwe ni pia kupata viongozi wa kisiasa ikiwa ni pamoja na wabunge wenye nia ya dhati wa kusimamia serikali kuu, halmashauri na serikali za mitaa ili ziwajibike ipasavyo kwa wananchi na si kupewa fedha.

Alisema, nchi za Kenya na Sudan ambako mifuko ya CDF ilianzishwa, imekuwa ni chanzo cha kutajirisha wabunge wenyewe, ndugu zao, marafiki zao, washirika wao huku wananchi ambao ndio walengwa wa mifuko hiyo wakibaki maskini wa kutupwa.

Serikali: Ripoti ya chanzo cha milipuko ya Mbagala haijakamilika

Salim Said
SERIKALI imesema ripoti ya chanzo cha milipuko ya Mabomu iliyotokea kwenye eneo la kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam Aprili 29 mwaka huu bado haijakamilika.


Tayari miezi mitatu imetimia tangu kutokea kwa milipuko hiyo iliyosababisha mamia ya wakaazi wa eneo hilo, kuishi katika Mahema na kwa chakula cha msaada kwa muda.

Milipuko hiyo iliyolitikisa jiji la Dar es Salaam, iligharimu pia maisha ya zaidi ya watu 20 huku mamia wakijeruhiwa na kuachwa bila ya makaazi baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na milipuko hiyo.

Katika juhudi za kutafuta chanzo cha milipuko hiyo, serikali kupitia wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, iliunda Baraza Huru la uchunguzi kwa ajili ya kubaini chanzo cha milipuko hiyo iliyoacha maafa makubwa nchini.

Uamuzi huo wa kuundwa kwa baraza la uchunguzi ulitangazwa na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Emanuel Nchimbi siku chache baada ya milipuko katika mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Ngurdoto, jijini Arusha.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya Simu jana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alisema ripoti ya chanzo cha milipuko hiyo haijakamilika na kwamba wataitangaza mara tu itakapokamilika.


“Ripoti bado haijakamilika, bado inafanyiwa kazi hadi hapo itakapokamilika katika hatua zote tutaitangaza tu ikikamilika,” alisema Dk. Mwinyi.

Alipoulizwa kuwa, ni lini ripoti hiyo itakuwa tayari na kutangazwa kwa wananchi Dk. Mwinyi alijibu:

“Kwa sasa siwezi kusema siku gani itakamilika na kutangazwa kwa sababu bado inafanyiwa kazi,” alisema Dk. Mwinyi na kusisitiza:

“Wewe ukiona kimya ujue ripoti haijakamilika na ikikamilika siku yoyote ile basi tutawapatia taarifa zake.”

Aidha Dk. Mwinyi alisema, Satelati kwa ajili ya kubaini mabaki ya mabomu yaliyokuwa yamezagaa baada ya milipuko hiyo, nayo bado haijafika nchini na kwamba siku yoyote itakapofika watatoa taarifa kwa wananchi.

Siku chache baada ya milipuko hiyo baadhi ya wanaharakati na wanasiasa nchini walitoa wito wa kujiuzulu kwa Dk. Mwinyi na Naibu wake Dk Emanuel Nchimbi pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Davis Mwamunyange, kwa madai kwamba milipuko hiyo ilitokea kwa uzembe.

Hata hivyo Dk. Mwinyi aliahidi kujiuzulu iwapo baraza la uchunguzi litabaini kuwa milipuko hiyo ilitokea kwa sababu ya kukiukwa kwa taratibu za utendaji au sheria.