MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Friday, July 31, 2009

CUF: Masha, Mwema wawajibike kwa kujiuzulu

Salim Said
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimewataka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Laurence Masha na Mkuu Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema kujiuzulu mara moja kutokana na madai kwamba wameshindwa kudhibiti wimbi la ajali nchini.

Mwenyekiti wa CUF taifa Profesa Ibrahim Lipumba alisema jijini Dar es Salaam jana, ajali zinazoendelea kuikumba nchi zinatokana na utendaji mbovu wa wakuu hao pamoja na uzembe wa madereva.

Alisema ajali hizo zimekuwa zikisababisha upotevu wa nguvu kazi na rasilimali za taifa na kuongeza idadi kubwa ya watu wenye ulemavu.
Profesa Lipumba alisema, Waziri Masha na IGP Mwema, wamezidiwa nguvu na wauaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) pamoja na madereva wazembe, jambo linalosababisha kukuwa kwa uhalifu nchini.

“Kwa hivyo tunawataka waziri Masha na IGP Mwema wawajibike kwa kujiuzulu nyadhifa zao mara moja, ili kunusuru nchi na kuwapisha wengine watakaomudu na kulinda usalama wa raia na mali zao,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Pia serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inapaswa kuchukua hatua mahsusi za kubaini vyanzo vya ajali za zinazotokea mara kwa mara nchini, ili kuweza kuzidhibiti pamoja na kuangalia upya adhabu kwa wanaopatikana na makosa ya kusababisha ajali hizo”.

Wakati huohuo CUF imetoa salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa, familia na marafiki watu 27 waliokufa katika ajali ya Basi la Mohamed Trans, iliyotokea juzi baada ya basi hilo kugongana na lori la mizigo wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Basi hilo lililikuwa njiani kutoka Nairobi Kenya kuja Dar es Salaam Tanzania, liligongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa limebeba bia katika eneo hilo.

Profesa Lipumba alisema kwamba, “tumepokea habari za msiba huo kwa masikitiko makubwa na tunatoa salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na familia za marehemu wote, pia tunamuomba awalaze mahali pema, sambamba na kuwapa nafuu majeruhi wote”.

Alisema CUF inaamini kuwa ongezeko la ajali za barabarani nchini, linachangiwa kwa kiasi kikubwa na madereva wazembe na wanaokwenda mwendo wa kasi.

Alifafanua kuwa madereva hao wamekuwa na kiburi, dharu na kutowajali askari wa usalama barabarani kwa kile alichodai kuwa wanawahonga pindi wanapowakamata.

Alisema pia CUF inaamini kwamba ongezeko hilo la ajali linachangiwa kwa kiasi kikubwa na magari mabovu yasiyofanyiwa ukaguzi makini na kwamba uzembe huo unashamiri zaidi kutokana na chombo cha usalama barabarani kugubikwa na vitendo vya rushwa.

“Rushwa zinawajengea kiburi madereva na wamiliki wa magari kufanya watakavyo,” alisema Profesa Lipumba.

Aliitaka Idara ya Usalama barabarani kuwa makini na hali za magari yaingizwayo nchini ili nchi yetu isigeuzwe dampo la magari mabovu na kutahadharisha kwamba bila ya kufanya hivyo ajali zitaendelea kuiathiri nchi.

Wakulima Kigoma Kusini watishia kuishitaki serikali

Salim Said
WAKULIMA wa Kata tatu za Jimbo la Kigoma Kusini wanatarajia kuishitaki serikali katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora baada ya kuhamishwa katika makazi yao, bila kulipwa fidia.


Wakulima hao ni kutoka Kata za Nguruka, Mganza na Mtego wa Noti ambao walihamishwa na serikali ili mashamba yao, yatumike kwa ajili ya hifadhi ya mbuga za wanyama.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam jana, Mshauri wa wakulima hao David Kafulila alisema tayari wamepata ushauri wa kisheria kutoka kwa mwanasheria wao Tundu Lissu na kukubaliana kufungua kesi hiyo mwishoni mwa mwezi ujao.

“Tayari tumepata ushauri wa kisheria kutoka kwa mwanasheria wetu Tundu Lissu na ametushauri kufungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, tunatarajia kufanya hivyo mwishoni mwa Agosti,” alisema Kafulila.

Alisema wakati wa kuwahamisha wakulima hao, zaidi ya wakulima 500 waliamishwa na kuathirika baada ya mazao yao kufyekewa na nyumba kubomolewa bila ya kulipwa fidia.

“Kiutaratibu kabla ya kumuhamisha mtu katika eneo lake, unatakiwa kumpatia notisi ya miezi mitatu, kufanya uthamini wa hasara ya mali zake na kumlipa fidia, lakini hakuna hata moja lililofanywa na serikali kati ya haya,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kafulila alisema wanafanya mpango wa kupeleka bungeni malalamiko ya waliokuwa wafanyakazi wa Mgodi wa Chumvi wa Nyanza ili waweze kusaidiwa.

Alisema wafanyakazi hao zaidi ya 300 hawakulipwa mafao yao na kwamba wamekuwa wakifuatilia tangu mwaka 1998 bila mafanikio.

“Lakini hata walipofungua kesi mahakamani haikusikilizwa kwa sababu ilikuwa imepitwa na wakati.

“Kwa hiyo, tunawatumia wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuyafikisha bungeni malalamiko yao, ili wabunge waweze kuwasaidia kupata haki zao,” alisema.

Alisema endapo itashindikana kwa njia hiyo, watafanya mpango wa kuwakutanisha wazee zaidi ya 300 na Rais Jakaya Kikwete ili waweze kumueleza shida zao.

Migogoro ya ardhi na tatizo la wafanyakazi kucheleweshewa mafao nchini, limekuwa sugu na kusababisha kero kwa watu mbalimbali wanaodai haki zao.

Sera ya lugha ya Tanzania ni mbaya: profesa Mulokozi

Salim Said
MSOMI mashuhuri nchini na mtaalamu wa lugha ya Kiswahili Profesa Mugyabuso Mulokozi, amesema sera za lugha na elimu za Tanzania zina matatizo mingi na zinahitaji kuangaliwa upya.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii ofisini kwake jijini Dar es Salaam Profesa Mulokozim, alisema sera hizo zinawachanganya vijana wa kitanzania tangu ngazi ya elimu ya msingi.

Alisema, wakati wa uhuru Tanzania ilikuwa inafuata sera ya elimu na lugha za kikoloni ambapo zilibadilishwa baada ya uhuru na serikali ya awamu ya kwanza kuundwa chini ya uongozi wa baba wa taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Mwanzo tulikuwa tunatumia lugha na mitaala ya kikoloni katika shule zetu za msingi na hata sekondari, lakini tulipopata uhuru tulifanya mabadiliko na kuanza kutumia lugha na mtaala wetu ambao umetungwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA),” alisema Profesa Mulokozi.

Alisema, mabadiliko hayo hayakudumu sana ambapo hivi sasa tayari mwelekeo umebadilika na kwamba shule za Tanzania zimerudia lugha za kikolono na kufuata mtaala wa kikoloni yaani Cambridge.

“Sasa utakuta sera yetu ya lugha ina matatizo makubwa kwa sababu inamchanganya mwanafunzi. Zamani kiengereza kilikuwa kinafundishwa katika ngazi ya darasa la nne, lakini hivi sasa kinatumika kama njia ya kufundishia tena kuanzia shule za awali,” alisema Profesa Mulokozi na kuongeza:

“Mathalan herufi ‘A’ mwalimu wa Kiswahili akiingia darasani anamfundisha mwanafunzi kwa matamshi ya lugha hiyo na wa kiengereza naye anamfundisha kwa matamshi ya kiengereza, mwanafunzi huyu hata kuzungumza vizuri, kwa hiyo utakuta sera inawachanganya kwa kutumia lugha ya kigeni kuwa ya kufundishia.”

Alisema, matokeo yake ni kwa wanafunzi wa Tanzania kusoma kwa kukariri badala ya kusoma kwa kuelewa.

Aidha, alisema kuwepo kwa mitaala zaidi ya mmoja nchini kunarudisha nyuma ubora wa elimu ingawa ni mfumo wa utandawazi na biashara huria.

Alisema, baadhi ya shule nchini zinafuata mtaala wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) huku shule nyingine zikitumia mtaala wa kiengereza yaani Cambrije.

Mjadala wa lugha gani itumike kama njia ya kufundishia katika shule za msingi hadi vyuo vikuu umekuwapo kwa muda mrefu nchini huku wadau wa elimu wakigawika katika kambi mbili ambazo ni ile yawanaotaka Kiswahili na wanaotaka Kiengereza.

Tamwa: Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ni ufisadi

Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimewataka Watanzania kuupinga kwa nguvu zao zote Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF), unaotaka kuanzishwa na serikali kwa madai kuwa ni ufisadi.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya alisema uanzishwaji wa mfuko huo ni ufisadi.

Alisema Watanzania wanapaswa kupinga kwa nguvu zote kuanzishwa kwa mfuko huo, kwa sababu kutokana na hali ilivyo hivi sasa utatumiwa na wanasiasa mafisadi kufanikisha malengo yao binafsi ya kisiasa na kiuchumi, badala ya kuwezesha miradi ya maendeleo kwenye majimbo.

“Watanzania wanapaswa kuupinga kwa nguvu zao zote mfuko huu, kwa sababu ni ufisadi na utatumiwa na wanasiasa mafisadi kufanikisha malengo yao binafsi ya kisiasa na kiuchumi,” alisema Nkya.

Alisema wabunge wanaoshabikia mfuko huo, uanzishwe wanafahamu kuwa utawanufaisha wao zaidi kuliko wananchi kutokana na ukweli kwamba, hakuna juhudi zilizofanyika kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kufuatilia kwa makini matumizi ya fedha zao zitakazowekwa katika mfuko huo kwa shughuli za maendeleo ya majimbo yao.

“Kama lengo la serikali kuanzisha CDF ni kuondoa umaskini majimboni, kabla hata sheria ya kuanzishwa kwake kupitishwa na Bunge, serikali ingetenga bajeti mahususi kwa ajili ya vyombo vya habari kuelimisha wananchi umuhimu wa mfuko, ushiriki wao katika kuendesha kwa ufanisi na changamoto katika usimamizi wa fedha zao,” alisema Nkya.

Alisema Tamwa wanahoji sababu za serikali kufanya haraka kupeleka muswada wa kuanzisha CDF, bungeni kabla ya kuwashirikisha wananchi katika majimbo yote ambao ndio walengwa na wadau wakuu wa mfuko huo.

Aliihoji, serikali kuwa itawahakikishiaje wananchi kwamba fedha za CDF zitatumika kwa kutekeleza vipaumbele vya wananchi na hazitaibwa na wanasiasa mafisadi, endapo fedha za umma zimewahi kuibiwa katika vyombo nyeti ikiwa ni pamoja na Sh133 bilioni zilizoibwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania(BoT).

“Ni kwa nini serikali iharakishe kupeleka muswada wa CDF bungeni bila kujiridhisha kwanza kwamba wananchi, wametayarishwa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha fedha za umma zitakazopitia katika mfuko huo zinaendesha miradi majimboni kwa viwango na kwa wakati,”alihoji Nkya.

Aliihoji serikali iwapo haioni kuwa kuwashirikisha wabunge kusimamia mfuko wa CDF, ni kudhoofisha utawala bora na hivyo kuimarisha ufisadi, ambao ni kikwazo kikubwa cha haki na maendeleo ya wanyonge nchini.

“Tamwa tunaamini kuwa Tanzania ni moja ya nchi chache duniani ambazo zimeweka utaratibu mzuri wa kuwafikia wananchi kuanzia serikali kuu, halmashauri hadi ngazi za serikali za mitaa na kwamba kinachohitajika sasa ni kuondoa umaskini majimboni na si kuanzisha mfumo mpya,” alisema Nkya.

Alisema, lengo iwe ni pia kupata viongozi wa kisiasa ikiwa ni pamoja na wabunge wenye nia ya dhati wa kusimamia serikali kuu, halmashauri na serikali za mitaa ili ziwajibike ipasavyo kwa wananchi na si kupewa fedha.

Alisema, nchi za Kenya na Sudan ambako mifuko ya CDF ilianzishwa, imekuwa ni chanzo cha kutajirisha wabunge wenyewe, ndugu zao, marafiki zao, washirika wao huku wananchi ambao ndio walengwa wa mifuko hiyo wakibaki maskini wa kutupwa.

Serikali: Ripoti ya chanzo cha milipuko ya Mbagala haijakamilika

Salim Said
SERIKALI imesema ripoti ya chanzo cha milipuko ya Mabomu iliyotokea kwenye eneo la kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam Aprili 29 mwaka huu bado haijakamilika.


Tayari miezi mitatu imetimia tangu kutokea kwa milipuko hiyo iliyosababisha mamia ya wakaazi wa eneo hilo, kuishi katika Mahema na kwa chakula cha msaada kwa muda.

Milipuko hiyo iliyolitikisa jiji la Dar es Salaam, iligharimu pia maisha ya zaidi ya watu 20 huku mamia wakijeruhiwa na kuachwa bila ya makaazi baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na milipuko hiyo.

Katika juhudi za kutafuta chanzo cha milipuko hiyo, serikali kupitia wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, iliunda Baraza Huru la uchunguzi kwa ajili ya kubaini chanzo cha milipuko hiyo iliyoacha maafa makubwa nchini.

Uamuzi huo wa kuundwa kwa baraza la uchunguzi ulitangazwa na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Emanuel Nchimbi siku chache baada ya milipuko katika mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Ngurdoto, jijini Arusha.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya Simu jana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alisema ripoti ya chanzo cha milipuko hiyo haijakamilika na kwamba wataitangaza mara tu itakapokamilika.


“Ripoti bado haijakamilika, bado inafanyiwa kazi hadi hapo itakapokamilika katika hatua zote tutaitangaza tu ikikamilika,” alisema Dk. Mwinyi.

Alipoulizwa kuwa, ni lini ripoti hiyo itakuwa tayari na kutangazwa kwa wananchi Dk. Mwinyi alijibu:

“Kwa sasa siwezi kusema siku gani itakamilika na kutangazwa kwa sababu bado inafanyiwa kazi,” alisema Dk. Mwinyi na kusisitiza:

“Wewe ukiona kimya ujue ripoti haijakamilika na ikikamilika siku yoyote ile basi tutawapatia taarifa zake.”

Aidha Dk. Mwinyi alisema, Satelati kwa ajili ya kubaini mabaki ya mabomu yaliyokuwa yamezagaa baada ya milipuko hiyo, nayo bado haijafika nchini na kwamba siku yoyote itakapofika watatoa taarifa kwa wananchi.

Siku chache baada ya milipuko hiyo baadhi ya wanaharakati na wanasiasa nchini walitoa wito wa kujiuzulu kwa Dk. Mwinyi na Naibu wake Dk Emanuel Nchimbi pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Davis Mwamunyange, kwa madai kwamba milipuko hiyo ilitokea kwa uzembe.

Hata hivyo Dk. Mwinyi aliahidi kujiuzulu iwapo baraza la uchunguzi litabaini kuwa milipuko hiyo ilitokea kwa sababu ya kukiukwa kwa taratibu za utendaji au sheria.

Monday, July 27, 2009

Profesa Ngugi kunguruma UDS

Salim Said
PROFESA Ngugi wa Thiong’o kutoka Kenya anatarajiwa kuhutubia Kongamano la sita la Usomaji kwa Wote katika nchi za Afrika litakalofanyika katika chuo kikuu cha Dar es Salaam kuanzia Agosti 10 hadi 14 mwaka huu.
Kongamano hilo, linafanyika chini ya ushirikiano wa Chama cha Usomaji wa Kimataifa, Kamati ya Kimataifa ya Afrika, Chama cha Usomaji Tanzania na Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania (CBP).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya kongamano hilo Profesa Mugyabuso Mulokozi alisema, kongamano hilo litawashirikisha wadau na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka ndani na nje ya nchi.

“Katika kongamano hili Profesa Ngugi atakuwa mgeni rasmi na washiriki kutoka nchi mbalimbali watakutana kubadilishana maarifa, uzoefu, taarifa, na kupanga mikakati mbalimbali ya kuboresha masuala ya usomaji na ikiwa ni pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za usomaji,” alisema Profesa Mulokozi.

Alisema, kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Usomaji wa Vitabu kwa ajili ya Kuleta Maegeuzi na Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi.

“Kongamano hili litawakutanisha wakereketwa wa usomaji wakiwamo walimu, wakufunzi, watafiti, wahadhiri, wakutubi, waandishi, wachapaji, wauza vitabu, viongozi, watunga sera na wasomaji mbalimbali kutoka Afrika na kwenmgineko,” alisema Profesa Mulokozi,.

Alisema, zaidi ya washiriki 200 watawasilisha maandiko yao katika kongamano hilo, na kwamba washiriki 200 kutoka nje ya nchi watashiriki na 300 kutoka Tanzania.

Alisema katika kongamano hilo kutakuwa na zawadi kwa washindi wa tatu wa shindano la uandishi wa fasihi katika bara la Afrika pamoja na uzinduzi wa kitabu cha prfesa Ngugi kijulikancho kwa jina la ‘Re-Membering Afrika’.

Kongamano hili ni la sita ambapo yaliyopita yalifanyika katika nchi za Afrika ya Kusini 1999, Nigeria 2001, Uganda 2003, Swaziland 2005 na Ghanna mwaka 2007.

Wadau wapinga mfuko wa jimbo

Salim Said
WADAU wa masuala ya kisiasa na uchumi nchini wameipinga vikali nia ya serikali kuanzisha Mfuko wa Kuhudumia Jimbo kwa sababu mfuko huo utakuwa na harufu mbaya ya ufisadi.

Wakati wadau wakiupinga uanzishwaji wa mfuko huo, serikali inakusudia kukusanya maoni ya wananchi kuhusu uanzishwaji wa mfuko huo wiki ijayo.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana wadau hao walisema, mfuko huo una harufu ya ufisadi ndani yake.

Profesa Ibrahim Lipumba alisema, hauungi mkono mfuko huo kwa sababu una harufu ya ufisadi na upendeleo kwa wabunge wenye majimbo.

“Mimi siuungi mkono kwanza una harufu ya mbaya ya ufisadi lakini pia wabunge wenye majimbo watakuwa na upendeleo katika matumizi ya fedha hizo,” alisema profesa Lipumba.

Alisema, hakuna haja ya kuanzishwa kwa mfuko huo kwa sababu kuna halmashauri za Wilaya ambazo zinatosha kutumika kusimamia fedha za maendeleo ya wananchi.

“Serikali inaweza kupitishia fedha hizo katika halmashauri na kugaiwa katika kikao cha Baraza la Madiwani ambacho mbunge ni mjumbe wa kikao hicho ataweza kushiriki katika njia hiyo na si kumkabidhi fedha,” alisema Profesa Lipumba.

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. Benson Bana alisema, hakubaliani kabisa na nia ya serikali kuanzisha mfuko huo kwa sababu tayari kuna mifuko mingi ya maendeleo katika ngazi za Halmashauri.

“Mfuko huu unatoka wapi na kwa nini uwe wa jimbo, kwa sababu ngazi za maendeleo katika halmashauri si jimbo tu na kwa nini usiwe wa ngazi nyingine. Kwa kweli mfuko huu unazua maswali mingi kuliko majibu,”alisema Dk Bana.

Dk Banna alihoji, sababu ya serikali kutaka kuanzisha mfuko huo hivi sasa na kwa nini haukuanzishwa katika miaka 10 iliyopita.

“Mfuko huu kwa mazingira ya Tanzania na ukata tuliwonao lazima utazua na kuongeza mitafaruku na migongano majimboni kutokana na upendeleo wa wabunge,” alisema Dk. Bana.

Alisema, hakuna haja ya kumuongezea Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kazi ya kufanya ukaguzi katika mifuko isiyo na idadi.

“Halmashauri zinatosha kabisa kusimamia fedha, kama serikali ina fedha inataka kuzipeleka kwa wananchi izipitishie katika halmashauri tu na hakuna haja ya kuongeza idadi ya mifuko,” alisema Dk. Banna na kuhoji:

“Tuna mfumo uliokamilika katika ngazi ya halmashauri wa kusimamia fedha za serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, kwa nini tusiutumie au tunataka kuwapa mdomo wabunge waliopo madarakani.”

Shabiby: Aataka EWURA, TRA kudhibiti bei za mafuta

Salim Said
MBUNGE wa Gairo (CCM) Ahmed Mabkhut Shabiby amezitaka Mamlaka za Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha wanadhibiti upandaji wa ovyo wa bei za mafuta katika majiji nchini.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Shabiby alihoji kwa nini bei ya mafuta katika jiji la Dar es Salaam iko juu na mikoani iko chini.

Alisema, upandaji wa mara kwa mara wa bei za mafuta kwenye majiji makubwa nchini hususan Dar es Salaam unatia shaka na kutishia amani kwa watumiaji.

Akizungumza huku akitolea mifano baadhi ya makampuni ya mafuta nchini, alisema Dar es Salaam ndiyo sehemu ambayo mafuta hushuka kutoka nje ya nchi, lakini bei yake iko juu kuliko mikoani ambako husafirishwa baada ya kushushwa jijini hapa.

“Hivi hizi bei elekezi za EWRA zinafanya kazi kweli, kwa sababu Dar es Salaam ambako mafuta hayo hushushwa yanauzwa kati ya 1500 na kuendelea, lakini Dodoma mfano yanauzwa sh 1450, napata wasiwasi na ushirikiano wa TRA na EWRA katika kazi zao,” alisema Shabiby.

Alisema, kama kuna ushirikiano kati ya mamlaka hizo, wangekaa na kuangalia kwa makini faida na gharama ya kila lita moja ya mafuta na kuweza kupanga bei ambayo itakuwa inakidhi mahitaji ya watumiaji na isiyobadilika ovyo ovyo.

“Kinachofanyika katika kupanga bei hapa ni kwamba hawaangalii gharama bali huangalia wingi wa magari (mahitaji) katika mji. Kama magari ni mingi bei itakuwa juu na kama ni kidogo bei itakuwa chini, hivi si sahihi hata kidogo,” alisema Shabiby.

Alitolea mifano katika nchi jirani ya Kenya ambapo sehemu zenye bandari ambapo mizigo hushukia bei ya mafuta huwa chini kwa sababu mamlaka za mapato na za udhibiti wa huduma za mafuta zinafanya kazi kwa na ushirikiano mkubwa.

Sunday, July 26, 2009

Kafulila ajitupa jimboni

Salim Said
AFISA Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) David Kafulila ametangaza rasmi nia yake ya kugombea kiti cha ubunge kwenye jimbo la Kigoma Kusini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Jimbo hilo, ambalo lipo jirani na la Kigoma Kaskazini la mbunge wa Chadema Zitto Kabwe, kwa sasa linashikiliwa na Manju Msambya kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake Kinondoni jijini Dar es Salaam jana, Kafulila alisema tayari ameanza harakati mbalimbali za kuhakikisha kuwa anajenga uhusiano mzuri na wananchi wa jimbo hilo pamoja na mtandao mzuri wa Chadema.

“Ya ni kweli nna nia ya kugombea ubunge wa Kigoma Kusini na nimeshaanza maandalizi tangu mwaka juzi kwa kuwasaidia wananchi katika matatizo mbalimbali yanayowakabili,” alisema Kafulila.

Alisema, jimbo la Kigoma Kusini linashikiliwa na Msambya wa CCM, lakini matatizo ya jimbo hilo yamekuwa yakizungumzwa na wabunge wa Chadema zaidi kuliko yeye aliyepewa dhamana na wananchi.

“Sasa utashangaa Msambya badala ya kuwa msemaji mkuu wa matatizo ya wananchi wa Kigoma Kusini badala yake yamekuwa yakifikishwa bungeni na wabunge wa Chadema akiwamo Zitto, Halima Mdee na Muhonga Said,” alisema Kafulila.

Alisema, anaamini kuwa kwa kushughulikia matatizo ya kijamii ya watu wa Kigoma Kusini itawafanya kuwa na imani naye pamoja na chama chake cha Chadema.

Alifafanua, katika juhudi anazofanya kuimarisha mtandao wa Chadema katika jimbo hilo, chama chake kinakusudia kupeleka Operesheni Sangara mwezi ujao.

“Jimbo lile hadi hivi sasa inaonesha kuwa limo katika mikono ya upinzani licha ya kuwa mbunge wake anatoka CCM, kwa sababu vijiji 27 vinashikiliwa na upinzani na vijiji 16 tu ndio vya chama tawala,” alisema.

Mbio za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010 zimeanza huku kila mwanasiasa akijiimarisha katika jimbo lake ili kuhakikisha anapata kuungwa mkono na watu wa jimbo lake.

BoT kuwabana wadanganyifu ugawaji wa mabilioni ya mtikisiko wa uchumi

Salim Said
SERIKALI imeiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya mchanganuo wa kampuni 50 ambazo zitapata uhalali wa kuingia katika orodha ya kampuni zitakazofidiwa na serikali baada ya kupata hasara kubwa kutokana na athari za mtikisiko wa uchumi ulioikumba dunia kuanzia mwaka jana.

Fedha hizo ni kiasi cha sh 21.9 bilioni zilizotengwa na serikali kwa ajili ya kuwanusuru wale wote waliopata hasara kutokana na kuanguka kwa bei ya mazao katika soko la dunia kutokana na athari za mtikisiko wa kiuchumi ulioikumba dunia.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi Ramadhan Khijja aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba, tayari BoT imeanza mchakato wa kuratibu kampuni hizo, ili kuweza kupata kampuni 50 zilizoathirika sana kwa lengo la kuanza kuzipatia fidia.

“Tayari BoT inafanya mchanganuo wa kuzitambua kampuni 50 ambazo ziliathirika zaidi na mtikisiko huu, kwa kula hasara kutokana na kununua mazao kwa bei kubwa na kuyauza kwa bei ndogo, baada ya bei kushuka katika soko la dunia,” alisema Khijja mara baada ya kufungua Mkutano wa Mwaka wa Shirikisho la Wenyeviwanda Tanzania (CTI).

Alisema, mchanganuo huo yakinifu utaweza kubaini ni kampuni gani iliyoathirika sana na mtikisiko huo na ipi ambayo haikuathirika sana na mtikisiko.

“Baada ya mchanganuo wa BoT tutaweza kujua ni kampuni gani inastahiki kupata fedha hizo na ipi haistahiki ili tusijekuingia katika hasara kwa kutoa fedha kwa kampuni ambazo hazikustahiki,” alisema Khijja.

Khijja alibainisha kuwa, kuna baadhi ya kampuni ambazo zimekula hasara miaka mingi iliyopita lakini tayari kuna kampuni ambazo zimejitokeza na kujifanya kama kwamba zimekula hasara katika mtikisiko wa uchumi wa mwaka jana ili ziweze kufidiwa.

“Shilingi 21.9 bilioni ambayo imetengwa na serikali kuwafidia wafanyabiashara ni kwa wale tu ambao wamekula hasara kutokana na mtikisiko wa mwaka jana, ujanja huu tumeugundua na ndio maana serikali imeiagiza BoT kufanya uchanganuzi,” alisema Khijja.


Khiija alisema, wataziomba benki nchini kuowaongezea muda wa kurudisha mikopo baadhi ya kampuni ambazo zimepata hasara katika biashara zao kutokana na kuyumba kwa uchumi wa dunia.

Aidha alisema, serikali imeahidi kuzichukulia dhama baadhi ya kampuni ili kuweza kupata mikopo katika benki mbalimbali nchini lakini itafanya hivyo kwa zile kampuni ambazo hazina historia nzuri katika sura kibenki.

“Benki nyingi zinaingia katika hasara kutokana na kuwakopesha watu ambao hawana historia nzuri, hawajulikani mali zao, mahali wanapoishi, ufanisi wake katika biashara na hata uaminifu wake iwapo je alishawahi kukopa na kurejesha mkopo kwa wakati,” alisema Khijja na kusisitiza:

“Dhamana hii tutaoa kwa watu ambao hawajajenga historia katika benki ili kuweza kujenga wateja wazuri kwa mabenki kwa lengo la kuziondoa katika hatari ya kula hasara, halafu sisi tutasiamamia wale tuliowachukulia dhamana.”


Kwa upande wao baadhi ya wajumbe wa CTI walilaumu ukubwa serikali na gharama za uendeshaji kama ndio kikwazo kikubwa katika maendeleo ya Tanzania, huku wakihimiza miundombinu kuwa ndio njia ya mkato ya kuinua uchumi wa nchi.

Mwenyekiti wa Zamani wa CTI na Waziri Mstaafu katika serikali ya Tanzania Iddi Simba alisema, ukubwa wa serikali bado ni kikwazo katika maendeleo ya Tanzania.

“Kama tunatambua kuwa sekta ya viwanda kuwa ni injini ya uchumi wa nchi, lazima tuangalie kwa makini ukubwa wa serikali na gharama za uendeshaji wake,” alisema Simba na kusisitiza:

“Ukuaji wa uchumi wowote duniani ni matokeo ya uwekezaji, usimamiaji na matumizi sahihi ya rasilamali za nchi. Amani, ulinzi na usalama wan chi hii unaangalia ni namna gani tutapunguza au kuondoa umasikini ambao unazidi kukua siku hadi siku.”


Alisema, serikali ya Tanzania ni kubwa sana na ina matumizi makubwa hivyo kama kweli kuna nia ya kumkomboa mtanzania ni lazima serikali ipunguze ukubwa na matumizi yake.

Naye Mwenyekiti wa CTI Reginald Mengi aliipongeza serikali kwa kutenga sh1.7 trilioni kama fungu maalumu (stimulus package) kwa ajili ya kunusuru uchumi wa nchi baada ya kuyumba kutokana na mtikisiko.

“Fedha hizi ni nzuri na naipongeza serikali, lakini pekee haitoshi bali inataka kuungwa mkono kwa serikali kupunguza kodi ya bidhaa kutoka nje, kuongeza uzalishaji wa ndani kwa kutumia mali ghafi zetu, kutafuta soko la nje kwa bidhaa za ndani na serikali kutoa ruzuku,” alisema Mengi.

Aliitahadharisha serikali, kuwa makini na mafisadi katika matumizi ya fedha hizo ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa bila ya kufujwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Maendeleo ya Viwanda Vidogovidogo (Sido) Mike Laiser alilalamikia mabenki nchini kwa kutoza riba kubwa kwa wakopaji na kuweka riba ndogo kwa mtu anapoweka fedha benki.

“Ukikopa unapigwa riba kati ya asilimia 18 hadi 25 lakini wewe ukiweka fedha benki riba yake ni asilimia mbili hadi nne, hili bado ni tatizo kubwa katika maendeleo ya SMEs,” alisema Laiser.

Mtikisiko wa kiuchumi duniani ulianzia marekani mwaka 2007, baada ya mabenki ya taifa hilo kiongozi duniani kukithiri katika kutoa mikopo ya nyumba na hatimaye kufilisika.

Kutokana na uhusiano mkubwa uliopo baina ya uchumi wa Marekani na mataifa mengine hatimaye mtikisiko huo ulianza kuenea katika mataifa ya Ulaya, Asia na Afrika.

Tanzania iliathirika na mtikisiko huo katika sector za kilimo, biashara, utalii, ajira, madini, uwekezaji wan je (FDI), viwanda na nishati.

Friday, July 24, 2009

Chadema: suluhu ya muungano ni serikali tatu

Salim Said
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema migogoro na malumbano kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar itaendelea iwapo nchi haitafuata mfumo wa serikali tatu au serikali moja.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala kuhusu mambo ya Muungano huku pande zote mbili zikishutumiana mara kwa mara kama ndio chanzo cha migogoro hiyo.

Malumbano makubwa kuhusu muungano baina ya pande mbili hizo, yamezuka miezi ya karibuni baada ya kuzuka kwa tetesi kwamba kuna uwezekano wa kuwapo kwa mafuta na gesi asilia katika visiwa vya Zanzibar.

Akizungumza na Mwananchi Ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema Victor Kimesera alisema, mvutano kati ya pande mbili za muungano hautoisha iwapo mfumo wa serikali hautabadilika.

“Suluhu ya mivutano hii isiyoisha kati ya pande mbili za muungano ni kuwapo kwa serikali tatu au serikali moja tu nchini na sio serikali mbili,” alisema Kimesera.

Alisema, uwepo wa serikali mbili yaani ya Zanzibar na Muungano kunasababisha malumbano na mivutano ya mara kwa mara kati ya pande mbili za muungano huo.

“Chaguo na msimamo wa Chadema kikatiba hasa, ni kuwepo kwa serikali tatu au serikali moja nah ii ndio dawa kubwa ya malumbano na mivutano baina ya pande mbili za muungano,” alisema Kimesera.

Juzi Waziri Mkuu Mizengo Pinda alionya uwezekano wa Muungano huo kuvunjika endapo malumbano kuhusu gesi asilia na mafuta yataendelea.

Alisema baada ya muungano huo kuvunjika lazima upande mmoja wa muungano utapata shida.

Hivi karibuni Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilitoa msimamo rasmi wa kutaka suala la mafuta na gesi asilia liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano.

Thursday, July 23, 2009

Masha: kuna nini mradi wa vitambulisho vya utaifa

Salim Said na Kizitto Noya
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha amewajia juu vigogo wenzake serikalini kwa kumzuia kusimamia ipasavyo kazi ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa inayotarajiwa kugharimu kiasi cha Sh200 bilioni.

Akitoa majumuisho ya bajeti ya wizara yake bungeni mjini Dodoma jana, Waziri Masha alisema baadhi ya vigogo walimzuia kuhoji dosari aliyoiona katika mchakato wa zabuni ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa, wakati yeye ndiye waziri mwenye dhamana na wizara hiyo.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Waziri Masha alidaiwa kumwandikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa kuna kigogo mmoja Ikulu (jina tunalihifadhi) alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupeleka taarifa ya utekelezaji wa mradi wa vitambulisho kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri.

Ilidaiwa katika malalamiko ya Masha kwa Waziri Mkuu kuwa hatua hiyo ya kigogo huyo wa Ikulu haikumridhisha (Masha) kwa madai kwamba, hakumhusisha kwa vile yeye ndiye atakayeiwasilisha taarifa hiyo kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri na ndiye atakayewajibika kwa maamuzi yoyote yatakayofanyika wizarani kwake, bila kujali kama maamuzi hayo yalipata baraka (ya kigogo huyo) au la.

Kwa mujibu wa habari ambazo ziliandikwa na vyombo vya habari na kuthibitisha na Waziri Mkuu wakati akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni, alikiri kupokea barua ya Waziri Masha, lakini habari hizo zilivuja baada ya nyaraka kunyofolewa katika Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Masha alimwandikia Waziri Mkuu barua akimlalamikia kwa madai ya kigogo huyo kumwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani kuwasilisha taarifa hiyo kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri bila kumhusisha yeye kama Waziri.

Akiongea bungeni jana, Waziri Masha alisema wabunge wengi wamehoji mradi wa vitambulisho katika hoja tatu ambazo ni kwa nini vinachelewa, kwa nini waziri aliingilia na kwa nini halijapelekwa katika Baraza la Mawaziri.

“Mheshimiwa Naibu Spika, mheshimiwa Anna Komu ameuliza swali zuri hapa kwamba katika mradi wa vitambulisho kuna nini? Na mimi nauliza katika mradi wa vitambulisho kuna nini,” alihoji Masha.

Akizungumza huku akikariri mara kwa mara swali la kuna nini katika mradi wa vitambulisho, Waziri Masha alisema, kuna baadhi ya wabunge walimuona kafanya makosa yeye kumuhoji Katibu Mkuu na kumuandikia Waziri Mkuu kumuelezea dosari aliyoiona katika mchakato.

“Mradi upo katika mchakato, lakini baadhi ya watu hawaridhiki. Mimi niliuliza swali kwa katibu mkuu wangu, nikaambiwa nimeingilia mchakato na sina haki ya kuuliza, lakini bunge lina haki ya kunihoji mimi. Nami nauliza katika mradi huu kuna nini,” alihoji na kuongeza.

“Cha ajabu ni kwamba, mimi niliuliza ili nitakapokuja ulizwa bungeni niweze kujibu, lakini kumuuliza kwangu ilikuwa ni kosa, naambiwa hukutakiwa kuuliza. Kwa nini Bunge liniulize mimi halafu mimi nisiwe na haki ya kuuliza watendaji wangu. Hivi ndani ya mradi wa vitambulisho kuna nini?”

Waziri Masha alihoji zaidi kuwa kuna nini Watanzania na baadhi ya wabunge wasiipe muda serikali kukamilisha mradi huo, badala yake wanamtaka waziri mwenye dhamana asihoji wala kuingilia mchakato wake.

Alifafanua kuwa cha ajabu ni kwamba, kuna hoja inayotaka hata Rais na Baraza la Mawaziri hawatakiwi kupewa taarifa, huku ikisema kuwa Bunge linapaswa kujua.

“Cha ajabu kuna hoja bungeni kwamba, hata rais na baraza lake la mawaziri hawapaswi kupata taarifa za mchakato huu, lakini Bunge linapaswa kupewa taarifa, hivi kuna nini kwenye mradi huu,” alihoji Waziri Masha.

Alisema suala la mradi wa vitambulisho lipo katika mchakato na kwamba, anawaomba wabunge wampe muda kukamilisha mchakato wa zabuni ya mradi huo.

“Tumeshapokea taarifa ya PPRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi), sasa tunasubiri taarifa ya Mwanasheria Mkuu wa serikali ili suala hilo lifikishwe kwa Baraza la Mawaziri. Napenda kuona kabla ya kumalizika kwa Bunge huu mradi unaanza,” alisema.

Awali Waziri Masha alilalamika kuwa asibebeshwe lawama kwa kuchelewa vitambulisho hivyo kwa kuwa suala hilo lilianza kabla hajazaliwa mwaka 1968 huku mama yake akiwa na umri wa miaka 19 tu.

Alisema, sheria ya vitambulisho hivyo ilitungwa mwaka 1986 na mwaka 1995 tenda ya kwanza ikatangazwa ambayo hata hivyo haikufanikiwa.

Alisema, mnamo mwaka 2004 upembuzi yakinifu ulifanyika na Febuari mwaka 2007 ikakubali ushauri na kuiteua kampuni ya Gotham kuwa mshauri mwelekezi wa mradi huo.

“Hapo ndipo Masha alipofahamu mradi wa vitambulisho. Kwa hiyo hata mimi nauliza kuna nini ndani ya mradi huu,” alilalamika Masha.

Alisema hadi sasa mamlaka ya kusimamia na kuratibu utoaji wa vitambulisho hivyo (NIDA) imezinduliwa, watendaji watajiriwa na kamati ya uongozi kuteuliwa na kasha kuanza kazi.

“Pia wizara imekamilisha hatua ya kwanza ya kumpata mkandarasi ambaye ataweka mfumo wa kutunza taarifa za watu watakaopewa vitambulisho,” alisema.

Kwa mujibu wa Masha, miradi hiyo inaenda sambamba na maandalizi ya utoaji zabuni ya vitambulisho hivyo yanayoendelea sasa.

“Naomba kuwathibitishia Watanzania kupitia Bunge lako tukufu kwamba, mradi wa vitambulisho utakamilika kwa kufuata sheria na utaratibu, bila mizengwe, kwa uwazi unaostahili na bila upendeleo,”alisisitiza.

Baada ya Waziri Masha kumaliza kutoa hoja alisimama mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, (CCM) na kusema kwa jazba kuwa wanachokitaka kwa Waziri ni lini vitambulisho hivyo vitapatikana.

“Kama waziri mwenyewe hajui kinachoendelea katika wizara yake ina maana hakuna kinachoendelea, halafu anatuambia mchakato unaendelea, mchakato gani huo,” alihoji Shelukindo.

Masha alijibu, kwa kusema, “Mheshimiwa Naibu Spika narudia tena kuhoji katika mradi wa vitambulisho kuna nini? Waraka wa Baraza la Mawaziri ni siri.”

“Kuna nini katika mradi wa vitambulisho kinachawanfanya baadhi ya wabunge wasitake sisi kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali? Nauliza tena kuna nini,” alihoji Waziri Masha kwa sauti ya chini kabisa.

Alisema, Masha ni yule yule hajabadilika, amaamini kuwa anaweza, lakini na aliuliza tena kuna nini katika mradi wa vitambulisho.

Jambo hili lilisababisha Naibu Spika Anne Makinda kusimama na kutoa ufafanuzi akisema: “Mheshimiwa waziri na mheshimiwa mbunge hapa tunasikilizwa na wananchi nchi nzima, wanachotaka kujua ni je, vitambulisho watavipata au hawatavipata? Hilo ndilo wanalohitaji na sio kuna nini”.

Waziri Masha baada ya hapo alisimama na kujibu kwa ufupi kuwa, vitambulisho hivyo vitapatikana ndani ya mwaka huu wa fedha.

“Mheshimiwa Naibu Spika, vitambulisho vitapatikana ndani ya mwaka huu wa fedha,” aliahidi.

Hata hivyo, kambi ya upinzani ilieleza wasiwasi kuhusu kukamilika kwa mradi huo, ikisema serikali imekuwa ikiahidi bila kutekeleza.

Msemaji wa kambi hiyo katika wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ibrahin Muhammed Sanya alisema serikali imekuwa ikitoa ahadi zisizotekelezeka kuhusu suala la uraia wa nchi mbili na vitambulisho vya Uraia.

“Katika hotuba zetu za kambi miaka 2006/2007, 2007/2008 na 2008/2009, tumekuwa tukizungumzia suala la uraia wa nchi mbili, Na katika majibu ya Serikali mara zote ni kwamba mchakato unaendelea huku muda ukiyoyoma. Je, mchakato huo utamalizika lini? alihoji Sanya.

Akinukuu majibu ya serikali ya mwaka 2006 kuhusu vitambulisho vya uraia, Sanya alihoji: “Toka mwaka huo hadi sasa 2009, bado mchakato unaendelea tu. Kila siku tunaambiwa hadithi mpya kuhusiana na vitambulisho hivyo. Fedha za walipakodi zinazidi kuwaneemesha baadhi ya watu katika kadhia nzima ya vitambulisho vya uraia. Je Serikali inawatendea haki Watanzania?”

RAAWU yaingilia katia uhamishwaji watumishi NECTA

Salim Said
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (RAAWU), Adelgunda Mgaya amesema uhamishaji wa wafanyakazi 70 wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) uliofanywa na Wizara ya Elimu hivi karibuni umegubikwa na mizengwe mingi.

Hivi karibuni, wafanyakazi 70 wa Necta waliwahamishwa kutoka katika vituo vyao vya kazi na kupangiwa katika vituo vipya kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza na Mwananchi Ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Mgaya alisema uhamisho huo uligubikwa na mizengwe pamoja na ukiukwaji mkubwa wa kanuni na taratibu za uhamisho wa watumishi wa umma.

Alisema, wafanyakazi hao walitakiwa kusaini barua za uhamisho wao chini ya ulinzi mkali wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wenye silaha, askari wa usalama wa raia na askari wa kmpuni binafsi ya ulinzi.

“Kwa kweli uhamisho ule haukuwa wa kawaida kwa sababu uligubikwa na mizengwe. Katika mazingira ya kawaida haiwezekani kumtaka mfanyakazi asaini barua ya uhamisho chini ya ulinzi mkali wa FFU tena wenye silaha,” alisema Mgaya.

“Hata wewe niambie kampuni yako ya Mwananchi inakuhamisha kikazi labda kwenda tawi la Mwanza, unakuja unasainishwa barua ya uhamisho chini ya ulinzi wa FFU wenye silaha, halafu unaambiwa ukishasaini barua uondoke hata ndani huruhusiwi kuingia, utakuwa umetendewa haki,” alihoji Mgaya.

Alisema, hivyo ndivyo walivyafanyiwa wafanyakazi 70 wa Necta, kwamba mara baada ya kusaini barua zao walitakiwa kuondoka na hawakuruhusuiwa hata kuingia ndani ya ofisi kuchukua vitu vyao.

“Unajua unapokaa katika ofisi kwa muda mrefu, huwa unaweka vitu vyako vingi, leo unamuhamisha mfanyakazi bila kumruhusu kuingia ndani na kuhamisha vitu vyake, je utakuwa umefuata taratibu za uhamisho,” alihoji.

Mgaya alisema, kwa sasa hana mengi ya kusema kwa sababu anafanya mawasiliano na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mazungumzo zaidi kuhusiana na ukiukwaji wa kanuni katika uhamisho huo.

“Barua zile zilisainiwa na Katibu Mkuu wizarani hivyo nafanya mawasiliano naye ili tukutane anieleze kwa nini amekiuka taratibu za uhamisho, je ni kwa makusudi au alikuwa hajui,” alihoji Mgaya na kuongeza:

“Kama kutakuwa na maridhiano basi tutasema na kama hakutakuwa na maridhiano pia tutaeleza hatua gani tutachukua zaidi kutetea haki za wanachama wetu.”

Pamoja na hayo, Mgaya alisema Wizara haikuwashirikisha wao kama watetezi wa haki za wafanyakazi hao kabla ya kuwahamisha, jambo ambalo limesababisha hata kuathirika kwa Tawi la RRAWU katika ofisi za Necta.

“Kisheria kwa sababu wafanyakazi waliohamishwa wengi ni viongozi wa tawi letu pale, wizara ilitakiwa kutushirikisha ili tutafute mtu mwengine wa kumuweka badala yake lakini haikufanya hivyo,” alisema Mgaya na kuongeza:

“Jambo ambalo limedhoofisha nguvu ya tawi letu kwani ni kiongozi mmoja tu aliyebaki waliobakia wote wameingia katika uhamisho bila ya kuwa na mbadala wake.”

Kwa muda baadhi ya watendaji wa Necta wamekuwa wakilalamikiwa kutokana na kuvuja kwa mitihani ya taifa, ambapo suala la wafanyakazi kukaa katika kituo kimoja cha kazi kwa miaka mingi ikitajwa kuwa miongoni mwa sababu za kuvuja kwa mitihani hiyo.

Watu wenye ulemavu wataka misaada

Salim Said
SHIRIKISHO la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shivyawata), limezitaka taasisi mbalimbali nchini kulitupia macho shirika hilo, kwa kuwapatia misaada badala ya kuthamini taasisi na sekta nyingine pekee.


Wito huo ulitolewa jana na Katibu Mkuu wa Shivyawata Felician Mkude alipotoa shukurani kwa baadhi ya taasisi chache zilizolipatia misaada mbalimba shirika hilo.

“Pamoja na kuzishukuru baadhi ya taasisi zilizotupatia misaada, lakini pia tunaziomba taasisi nyengine kutupia macho masuala ya watu wenye ulemavu, kwani nalo ni kundi tete lililosahaulika na linalohitaji kuwezeshwa ili kujiendesha,” alisema Mkude na kuongeza:

“Shivyawata inatoa wito kwa mashirika mbalimbali, makampuni binafsi, wizara na Idara za serikali, taasisi za dini, wafanyabiashara na watu binafsi wa ndani na nje ya nchi kuchangia kwa hali na mali, maendeleo na ustawi wa watu wenye ulemavu nchini.”

Mkude alisema, mtu mwenye ulemavu anaweza iwapo jamii itamuwezesha kwa kumuunga mkono katika juhdi zake za kutafuta maendeleo.

Alisema, Shivyawata linazipongeza taasisi zote za ndani na nje zilizojitokeza kuwasaidia kwa njia moja au nyengine, hususan mashirika ya Iternational Sustainable Cities (ISC) la Kanada, Magdala Foundation (MF) ya Madrid Hispania, na kampuni ya MMI Steel ya jijini Dar es Salaam.

Alisema, ISC iliwezesha wajasiriamali wenye ulemavu mkoani Dar es Salaam (Uwawada) kwa kuwatunishia mfuko wao wa kuweka na kukopa ambao kwa sasa umefikia miaka miwili.


Aidha MF iliwawezesha wanawake 50 wenye ulemavu kupitia Saccoss hiyo kwa kutoa fedha ambazo zitatumika kuwakopesha sh250,000 kwa awamu mbili tofauti.

“Halikadhalika kampuni ya MMI Steel, imetoa msaada wa vifaa vya kusikia kwa ajili ya watoto viziwi vyenye thamani ya milioni 15, ambavyo wamevikabidhi kwa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA),” alisema Mkude na kusisitiza:

“Vifaa hivi vitawasaidia vijana hao katika kuendeleza elimu yao hususan kwa watoto wenye ulemavu nchini.”

Wednesday, July 22, 2009

CUF yawavaa JK, Pinda

Salim Said
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitoweza kujivua na lawama za kutokea kwa machafuko visiwani Zanzibar katika uchaguzi mkuu 2010, kwa sababu inaridhia vyombo vyake kutumiwa vibaya na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika maandalizi ya uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka CUF, SMZ chini ya uongozi wa Rais Amani Karume imekuwa ikivitumia vibaya vyombo vya dola vya serikali ya Muungano katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hususan uboreshaji wa daftari la wapigakura.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Salim Bimani ilisema, miongoni mwa vyombo hivyo ni Usalama wa Taifa na Polisi.

Kwa mujibu wa Bimani Usalama wa taifa ni miongoni mwa mambo ya Muungano na kwamba idara hiyo inasimamiwa moja kwa moja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

“Kwa mantiki hiyo, hakuna namna yoyote ambayo Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wanaweza kujivua na lawama za kutokea kwa vurugu kabla, wakati au baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka 2010,’ alisema Bimani

Alisema hiyo ni kwa sababu inaonesha wazi kuwa viongozi hao wanaridhia uvamizi wa vyombo hivyo vya dola katika kazi za ZEC au hawajali kile kinachofanywa na vyombo hivyo.

“Lolote kati ya hayo mawili linamaanisha kwamba wao ndiwo wanaopaswa kubeba dhima na lawama za hali ya juu kwa hali yoyote mbaya katika uchaguzi wa 2010 visiwani Zanzibar,” alisema Bimani.

Alisema, CUF inachukua fursa hiyo kuwakumbusha viongozi hao wakuu wa serikali ya Muungano kwamba, wao ndiwo wenye dhima ya kulinda usalama na haki zote za kikatiba za wananchi wa Tanzania wakiwamo na wa Zanzibar.

“Tunachukua nafasi hii tena na tena kuwakumbusha viongozi wakuu hawa wawili, wajue kama walikuwa hawajui kuwa wao ndiwo wenye jukumu la kulinda usalama na haki zote za kikatiba za wananchi wa Tanzania (bara na Zanzibar),” alisema Bimani.

Alisema, kisingizio kwamba Zanzibar ina sheria zake za uchaguzi si sababu ya wao kuviachia vyombo vya dola vilivyo chini ya mamlaka yao kuvunja haki za binadamu na wananchi kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa, suala la Zanzibar kuwa sheria zake si sababu ya msingi pia ya kudharau ukweli kwamba uchaguzi wa Zanzibar unavurugwa na vyombo vile vile ambavyo vilitarajiwa kuusimamia.

“Hili la kuwanyima wananchi haki ya kuandikishwa katika daftari la wapiga kura na kuweka vyombo vya dola ili kuhakikisha haki hiyo haipatikani ni katika mifano halisi ya ukiukwaji haki za binadamu,” alisema Bimani.

Alisema, wakati CUF inathamini nafasi ya vyombo vya dola, ikiwemo idara ya usalama wa taifa katika kuifanya nchi kuwa katika amani, umoja na mshikamano lakini chama chao hakikubaliani na dhana kwamba jukumu la Idara hiyo ni kuhakikisha kuwa wananchi wenye mawazo tafauti ya kisiasa na watawala hawana haki katika nchi yao.

Aidha Bimani alisema wamefadhaishwa na vitendo ya maafisa wa hao katika Wilaya ya Micheweni kuingilia kati utendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Alisema, tukio hilo linaonesha kwamba ZEC haiko huru na inafanya kazi zake kwa kufuata maagizo kutoka katika Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

“Vitendo hivi si tu kwamba vinathibitisha kauli yetu ya muda mrefu kwamba ZEC inaendesha uchaguzi kwa kufuata maagizo ya Idara ya Usalama wa Taifa, bali pia vinapigilia misumari mingine kwenye jeneza la kuizikia demokrasia ya Zanzibar,” alisema Bimani na kuongeza:

“Kila mara tumekuwa tukisema kwamba vyombo vya dola ndivyo vinavyosimamia na kuendesha uchaguzi wowote unaofanyika Zanzibar, huku ZEC ikiwa kama ni alama tu ya kuwepo kwa chombo huru kinachoendesha shughuli za uchaguzi.”

Alisema, kwa mujibu wa taarifa walizozikusanya kutoka katika vituo vya uboreshaji wa daftari hilo vya Wingwi Mapofu, Mgogoni, Kinyasini, Finya na Konde zinaonesha kwamba vyombo vya dola vimekuwa vikishiriki kikamilifu katika kutoa maelekezo kwa watendaji wa ZEC.

“Miongoni mwa maelekezo hayo ni pamoja na kuwazuia masheha wa Shehia kuzungumza na waandishi wa habari ambao huwa wanataka kujua usahihi wa madai yanayotolewa dhidi ya masheha hao,” alisema Bimani.

Katika uchaguzi wa 2001 CUF ilipinga matokeo ya urais Zanzibar na wananchi kuingia barabarani jambo ambalo lilisababisha vifo vya askari mmoja na raia zaidi ya 30.

Tuesday, July 21, 2009

Lwakatare amejimaliza kisiasa; Dk. Bana

Salim Said
KWA miaka mingi watanzania wamekuwa wakishuhudia wanachama na viongozi kutoka vyama vya upinzani wakihamia chama tawala cha Mapinduzi (CCM), lakini upepo wa kisiasa umeanza kubadilika kwa viongozi upinzani kutoka chama kimoja cha upinzani kwenda kingine cha upinzani.

Kwa mara ya kwanza watanzania wameshudia kiongozi mmoja wa ngazi za juu kutoka chama cha upinzani akikihama chama chake na kuhamia chama kingine cha upinzani.

Si mwengine huyu bali ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara Wilfred Lwakatare, ambaye amajiunga rasmi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), sababu kubwa ikiwa ni kukosa nafasi yake baada ya mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika ndani ya chama hicho Machi mwaka huu.

Kwa mujibu wa Lwakatare, ameamua kuhama CUF kutokana na tabia ya majungu, roho mbaya, unafiki, fitna na mtima nyongo walizonazo baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho na kumsababishia kuukosa nafasi yake.

“Jina langu liliachwa katika kutetea nafasi yangu ya unaibu Katibu Mkuu wa chama kwa sababu ya viongozi wa CUF kusikiliza na kuamini majungu na fitna kutoka kwa baadhi ya viongozi, kwamba mimi ni mbadhirifu wa fedha za chama,” anasema Lwakatare.

Lakini kuhama kwa Lwakatare ndani ya chama chake cha CUF kunachukuliwaje na wananchi, wasomi na wanasiasa?

Baadhi ya wadau wa masuala ya kisiasa wanaona kwamba nguvu ya upinzani imeanza kupoteza mwelekeo wa kisiasa.

Kwa mtazamo wa chama cha NCCR-Mageuzi wanaona kuwa, Lwakatare kwenda Chadema, ni hujuma na ufisadi wa kisiasa ambapo chama hicho kinatumia ubaguzi kuiba viongozi wa vyama vingine vya upinzani kwa lengo la kuudhoofisha.

Dk. Benson Bana, ni Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Siasa cha Chuo kikuu cha Dar es Salaam, anasema kwa alivyomsikiliza Mwenyekiti wa CUF taifa Profesa Ibrahim Lipumba, sababu za kumuacha Lwakatare hajazitaja na kwamba kuna sababu nyingine za kumuacha kigogo huyo Naibu Katibu Mkuu huyo wa zamani.

“Kumuacha mtu kwa sababu eti akiwa Naibu Katibu Mkuu anakosa muda wa kuimarisha chama si kweli. Ni tofauti akiingia kiongozi jimboni kwake kama Naibu Katibu Mkuu na akiingia kama mwanachama wa kawaida. Mbona tuna Mawaziri wa CCM, lakini wanafanya kazi ya kuimarisha chama vizuri tu,” anasema Dk. Bana.

Dk. Bana anakiri kuwa, Chadema ni chama namba moja cha upinzani kwa upande wa Tanzania bara, lakini pia anikiri kuwa haina nguvu kubwa kuliko CUF katika Wilaya ya Bukoba.

“Chadema ni chama chenye nguvu sana Tanzania bara kwa sababu kina wanachama wengi na hata wabunge wake ni imara sana,” anasema Dk. Bana.

Anafafanua kwamba, Lwakatare amebeba hatari ya kisiasa (Political risk) mgongoni mwake kwa kuwa ni vigumu sana kile ambacho kilimfanya ahame CUF kukipata ndani ya Chadema.

“Kwanza Lwakatare si mwanasiasa makini, huwezi kumlinganisha na maalim Seif Sharif au Juma Duni hawa wana akili sana na pia ni hazina katika siasa za Tanzania. Ni kweli CUF imeathirika lakini hata hivyo pengo aliloliacha si kubwa sana kama anavyodhani mwenyewe,” anasema Dk. Bana.

Anasema, Chadema haiwezi kumuondoa Zitto Kabwe na kumuweka Lwakatare na kwa kugombea ubunge kupitia Chadema hawezi kushinda kwa sababu tayari kura zake ameshazigawa, waumini wake lazima watagawika kwani wapo watakaomfuata na wapo watakaobakia CUF.

“Si dhani kama anaweza kupata nafasi ya juu kama aliyokuwanayo CUF ingawa pia sijui aliahidiwa nini mpaka akashawishika kuhama chama chake na kuingia Chadema,” anasema Dk. Bana.

Dk. Bana anasema, Lwakatare anakabiliwa na upinzani mkubwa wa mbunge wa Bukoba Mjini Hamisi Kagasheki, ambaye tayari amejiimarisha vya kutosha jimboni humo.

“Kagasheki ana nguvu sana Bukoba, amejimarisha vya kutosha, amesaidia kuboresha hospitali, ameimarisha shule za sekondari na ameafanikiwa kuanzisha kituo chake cha redio, jambo ambalo limemrahisishia kuwafikia watu wengi na kwa muda mfupi, ili kuwauzia sera zake,” anaeleza hali ngumu inayomkabili Lwakatare.

Anasema, kwa miaka mitano aliyokaa madarakani mbunge Kagasheki, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amefanikiwa kuwafanya wananchi wa Bukoba Mjini kutokuwa na usongo naye na anaingia katika uchaguzi 2010 akiwa anajiamini.

Dk. Bana ambaye pia ni mwenyeji wa Bukoba anasema, Lwakatare ana mambo mingi ya kujifunza kwa sababu wananchi wake hawamchagui mtu kama yeye, bali wanaangalia sera, ilani, msimamo na itikadi ya chama cha mgombea wao.

“Watu wa Bukoba wanaelewa vizuri siasa, naweza kuwafananisha na wazanzibari hasa wa kisiwa cha Pemba, wao si bendera kwamba wanafuata upepo tu. Si dhani kama Lwakatare alifanya utafiti na kujitathmini kabla ya kuchukua uamuzi wa kuhama CUF. Na hata kama angesimama kama mgombea binafsi yeye si Nabii jimboni kwake kwamba anapendwa sana,” ansema.

Dk. Bana ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa kitaaluma, anaweka hadharani sababu za msingi zilizomfanya Lwakatare kujitoa katika chama cha CUF.

“Unajua Naibu Katibu Mkuu ni nafasi ya mshahara, marupurupu, usafiri na baadhi ya wakati hata nyumba unapewa, lakini wanasiasa wengi wanategemea kazi yao ya siasa kama chanzo cha kujipatia fedha. Hivyo baada ya kuikosa ndio kashindwa kuvumilia,” anasema Dk Bana.

Anasema, jambo baya zaidi kwa Lwakatare ni kuchukua maamuzi haraka tena ndani ya muda mfupi tu tangu kukosa unaibu Katibu Mkuu, jambo ambalo hata mtoto anaanza kuhoji uvumilivu wake na kujua kwamba ametoka katika chama kwa kukosa cheo, mengine yakiwa ni visingizio tu.

“Kimsingi Lwakatare hajatoka ndani ya chama kwa kujenga chama, bali ametoka ndani ya chama kwa maslahi yake binafsi, baada ya kukosa mshahara na marupurupu,” anasema Dk Bana.

Anasema, kwa kawaida mwanasiasa yeyote huingia au kukihama chama kwa mambo manne tu, ambayo ni sera, msimamo wa chama, ilani na Itikadi, “sasa sina uhakika kwamba sera, itikadi, ilani na msimamo wa CUF umebadilika au Chadema wameiba vitu hivyo kutoka CUF na yeye akaona kwamba amepata chama mbadala chenye sera zinazolingana na cha kwake?”

Dk. Bana ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam katika Fani za Sayansi za Siasa, anaelezea madhara ya uamuzi wa mbunge huyo wa zamani wa jimbo la Bukoba Mjini na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kupitia CUF.

“Hii ni sifa mbaya sana katika jamii kiongozi kuhama chama kwa kukosa madaraka, utahama na kuhamia vyama mara ngapi? Kwa sababu usidhanie kuwa utakuwa kiongozi mkubwa milele katika chama. Jamii inaweza kumtafsiri kuwa ni mlafi wa madaraka na fedha kwa kufanya maamuzi hayo baada ya kukosa madaraka na mshahara,” anasema.

Anaongeza kuwa, wanasiasa makini watamdharau na kumtoa thamani sana kutokana na maamuzi yake, kwa kuwa siasa si ajira bali ni kazi ya kuutumikia umma ili ujijengee jina.

“Ni jambo baya sana kwa kiongozi kuyumbishwa kidogo akaonesha udhaifu wa kuyumbika. Si vizuri hata kidogo, unatakiwa kuwa na msimamo na kusimamia kile unachokiamini siku zote. Lakini anaanza kukosa uvumilivu hata jamii inajua, kwa kweli amejimaliza na kujiharibia kisiasa,” anasema.

Dk. Bana anasema, Lwakatare amejimaliza kwa sababu amesafisha njia na kumtengenezea mpinzani wake CCM ajenda ya kuiuza kwa wananchi wa jimbo hilo katika kampeni za uchaguzi mkuu wa 2010.

CCM watawambia wapigakura, ‘Sisi tunahitaji viongozi makini, wenye msimamo na wavumilivu katika siasa na matatizo, sasa mwangalieni Lwakatare ana uvumilivu, msimamo na umakini gani? Anahangaika tu katika vyama kwa kukosa madaraka’ “hii ni ajenda tayari imeshanunuliwa na Kagasheki mbunge wa Bukoba Mjini CCM,” anasema.

Anasema, Lwakatare amezidi kudhoofisha nguvu ya upinzani kwa sababu, “awali tulikuwa tunaona wapinzani wanahama na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM), lakini upepo umebadilika na sasa wanaanza kuzunguka humohumo, hii ni ishara mbaya kwa kambi ya upinzani,” anasema Dk. Bana.

Anasema, Upizani wa Tanzania haujui kufaya kazi ya siasa kwa kuwa wameingia katika mtego wa CCM, imefanikiwa kujenga mtandao kuanzia ngazi ya Jamii Msingi (grass root) hadi taifa, na sio kutembea na Helicopter tu wakati wa kampeni za uchaguzi.

“Kutembea na helicopter katika uchaguzi si kuimarisha chama. Nawashauri wapinzani wawe na mpango mkakati wa kuimarisha vyama vyao kama kweli wana nia na utashi wa kisiasa wa kupambana na CCM. Walete mambo ambayo hayajaletwa na CCM,” anasema.

Kwa upande wake, Profesa Lipumba anasema, taarifa za kuhama kwa Lwakatare zimewasikitisha sana kwa sababu hawakutegemea kutokana na ukweli kwamba mtu kukosa cheo ndani ya chama haijawa sababu ya kumfanya ahame.

Monday, July 20, 2009

ZEC: Wawakilishi walitafsiri vibaya Katiba ya Zanzibar

Salim Said
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema, baraza la Wawakilishi la Zanzibar limetafsiri vibaya Katiba ya Zanzibar katika kutunga sheria namba 7 ya uchaguzi ya mwaka 1984 toleo la mwaka 2004.

Sheria hiyo ambayo imetungwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2003, inapingana na sheria ya Uchguzi ya Zanzibar ya mwaka 2004 katika kufafanua sifa za mzanzibari anayepaswa kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Tatizo hilo limesababisha mkanganyiko mkubwa katika zoezi zima la uandaaji na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapikura, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wazanzibari kukosa haki zao za kupigakura katika chaguzi mbalimbali visiwani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo namba moja cha uandikishaji wa daftari hilo jimbo la Konde kisiwani Pemba, Mkuugenzi wa ZEC Salim Kassim, alisema licha ya kuwa katiba ya Zanzibar iko juu lakini mzanzibari anaweza kukosa haki ya kupiga kura kutokana na sheria ya uchaguzi.

“Sheria au katiba inaweza kumnyima mtu haki ya kupiga kura bila kujali kwa ni ipi iliyo juu au hdhi zaidi kati ya hivyo,” alisema Kassim.

Alisema, tatizo hilo limesababishwa na Baraza la Wawakilishi kuitafsiri vibaya katiba ya Zanzibar wakati wa kutunga sheria namba 7 ya uchguzi.

“Ni kweli baraza la wawakilishi limetafsiri vibaya katiba ya Zanzibar na ndio maana kuna malalamiko ya hapa na pale katika zoezi hili, lakini hebu jaalia kama vifungu vyote vya sheria vingekwa vimekosewa tungefanyaje kazi? Kwa hiyo tunafanya tu licha ya kuwa kuna hizo kasoro katika tafsiri” alisema Kassim huku akionesha kitabu cha sheria hiyo.

Baaadhi ya wananchi visiwani humo wamekuwa wakilalamika kunyimwa haki zao za kuandikishwa katika daftari hilo kwa kukosa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Lakini Kifungu namba 7 (1) cha Katiba ya Zanzibar kinasema, kila mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka 18 anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa Zanzibar na kwamba haki hiyo itatumiwa kwa kufuata masharti ya kifungu cha pili cha kifungu hiki pamoja na masharti mingine ya katiba hii na ya sheria ya uchaguzi inayotumika Zanzibar.

Kwa mujibu wa katiba hiyo hiyo kifungu kidogo cha pili, baraza la wawakilishi laweza kutunga sheria na kuweka masharti ya kumzuia mzanzibari asitumie haki ya kupiga kura kutoka na oyote kati ya sababu zifuatazo.

“Kuwa na uraia wa uraia nchi mbili, kuwa na ugonjwa uliothibitishwa na mahakama kuu, kutiwa hatiani na kuendelea kutumikia adhabu kwa kosa la jinai isipokua aliewekwa rumande anaweza kuandikshwa,” inaeleza katiba hiyo na kuongeza.

“Kukosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpiga kura.”

Hata hivyo baadhi ya wananchi wameilalamikia sheria kumzuia mtu kuandikishwa kwa sababu ya kukosa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi wakati katiba ikitak kitambulisho cha uraia.

Wakati katiba ikieleza hayo, sheria namba 7 ya Uchaguzi inapingana na katiba kwa kusema, hakuna mtu ataeandikishwa kuwa mpiga kura ila awe ametimiza masharti ya uandikishaji kama yalivoelezwa katika kifungu cha 7(2) cha katiba, ameonesha kitambulisho cha uzanzibari na kwamba hakuna mtu atakaeandikishwa kuwa mpiga kura katika zaidi ya jimbo au eneo moja la uchaguzi.

Kassim alisema, hawapokei vyeti vya kuzaliwa kama kigezo cha mtu kuandikishwa kwa sababu hata hicho kitambulisho cha ukaazi hakitolewi bila ya kuonesha cheti cha kuzaliwa.

Hata hivyo baadhi ya watu walithibitisha kupata vitambulisho vya ukazi bila ya vyeti vya kuzaliwa na wengine kuonesha vyeti vya kuzaliwa na kunyimwa vitambulisho vya ukaazi.

Aidha, Kassim alisema kati ya wapigakura 8947 walioandikishwa katika Jimbo la Konde mwaka 2005 hadi sasa awamu ya kwanza inaisha wameandikisha watu 582 ambao ni pungufu ya watu 3000.

Kwa mujibu wa Kassim awamu za uboreshaji wa daftari hilo zilipangwa kuwa tatu, lakini kwa sasa zitafanyika mbili tu kwa sababu moja imekufa kutokana na uchaguzi mdogo wa Magogoni uliofanyika mwezi uliopita.

Muhene Said Rashid ni Katibu wa Uchaguzi wa Chama cha Wananchi (CUF) anathibitisha kupokea malamiko ya watu 508 walionyimwa kuandikishwa kwa sababu ya kukosa kitambulisho cha ukaazi.

“Leo ikiwa ni siku ya mwisho katika shehia hizi sita tayari tumepokea malalamiko ya watu 508 kutoandikishw kwa sababu hawana vitambulisho vya uzanzibari mkaazi,” alisema Rashid na kuongeza.

“Cha ajabu kuna mkanganyiko mkubwa kati ya sheria ya uchaguzi na katiba ya Zanzibar . Sheria inapingana na katiba ya Zanzibar jambo ambalo linasababisha wananchi wengi kukosa haki zao za msingi.”

Zoezi hili limekamilika jana katika shehia sita za jimbo la Konde wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba na leo linaendelea katika shehia nyengine za jimbo la Mgogoni kisiwani hapa.

Hofu yatanda kisiwani Pemba

Salim Said, aliyekuwa Pemba
MWELEKEO wa hali ya kisiasa katika kisiwa cha Pemba ni mbaya kufuatia kuanza kwa awamu ya kwanza ya zoezi la uboreshaji wa Dafati la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) Julai 6 mwaka huu katika Wilaya ya Micheweni kwa kuwaacha bila ya kuwaandikisha baadhi ya wakazi wa kisiwa hicho kwa kutokuwa na vitambulisho vya ukazi.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa wiki nzima iliyopita umeonyesha kuwa wananchi kisiwani humo hususan katika mkoa wa Kaskazini karibu obo yao wamekataliwa kujiandikisha hali inayowasababishia hofu kubwa ya kunyimwa haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2010.

Awamu ya kwanza ya uboreshaji wa DKWK kisiwani humo imeanza vibaya kufuatia maelfu ya wananchi kukataliwa kusajiliwa katika daftari hilo, huku awamu ya pili na ya mwisho kabla ya uchaguzi mkuu ikitarajiwa kuanza Januari 2010.

Mwanachi ilishuhudia maelfu ya watu waliokataliwa kusajiliwa katika DKWK kwenye vituo 12 vya uboreshaji wa daftari hilo katika majimbo ya Konde na Mgogoni Wilaya ya Micheweni kisiwani humo.

Abdallah Haji ni Wakala wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) katika kituo cha Mgogoni alisema, zoezi hilo ni gumu na kwamba hali ni mbaya sana kwa sababu maelfu ya wananchi wenye sifa wanakataliwa kujiandikisha katika DKWK kila siku.

Hali hiyo ya watu wengi kukataliwa, imesababisha watu kujikusanya katika vikundi vidogovidogo kujadili hatma yao, jambo linalosababisha hofu ya kutokea vurugu na hivyo kuwafanya askari wa vikosi vya kutuliza ghasia (FFU) kuzunguka zunguka kwenye magari yao (Defender) na kupeperusha bendera nyekundu kuashiria hali ya hatari.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umegundua kuwa, kituo kimoja cha kujiandikisha kisiwani hapa hulindwa na kati ya askari 10 hadi 15 wenye silaha na wachache wasio na silaha ambao hukaa sehemu za wazi na wengine kujificha kwenye vichaka vilivyozunguka kituo husika.

Askari hao ni pamoja na FFU, usalama wa raia, askari wa usalama barabarani na vikosi mbalimbali vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (KVZ) maafisa wa usalama wa taifa.

Utafiti unaonesha kwa, vyombo vya dola hufanya kazi ambazo sio zao ikiwa ni pamoja kuwaondosha watu katika mistari kwa madai hawana Zan ID au kadi ya mpigakura ya 2005, kuwakataza masheha wa Shehia kuzungumza na waandishi wa habari na kukaa na silaha ndani au mita chache kutoka katika kituo cha uandikishaji.

“Cha ajabu ni kwamba, mwandishi wa habari haruhusiwi kuingia katika kituo, pia hatakiwi kuhojiana na wananchi bila ya kuwa na kitambulisho cha ZEC au akae mita 200 kutoka kituoni, lakini kwa nini askari mwenye silaha anaingia kituoni. Hii ni demokrasia,” alihoji Mwandishi mmoja.

Alisema, lengo la ZEC kuweka masharti hayo ni katika kubana uhuru wa habari, ili yale waliyoyapanga kuyafanya yafanikiwe vizuri, huku wananchi, mashirika ya haki za binadamu na mashirika ya kimataifa yasipate taarifa yoyote.

Salim Hamad Mwijaa ni Afisa wa Usalama wa Taifa kutoka Wilaya ya Michweni, aliomba msaada kutoka kwa mabosi wake baada ya waandishi wa habari kuanza kuchukua malalamiko kutoka kwa wananchi katika kituo cha Mgogoni.

“Naona bosi hapatikani kwenye simu zake zote mbili, naomba msaada wenu kwa sababu hapa kuna watu hawana vitambulisho vya ZEC na wanachukua maelezo kwa wananchi hali imebadilika na imekuwa ya vurugu. Naomba msaada haraka,” alisema Mwijaa.

Baada ya muda mfupi lilitokea gari la polisi (Defender) likiwa na askari wa FFU waliobeba silaha za moto na kupeperusha bendera nyekundu lakini bila ya hata kusimama na kufanya chochote lilizunguka katika uwanja wa kituo hicho na kurudia lilikotoka.

Aidha, Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (Zan ID), kadi ya mpiga kura katika uchaguzi uliopita vinatumika kuwakwamisha wananchi kuandikishwa katika daftari hilo.

Pia Masheha wamekuwa wakitumika kukwamisha zoezi la uboreshajiwa Daftari hilo kwa kutotoa fomu za kuombea Zan ID na barua za wananchi kupotelewa na mali zao ili kwenda polisi kwa msaada zaidi.

Mashehao ambao ni watendaji wa chini katika mtiririko wa uongozi wa SMZ huteuliwa na kuapishwa na Wakuu wa Mikoa, huamua kufunga ofisi zao bila ya kuweka msaidizi wanapotumiwa na ZEC kwa uwakala.

Khatib Hassan (27) mkaazi wa Wingwi Mjananza aliesema, kila anapofika kwa Sheha kutaka huduma huambiwa yuko katika uboreshaji wa DKWK na akimfuata jioni hujibiwa na Sheha huyo kwamba bendera imeshushwa na muda wa kazi umeisha.

“Mchana haonekani anakuwa ni mfanyakazi wa tume, lakini ukimfuata jioni anasema, bendera imeshushwa na muda wake wa kufanya kazi umeisha hivya mpaka siku ya pili na siku ya pili ukienda majibu ni hay ohayo,” alisema Hassan.

Sambamba na hilo la kufungwa kwa ofisi nyingi za Masheha, pia wapo baadhi ya Masheha wanaowatangazia wananchi kuwa serikali imesitisha utoaji wa fomu za kuombea Zan ID na hata Vitambulisho vyenyewe vya Mzanzibari Mkaazi hadi hapo awamu ya kwanza ya zoezi hilo itakapomalizika.

Hata hivyo Mkurugenzi wa ZEC Salim Kassim na Mkurugenzi wa Idara ya Zan ID Mohammed Ame walikataa malalamiko hayo lakini Ame alisema atafuatilia ili kujua ukweli wa hali hiyo.

Maafisa Usalama wawatimua wananchi katika vituo vya uandikishaji

Salim Said, Pemba
ZOEZI la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Jimbo la Mgogoni Wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba limeingia dosari katika siku yake ya kwanza, baada ya maamia ya wananchi kutimuliwa katika baadhi ya vituo vya uandikishaji na maafisa Usalama na hivyo kukosa kujiandikisha.

Wananchi hao kutoka vituo vya Kinyasini, Finya na Wingwi Mapofu waliofika katika vituo hivyo na kupanga foleni mapema jana asubuhi, walijikuta wakitimuliwa vituoni na maafisa hao kwa kuwa hawana vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (Zan Id).

Maafisa hao waliwambia wananchi hao kwamba hawapaswi kuonekana katika vituo hivyo kwa sababu hawana Zan ID.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa hasira huku wakionekana kuchoka nje ya baadhi ya vituo, baadhi ya wananchi walisema maofisa wa usalama waliokuwa wamekaa karibu na maeneo hayo waliwataka waondoke mara moja vituoni hapo.

Katika kituo cha Wingwi Mapofu walionekana maofisa wa usalama waliokuwa wamekaa katika baraza za jengo la kituo hcho wakitoa maelekezo kwa watendaji wa tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

“Ukifika pale kituoni unaambiwa uondoke na maafisa usalama kwa sababu huna Zan ID, hii ni haki kweli? Mimi nina cheti cha kuzaliwa, kipande cha kupigia ktika uchaguzi mkuu wa 2005, na uchaguzi mdogo wa mwaka 2003 (kura za maruhani),” alisema Khatib Hassan (27).

Hassan alilalamika kuwa, anapokwenda kwa Sheha ambaye anapaswa kutoa fomu za kuombea Zan ID anaambiwa aende Wilayani na akifika Wilayani hutakiwa kurudi kwa sheha.

”Ukieda kwa Sheha anakwambia nenda Wilayani na ukienda Wilayani unaambiwa nenda kwa Sheha. Wametufanya kama mpira wa kona Sheha apiga chenga wilaya yafunga goli. Wanatunyima haki zetu hivi hivi,” alilalamika Hassan.

Naye Mbarouk Rubea (48) alisema, ana sifa zote za kuandikishwa kuwa mpigakura kwa mujibu wa katiba ya zanzibar lakini hadi sasa anahangaishwa hajapata kitambulisho na hatimaye amenyimwa kujiandikisha katika daftari hilo.

Akiwa amesawajika na mtoto mgongoni Rehema Khamis (32) alisema, ameanza kukata tamaa ya kupiga kura katika uchaguzi ujao kwa sababu hajapatiwa kitambulisho hadi licha ya kuwa ameshalipa sh 500 za Zan ID.

”Hivi sasa nakaribia kulia mana nimeacha kwenda kuvuna mpunga wangu nikaamua kuja huku lakini nahangaishwa tu na mtoto mgongoni. Nanyimwa haki yangu na maofisa wa usalama wanatufukuza hapa,” alisema Rehema.

Hata hivyo, maofisa wa usalama waliokuwa vituoni hapo na kutuhumiwa kuwatimuwa wananchi wasiokuwa na Zan ID walikataa kuzungumza na waandishi wa habari na kuwapiga marufuku watendaji wa tume kufanya hivyo.

Sheha wa Shehia ya Mjananza Hamad Said, ambaye pia ni wakala wa ZEC alikatazwa na maafisa wa Usalama kuzungumza na waandishi wa habari waliofika kituoni hapo.

Waandishi waliwaomba mmoja wa askari wa usalama wa raia waliokuwapo kituoni hapo kumuita sheha huyo ili kuzungumza naye, lakini alipotoka na kusalamiana na waandishi ghafla aliitwa na maofisa wa usalama na kuagizwa kutozungumza na waandishi hao.

”Nimekatazwa na wale pale nisiongee na ninyi,” alisema Said huku akiwaandalia maofisa hao na kuingia katika kituo cha uandikishaji.

Aidha katika vituo hivyo, vilikuwa na ulinzi mkali wa dola wakiwamo askari polisi wa usalama wa raia, askari wa kutuliza ghasia wenye silaha (FFU), askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanibar (SMZ) na usalama wa taifa.

Mwananchi ilibaini kuwa, wananchi wengi kisiwani Pemba hawana Zan ID hususan wale waliotimiza miak 18 na wale waliokuwa nje ya zanzibar kwa muda kidogo.

Hiyo ni kutokana na sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kuagiza kwamba mtu yeyote hapaswi kupewa kitambulisho cha ukaazi bila ya kufikia umri wa miaka 18.

Aidha, Mwananchi ilishuhudia mamia ya wananchi wakiondoka katika vituo huku wakilalamikia maafisa wa tume ya uchaguzi, serikali na Chama cha Mapinduzi kwa kuwanyima haki zao.

”Hivi kwani hawa watu wa tume ya uchaguzi wamekuja kufanya nini hapa, mana kama ni kuandikisha hawatuandikishi,” alihoji bwana mmoja kwa hasira.

Katika vituo vitatu ambavyo waandishi walitembelea, waligundua mamia ya wananchi kunyimwa haki hiyo kwa kukosa Zan ID huku wakiwa wamekaa katika vikundi vidogo vidogo ili kujadiliana.

Mwnyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Micheweni Abdallah Ali Said alithibitisha kupokea malalamiko hayo katika siku ya kwanza ya zoezi hilo kwenye jimbo la Mgogoni kisiwani hapa.

Masheha wakwamisha daftari la wapigakura

Salim Said, Pemba
MASHEHA wa Shehia za Wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba wameshutumiwa kukwamisha awamu ya kwanza ya zoezi zima la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika wilaya hiyo, kwa kuwanyima wananchi huduma katika ofisi zao.

Masheha ambao pia ni mawakala wa ZEC ni watendaji wa serikali katika ngazi ya Shehia ambayo ndio ngazi za chini kiutawala katika Serikali ya Zanzibar (SMZ) kwa kawaida huteuliwa na kuapishwa Wakuu wa Mikoa pindi wanapoteuliwa na rais baada kuingia madarakani.

Aidha malalamiko dhidi ya Masheha yalijitokeza katika vituo vyote sita vya vya jimbo la Mgogoni na baadhi ya shehia za jmbo la Konde Wilaya ya Micheweni kisiwani hapa.

Malalamiko hayo, ni ya kutowapatia wananchi fomu za kupatia vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (Zan ID), fomu za uthibitisho wa kukataliwa kuandikishwa katika daftari hilo (2KK) na barua za kuthibitisha kupotelewa na vitambulisho vyao.

Kwa mujibu wa sheria ya Zanzibar mtu yeyote anayepotelewa na mali yake hupaswa kuripoti Polisi ambapo Polisi huwa haitoi barua hadi mlalamikaji huyo anapopata barua ya Sheha kuthibitisha kuwa aliyepotelewa ni mkaazi wa eneo lake.

Wakizungumza na Waandishi nje ya vituo tofauti vya kuandikishia wapiga kura, baadhi ya wananchi walisema Masheha ndio kikwazo kikubwa cha zoezi hilo .

Said Salim (22) wa Shehia ya Mgogoni alisema, tangu mwaka 2005 amekuwa akienda kwa Sheha kuomba fomu ya kombea Zan ID lakini hadi hii leo hajapata fomu hiyo.

“Mwaka 2005 nilienda kwa Sheha kuomba fomu akaniambia sipati, nikakaa mwaka jana nilienda tena akaniambia sipati, nikampelekea na hata cheti cha kuzaliwa lakini hadi hivi sasa ninavyozungumza sijapatiwa fomu hiyo,” alisema Salim na kuongeza.

“Sisi tunaenda vituoni tunakataliwa kujiandikisha lakini hatuwezi kwenda mahakamani kwa sababu hatuna ushahidi na ili tuwe na ushahidi ni lazima tupate fomu za 2KK ambazo masheha wamegoma kabisa kutupatia. Huu ni mkakati.”

Khatib Haasan (27), wa kituo cha Wingwi Mapofu alisema wamekuwa wakizungushwa kati ya ofisi ya sheha na Ofisi ya Vitambulisho wakati wa kutafuta fomu za kuombea Zan ID.

”Mimi nina cheti cha kuzaliwa, kipande cha kupigia ktika uchaguzi mkuu wa 2005, na uchaguzi mdogo wa mwaka 2003 lakini hadi sasa sijapewa Zan ID licha ya kufanya juhudi kubwa kukitafuta,” alisema Hassan.

Baadhi ya Masheha walioingizwa moja kwa moja katika tuhuma hizo ni Omar Khamis Faki (Kifundi), Said Hamad Ali (Mjananza), Mohammed Omar (Konde) na Said Hamad Khamis (Mgogoni).

Lakini waandishi wa habari walishindwa kuzungumza na masheha hao kutokana na Maafisa wa Usalama wa Taifa kuwakataza watendaji hao wa SMZ kuzungumza na mwandishi yeyote.

“Mimi nimekatazwa na mabosi wangu kuzungumza chochote na mtu nisiyemjua,” alisema Khamis ambaye ni Sheha wa Mgogoni baada ya kuashiriwa kuingia ndani ya kituo na Afisa wa Usalama aliyekuwapo.

Kwa mujibu wa wananchi wanapofika kwa Sheha ofisi huwa imefungwa wakati wa mchana na wakienda jioni au usiku huwajubu kuwa bendera imeshushwa kwenye mlingoti na muda wa kazi umeisha.

Mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Salim Hamad Mwijaa alisema kuwa yeye ni Afisa wa Usalama wa Taifa kutoka ofisa ya Wilaya ya Micheweni alimkataza sheha wa Mgogoni kuzungumza na waandishi.

“Haloo, mbona namba ya bosi siipati? Maana hapa kumekuja watu hawana vitambulisho vya tume na wanachukua maelezo kutoka kwa wananchi hapa. Tunaomba msaada wenu,” alisikika Afisa huyo wa usalama akiongea kwa nji ya simu.

Aidha baada ya muda mfupi sana lilitokea Gari la Polisi aina ya Difender huku likipeperusha bendera nyekundu juu na askari wa kutuliza ghasia wenye silaha na kuzunguka katika uwanja wa mpira wa kituo cha Mgogoni na kurudi lilikotokea.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Salim Kassim alithibitisha kupokea malalamiko ya Masheha kutotoa barua na fomu hizo na kuongeza kwamba jambo hilo linakoroga kazi ya uboreshaji wa daftari hilo katika awamu ya kwanza.

”Masheha wantukoroga hasa sheha wa Kifundi kwa sababu hawatoi fomu za Zan ID na barua za kwa wananchi waliopotelewa na vitambulisho vyao,” alisema Kassim na kuahidi kulifuatilia tatizo hilo.

Kassim pia alisema, jambo hilo la kufuatilia ukorofi wa masheha ni msaada wao wanaoutoa kwa wananchi hao kwa sababu ZEC wala yeye hatoi vitambulisho vya ukaazi.

”Sisi ni msaada tu huu lakini ZEC wala mimi sitoi Zan ID wanaohusika ni serikali yaani ofisi ya vitambulisho,” alisema Kassim.

Baadhi ya Wananchi walijaza fomu za vitambulisho na kulipia ada ya sh500 na kupatiwa stakabadhi zao lakini hadi sasa hawajapatiwa vitambulisho hivyo kwa sababu tofauti zinazotolewa na ofisi ya Zan ID wilaya ya Micheweni.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Abdallah Ali Said alithibitisha kuwepo kwa hali hiyo ambapo pia aliwaonesha waandishi wa habari stakabadhi kadhaa za watu waliolipa mwaka 2005 na 2006 lakini hadi sasa hawajapatiwa Zan ID.

“Unaona hawa ni watu 10 katika Shehia ya Wingwi Mjananza wamelipia ada ya Zan ID tangu mwaka 2005 na 2006 lakini hadi hii leo hawajapatiwa vitambulisho. Wanazungushwa tu wakienda wialyani wanarudishwa kwa sheha na sheha hatoi vitambulisho. Nimejaribu kuwasiliana na Mkuu wa Mkoa na Kaskazini na Mkuu wa Wilaya ya Micheweni lakini hakuna jibu,” alisema Said.

Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Vitambulisho wilaya ya Micheweni Hamad Shamata alikataa kujibu tuhuma hizo kwa madai kwamba kuna maelekezo maalumu waliyopewa.

“Aaah.. sisi tuna maelekezo maalumu tuliyopewa naa... naa….,” alisita kidogo na kuongeza: ” Kama ninyi ni waandishi mtafuteni Mkurugenzi wa Idara ya Zan ID.”

Hata hivyo juhudi za kumpata Mkurugenzi wa Idara ya Zan ID Zanzibar Mohammed Ame hazikufanikiwa baada ya simu yake ya mkononi kutokuwa hewani kila alipopigiwa.

Zaidi ya watu 2500 wamekataliwa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura katika Jimbo la Konde na Mgogoni wilaya ya Micheweni kisiwani hapa kwa sababu ya kukosa Zan ID. Zoezi hili linaingia katika siku ya tatu leo katika Jimbo la Mgogoni baada ya kukamilika katika jimbo la Konde hapo juzi.

Hali tete kisiwani Pemba

Salim Said, Pemba
ZOEZI la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura katika Wilaya ya Micheweni limezidi kuzorota katika siku yake ya tisa jana, baada ya baadhi ya wananchi kukataliwa kuandikishwa katika daftari hilo licha ya kuonesha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (Zan ID).
Wananchi hao ambao wengi wao wana Zan ID lakini hawana kadi ya mpiga kura ya mwaka 2005 wameonekana katika vituo mbalimbali vya uandikishaji wa daftari hilo kisiwani Pemba .

Awali kikwazo kikubwa cha wananchi wengi ilikuwa ni Zan ID lakini, jana watu wengi walishindwa kupata kuandikishwa katika daftari hilo kwa sababu ya kupoteza kadi ya mpiga kura ya mwaka 2005.

Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya vituo mbalimbali vya uandikishaji wananchi hao walisema, imeonekana wazi kuwa kuna mkakati maalum wa kuwanyima haki yao ya kupiga kura.
Salim Khalfan Said (23) mkaazi wa Finya jimbo la Mgogoni alisema, licha ya kuwa na Zan ID lakini amenyimwa kuandikishwa katika daftari hilo .

“Mimi ninayo Zan ID lakini nimekataliwa kujiandikisha kwa sababu sina kadi ya mpiga kura ya mwaka 2005, na hata jina langu hawakutaka kuliangalia katika daftari kwa sababu naamini limo labda walitoe hivi sasa,” alisema Said na kuongeza:

”Mimi kadi yangu ya mpigakura imepotea lakini mwaka 2005 nilipiga kura hapa hadi chumba nilichopigia kura nakikumbuka nilimpigia babu yangu kwanza halafu nikapiga na mimi, leo wanasema sionekani kwenye daftari.”

Said alionesha kitambulisho chake cha Mzanzibari Mkaazi (Zan ID) ambacho kilionesha kuwa kinapitiwa na muda wake miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Salim Kassim alisema, ili mtu aweze kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapigakura ni lazima awe na Zan ID.

“Huwezi kuwa na simu bila ya kuwa na kadi ya simu (line) hivyo huwezi pia kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapigakura kama huna Zan ID,” alisema Kassim.

Kassim alikanusha taarifa za kuwa kuna baadhi ya wananchi wanaandikishwa katika daftari hilo kwa sababu ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) bila ya kuonesha Zan ID kama kigezo kikubwa cha ZEC.

“Habari hizo si za kweli, na naweza kusimama mahali popote kuyasema haya, lakini kama umemuona mtu aliyeandikishwa bila ya Zan ID na kutumia kigezo cha itikadi ya chama chake basi niletee stakabadhi yake,” alisema Kassim na kusisitiza:

“Hizo habari ni za uongo, uzushi na za kupotosha, na nakuomba usiandike habari hizo, hao ni waongo na ukiandika nakwambia nitakushtaki.”

Wakati Kassim akisisitiza hayo Mwananchi ilishuhudia kijana Salim Khalfani (23) akikataliwa kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura katika kituo cha Finya jimbo la Mgogoni licha ya kuonesha Zan ID.

Wakati kijana huyo akikataliwa kuingia katika daftari hilo, kijana mwengine Assaa Ismail Nassor (25) mkaazi wa Mtemani Wingwi alisema, yeye amekataliwa kuingia katika daftari hilo kwa sababu ni mwanacham wa Chama cha Wananchi (CUF), wakati mdogo wake ambaye ni mwanachama wa CCM alikubaliwa bila ya kuwa na Zan ID.

“Mimi nimekataliwa kuingia katika daftari la kudumu la wapiga kura na ninayo kadi ya mwaka 2005, lakini mdogo wangu amekubaliwa wakati hana chochote. Sijui hata kama umri wa miaka 18 ametimiza, lakini kwa sababu yeye ni CCM lakini amekubaliwa,” alisema Nassor.

Aidha Mwananchi ilishuhudia mamia ya wananchi wakiwa wamekaa nje ya vituo katika vikundi vidogo vidogo wakijadiliana baada ya kukataliwa kuingia katika daftari hilo .

Wakati huohuo baadhi ya wazee wamelalamika kuwa kigezo cha kuonesha cheti cha kuzaliwa ili upate Zan ID si sahihi kwa sababu kimelenga kuwakatisha tamaa.

Juma Kombo Ali (56) alisema, “ikiwa mzee kama mimi unanidai kitambulisho wakati barua ya sheha ninayo, unakusudia nini kama si kunikwamisha ili nikate tamaa.”

”Huyo sheha mwenyewe wala baba yake hana cheti cha kuzaliwa kwa sababu vyeti hasa vimeanza baada ya Mapinduzi, lakini cha ajabu wanadai vyeti hivyo,” aliongeza Ali.

Alisema, zaidi ya watu 2000 hawajaandikishwa kwa sababu hawana Zan ID na kuhoji kwamba watapiga wapi kura za kumchagua rais wa Muungano na Wabunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
”Je hawa watapiga wapi kura za Muungano, maana si watanzania hawa wala si wazanzibari, basi tunaiomba serikali iwatafutie nchi iwapeleke kama ni Kenya, Uganda au Marekani kwa Obama huko watapewa haki zao,” alisema.

Awamu hii ya kwanza ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika majimbo ya wilaya ya Micheweni inaendelea huku kukiwa na malalamiko mengi kuhusu watendaji na Mawakala wa ZEC ambao ni pamoja na Masheha.

Masheikh waionya serikali

Salim Said
SIKU moja baada ya serikali kuutua mzigo wa mahakama ya Kadhi kwa Waislaam, viongozi wa dini ya hiyo wamepinga vikali uamuzi huo na kusema kama serikali inaona gharama kutumia fedha kudumisha amani iliyopo, itakuja kutumia fedha hizo kuitafuta amani hiyo baada ya kutoweka.

Akizungumza Bungeni juzi Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema, waislaam ruksa kuanzisha mahalama ya Kadhi lakini kwa sharti iwe nje ya dola na Katiba ya nchi.

Wakizungumza mara baada ya Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Kituo cha Kiislaam (TIC) Magomeni jijini Dar es Salaam jana Masheikh mbalimbali walisema hawakubaliani na kauli hiyo ya Waziri Mkuu kwa sababu bado haijawatendea haki waislaam nchini.

Amir wa Shura ya Maimamu Tanzania Sheikh Mussa Kundecha alisema, kauli ya Waziri Mkuu ni ya kisiasa na kwamba kama serikali inaona gharama ndogo kwa kutumia fedha kulinda na kudumisha amani ya nchi, itakuja kutumia gharama kubwa zaidi kuitafuta baada ya kutoweka.

“Kauli hii bado haijawapatia waislaam majibu sahihi ya hoja yao na ni yakisiasa zaidi, mambo ya kuwambia waislaam haya fanyeni nje ya dola na katiba hatukubaliani nayo. Lakini kwa nini serikali inaona tabu kutumia gharama kudumisha amani? Matokeo yake itakuja kutumia fedha nyingi kutafuta amani baada ya kutoweka,” alisema sheikh Kundecha.

Alisema, msimamo wa waislaam ni kwamba Mahakama ya Kadhi lazima iwepo na ipewe hadhi ya kisheria na kikatiba ikiwa ni pamoja na kusimamiwa na kugharamiwa serikali ya Tanzania.

“Mahakama ya kadhi lazima iwepo na lazima igharamiwe na serikali na ipewe hadhi ya kikatiba na kisheria nchini. Kuinyima hadhi ya kikatiba na kisheria ni sawa na kuikataa,” alisema Sheilh Kundecha na kusisitiza:

“Mambo ya kusema serikali haipingi mahakama ya kadhi lakini iundwe nje ya dola, ni kama mambo mengi ambayo serikali inajidai imeyakubali lakini haijayakubali yakiwamo ya mirathi, talaka na ndoa za kiislaam.”

Alizungumza huku akitoa mifano Sheikh Kundecha alisema, siku zote yanapokuja mambo yanayowahusu waislaam, serikali hufanya ujanja ujanja na ubabaishaji kwa lengo la kuwanyima haki zao.

“Serikali inawajibika kugharamia mahaka ya kadhi kama inavyowajibika kugharamia taasisi za madhehebu au dini nyingine nchini kwa sababu jambo hili linawahusu walipa kodi ya Tanzania na wala si wa nje ya nchi,” alisema.

Alihoji kuwa, kodi za nchi hii zinalipwa na watanzania wote wakiwamo waislaam, wakristo na dini nyingine lakini kwa upande mmoja taasisi zao zigharamiwe na serikali halafu upande mwengine ukataliwe.

“Serikali katika tangazo la wazi kabisa imetangaza kulipa mishahara ya hospitali inayomilikiwa na taasisi ya dini ya CCBRT na imeipandisha hadi kuwa ya mkoa. Si hilo tu bali imetenga eneo na kuahidi kugharamia ujenzi ili kuipanua, kwa nini waislaamu wasigharamiwe vya kwao,” alihoji sheikh Kundecha.

“Kuna memorandum of understanding na ubalozi wa Holy Sea wala si wa Vatican, vyote hivi vinagharamiwa na serikali. Wakrsto wana vingapi vinagharamiwa na serikali? Halafu inaonekana upande mmoja unafanya kazi zaidi kuliko mwengine kumbe wanagharamiwa,” aliongeza.

Alisema, msimamo wa waislaam mahakama ya kadhi iwepo na serikali isimamie na kugharamia ila uteuzi wa kadhi na utendaji wa mahaka hiyo liwe jukumu la waislaam.

Naye Imamu wa Msikiti wa Riyaadha wa Mjini Arusha sheikh Shaaban Juma alisema, serikali ya Tanzania ni serikali ya amani hivyo inapaswa kuhakikisha kuwa amani hiyo inaendelea kwa kuwapa waislaam haki yao.

“Tangu rais wa kwanza, wa pili, wa tatu na huyu wa nne tunadai mahakama ya kadhi hatujaipata, hivyo tukinyimwa tutakasirika sisi na tukikasirika amani itatoweka,” alisema sheikh Juma na kuhoji:

“Hivi hii serikali ya amani imeichoka hii amani? Kutunyima mahakama ya kadhi kwa kutumia lugha za ubabaishaji kama hii ya Pinda ni sawa kutudhulumu, ukiibiwa fedha umedhulumiwa na ukinyimwa haki yako ya kidini pia umedhulumiwa na Allah awalaani wote wanaoendesha dhulma hii,” aliongeza sheikh Juma huku waislaam wakimjibu, “aammiiin.”

Kwa upande wake sheikh Hussein Hashim kutoka Tanga alisema, kauli ya Pinda ni ya ubabaishaji lakini waislaam hawatokubali tena kubabaishwa.

“Mahakama ya kadhi lazima iwepo na tena iwe chini ya dola,” alisema sheikh Hashim huku akinukuu baadhi ya aya za Kur-an na Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W) kukazia hoja yake.
Mwisho.

Mbunge: ZEC yaanza kutupunguzia kura zetu za urais Pemba

Salim Said, aliyekuwa Pemba
MBUNGE viti maalum Wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba (CUF), Mgeni Jadi Kadika amesema, vikwazo wanavyowekewa wananchi katika shughuli ya kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura (DKW) kisiwani hapa ni mkakati wa ZEC wa kupunguza kura za wapinzani katika uchaguzi mkuu wa 2010.


Shughuli hiyo, ilianza Julai 6, mwaka huu katika awamu ya kwanza na watu 7,000 wamekatalwia kujisajili katika daftari hilo.

Akizungumza na Mwananchi kisiwani hapa mwishoni mwa wiki, Kadika alisema baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar kuona kuwa hawana ubavu wa kuchukua Jimbo la Pemba, wameamua kupunguza kura za urais za mgombea wa Chama cha upinzani.

“Jimbo la Pemba, CCM hawapati, lakini wanachofanya sasa ni kupanga mikakati mbalimbali kwa kuunda utatu usio mtakatifu ambao ni wa ZEC, Idara ya Zan ID na Masheha ili kutupunguzia kura zetu za urais.

“Maana kama utawahesabu wanachama wa CCM katika majimbo ya Wilaya yangu, basi utapata 500 tena ukijumlisha mpaka watoto wanaonyonya ndio wanafikia idadi hiyo,” alisema.

Akitoa mfano, alisema Jimbo la Mgogoni kisiwani hapa, Kadika alisema katika uchaguzi wa mwaka 2005 idadi ya wananchi walioandikishwa walikuwa zaidi ya 7,000, lakini baada ya kumalizika kwa shughuli ya kuboresha DKW katika jimbo hilo, ni watu 4,300 tu waliosajiliwa.

“Kwa hiyo hapa utaona kuna zaidi ya kura zetu 3,000 zimekatwa katika jimbo moja tu, wakati sisi tulikuwa na matarajio ya kuongezeka kwa watu hadi kufikia 9,000 au 10,000. Hivi tuseme sisi huku kwetu hatuongezeki tunapungua tu tena kwa kasi yote hiyo.


“Wakishafanikiwa hapa, basi wataruhusu mawakala hadi kwenye vyumba vyao vya kulala, lakini wanajua kuwa wameshajihakikishia ushindi kwa njia hiyo. Halafu utasikia uchaguzi ulikuwa huru na haki, hakuna nguvu iliyotumika kumbe mchezo ulishachezwa zamani.” alisema.

Mkurugenzi wa Idara ya Zan ID Zanzibar Mohammed Ame alisema kazi ya kutoa vitambulisho vya Zan ID, halijasitishwa na kwamba hajapata malalamiko yoyote kuhusu shughuli hiyo.

“Hatujasitisha utoaji wa Zan ID, tunaendelea kutoa kila siku na watu wote wenye sifa na vigezo vya kupata basi wanapewa. Sijapata malalamiko yoyote kutoka kisiwani Pemba, lakini kama kuna hali hiyo basi nitafuatilia,” alisema Ame.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa ZEC Salim Kassim alisema, kasoro zinazojitokeza katika uboreshaji wa DKW kisiwani Pemba hazitaathiri uchaguzi mkuu wa 2010 na kwamba utakuwa huru na wa haki.

Sunday, July 19, 2009

Tatizo si wakristo bali ni maaskofu

Mwandishi Wetu
MWAKA 2006 tulishuhudia machafuko na mauaji katika wa nchi jirani ya Kenya Ingawa machafuko yalikuwa ya kisiasa lakini hasa yalikuwa ya kikabila.

Machafuko na mauaji yalitokea kwa kutokana na kile kilicho0nekana kuwa kabila moja kukandamiza makabila mengine. Kwa miaka mingi makabila mengine yalivumilia, lakini ikafika siku uvumilivu ukawashinda na wote tulishuhudia mauaji ya kikatili.


Huko Yugoslavia pia mauaji yalitokea miaka ya nyuma kwa sababu ya kidini yakihusisha Wakristo na Waislamu. Maelfu na maelfu ya watu waliuawa na hasa zaidi Waislamu.
Nasi Watanzania tusipokuwa makini basi, siku si nyingi tunaweza kujikuta tukianza kuchinjana kwa sababu ya kidini.


Kwenye bajeti ya mwaka huu Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema ya kuwa mapadri watano na mashehk wawili walimfuata nyumbani kumweleza matatizo yanayowakabili kuhusu misamaha ya kodi iliyokuwa imefutwa na Serikali.

Aliwataja mapadri kwa majina lakini masheikh hawakutajwa. Hili limechukuliwa na Waislamu kama ni dharau kwao. Likazua joto kwa Waislamu. Nao hawakulisemea hili lakini wakaanza kusema mambo ya Mahakama ya Kadhi na mambo ya kujiunga na OIC.


Mimi binafsi nashindwa kuelewa mambo yanayopingwa na ndugu zetu, si wakristo lakini maaskofu kama ifuatavyo.

Kuanzishwa Mahakama ya Kadhi kunawahusu au kuwapotezea usingizi vipi kwa kuwa atakayehukumiwa ni Muislamu na si Mkristo? Vile vile mambo mengi yatakayohukumiwa ni ya mashauri ya mirathi na ndoa, si ya makosa ya jinai. Sasa kinachowasumbua wenzetu ni kipi hasa.

Hakika kwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi hakuwezi kuifanya nchi kugeuka ya Kiislamu.kenya na Uganda ni majirani zetu wa karibu kabisa ambazo asilimia 20 au 30 raia wao ni waislamu.

Hapa kwetu zanzibar kuna mahakama ya kadhi, je lini tumesikia kuna mtu kakatwa mkono au ameuwawa kwa kupigwa mawe na hata ikitokea basi ndiyo dini ya waislamu inavyosema.je hizo nchi za Kenya na Uganda zimegeuzwa kuwa za kiislamu. Asilimia zaidi zaidi 30 ni waislamu lakini wamepewa haki yao , sisi sembuse zaidi ya asilimia 50?

Pili, kuhusu Tanzania kujiunga na OIC. Kwanza kabisa kujiunga na IOC hakuifanyi Tanzania kuwa nchi ya Kiislamu. Je , Uganda imekuwa nchi ya Kiisalamu baada ya kujiunga na OIC ? zambia na Malawi wana asilimia 5 peke yake ya waislamu nao wamejiunga na OIC je kumekuwa na matatizo gani.


Kama kuna faida ya kujiunga na OIC kwa kupata misaada kuna tatizo gani? Watakao faidika na misaada ni Watanzania si Waislamu peke yao .

Tulipojiunga na umoja wa nchi za madola mbona mashekhe hawakupiga makelele wala kulalamika.Nchi mama wa jumia za madola ni Uingereza na Uengereza na nchi ya kikristo.
Kama nchi yetu haina itikadi ya dini basi nasisi tujitoe kwenye jumiya hiyo.


Watanzania wenye dini mbali mbali hawaoni tatizo kuwa mwanachama wa jumuiya la madola ingawa ni ya kikristo kwani wano faidika ni watanzania wote sio wakristo pekee yao , kama vile vile watakao faidika na OIC in watanzania na sio waislamu peke yao .

Mbali na kuwa mwanachama wa jumiya ya madola ingawa Tanzania haina itikadi ya dini bado Tanzania ina uhusiano wa kibalozi na Vatican ambayo kwa 100% ni mamlaka ya kanisa katholiki.Hapa anayo uongoza Vatican na mwakilishi wake nchini na Tanzania inawakilishwa na balozi wetu Italia.

Kuna siku Mh Membe alisema ya kuwa Tanzania inafikiria kujiunga na OIC, maaskofu wakaja juu na kushika mapanga kumshambulia Mh Membe Mbona sisi Waislamu tukiumwa tunakwenda kutibiwa kwenye hospitali za misheni ( za Wakristo )?

Je, baada ya kupata matibabu Waislamu hugeuka kuwa Wakristo ?. kwakweli maaskofu hawana hoja hata moja lakini wamekuwa wanataka kuyumbisha serekali. Sijui kwa faida ya nani ? au wana lengo ambalo sijalijua.

Watoto wetu vile vile wanasoma shule za misheni ikibidi hata kubadilisha jina ilimradi apate elimu. Kwa kubadilisha jina mtu hawi Mkristo au Muislamu. Mtu anaweza kuuliza je, dini kweli inaweza kubagua kingilio kwa kubagua mtoto ana dini gani mpaka aamue kubadilisha jina? Huo ni ubaguzi, na hakuna dini inayokubali ubaguzi.

Nchi yetu imekuwa na sifa kubwa kabisa ya utulivu na amani. Sifa hiyo haiwapendezi watu wengi wa nje na hasa nchi za Magharibi na Marekani. Si ajabu kuwa nchi hizo ndiyo zinazochangia vurugu hizi ili umoja wetu ututoke na sisi tuwe kama nchi nyingine za Afrika. Vurugu na fujo kila siku.


Ni mataifa haya yaliyoleta sumu ya majina kama mtu mwenye siasa kali, mujahidina. Lakini Muislamu anayeitwa siasa kali ni yule masikini anayeswali mara tano, anaye funga mwezi mtukufu wa Ramadhani anaye shika nguzo tano za dini. Wanampachika jina baya ili wengine wasimfuate kushika nguzo tano.

Kwa upande wa wenzetu mtu akishika dini sawa sawa basi anapachikwa jina la mlokole. Jina mlokole anatafsiriwa kama mtu safi sana hatendi dhambi zozote. Jamani hii kweli ni sawa.
Mtu safi anayeshika dini ya Kiislamu au ya Kikristo anatakiwa apewe heshima sawa sawa si moja mlokole (msafi) na siasa kali (mkorofi). Mambo haya yanawakera Waislamu hata kama wamekaa kimya.


Miaka ya majuzi kulikuwa na Muislamu ambaye alikuwa anajenga miskiti katika Mkoa wa Iringa. Kwa shinikizo la Marekani akakamatwa na kuvuliwa uraia wa Tanzania na kurudishwa Saudia.

Je, mbona Waislamu hawaulizi makanisa tena makubwa yanajengwa kila siku hizo pesa zinatoka wapi. Lakini misikiti ikijengwa tu basi maswali 50 yatajitokeza.

Mimi binafsi sina tatizo kabisa na kujengwa hospitali au shule za kanisa. Kwani kazi kubwa ya dini ni kufundisha utulivu na amani. Nawashanga hao wanaopinga Waislamu wanapojenga misikiti na shule.

Niseme tu ya kuwa Watanzania tusipokuwa makini tutafika pabaya. Tuchezee kila kitu, lakini tusichezee moto wa kidini. Hakuna atakayepona ukianza kuwaka.

Tunaambiwa kuwa ukizungumza maswala haya serekali itakupeleka pabaya. Lakini kwa kuwa naependa nchi yangu yenye utulivu, sina budi nikayazungumza. Waswahili wanasema “ usipoziba ufa utajenga ukuta”.

Nawaomba waheshimiwa wabunge wapime uziri na ubaya wa wakujiunga na OIC halafu watoe maamuzi yao . Kwani wao sio wawakilishi wa makanisa au misikiti, wao wamekula kiapo ya kuwatumikia nchi yao bila kujali Rangi,Dini au Kabila.