MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Friday, July 27, 2012

WATEMBEA NUSU UCHI, MAKOBE MARUFUKU ZNZ


Khamis Amani, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imepiga marufuku mambo mbali mbali yanayoenda kinyume na maadili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ikiwemo uvaaji wa nguo zisizokuwa na heshima, ili kulinda heshima ya mwezi huo.
Pamoja na marufuku hiyo, serikali imetanabahisha kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wote watakaokiuka agizo hilo la serikali.
Mawaziri wa wizara za Katiba na Sheria Abubakar Khamis Bakary, pamoja na waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, waliyasema hayo katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani walipozungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali.
Katika taarifa hiyo, Mawaziri hao walisema katika kipindi cha nyuma mwezi mtukufu wa Ramadhani umekuwa ukipoteza heshima yake, kutokana na waumini wake kuwa mstari wa mbele kuudharau mwezi huo.
“Tumezowea kuona watu wanakula ovyo, wanapiga disko mchana, uvaaji wa nguo zisizokuwa na heshima kwa wanawake pamoja na mambo mengine, ambayo yanaupotezea heshima mwezi huo mtukufu wa Ramadhani”, alisema waziri wa Katiba na Sheria.
Hivyo waziri Abubakar alisema kwa kuona hayo serikali imeona ipo haja ya kuendeleza tabia na hulka ya kuheshimu mwezi huo, kwa kupiga marufuku mambo yote yanayokwenda kinyume na mila, silka na maadili ya mwezi huo wa Ramadhani.
Katika marufuku hiyo, waziri Abubakar amepiga maruku kuwepo kwa magenge ya vyakula (mama ntilie) na hoteli ndogo ndogo za kawaida kwa mchana wote wa mwezi mtuku wa Ramadhani.
Waziri Abubakar alisema Serikali, haitoruhusu mtu yoyote wakati wa mchana wa mwezi wa Ramadhani hata kwa yule asiyekuwa muumini wa dini ya Kiisilamu, kuonekana akila, akinywa au akilewa hadharani, au kufanya jambo lolote ambalo ni kinyume na maadili na silka za Zanzibar.
Pamoja na marufuku hiyo amepiga marufuku kwa mtu yoyote kwa wakati wote kuvaa nguo zisizokuwa za heshima na zinazoonesha maumbile yake ya siri, au nguo zinazobana ili kumfanya binaadamu mwengine kuwa na hisia tofauti.
Sambamba na hayo, pia amepiga marufuku ‘disko toto’ kwa wakati wowote ule, kwa madhumuni ya kuwafundisha watoto maadili mazuri ya Kizanzibari na siyo kuiga mambo yasiyo na tija kwa vijana ambao ndio wazee na viongozi wa taifa hili hapo baadae.
Alifahamisha kuwa, katika kipindi hicho cha sikukuu watoto wadogo hawataruhusiwa kwenda katika sherehe baada ya saa 12 za jioni, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa mzee wa mtoto atakaekamatwa akikiuka utaratibu huo.
“Tunaviomba vyombo vya dola na Baraza la Manispaa kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaohusika”, alisisitiza Waziri huyo wa Katiba na Sheria.
Kwa upande wake, waziri wa Habari, Utamauni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk amesema kuwa, msimu wa utalii mwaka huu umeingia katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, hivyo jukumu la wadau wote wanaujishughulisha na biashara hiyo pamoja na wananchi kwa ujumla kuwakumbusha na kuwaelekeza wageni kujiepusha kabisa na mambo yote ambayo hayaruhusiwi kufanywa wakati wanaofunga wakiwa katika ibada hiyo.
“Tuwakumbushe wageni wetu mambo yasiyostahiki kwa mfano kula, kunywa, kuvuta sigara na kubusiana hadharani ni mambo ambayo hayaruhusiwi na yanakwenda kinyume na mila, silka na maadili yetu”, alisema Waziri Mbarouk.
Alisema kuwa hali hiyo, itasaidia kuwaepusha na matendo yoyote yanayoweza kuleta na kusababisha waliofunga kutokubali kufanywa kwa vitendo hivyo hadharani, na hivyo kuwa chanzo cha vurugu baina ya waumini wa Kiisilamu na wafuasi wengine.
Alisihi kuwa, ikitokezea kwa mgeni kwenda kinyume na hayo, jamii iepuke matumizi ya nguvu katika kurekebisha hali hiyo na badala yake itumike busara zaidi, na kuwafahamisha wageni nini cha kufanya na maeneo gani wanaweza kupata huduma za lazima bila ya kuvunja sheria.
Alifahamisha kuwa, kikawaida watalii ni wageni wenye uwerevu, usikivu, utiifu na wepesi wa kufuata maelekezo ya wenyeji wao, kwa kuzingatia hayo kila mmoja ana wajibu wa kushirikiana nao.
Alisema wizara kupitia Kamisheni ya Utalii, tayari imeshasambaza toleo ‘circular’ maalumu katika taasisi zote zinazohusika na utalii, kwa nia na madhumuni ya kuendeleza utalii uwe endelevu.

MUM YAPOTEZA 14 AJALI YA MV SKAGIT

CHUO Kikuu cha Waislamu kilichoko mkoani Morogoro kimepoteza wanafunzi 14 wa mwaka wa kwanza katika ajali ya boti ya Mv Skagit iliyotokea Julai 18, mwaka huu katika Bahari ya Hindi karibu na kisiwa cha Chumbe.
Waliofariki na sehemu wnazotoka katika mabano ni Abdalla Mohamed wa Unguja; Suleimani Ally (Pemba); Othumani Mwinyi Hussein (Unguja); Rashid Salehe (Unguja); na Rashidi Juma (Pemba).
Wengine ni Hussan Seif (Unguja); Mangi Haji (Unguja); Asha Abdalla (Pemba); Said Iddi (Unguja); Khadija Khamis (Pemba); Mgeni Omari (Unguja); Patima Simai (Unguja); Said Khatib (Pemba) na Khamis Suleimani (Unguja). 
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisa Habari wa chuo hicho, Saddy Ally, ilisema miili ya wanafunzi 12 ilipatikana na kuzikwa na miwili haijapatikana.
Alisema kuwa msiba huo ni mkubwa na pigo kubwa kwa chuo hicho na kwa Taifa kwa ujumla.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Hamza Njozi, aliwapa pole wale wote waliofikwa na msiba huo na kuwaomba ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Aidha, Profesa Njozi alisema ni jambo la kusikitisha sana kwani chuo kimepoteza wanafunzi wengi ambao walikuwa ni wa mwaka wa kwanza licha ya kwamba pia katika ajali ya Mv Spice iliyotokea mwaka jana wanafunzi wawili wa chuo hicho waliopoteza maisha.

HAMAD MASOUD AWAJIBIKA KISIASA


Salma Said, Zanzibar
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad amejiuzulu wadhifa wake leo jioni imeelezwa. 
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee ilisema tayari Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein amekubali ombi la Waziri Hamad Masoud kujiuzulu.
“Tarehe 20 Julai,2012 Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Mheshimiwa Hamad Masoud Hamad alimuandikia barua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk Ali Mohammed Shein ya kumuomba ajiuzulu kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Skagit iliyotokea Julai 18,2012” Ilisema taarifa ya Dk. Mzee.
Kufuatia kujiuzulu kwa waziri huyo, Rais Dk Shein amemteua Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani(CUF) Rashid Seif Suleiman kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano.
“Kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano,Rais amemteua Rashid Seif Suleiman kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano” Taarifa ya Ikulu ilisema.
Uteuzi wa Waziri mpya wa Miundombinu na Mawasiliano umeanza Julai 23 mwaka huu.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein ameunda Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Skagit.
Mwenyekiti wa Tume hiyo ni Jaji Abdulhakim Ameir Issa, wajumbe ni Meja Jenerali S.S. Omar, COMDR. Hassan Mussa Mzee, Kapteni Abdulla Yussuf Jumbe, Kaptein Abdulla Juma Abdulla, Salum Taoufiq,Kaptein Hatibu Katandula, Bi. Mkali Fauster Ngowo, Ali Omar Chengo na Shaaban Ramadhan Abdalla Katibu wa Tume.

WAZANZIBAR WAMECHOKA KUTUMIWA ROHO ZAO KUWA CHOMBO CHA PUBLICITY


Imefika wakati Shein na Balozi Seif Idd waone aibu kutokea mbele ya kamera za wanahabari kupokea rambirambi ambazo lengo lake kubwa ni watu, makampuni, taasisi na asasi za serikali kujitafutia umaarufu kupitia vifo vya watu.
Swali la kujiuliza kwa nini hao wanaojiita wasamaria wema hawataki kukabidhi misaada au rambirambi zao bila ya kuwapo kwa kamera za wanahabari au kukabidhi kwa viongozi wa ngazi za chini katika nchi.
Kila siku lazima wampate rais au makamu wa rais hata waziri, naibu, katibu mkuu na mkurugenzi wa wizara husika hawawataki.
Ni vyema Shein na Seif Idd wakakumbuka kuwa fedha wanazopokea zina damu kwani hazina nia nzuri ya kusaidia na wazanzibari wamechoka na tabia ya kutumiwa roho za ndugu na jamaa zao kama daraja la wafanyabiashara na wanasiasa kujipatia umaarufu.
Tafakarini halafu muchukue hatua.

UNAFIKI WA MAKINDA

Utadhani sie aliyepembejewa bunge liahirishwe kutokana na ajali ya MV SKAGIT na akakataa.

SMZ YATILIA 'VIRINGI NGU ZA KUAZIMA', YATANGAZA BAKHERESA ATALETA MELI, BADALA YA KUWAELEZA WANANCHI NINI ITAFANYA KUMALIZA ADHA YA USAFIRI

Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar imezifutia rasmi hati ya kufanya kazi Meli ya Mv.Kalama, Mv.Seagul na Mv.Sepideh kutokana na meli hizo kutokukidhi hali ya usalama wa abiria katika meli hizo. 
Aidha meli hizo zimepewa muda wa mwezi mmoja kuanzia leo kuhakikisha zimeondoka katika maeneo ya Zanzibar kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi ya wamiliki wa Meli hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Afisini kwake kuhusu hali ya usafiri wa baharini na usalama Zanzibar.  
Amesema Mamlaka hiyo imefanya tathmini na uhakiki wa kutosha na kujiridhisha kuwa Meli hizo hazifai kufanya kazi katika maeneo ya Zanzibar jambo ambalo limepelekea kuchukua hatua za kufuta hati za kufanyia kazi meli hizo.
Amefahamisha kuwa sababu kuu zilizopelekea Mamlaka kufanya maamuzi hayo ni pamoja na uchakavu,umri wa meli hizo kuwa mrefu na kupata matatizo mara kwa mara katika safari zao. 
Kombo amefahamisha kuwa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri na Bandari Zanzibar ya mwaka 2006 kifungu cha 17.1 inampa mamlaka Msajili wa Meli kuifuta meli yoyote ambayo itakuwa haikidhi usalama wa abiria. 
Kufuatia sheria hiyo Kombo amesema watawataka wamiliki wa Meli hizo kuzirudisha hati za kufanyia kazi meli hizo ili waende kutafuta sehemu nyengine za usajili kinyume na maeneo ya Zanzibar.   
Akizungumzia Meli ya Mv.Serengeti Kombo amesema wamelazimika kuiagiza meli hiyo kupunguza idadi ya abiria kutoka watu 800 hadi 350 na tani za mizigo kutoka 100 hadi 50  hadi pale ambapo watajiridhisha kutokana na hali ya meli hiyo ilivyo. 
Aidha amegusia kuwa Kampuni ya Bakhresa italeta Meli kubwa ya abiria itakayofanya kazi zake Zanzibar ambapo pia Serikali ya Mapinduzi nayo iko mbioni kuhakikisha wanaleta meli inayokidhi mahitaji ya wananchi wa Zanzibar.