MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, May 20, 2009

Mwenyekiti wa mtaa adaiwa kupandisha nauli za daladala

Salim Said

WAKAZI wa Kimara wisho na Bonyokwa jijini Dar es Salaam, wamemtuhumu Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kimara Mwisho, Gabriel Kilave, kwa kupandisha nauli ya daladala kutoka Sh 250 bei ya serikali hadi Sh300 ambayo ni bei yake.

Nauli hiyo, inatozwa kwa kila kichwa umbali unaokadiriwa kuwa wa kilometa 3, kutoka Kimara Mwisho hadi wa Bonyokwa.

Mwenyekiti huyo, alisema Msafiri anapaswa kulipa Sh 250 kutoka Kimara Mwisho hadi vyumba vinane ambako kuna umbali wa kilometa 1.5 wakati wanaoendelea na safari hadi Bonyokwa wamekuwa wakilazimishwa kulipa Sh 300 kwa kila safari.

Wakizungunza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi hao walisema, mwenyekiti huyo na watendaji wamepandisha nauli na kwamba kila mwisho wa wiki madereva na wapiga debe wanawalipa kiasi fulani cha fedha.

“Mwenyekiti ameamua kupandisha nauli kinyume na sheria kwani anaestahili kufanya hivyo ni Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na majini (Sumatra) pekee na wala si mwenyekiti wa mtaa,” alisema Hashim Juma ambaye ni mkazi wa Kimara.

Juma alisema Mwenyekiti alipandisha nauli kienyeji baada ya kupelekewa malalamiko na madereva wa daladala kuwa barabara hiyo ni mbovu na aliamua kupandisha nauli kienyeji bila kushirikisha mamlaka husika.

“Tunajua hawa madereva walikaa kikao na kuamua kwenda kuonana na uongozi wa serikali ya mtaa kwa sababu walishasema mapema suala la nauli kupanda ni lazima na leo azma hiyo, imetimia tena kwa barua iliyosainiwa na mwenyikiti,” alisema.

Naye Emmanuel Magige alisema, anashangazwa na hatua ya kupandishwa kwa nauli hiyo kiholela kwa kutumia mwamvuli wa serikali ya mtaa.

“Tunashangaa, kama yeye anataka kuwa mtu wa Sumatra si aombe kazi huko? Mbona kazi ya kusimamia hata matengenezo ya hii barabara yamemshinda na kurukia suala la kupandisha nauli kwa kuwakomoa wananchi badala ya kuwatetea?” alisema Magige.

Kilave alikiri kupandishwa kwa nauli hiyo, lakini alikanusha kuandika barua ya kuhalalisha suala hilo.

“Ni kweli tulipandisha nauli, lakini baada ya malalamiko ya makonda na madereva kuwa barabara ni mbovu. Kwanza tulikutana kwa pamoja wenyeviti wa mtaa wa Matangini, Mavurumza na madereva hao na muhutasari wa kikao upo, kabla ya kuamua kupandisha nauli” alisema Mwenyekiti huyo.

Meneja wa Uhusiano kwa Umma wa Sumatra,David Mzirai alisema, kitendo cha wenyeviti hao ni kinyume na sheria na kwamba viwango halali vya nauli ni vile vilivyopitishwa na mamlaka hiyo tu.