MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, October 7, 2009

Lipumba:Kikwete anapaswa kubeba msalaba wa Richmond

Salim Said, Mtwara
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, amesema Rais Kikwete Jakaya Kikwete, anapaswa kubeba msalaba kuhusu Kampuni feki ya Richmond, iliyopewa zabuni ya mradi wa kufua umeme wa dharura.

Profesa Lipumba aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia katika uzinduzi wa operesheni zinduka katika Kanda ya Kusini, iliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara,

Alisema Rais Kikwete kama Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, hawezi kukwepa lawama kuhusu zabuni hiyo, iliyoisababishia kashfa serikali yake.

Alisema, maamuzi ya kusainiwa kwa mkataba wa zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa Kampuni ya Richmond yalifanywa na Kikwete na kwamba kwa msingi huo, yeye ni mtuhumiwa namba moja katika suala hilo.

“Mtuhumiwa na mshitakiwa namba moja wa kashfa ya Richmond ni Rais Kikwete kwa sababu maamuzi ya kuingia zabuni hiyo yalifanywa na yeye,” alisema Profesa Lipumba.

“Kwa sababu hakuna mtu mwingine yeyote anayeweza kutengua au kubariki maamuzi ya baraza la mawaziri, isipokuwa rais, yeye ndiye mhusika nambari moja na anayepaswa kubeba msalaba wa Richmond," alisisitiza kiongozi huyo wa CUF.

Profesa Lipumba alielezea kusikitishwa kwake juu hatua ya Katibu Mkuu Kiongozi (Luhanjo), ya kuwasaliti na kuwafanya Watanzania kuwa ni watu wasio na akili hasa baada ya kujitokeza na kudai kuwa Rais Kikwete, hahusiki na Richmond.

“Luhanjo anayajua yote kuanzia mchakato hadi kusainiwa kwa zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa kampuni ya mkobani ambayo haina hata uwezo wa kuunganisha waya kwenye nyumba. Leo anawadanganya Watanzania,"alisema Profesa Lipumba.

Alidai kuwa hatua hiyo inadhihirisha kuwa CCM wote ni mafisadi na ndiyo maana wameamua kuficha ufisadi na kuwasaliti Watanzania, waliowaweka madarakani.

“Ndugu zangu kiongozi aliyeingia madarakani kwa ufisadi hawezi kupambana na ufisadi hata kidogo. Rais Kikwete si mpambanaji wa ufisadi,” alisema Lipumba.

Alielezea kushangazwa kwake na kauli za baadhi ya viongozi wa CCM kwamba ufisadi umekithiri lakini bila kumhusisha Rais Kikwete ambaye alidai kuwa naye anayendesha ufisadi.

“Kama kweli ni wazalendo na wana nia ya dhati ya kupambana wamtaje, Rais Kikwete na wawambie Watanzania wasimchaguwe katika uchaguzi wa mwaka 2010," alisisitiza.

Alisema Tanzania ina uongozi dhaifu wa rais Kikwete na kwamba hata wanamtandao walimkubali kwa tamaa ya kupata madaraka tu.

No comments:

Post a Comment