Salim Said
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitaka serikali kuianika hadharani ripoti ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ufisadi ndani ya stendi ya kuu ya mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani ya Ubungo (UBT) pamoja na kuiwajibisha familia ya Kingunge Ngombale Mwiru inayodaiwa kuendesha ufisadi katika stendi hiyo.
Miezi michache iliyopita Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifanya ziara ya kikazi jijini la Dar es Salaam na kugundua harufu ya ufisadi UBT ambapo alimuagiza CAG kufanya ukaguzi katika stendi hiyo.
Akifungua mkutano mkuu wa jimbo la Ubungo (Chadema) katika ukumbi wa mikutano wa Urafiki Dar es Salaam jana, mkurugenzi wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa wa Chadema John Mnyika, alisema ana taarifa za uhakika kwamba CAG amemaliza kazi yake na kugundua ufisadi wa mamilioni ya fedha.
“Nina taarifa za uhakika kwamba CAG amemaliza kazi yake na amegundua ufisadi wa mamilioni, kwa hivyo tunawataka wananchi wa jimbo la Ubunge tushirikiane kuibana serikali kuianika hadharani ripoti yake,” alisema Mnyika na kuongeza:
“Si hilo tu bali serikali iiwajibishe kwa kuifikisha mahakamani familia ya mzee Kingunge ambayo ndiyo inahusika na wizi huu wa mamilioni ya fedha ambao unawakosesha huduma nyingi wananchi wa Ubungo na halmashauri nzima ya Kinondoni”.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, CAG Ludovick Utouh alithibitisha kukamilika kwa uchunguzi huo na kwamba ripoti yake imekamilika.
“Ni kweli ripoti ya uchunguzi wa ufisadi ndani ya stendi ya mabasi Ubungo imekamilika na nimeshaipeleka kunakohusika kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda,” alisema Utouh.
Alipoulizwa iwapo kuna ufisadi wowote aliougundua katika uchunguzi huo alijibu.
“Ahh hilo siwezi kuzungumzia si kazi yangu mimi kazi yangu niliambiwa nichunguze tu, mwenyewe Waziri Mkuu ndio mwenye haki ya kuzungumzia matokeo ya uchunguzi huo,” alisema.
Mnyika alisema mwaka 2005 aliwaeleza wananchi wa Ubungo kuwa familia hiyo ya Mbunge wa kuteuliwa na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (NEC) kuwa inafanya ufisadi mkubwa katika mkataba wa ukusanyaji mapato UBT lakini serikali ilipinga.
No comments:
Post a Comment