Salim Said
ZAIDI ya watu 300 kisiwani Unguja jana walikusanyika kwenye ofisi ya Idara ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (Zan ID) na kuwafungia ndani wafanyakazi wa idara hiyo wilayani Kaskazini ‘A’ wakidai kuwa wamenyimwa vitambulisho.
Wananchi hao walianza kumiminika kwenye ofisi hiyo iliyo eneo la Gamba majira ya saa 1:00 asubuhi na baadaye kuchukua uamuzi wa kufunga ofisi baada ya kubaini kuwa wengi matatizo yao yanafanana.
Wakizungumza na Mwananchi jana kwenye eneo hilo, baadhi ya wananchi hao walisema wamechoshwa na usumbufu ambao wanaupata kutoka kwa ofisi hiyo serikali katika kudai haki zao.
Mmoja wa wananchi hao Faki Ali alisema, amejaza fomu kutoka kwa Sheha na kuirudisha katika ofisi ya Zan ID na kupatiwa stakabadhi lakini amekuwa akizungushwa kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
“Tumechoka kabisa kuacha kazi zetu kila siku kwa kufuatilia kitambulisho halafu hatupewi, tumekamilisha taratibu zote lakini wanatuzungusha tu kila siku,” alisema Ali na kuongeza:
“Sisi tumekaa zaidi ya vijana 300 nje ya ofisi za wilaya za vitambulisho hata hawatujali wanachotuonesha ni dharau tu tukaamua tuwafungie ndani wafanyakazi wao”.
Alisema kejeli na dharau za wafanyakazi wa ofisi ya vitambulisho zimechupa mipaka na kuhoji kuwa hawajui kiburi hicho wanakitoa wapi.
Naye Juma Khamis Ngwali alisema, waliamua kuwafungia ndani wafanyakazi hao majira ya adhuhuri baada ya kukaa nje ya ofisi hiyo kwa muda mrefu bila ya kuhudumiwa.
“Kama huna kitambulisho cha mzanzibari mkaazi tume haikusajili ndani ya daftari la kupiga kura, huku tumefuata taratibu zote hadi mahakama imetoa hati watu wapewe vitambulisho lakini wanatuzungusha tu,” alisema Ngwali.
Alisema walikaa nje ya ofisi hiyo ya Idara ya Vitambulisho ya Wilaya ya Kaskazini A Uguja kwa zaidi ya saa nane bila ya hata kuulizwa.
Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho Zanzibar Mohammed Ame alithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana ambazo alizipata kutoka kwa Mkuu wa Ofisi ya Wilaya ya kaskazini A.
“Nikweli nimezipata taarifa hizo kupitia kwa ‘incharge’ msimamizi wa ofisi kwamba kuna vijana wamejikusanya wengine wakiwa hawana vyeti vya kuzaliwa na wengine hawana barua za sheha lakini wanalazimisha wapewe vitambulisho,” alisema Ame.
Hivi karibuni matukio ya vurugu yamekuwa yakitokea Zanzibar kufuatia kuanza kwa awamu ya kwanza ya uboreshaji wa daftari la wapigakura ikiwa ni pamoja na Sheha wa Shehia ya Ole Mussa Ali alimwagiwa tindikali usoni tukio ambalo lilipelekea kukamatwa kwa Katibu wa Tawi la Kianga la CUF Ali Mussa Salim.
Juzi ZEC iliahirisha zoezi la uandikishaji wa wapigakura kisiwani Pemba baada ya wananchi kugoma kwenda vituo kujiandikisha kwa sababu kila anayekwenda anakataliwa kwa sababu ya kukosa Zan ID.
Hatua hiyo ilisababisha askari wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (KVZ) kufyatua risasi hewani na kuongeza vurugu huku vijana wawili wakikamatwa na kuwekwa ndani.
No comments:
Post a Comment