MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, October 7, 2009

Vurugu zaibuka uandikishaji daftari wasimama Pemba


Mohamed Ghasan, Pemba na Salim Said


KWA mara ya kwanza tangu kuanza kwa zoezi la kurekebisha Daftari la wapiga kura, Pemba, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imelazimika kufunga vituo vya uandikishaji kufuatia vurugu zilizoibuka baina ya maafisa wake na wananchi walioshiniza kuwa watu wote waandishwe.

Mwenyekiti wa ZEC, Khatibu Mwinchande, alisema wamefunga vituo vyote vitatu vya uandikishaji katika jimbo hilo la Ole na kusisitiza kuwa endapo hali hiyo itajitokeza tena leo, watashauriana kwa pamoja kabla ya kuamua kuhamisha zoezi hilo katika jimbo la Mtambwe.

Hivi karibuni Sheha wa Shehia ya Ole Mussa Ali alimwagiwa tindikali na kusababishwa kukamatwa kwa Katibu wa Tawi la Kianga la Chama cha Wananchi (CUF), Ali Mussa Salim.

Hatua hiyo imekuja katika siku ya kwanza ya uandikishaji katika Jimbo la Ole lililopo Wilaya ya Wete kisiwani Pemba ambapo maelfu ya wananchi waliojitokeza kuandikishwa walionekana kutoridhika na maelezo ya waandikishaji wa tume ya uchaguzi waliotaka kila mmoja kuwa na kitambulisho cha ukaazi.

Katika kituo cha Minungwini, wananchi wakiwemo wenye vitambulisho waligoma na kupinga kuandikishwa kwa mtu yoyote kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kuwanyima haki wasioukuwa na vitambulisho.

"Hapa haandikishwi mtu, kama mnataka mtuandike wote, hii ni haki ya kila mwananchi, msitufanyie ubaguzi, kama hamuwezi ondokeni, lakini msimamo wetu ndio huu, sisi tuna vyeti vya kuzaliwa ambavyo tulivitumia tulipoandikishwa 2005," alisema mmoja wa wananchi hao huku akishangiliwa na wenzake.

Viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi na Mkuu wa Wilaya ya Wete, Omar Ali walijaribu kila njia kuwashawishi waliokuwa na vitambulisho vya ukaazi wajiandikishe, lakini juhudi zao ziligonga mwamba kutokana na msimamo mkali waliouonesha.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wananchi hao kumpatia hati za kuzaliwa walizokuwa nazo, lakini bila ya kutegemea alikataliwa huku akitupiwa maneno makali yakiwemo ya kutomwamini.

Kufuatia hali hiyo, ilibidi kuimarishwa kwa ulinzi katika katika kituo hicho na Jeshi la Polisi lilituma magari mawili yaliyobeba askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), JKU, Mafunzo na Valentia wote wakiwa na silaha za moto.

Wakati wananchi hao wakiendelea na msimamo wao wa kutotaka kuandikishwa, Mkuu wa Mkoa alilazimika kuzungumza na Mwakilishi wa Jimbo la Ole, Hamad Masoud akimtaka kuzungumza na wananchi ili waondoke katika eneo hilo, ombi ambalo Mwakilishi alilikataa kwa madai kuwa sio kazi yake.

"Mimi sio kazi yangu kuwaondoa, unataka niwaondoe kwa mamlaka gani ya sheria, siwezi, wewe ndiye mkuu wa mkoa uko na mkuu wa wilaya na hawa ni wananchi unajuaje kama ni wafuasi wangu, kwani hakuna wanachama wa CCM, ndipo uniambie kuwa wote hawa ni CUF?" alihoji mwakilishi huyo.

Baada ya muda mfupi walitokea viongozi wa Zec wakiongozwa na Mwenyekiti Mwinchande alikifuatana na makamishna wake ambao walifanya mazungumzo na waandikishaji na baadae mwakilishi wa jimbo hilo kuhusiana na suala hilo.

Majadiliano hayo yaliyochukua zaidi ya nusu saa huku wakibishana kisheria kuhusu uwezo wa mwakilishi kuwaondoa wananchi katika eneo hilo na kuwataka kuandikishwa wenye sifa. Hata hivyo mwakilishi huyo alishikilia msimamo wake kuwa hiyo si kazi yake bali inapaswa kufanywa na tume ya uchaguzi.

Utaratibu unaotumiwa na tume ya uchaguzi ni kuandikisha wapiga kura wapya kwa muda wa siku mbili wakati wale waliondkishwa mwaka 2005 utaratibu wao huchukua muda wa siku tano.

Awali akizungumza na Mwananchi mwakilishi wa jimbo hilo alisema, zoezi hilo limesimama katika vituo vya Kambini na Kiuyu Minungwini, Mjini Kiuyu tangu vituo vilipofunguliwa leo (jana) asubuhi kwa sababu wananchi wamekataa kwa kuwa wenzao wamezuiwa.

“Kila kituo kimesimama kwa sababu kila anayeingia kituoni anakataliwa kwa sababu hana kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (Zan ID) au kadi ya kupigia katika uchaguzi wa 2005. kwa hiyo wananchi wote wameamua kwa umoja wao kugomea zoezi hadi hapo wenzao wote wenye sifa watakapoandikishwa,” alisema Masoud.

Alisema Sheha wa Kambini, Ali Said Ali amekuwa akiwambia wananchi kuwa yeye si sheha kila wanapomfuata ofisini kwake kutaka fomu za kutafutia vitambulisho vua ukazi (Zanzibar ID).

“Pia wananchi baada ya kumuona katika kituo cha uboreshaji wa daftari la wapigakura wamemkataa sheha wao kwa sababu kila siku huwambia yeye si sheha, sasa wanashangaa kumuona kitioni,” alisema Masoud.

“Kwa kweli hali ni mbaya, mbaya, mbaya kupita maelezo, dhuluma tunayofanyiwa Wapemba imepita mipaka. Walipitisha sheria yao ya uchaguzi na ya vitambulisho, lakini wanashindwa kuidhibiti na kuisimamia ili wananchi wapate haki zao. Sasa katiba ya Zanzibar imekuwa haina tena maana mbele ya sheria,” alisema Hamad.

Alisema wako tayari kuuawa tena au kupigwa risasi na mabomu kwa mara ya pili lakini hawatakubali kudhulumiwa haki zao za kupiga kura.

Awamu ya kwanza ya uboreshaji wa daftari la kudumula wapiga kura kisiwani humo lilianza Julai 6, mwaka huu na awamu ya pili na ya mwisho inatarajiwa kuanza Januari mwakani.

No comments:

Post a Comment