MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Sunday, June 14, 2009

CHENGE


Chenge

SEMINA


Baadhi ya wajumbe wa Semina ya mafunzo ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu wakisikiliza kwa makini mada iliyokuwa ikiwasilishwa. Kushoto ni Mwenyekiti wa Shirika la Vyama vya Watu hao Tanzania (Shivyawata) Lupi Mwaisak. Pix na Salim Said

NIPO MAKINI NASIKIA


Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Viungo Tanzania (Chawata) Shida Salum akisikiliza kwa makini katika semina ya mafunzo kuhusu Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu jijini Dar es Salaam jana. Pix na Salim Said.

TUPO MAKINI


Afisa Mipango wa umoja wa walemavu znz Salma Saadat (kulia) naMkurugenzi wa Baraza la walemavu znz Abeida Rashid wakiwa katika semina ya mafunzo jijini Dar es Salaam. Pix na Salim Said

Baraza limenisukuma kujiuzulu: Lwakatare

Salim Said na Neema Materu

SIKU moja baada ya Baraza Kuu la Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kuwatimua maofisa watatu wa uchaguzi, aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa chama hicho,Wilfred Lwakatare, amesema mamuzi hayo ndiyo yaliyomfanya kuwasilisha barua ya kuachia ngazi nyadhifa zake zote ndani ya chama.

Juzi Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba, alitangaza, kuwatimua Maole Kuchilingulo, aliyekuwa Katibu wa Tume ya Uchaguzi ya CUF, Hussein Mmasi na Juma Wandwi wajumbe, baada ya kubainika kuwa walikihujumu chama chao katika uchaguzi mdogo wa Busanda.

Lwakatare ambaye alishawahi kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini, alimewasilisha barua ya kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya chama hicho na jana alithibitisha habari hizo.

Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam, alisema amefikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho.

“Ni kweli nimewasilisha barua hiyo, kwa sababu sikuridhishwa na uamuzi wa vikao vya Baraza kuu wa kuwatimua maAfisa watatu wa uchaguzi wa chama chetu,” alisema Lwakatare.

“Nimeona maamuzi ya baraza hilo si ya mustakbali mzuri ndani ya chama chetu,” alisema.

Kauli hiyo imekuja huku kukiwa na taarifa kuwa, kigogo huyo wa CUF ana mpango wa kukihama chama hicho na kuhamia Chadema.

Lwakatare, alikiri kusikia uvumi huo.

“Hata mimi nasikia hivyo hivyo lakini hakuna mtu rasmi aliyeniambia taarifa hizo. Mimi sina uwezo wa kuzungumzia hilo kwa sababu uamuzi wa hilo wanao wananchi na si mimi,” alisema Lwakatare.

Bajeti yamchanganya Mkulo

Salim Said

KUPOROMOKA kwa uchumi na maandalizi ya kusomwa kwa Bajeti ya serikali 2009/10 vimemchanganya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo baada ya kusema kuwa watu ambao wanaacha kufikiria bajeti na kuelekeza hisia zao kwenye mambo mengine ni wapumbavu.

Wakati Mkulo akitoa kauli hiyo, mamilioni ya Watanzania waliopanda fedha katika taasisi ya Deci bila kuvuna, hadi sasa hawajui hatma ya mbegu zao baada ya serikali kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi kufunga shughuli hizo, kwa madai kuwa ni hatari kwa mali za wanachama.

Mkulo aliyasema hayo juzi saa 8:00 usiku takriban saa 22 kabla ya bajeti kusomwa kwa bajeti katika mahojiano yake na mwandishi wa kituo cha habari cha Wapo jijini Dar es Salaam, kuhusu hatma ya wanachama waliopanda mbegu zao katika taasisi hiyo.

Redio hiyo, kupitia mwandishi wake, ilimuuliza Waziri huyo, hatma ya wanachama wa Deci hasa baada ya wanachama hao, kutishia kuvunja jengo hilo, ili wagawane mali zilizomo.

Kutokana na hali hiyo, Polisi walitumia silaha za moto kutuliza kutawanya wanachama hao ofisini hapo, ili kutuliza amani kwa watendaji wa taasisi hiyo na mali zao.

Mkulo alipoulizwa hatma ya wanachama hao alijibu kuwa, mtazamo wa watu wengi hivi sasa uko katika suala la bajeti na kwamba hawafikirii suala la taasisi hiyo.

“Mtazamo wa watu wote sasa wenye akili wanangojea bajeti, nasema mtazamo wa watu wazima wote wenye akili timamu wanataka kusikia bajeti,” alisema Mkulo.

Alisema suala la hatma ya wanachama wa Deci ni muhimu kuzungumziwa hivi sasa katika jamii kwa kuwa wengi wao wanataka kujua hatma ya mbegu zao.

Alipoulizwa endapo ripoti ya tume iliyoundwa na serikali kuchunguza masuala ya taasisi hiyo, nayo itatoka baada ya bajeti au la, Mkulo alijibu kwa jazba na hasira huku akiangusha matusi kwa mwaandishi huyo.
“Sio siri, kama hiyo ni muhimu kwako jijibu mwenyewe,” alijibu Mkulo.

Hata hivyo juhudi za kumpata Mkulo kuzungumzia suala hilo, hazikufanikiwa baada ya simu yake ya mkononi kutopokelewa mara kadhaa.

Kilimo Kwanza ni kitendawili cha kejeli-Lipumba

Wakati huohuo, Chama cha Wananchi (CUF), kimeitaka serikali ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuhakikisha zinawasilisha bajeti za mwaka wa fedha 2009/10 zitakazowajali wananchi wa kawaida.

Akiwasilisha maazimio ya Baraza Kuu la uongozi la chama hicho kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema bajeti nzuri ni ile itakayowajali wananchi wa kawaida ili kuwapunguzia ukali wa maisha.

“Serikali lazima ijipunguzie mafungu ya matumizi ya anasa kwa lengo la kuwajali wananchi wa kawaida kwa kupeleka fedha nyingi katika miradi itakayoinua uchumi wa nchi na kuongeza ajira kwa vijana wetu,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Baraza kuu la uongozi la CUF linawataka mawaziri wa fedha wa serikali zote mbili kuonyesha katika hotuba zao za bajeti, mwelekeo wa serikali hizo katika kukabiliana na athari za mtikisiko wa uchumi duniani na vipi nchi itaweza kujikwamua kiuchumi”.

CUF inasikitishwa na ongezeko kubwa la watanzania wanaoishi katika dimbwi la umasikini na kwamba uchauni wa kaya unaendelea kudoro badala kukua hivyo kuwasababisha umasikini kupanda kwa kasi.

“Kwa watanzania waliowengi kauli mbiu ya ‘Maisha bora kwa Kila Mtanzania’ bado ni kitendawili cha kejeli kinachoteguliwa kwa maisha ya dhiki kila kukicha,” alisema Profesa Lipumba.

CUF yawatimua maafisa watatu kwa usaliti chamani

Salim Said

CHAMA Cha Wananchi (CUF), kimewatimua maafisa wake watatu wa uchaguzi kwa tuhuma za kukisaliti chama hicho katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Busanda.

Uamuzi huo uliofikiwa katika kikao cha Baraza Kuu kilichomalizika jana jijini Dar es Salaam baada ya wajumbe kuridhika kuwa moja ya sababu za CUF kushindwa katika uchaguzi huo uliompa ubunge mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni usaliti huo uliofanywa na maafisa wake.

Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, Baraza limefikia uamuzi huo kulinda maslahi ya chamasema, baraza kuu liliamua kuchukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha na makosa ya watu hao, ili kulinda maslahi ya chama chao.

Aliwataja maafisa hao kuwa ni Husein Mmasi aliyekuwa msimamizi wa shughuli zote za kuandaa mawakala katika uchaguzi huo, Katibu wa Tume ya Uchaguzi ya CUF Maole Kuchilingulo na Juma Wandwi, aliyekuwa mjumbe wa tume ya uchaguzi wa chama hicho.

Alisema mbali na uamuzi huo wa kuwavua madaraka, Baraza limetoa onyo kali kwa maafisa hao na kuweka wazi kuwa hakitovumilia vitendo vya aina hiyo wala kusita kuwaadhibu viongozi na watendaji wa chama kwa uzembe au hujuma.

Akielezea kwa undani tukio hilo, Profesa Lipumba alisema siku tatu kabla ya uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitangaza kuwafuta mawakala wa wa CUF, kwa kuwa majina yao hayakupangwa kwa mujibu wa vituo vya kupigia kura, kama sheria ya uchaguzi inavyotaka.

“Baraza kuu limeridhika kwamba kuzuiwa kwa mawakala wetu kulitokana na hujuma ya afisa wa ndani ya chama, kwa kutotekeleza kwa makusudi masharti hayo ya kisheria,” alisema profesa Lipumba.

Pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Wilfred Lwakatare ameamua kuachia ngazi nafasi zote za uongozi ndani ya Chama hicho kwa kile kilichoelezwa kuwa, anataka kurudi Jimboni kwake Bukoba kwa ajili ya kuimarisha chama chao.

Profesa Lipumba alithibitisha kupokea barua ya maombi ya kuachia ngazi kwa Lwakatare wakati wa kikao cha Baraza hilo, kilichoanza Juni 8 hadi 9 mwaka huu, akitaka kurudi jimboni kwake kuimarisha chama.

“Chama chetu ni cha demokrasia na katika demokrasia huwezi kumkataza mtu kujiuzulu, lakini hatujamjibu barua yake. Lwakatare tulikuwa naye na kushirikiana naye kwa mambo mingi na pia tutaendelea kushirikiana, ila kwa sasa ameamua kuwa mwanachama wa kawaida tu,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema, Lwakatare hajawahi kutuhumiwa na kashfa ya aina yoyote ndani ya chama na wala hajashinikizwa na mtu yoyote kujiuzulu, ila ameamua mwenyewe kujiuzulu na sisi kama Baraza kuu la uongozi hatuwezi kumzuiya kujiuzulu.

Aidha Profesa Lipumba alisema, CUF imeandaa operesheni maalumu kwa ajili ya uzinduzi na kuitangaza dira ya mabadiliko (vision for changes) ya chama chao ijulikanayo kwa jina la ‘Operesheni Zinduka’ itakayoanza Julai mosi mwaka huu.

“Operesheni hii itaongozwa na viongozi wa CUF na itatembea katika kanda zote saba za chama chetu, zikiwamo tano za Tanzania bara na mbili za Zanzibar kwa ajili ya kuwazindua wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu na ule wa taifa mwakani,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema katika hatua ya awali operesheni hiyo itanzia katika kanda ya Ziwa na kanda ya Dar es Salaam Julai mosi mwaka huu.

Wakati huohuo Profesa Lipumba aliwataka waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Mwinyi na Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Devis Mwamunyange, kuwajibika kwa kujiuzulu mara moja kufuatia uzembe wa mamlaka wanazoziongoza, uliosababisha milipuko ya mabomu Aprili 29 mwaka huu na kusababisha maafa makubwa kwa wananchi.

“Baraza kuu linalaani vikali ubaguzi wa dhahiri uliofanywa na unaondelea kufanywa kwa misingi ya kisiasa katika uhakiki na ugawaji wa misaada kwa waathirika wa milipuko hiyo,” alisema.

Alifafanua kuwa, baraza kuu la uongozi la CUF linalaani vikali matamshi ya dharau nay a kejeli yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Willim Lukuvi, ya kuwataka wananchi wa Mbagala kuzoeya milipuko ya mabomu na kuichukulia kama sehemu ya maisha kama wananchi wa Kipawa walivyozoeya sauti za ndege zinazoruka mara kwa mara katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

“Matamshi hayo yanaonesha dharau ya hali ya juu kwa wananchi walioathirika na vitendo vilivyosababishwa na uzembe na kutowajibika kwa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM),” alisema Profesa Lipumba.

Aliwata Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Machano Othman Said na Mkurugenzi wa Bandari ya Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe, kuwajibika kwa kujiuzulu mara moja kutokana na uzembe wa mamlaka wanazoziongoza uliosababisha vifo vya wananchi na hasara ya mali baada ya Meli ya MV Fatih kuzama ikiwa bandarini.

“Baraza linasikitishwa na uzembe uliofanywa na watumishi wa bandari ya Zanzibar kiasi cha Meli kuzama ikiwa bandarini nakupoteza maisha ya wananchi ambayo yangeweza kuokolewa,” alisema Lipumba na kusisitiza.

“Baraza kuu la CUF linazitaka serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar kuunda tume huru zikiwashirikisha wajumbe wa kambi ya upinzani Bungeni na katika baraza la wawakilishi wa Zanzibar kuchunguza chanzo cha milipuko na kuzama kwa meli ya MV Fatih na baadaye kutoa ripoti kwa wananchi.”

Kikao cha baraza kuu la uongozi la CUF kilimalizika juzi baada ya wajumbe kupitisha maazimio mbali mbali ya kiutendaji na kuhimiza uwajibikaji kwa serikali ya SMZ nay a Muungano.