MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Tuesday, August 14, 2012

MABAKI YA NDEGE ZA JESHI LA UGANDA YAPATIKANA KENYA

Mabaki ya Helikopta mbili za Uganda ambazo ziliripotiwa kutoweka siku ya Jumapili zimepatikana mashambani nchini kenya. Kanali Cyrus Oguna ambae ni msemaji wa jeshi la Kenya amesema hatma ya watu 14 waliokuwemo ndani ya chombo hicho haijulikani.
Ndege hizo mbili zilikuwa ni sehemu ya vifaa vilivyokuwa vikipelekwa nchini Somalia kuongezea nguvu kikosi cha umoja wa Afrika kilichoko huko.
Helikopta ya tatu ambayo pia ilikuwa katika msafari huo ilitua kwa ghafla katika eneo la mlima Kenya siku ya Jumapili.
Kanali Oguna amesema wote waliokuwa katika helikopta hiyo ya tatu waliokolewa.
Ni helikopta moja peke yake ndio faulu kutua vizuri na kuongeza mafuta katika mji wa Garissa ulioiko kaskzzini mwa Kenya.
Helikopta hizo nne ambazo zimetengezezwa Urusi ziliondoka siku ya Jumapili Uganda zikelekea Somalia kabla ya kukumbwa na mkasa huo.
Masalia ya helikopta hizo mbili ambazo awali ziliripotiwa kutoweka zilionekana juu ya mlima Kenya na maafisa wa Shirika la Wanyama pori, limeripoti gazeti la Daily Nation la Kenya.
Msemaji wa jeshi Kanali Oguna ameimbia BBC kwamba kikosi cha jeshi la Kenya linaelekea katika eneo hilo la Mlima Kenya , ambao ndio mlima wapili kwa urefu ,afrika.
Afisa huyo amefafanua kwamba moja ya helikopta hizo imeharibika kabisa ilhali ya pili imeharibika kiasi.
Helikpta hizo zilikuwa zinaelekea nchini Somalia kuongezea nguvu vikosi vya Umoja wa Afrika ambavyo vinajitayarisha kuvamia mji wa Kismayo na kuwafurusha wapiganaji wa Al Shabaab toka mji huo ambyo ndio ngome yao kuu.
CHANZO: www.bbcswahili.com

UNAIKUMBUKA HIII?

WIZZI MTUPPPPPPPPPPPPPPPP

TUNATAKA MATUTA


Wanafunzi wa Shule za Msingi Ndugumbi na Mwalimu Nyerere, Magomeni, Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakiandamana katika Barabara ya Kawawa, kushinikiza Wakala wa Barabara wa Serikali (TANROADS), kuweka matuta barabarani,baada ya wenzao wawili kugongwa.

BREAKIING NEWSSSS

MABOMU YA MACHOZI YANAENDELEA KUPIGWA KIGAMBONI BAADA YA WACHIMBA KOKOTO KUFANYA VURUGU NA KUFUNGA BARABARA

HALI sasa si shwari eneo la Mji Mwema, Kigamboni, Dar es Salaam, baada ya wachimba kokoto kufanya vurugu kwa kufunga barabara kwa mawe na kuwasha matairi barabaran wakipinga kitendo cha Serikali kuwazuia kuchimba kokoto.
Mkazi mmoja wa Mji Mwema aliye karibu na makazi ya Rais msitaafu wa wa Zanzibar Alhaji Aboud Jumbe, amesema hali ni mbaya kiasi cha asilimia kubwa ya wakazi wa eneo hilo kujifungia majumbani wakihofia vurugu hizo.

"Ndugu mwandishi wa habari, hali hivi sasa ni mbaya mno, mawasiliano ya usafiri yamekatika kwani wachimba kokoto waliozuiwa kufanya kazi yao, wameandamana huku wengine wakijaza kokoto na mawe barabarani na wengine wakichoma matairi, tunaogopa hivyo tumejifungia majumbani" alisema mama huyo.

Alisema mabomu ya machozi yanaendelea kupigwa na FFU ili kuwatawanya vijana hao, lakini inaelekea ni wabishi.

Blogu yako ya Kamanda wa Matukio itaendelea kuwapatia taarifa juu ya sakata hilo kwa kadri itakavyokuwa inazipata.
CHANZO: mwaikenda.blogspot.com

MAREKANI YAVURUGA MAMBO MASHARIKI YA KATI

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani ina nafasi haribifu kuhusiana na matukio ya Mashariki ya Kati.
Kuhusu mpango wa Marekani wa kutaka kuanzisha eneo lisiloruhusiwa kupaa ndege huko Syria, Ramin Mehmanparast Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa Marekani imeazimia kufanya uharibifu na mauaji huko Syria kama ilivyofanya huko Iraq, Afghanistan, Libya na katika nchi nyinginezo.
Amesema Marekani inajaribu kila inaloweza  kusababisha mauaji mengi miongoni mwa raia na umma wa Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati. Ramin Mehmanparast amesema Marekani inafanya kila iwezalo ili kunufaika zaidi sambamba na waitifaki wake. 
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hivi sasa kunafanywa njama kwa ajili ya kuandaa utangulizi wa kuzusha mapigano ya kijeshi huko Syria kupitia kutangazwa eneo lisiloruhusiwa kupaa ndege na kwamba hiyo ni tahadhari kwa nchi zote za eneo  kwamba fitna kubwa inafanywa ili kuzigombanisha nchi za Kiislamu katika eneo hili na kwamba Marekani na Uzayuni  zinafanya kila linalowezekana kwa malengo yao ya kisiasa  yakuzusha mapigano na kusababisha vifo vya raia wasio nan hatia na kusababisha hasara kubwa katika eneo hili kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni.

JAPAN YAKUMBWA NA TETEMEKO LA ARDHI

Mtetemeko wa ardhi wenye ukubwa wa 7.3 kwa kipimo cha rishta umeyatikisha maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Japan kama ilivyoripotiwa na kituo cha metorolojia cha nchi hiyo. 
Mtetemeko huo wa ardhi umetokea alfajiri ya leo na kitovu cha zilzala hiyo kilikuwa katika pwani ya Hokkaido katika bahari ya Okhotsk. 
Juni 18 mwaka huu pia mtetemeko wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 6.4 kwa kipimo cha rishta ulitokea katika bahari ya Pasifiki, umbali wa kilomita 28 kusini mashariki mwa mji wa Ofunato huko Japan. Hakuna taarifa zozote zilizotolewa hadi sasa kuhusu watu waliopoteza maisha yao na wala maafa yaliyosababishwa na zilzala hiyo ya leo. 
CHANZO REDIO NYUMBANI

MSOMALI AHUKUMIWA MAISHA JELA

Raia mmoja wa Somalia ambaye anayedaiwa kuwa alikuwa mzungumzaji wa maharamia katika kupokea vikomboleo kwa ajili maharamia wa Somalia walioteka nyara meli moja ya Marekani mwaka uliopita na kuwauwa mateka wanne raia wa Marekani amehukumiwa vifungo 12 vya maisha na mahakama ya Marekani. 
Mohamed Shibin alipatwa na hatia mwezi Aprili mwaka huu kwa makosa 15 yakiwemo uharamia, kuteka nyara na kula njama. Mahakma hiyo ya Marekani imesema kuwa Shibin alilipwa kati ya dola elfu 30 hadi 50 kwa kazi yake ya kuwa mzungumzaji wa maharamia kwa ajili ya kupatiwa kikomboleo. 
CHANZO: REDIONYUMBANI

JUMIKI YATOA UFAFANUZI

Ali Issa-Maelezo Zanziba
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) imepinga uvumi uliosambazwa nchini kuwa leo kutakuwa na maandamano ya Jumuiya hiyo na kudai kuwa propaganda hizo zinaendeshwa na baadhi ya watendaji katika jeshi la polisi na usalama wa taifa ambao hawaitakii mema Jumuiya yao.
Hayo yamesemwa na Amiri wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Ahmed wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo Zanzķbar kuhusiana na tuhuma ambazo wamezitoa kwa Jeshi la Polisi dhidi ya Jumuiya yao.
Amedai kuwa Jumuiya haijapanga maandamano kwani ni taasisi inayofanya kazi zake kisheria nakwamba hata ikitokezea kufanya maandamano basi watafuata taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kulitaarifu rasmi Jeshi la Polisi.
Aidha amedai kuwa kuna mkakati wa muda mrefu wa kutaka kuwabatiza viongozi wakuu wa jumuiya hiyo kesi za ugaidi hususan Amir Mkuu wa jumuiya ya Maimamu Zanzibar Sheikh Farid Hadi Ahmed ili kuzima vuguvugu la kudai Zanzibar huru.
Shekh Faridi amedai kuwa inasemekana kuna mahusiano makubwa baina ya watendaji ndani ya Jeshi la polisi pamoja na baadhi ya wageni wanaosadikiwa kuwa ni raia wa Marekani juu ya kuutekeleza mkakati huo baada ya kuwa tayari umeshakamilika.
Amedai kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za kirai ambao umekuwa ukifanywa na Jeshi la Polisi Zanzibar kwa kuwanyima haki ya kufanya mihadhara yao ndani ya Misikiti  ambapo Juni 17 mwaka huu wananchi mbalimbali walijeruhiwa kwa mabomu katika vijiji vya Donge,Mkwajuni na Mahonda.
Ameliomba Jeshi la Polisi kufanya kazi zake za kulinda usalama wa wananchi na mali zao na kuacha kufanya kinyume chake kwani huko ni kuchochea chuki kati ya Jeshi hilo na raia.
Amesisitiza haja ya wazanzibari kuungana na kuachana na Itikadi zao za kivyama katika kudai hadhi ya Rais na mamlaka ya Nchi ya Zanzibar ndani na nje ya Zanzibar pale tume ya mabadiliko ya Katiba itakapoanza kazi zake.
Kwa upande wake Naibu Naibu Amir Jumuiya Ya Uamsho Na Mihadhara Ya Kiisilam Sheikh, Azan Khalid Hamdan amewaomba wanahabari nao kuwa makini katika taaluma yao kwa kufanya usawa wa taarifa ambazo wamekuwa wakizitoa.
Hivi karibuni Jumuiya hiyo ilitangaza rasmi kushiriki kikamilifu katika zoezi zima la kutoa maoni yao katika mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kubadili msimamo wao wa awali wa kuisusia Tume hiyo.

KUFUATIA AJALI YA MV SKAGIT MELI 3 ZAFUTIWA USAJILI ZNZ

Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar imezifutia rasmi hati ya kufanya kazi Meli ya Mv.Kalama, Mv.Seagul na Mv.Sepideh kutokana na meli hizo kutokukidhi hali ya usalama wa abiria katika meli hizo.
Aidha meli hizo zimepewa muda wa mwezi mmoja kuanzia leo kuhakikisha zimeondoka katika maeneo ya Zanzibar kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi ya wamiliki wa Meli hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Afisini kwake kuhusu hali ya usafiri wa baharini na usalama Zanzibar.
Amesema Mamlaka hiyo imefanya tathmini na uhakiki wa kutosha na kujiridhisha kuwa Meli hizo hazifai kufanya kazi katika maeneo ya Zanzibar jambo ambalo limepelekea kuchukua hatua za kufuta hati za kufanyia kazi meli hizo.
Amefahamisha kuwa sababu kuu zilizopelekea Mamlaka kufanya maamuzi hayo ni pamoja na uchakavu,umri wa meli hizo kuwa mrefu na kupata matatizo mara kwa mara katika safari zao.
Kombo amefahamisha kuwa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri na Bandari Zanzibar ya mwaka 2006 kifungu cha 17.1 inampa mamlaka Msajili wa Meli kuifuta meli yoyote ambayo itakuwa haikidhi usalama wa abiria.
Kufuatia sheria hiyo Kombo amesema watawataka wamiliki wa Meli hizo kuzirudisha hati za kufanyia kazi meli hizo ili waende kutafuta sehemu nyengine za usajili kinyume na maeneo ya Zanzibar.
Akizungumzia Meli ya Mv.Serengeti Kombo amesema wamelazimika kuiagiza meli hiyo kupunguza idadi ya abiria kutoka watu 800 hadi 350 na tani za mizigo kutoka 100 hadi 50  hadi pale ambapo watajiridhisha kutokana na hali ya meli hiyo ilivyo.
Aidha amegusia kuwa Kampuni ya Bakhresa italeta Meli kubwa ya abiria itakayofanya kazi zake Zanzibar ambapo pia Serikali ya Mapinduzi nayo iko mbioni kuhakikisha wanaleta meli inayokidhi mahitaji ya wananchi wa Zanzibar.

TUMAINI LILILOPOTEA, LAIBUKA TENA

Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar,Balozi Seif Ali Idd amesema juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutafuta Meli kubwa kwa ajili ya wananchi wake zinaleta matumaini kutokana na Watendaji husika waliopewa agizo hilo kulisimamia kwa nguvu zote katika kulifanikisha.
Amesema Wizara ya Fedha Uchumi na Maendeleo kwa kushirikiana na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzķbar tayari imeanza mikakati ya kupatikana kwa Meli hiyo ikiwa ni pamoja na kukusanya pesa kutoka vyanzo mbali mbali vikiwemo vile vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Balozi Seif ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa hotuba yake ya kuahirisha kikao cha nane cha Baraza la Wawakilishi ambacho kilianza June mwaka huu huko Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.  
Amesema Serikali ya Mapinduzi imejipanga vyema kukabiliana na matatizo yanayowakabili wananchi likiwemo suala la usafiri wa baharini ambapo kupatikana kwa meli hiyo kutaweza kutatua tatizo hilo ambalo limeonekana linaathiri sana uchumi wa wananchi wa Zanzibar.  
Aidha amewahakikishia Wajumbe wa Baraza hilo kuwa ripoti iliyotolewa na Kamati ya kusimamia matumizi ya Serikali PAC, Serikali inaifanyia kazi kwa umakini ili kuweza kutoa maamuzi ya uhakika na sahihi.
Amewataka Wajumbe hao kuendelea kuwa na subra ili suala hilo liweze kukamilika na Serikali haitasita kueleza bayana juu ya maamuzi yake ambayo watayatoa.
Balozi amefahamisha kuwa katika kuwajengea uwezo Akinamama tayari Serikali imetafuta wataalamu wa kufanya uchambuzi yakinifu ili kuanzisha Benki ya Wanawake Zanzibar.
Kuhusu suala la utumiaji wa Madawa ya kulevya Balozi ameeleza kuwa suala hilo linawahusu wananchi wote na kwamba Serikali inawahakikishia usalama wale wote ambao wataweza kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na madawa hayo.
Akielezea juu ya umuhimu wa amani ya nchi Balozi amesema kuwa Amani ya nchi ndio rasilimali muhimu ambayo haifai kuchezewa na kwamba kila mwananchi anajukumu la kuienzi .
Amesema Serikali iko makini katika kukabiliana na viashiria vyovyote vya kuhatarisha amani ya nchi na haitochelea kumchukulia hatua mtu yeyote atakayeweza kuchezea na kuhatarisha amani hiyo.
Balozi amewataka wananchi ambao hawajapata nafasi ya kutoa maoni yao juu ya Katiba mpya kujitayarisha kutoa maoni yao pale zoezi hilo litakapoendelea katika maeneo ambayo bado halijafanyika.
Amesema ni vyema wananchi kujitayarisha vyema kwa kuiga wenzao ambao waliweza kuitumia nafasi hiyo vyema katika Mkoa wa Kusini Unguja na Kusini Pemba.
Kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichoanza mwezi wa Juni kimeahirishwa leo hadi Octoba 10 mwaka huu baada ya kupitisha makadirio ya matumizi ya fedha kwa Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

HIVI NDIVYO ALIVOPOKEWA ULIMBOKA


KAGASHEKI AWATOLEA UVIVU MAFISADI MALIASILI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu uamuzi wa Serikali wa kuwafukuza kazi watumishi watatu wa wizara hiyo kutoka na ukiukaji wa sheria na utekelezaji wa majukumu yao ya kazi kufuatia sakata la usafirishaji wa wanyama pori kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro kwenda Quatar.
Wizara ya Maliasili na Utalii imechukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wake tisa (9) kufuatia kadhia ya utoroshaji wa Wanyamapori Hai katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na masuala mengine yanayohusu Wanyamapori. Watumishi hao wamechukuliwa hatua husika kufuatia kukamilika kwa uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.
(1) Waliofukuzwa kazi kutokana na ukiukaji wa sheria katika utekelezaji wa majukumu yao ni:
- Bw. Obeid F. Mbangwa - Mkurugenzi wa Wanyamapori. Wakati wa kadhia hiyo alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori,
- Bw. Simon Charles Gwera – Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii – CITES na Utalii wa Picha Arusha,
- Bw Frank Mremi - Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii – CITES na Utalii wa Picha Arusha.
(2) Aliyeondolewa Cheo cha Madaraka kutokana na kutochukua hatua kamilifu za ulinzi ambazo zingeweza kuzuia kutokea kwa tukio la utoroshwaji wa wanyama ni:
- Bw. Bonaventura M.C. Midala – Mkurugenzi Msaidizi, Undelezaji Wanyamapori. Wakati wa tukio alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Kuzuia Ujangili.
(3) Wafuatao ni Maafisa Wanyamapori Daraja la II waliotekeleza maelekezo ya Wakuu wao wa kazi yaliyo kinyume cha Sheria ambao wamepewa Onyo Kali la Maandishi:
- Bibi Martha P. Msemo - Afisa Leseni, Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii, CITES na Utalii wa Picha Arusha.
- Bibi Anthonia Anthony – Afisa Leseni, Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii, CITES na Utalii wa Picha Dar es Salaam.
(4) Bw. Silvanus Atete Okudo ni Mkuu wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii, CITES na Utalii wa Picha Arusha aliyeshindwa kufuatilia kupata maelekezo ya Mkurungezi wa Wanyamapori kuhusu mtumishi wake aliyekiuka Sheria katika utoaji wa vibali. Aidha, alishindwa kupeleka kwa Katibu Mkuu taarifa kuhusu mtumishi huyo ili achukuliwe hatua za nidhamu.
- Silvanus Atete Okudo – amepewa Onyo Kali la Maandishi.
(5) Wafuatao ni Maafisa ambao uchunguzi dhidi yao unaendelea:
- Bw. Mohamed Madehele – Ofisi ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori
- Bibi Mariam Nyallu – Kituo cha Uwindaji wa Kitalii, CITES na Utalii wa Picha – Arusha.
Wahusika wengine katika kadhia hiyo wasiokuwa waajiriwa wa Wizara ya Maliasili na Utalii watachukiliwa hatua na mamlaka nyingine husika.
Mhe. Khamis Suedi Kagasheki
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
13 Agosti 2012
Imetolewa kwenye Press Conference iliyofanyika Katika Viwanja vya Bunge Dodoma tarehe 13 Agosti 2012)

JK NDANI YA ACCRAA, GHANA


Rais Jakaya Mrisho Kikwete alipowasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kotoka jijini Accra, Ghana, kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Marehemu John Evans Atta Mills aliyezikwa  Ijumaa Agosti 10, 2012.

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUWEPO KWA MGONJWA WA EBOLA, WILAYA YA KARAGWE MKOA WA KAGERA, TANZANIA

Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu tetesi zilizokuwa zimeenea hapa nchini kutoka kwenye vyombo mbali mbali vya habari kuhusu kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola,wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.
Mnamo tarehe 3 Agosti 2012, Wizara ya Afya na Ustawi Wa Jamii ilipokea taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe ya kuwepo kwa mgonjwa aliyekuwa anahisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola, katika hospitali ya  Wilaya ya Nyakahanga.
Aidha,taarifa hiyo ilibainisha kuwa mgonjwa huyo alikuwa ni mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka (6|)  kutoka katika kijiji cha Nyakatundu wilayani Karagwe. Mgonjwa huyu alikuwa na dalili za homa kali, kulegea, kutokwa damu puani, kutapika damu,  na kukojoa damu.
Maelezo kutoka kwa mama mzazi zilieleza kuwa mtoto huyu alianza kuugua kuanzia tarehe 30 Agosti 2012, ambapo alipatiwa dawa ya Septrin baada ya hospitali binafsi kuonyesha kuwa ana  ugonjwa wa“Typhoid”.
Uchunguzi wa awali katika hospitali ya Nyakahanga ulionyesha kuwa mtoto huyu  alikuwa anasumbuliwa na uambukizo kwenye haja ndogo (Urinary Tract Infection).Vile vile alifanyiwa uchunguzi wa kimaabara na Vipimo vya malaria, Hepatitis na Typhoid havikuonyesha kuwepo  kwa magonjwa haya. Hospitali inaendelea kumpatia matibabu mtoto huyu na imewaweka mgonjwa na mama yake anayemtunza kwenye chumba maalum (Isolatiom room) kwa ajili ya uangalizi zaidi.
Aidha mnamo tarehe 4 Agosti 2012, timu za wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na timu ya mkoa wa Kagera imeweza kufika na kumfanyia uchunguzi wa kina pamoja na kuchukua sampuli za damu kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika maabara ya Taifa ya uchunguzi wa magonjwa na Maabara za nje ya nchi, ili kubaini kama ameathirika na ugonjwa wa Ebola.
Timu hiyo ya wataalamu imetoa taarifa kuwa hali ya mgonjwa huyu kwa sasa imeimarika ikiwa pamoja na kutokuwa na homa, kutapika na kukojoa damu kumekoma pia, uchunguzi uliofanywa kwa mama wa mtoto umeonyesha kuwa hana dalili zozote za ugonjwa wa Ebola.Vile vile hakuna taarifa ya mtu mwingine yeyote kwenye familia hiyo au kwenye maeneo ya kijiji hicho au cha jirani kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Kufuatia taarifa hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera imechukua hatua zifuatazo;
  • Imepeleka timu ya wataalamu mbali mbali kutoka Wizarani na mkoa  kwa lengo la kwenda kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo. 
  • Imetoa elimu ya Afya kuhusu njia za kuzuia kuenea ugonjwa wa Ebola  pamoja na dalili za ugonjwa huu, kwa wananchi na watumishi wa afya katika hospitali ya Nyakahanga
  • Kupeleka vifaa kinga katika hospitali ya Nyakahanga pamoja na maeneo ya mipakani
  • Kutoa matangazo kwa jamii kwa kutumia vipaaza sauti na kupitia  radioni (Radio Karagwe) kuhusu ugonjwa huu.  Aidha, vipeperushi pia vimetolewa.
Hitimisho
Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola hapa nchini.Aidha, Wizara ya Afya imejiaanda kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huu iwapo utatokea hapa nchini.
Kwa sasa timu za wataalum  zipo katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha, kutoa elimu juu ya ugonjwa huu kwa wataalamu na kwa wananchi na vilevile kufuatilia ugonjwa huu sehemu za mipakani.
Wizara inaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa haraka kwenye kituo chochote cha kutolea huduma za afya, mara wanapoona dalili za ugonjwa huu.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,