Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Makamu
wa Pili wa Rais Zanzibar,Balozi Seif Ali Idd amesema juhudi za Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kutafuta Meli kubwa kwa ajili ya wananchi wake
zinaleta matumaini kutokana na Watendaji husika waliopewa agizo hilo
kulisimamia kwa nguvu zote katika kulifanikisha.
Amesema
Wizara ya Fedha Uchumi na Maendeleo kwa kushirikiana na Wizara ya
Miundombinu na Mawasiliano Zanzķbar tayari imeanza mikakati ya
kupatikana kwa Meli hiyo ikiwa ni pamoja na kukusanya pesa kutoka vyanzo
mbali mbali vikiwemo vile vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Balozi
Seif ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa hotuba yake ya kuahirisha
kikao cha nane cha Baraza la Wawakilishi ambacho kilianza June mwaka huu
huko Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Amesema
Serikali ya Mapinduzi imejipanga vyema kukabiliana na matatizo
yanayowakabili wananchi likiwemo suala la usafiri wa baharini ambapo
kupatikana kwa meli hiyo kutaweza kutatua tatizo hilo ambalo limeonekana
linaathiri sana uchumi wa wananchi wa Zanzibar.
Aidha
amewahakikishia Wajumbe wa Baraza hilo kuwa ripoti iliyotolewa na
Kamati ya kusimamia matumizi ya Serikali PAC, Serikali inaifanyia kazi
kwa umakini ili kuweza kutoa maamuzi ya uhakika na sahihi.
Amewataka
Wajumbe hao kuendelea kuwa na subra ili suala hilo liweze kukamilika na
Serikali haitasita kueleza bayana juu ya maamuzi yake ambayo watayatoa.
Balozi
amefahamisha kuwa katika kuwajengea uwezo Akinamama tayari Serikali
imetafuta wataalamu wa kufanya uchambuzi yakinifu ili kuanzisha Benki ya
Wanawake Zanzibar.
Kuhusu
suala la utumiaji wa Madawa ya kulevya Balozi ameeleza kuwa suala hilo
linawahusu wananchi wote na kwamba Serikali inawahakikishia usalama wale
wote ambao wataweza kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na madawa
hayo.
Akielezea
juu ya umuhimu wa amani ya nchi Balozi amesema kuwa Amani ya nchi ndio
rasilimali muhimu ambayo haifai kuchezewa na kwamba kila mwananchi
anajukumu la kuienzi .
Amesema
Serikali iko makini katika kukabiliana na viashiria vyovyote vya
kuhatarisha amani ya nchi na haitochelea kumchukulia hatua mtu yeyote
atakayeweza kuchezea na kuhatarisha amani hiyo.
Balozi
amewataka wananchi ambao hawajapata nafasi ya kutoa maoni yao juu ya
Katiba mpya kujitayarisha kutoa maoni yao pale zoezi hilo
litakapoendelea katika maeneo ambayo bado halijafanyika.
Amesema
ni vyema wananchi kujitayarisha vyema kwa kuiga wenzao ambao waliweza
kuitumia nafasi hiyo vyema katika Mkoa wa Kusini Unguja na Kusini Pemba.
Kikao
cha Baraza la Wawakilishi kilichoanza mwezi wa Juni kimeahirishwa leo
hadi Octoba 10 mwaka huu baada ya kupitisha makadirio ya matumizi ya
fedha kwa Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
No comments:
Post a Comment