MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Sunday, June 21, 2009

Dk. Bana aishauri Serikali


Salim Said
PAMOJA na Serikali kutengua uamuzi wa kufuta misamaha ya kodi kwa Taasisi na Mashirika ya Dini juzi, Msomi na Mchambuzi mashuhuri wa masuala ya kisiasa na uchumi Dk. Benson Bana, ameitaka serikali kuunda Tume Huru ya Wataalam kuchunguza matumizi ya misamaha hiyo kwa miaka mitano iliyopita katika kila dini na dhehebu nchini.


Alisema utitiri wa taasisi hizo unatishia amani ya pato la taifa na kusababisha baadhi yao kuitumia vibaya misamaha hiyo kwa maslahi yao binafsi jambo ambalo linaingizia hasara serikali, ambapo inatumia asilimia 30 ya mapato yake kila mwaka kugharamia misamaha hiyo.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum Ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana alisema, serikali imekuwa laini sana kwa kuwa inatoa misamaha lakini inashindwa kuisimamia.

“Serikali imekuwa laini sana, huwezi kutoa msamaha wa kodi halafu ukaachia huru bila ya kusimamia ni uzembe. Kwa hiyo lazima serikali iunde tume huru ya wataalamu kuchunguza matumizi ya misamaha kwa miaka mitano iliyopita,” alisema Dk Bana na kuongeza:

“Uchunguzi lazima ufanyike kwa dini zote na madhehebu yote na taasisi zitakazogundulika kutumia vibaya misamaha hiyo, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake. Huwezi kuwa na gari tatu halafu unaingiza tairi 400 kutoka nje ya nchi.”

Dk Bana ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam alifafanua, zamani Tanzania ilikuwa na dini nne tu lakini kwa sasa ina dini zaidi ya 100 na kila siku zinaendelea kuchepua kama uyoga.

“Zamani tulikuwa na dini ya kisslaam, Katoliki, Protestant na Hindu lakini sasa utashanga utitiri wa dini umekuwa mkubwa lazima serikali idhibiti hali hii, iache ulegelege. Kila mtu anaanzisha kanisa kwa maslahi yake wenzetu waislaam wamejitahidi,” alifafanua Dk Bana.

Aidha aliitaka serikali, kuangalia gharama za huduma zinazotiolewa na taasisi za dini kwa madai kuwa wanatoa huduma kwa gharama kubwa wakati wanapata misamaha ya kodi.

“Ndio! lazima serikali iangalie gharama wanazotoza ni kubwa ukilinganisha na huduma zao halafu wanapata misamaha ya kodi wanapoingiza vitu nchini,” alisema.

Alisema, misamaha ya kodi iwe katika vifaa na magari yanayoendana na mazingira halisi ya maisha ya watanzania na isiwe vya kifahari.

“Kwa maisha ya kitanzania haiwezekani kwamba Kanisa Bakwata linaingiza magari aina ya Landcruiser VX kwa kila kiongozi wake au hata kwa sheikh wa Mkowa, unaweza kuingiza VX ya baba Askofu au ya Mufti lakini sio kila kiongozi,” alisema Dk Bana.

Kwa upande wake Afisa habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), David Kafulila alisema, kutenguliwa kwa uamuzi wa kufutwa kwa msamaha wa kodi kwa taasisi za dini nchini kumetokana na maamuzi mabovu ya serikali.


Alisema, Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo alisema hawezi kufuta misamaha ya kodi kwa makampuni ya madini hadi hapo watakapokaa na makampuni hayo na kukubaliana lakini kwa mashirika ya dini ilifuta bila ya makubaliano na viongozi wa dini.

“Kutokana na uzembe huo, viongozi wa dini hawakubaliana na uamuzi huo na hatimaye serikali imetengua uamuzi wake. Huku ni kutokuwa makini kwa serikali inapofanya maamuzi yake,” alisema Kafulila.

Aliitaka serikali kuweka wazi mahali itakapopata fedha za kufidia au kugharamia misamaha ya kodi kwa taasisi za dini kwa kuwa haikuwamo katika bajeti na bajeti imepitishwa bila ya marekebisho katika kipengele hicho.

Lwakatare awashukia viongozi wa CUF

Salim Said
ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania bara, Wilfred Lwakatare amewashushia tuhuma nzito baadhi ya viongozi wa wa Chama hicho akidai kuwa jina lake liliachwa kwenye uteuzi wa kutetea nafasi yake kwa fitina na majungu yaliyojaa CUF.

Alisema, hiyo ndiyo sababu kuu iliyomfanya aandike barua ya kujiuzulu nafasi zote katika chama hicho na kubaki kama mwanachama wa kawaida.

Rwakatare alitoa shutuma hizo kupitia mtandao wa Bidii, ambapo alidai maelezo hayo ndiyo aliyoyawasilisha katika kikao cha Baraza Kuu la Taifa la CUF kilichofanyika tarehe 09/06/2009.

Alisema licha ya chama hicho kuyumbishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), pia kuna baadhi ya wanachama na viongozi wenye tabia mbaya ya majungu na fitina dhidi ya wenzao.

Akieleza alisema maelezo ya Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba kwamba uteuzi aliofanya katika nafasi hiyo bara na Zanzibar ulizingatia kifungu na 68,(l)(i) cha katiba ya Chama sio sahihi, jambo ambalo Lwakatare alisema si kweli.

“Majina hayo yaliteliwa kwa kusikiliza majungu, fitina, njama za unafiki, roho mbaya, uchoyo na mtimanyongo wa baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho,” alisema Lwakatare.

Lwakatare alimtuhumu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar ambaye pia ni Mkurugenzi wa Chumi na Fedha Juma Duni Haji kuwa anampikia majungu na ndiye aliyesababisha jina lake kuachwa.

Hata hivyo akijibu tuhuma hizo Duni alisema CUF haina kawaida ya kujibizana na viongozi wake walioacha au kuachwa kupitia vyombo vya habari.

“Sisi CUF hatuna kawaida ya kujibizana na viongozi tuliokuwa nao katika chama na baada ya kujitoa au kuachia ngazi nyadhifa zao kupitia vyombo vya habari,” alisema Duni.

Hata hivyo juhudi za kumtafua profesa Lipumba na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho Ashura Mustafa ambaye alituhumiwa na Lwakatare kwa madai ya kumpakazia kuwa aliangushwa katika unaibu kwa sababu uwezo wake kiutendaji umedidimia (amefulia), hazikufanikiwa.

Matokeo ya wanafunzi wa LST yawa mabovu

Salim Said
MATOKEO ya wanafunzi Chuo cha Sheria yameonyesha kuwa watahiniwa 178 sawa na asilimia 61.1 ya wanafunzi 288, wameshindwa mtihani.

Matokeo hayo ambayo yamebandikwa katika kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani yameonyesha kuwa wanafunzi waliofaulu mtihani huo ni 35 Hayo ni matokeo ya kwanza kwa wanafunzi wa chuo hicho ambao mtihani wao ulifanyika Juni mwaka huu.

Chuo hicho, ambacho ni sehemu ya chuo kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) pia kina ofisi zake Ubungo jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa matokeo hayo, jumla ya wanafunzi 178 sawa na asilimia 61.8 wanatakiwa kurudia mtihani wa baadhi ya kozi huku wanafunzi 45 sawa na asilimia 15.6 wameshindwa kabisa.

Wanafunzi 24 kati ya wanafunzi hao 288 ambao ni sawa na asilimia 8.3 waliahirisha kutokana na sababu mbalimbali ambazo hazikutajwa katika ubao huo, huku wengine sita wakiwa wameekewa mapengo.

Matokeo yalionyesha kwamba, watahiniwa waliofaulu zaidi katika mitihani ni wawili ambao wamepata wastani wa pointi (GPA) 2.5 kila mmoja.

Watahiniwa hao walifuatiwa na wenzao wawili waliopata wastani wa pointi (GPA) 2.4 kila mmoja na kufuatiwa na wengine wawili waliopata wastani wa pointi 2.3 kila mmoja. Watahiniwa waliobakia walipata kati ya wastani wa pointi 0.0 hadi 2.3 ambao ndio wingi.

Hata hivyo Mwananchi ilifika katika ofisi za Chuo hicho zilipo katika Jengo la Ubungo Plaza lakini hakukua na muhusika wa kutoa maelezo juu ya matokeo hayo mabovu ya wanafunzi wake katika mitihani.

Juhudi za Mwananchi kutafuta maoni ya utawala wa chuo hicho hazikuishia hapa, ambapo pia ilitembelea tovuti ya chuo hicho kwa ajili ya kutafuta namba za simu ili kufanya mawasiliano lakini pia hazikufaniwa baada ya kukosekana katika tovuti fiyo ya www.lst.ac.tz.

Mwananchi haikuweza kufahamu mara moja sababu za wanafunzi hao kuanguka kama hivyo katika mitihani yao. Hata hivyo juhudi za kuwatafuta wahusika wa chuo hicho ili kufafanua sababu za kuanguka kwa wanafunzi wao zitaendelea leo.