Salim Said na Ellen Manyangu
SIKU moja baada ya mjane Shamsa Nassor kuhamishwa nyumbani mwake kikatili, Kiluvya jijini Dar es Salaam, Mahakama ya Ardhi Wilaya ya Kinondoni imeamrisha mama huyo arudishwe nyumbani mwake.
Aidha, Kampuni ya Namic Auction Mart ilipewa kazi ya kumrudisha nyumbani mwake mjane huyo chini ya usimamizi mkali wa Polisi kutoka Wilaya ya kipolisi Kimara.
Amri hiyo, nakala tunayo, ilitolewa jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi Kinondini Joseph Kaale na kukabidhiwa kwa kampuni ya Namic kwa ajili ya utekelezaji.
“Mahakama imeamrisha kwamba muombaji katika ombi hili arudishwe nyumbani mwake ambamo alitolewa bila ya sababu za msingi, haraka iwezekanavyo” alisema Kaale katika nakala ya amri hiyo.
Safari ya kwenda kumrudisha nyumbani mwake mjane huyo, ilianzia Kinondoni kupitia kituo cha polisi Mbezi, ofisi ya serikali ya Mtaa Kiluvya na Mjumbe wa Shina la eneo hilo.
Ilichukua takriban masaa mawili hadi juhudi za Mkurugenzi Mtendaji wa Namic Michael Mwenda kufanikiwa kuopata asakari wawili kwa ajili ya kulinda amani na usalama wakati wa urudishwaji wa mjane huyo.
Aidha baada ya kufika eneo la tukio, askari wa Kampuni ya Ulinzi ya General na mwakilishi wa Abdallah Malik aliyejitambulisha kwa jina la Abdu Mkata waligoma kufungua lango la kuingilia licha ya askari waliotumwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kimara (OCD) N. Ndaki.
“Mimi sipo tayari kufungua nipo tayari hata kufa, kufungwa au kukamatwa na polisi. Subirini niwasiliane na Malik au turudini kwa OCD” alisema Mkata.
“Usikubali, usikubali bora tukalale ndani kuliko kumwachia huyu mama aingie humu ndani kwa kuwa Malik hatatuelewa,” alisistiza kumueleza Mkuu wa General Guard Haroub Mbelwa.
Hata hivyo, Mwenda aliamua kuwasiliana na OCD na kumueleza kwamba amri iliyotumika kumtoa mama huyo haikufuata utaratibu na kwamba amri kumrudisha ni halali na kwa hiyo atakaekaidi atashitakiwa.
Baada ya majibizano marefu kati ya askari hao na Viongozi wa Namic hatimae waliachia ngazi bila ya kutoa funguo na wao kuamua kurudi kituo cha polisi Mbezi kwa ajili ya kumuona OCD kwa majadiliano zaidi.
Baada ya wao kuondoka uamuzi wa kuvunja kufuli na minyororo katika milango ya kuingia ndani ya eneo na nyumba ya mjane huyo ulipitishwa na kufanywa na viongozi wa Namic.
Kwa upande wake Shamsa alilishukuru sana gazeti la Mwananchi kwa kuandika habari hiyo pamoja na mahakama ya ardhi kwa kumpatia amri ya kurudishwa ndani ya nyumba yake.
“Nimefurahi sana, pia natoa shukurani zangu kwa gazeti la Mwananchi maana leo (jana) tangu asubuhi napokea simu za pole kutoka na habari hiyo. Lakini nawaomba muendele kufuatilia, serikali nayo ifuatilie ili ijue ukweli wa kesi,” alisema Shamsa na kuongeza:
“Lakini hofu yangu ni usalama na amani yangu kwa kuwa tukio hili limenitisha sana na chochote kinaweza kikanitokea kutokana na vitisho nilivyopewa na shemeji yangu Malik.”
Hadi Mwenanchi inaondoka eneo la tukio jana majira ya saa 11:05 OCD Ndaki alipiga simu na kumtaka Shamsa kuripoti Polisi Kimara kwa taratibu zaidi za kipolisi.
Shamsa alihamishwa nyumbani mwake kwa nguvu juzi na kampuni ya Yono Auction Mart, kitendo ambacho kilimsababishia hasara na majeraha mwilini.