HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA MHESHIMIWA BERNARD KAMILLIUS MEMBE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kufuatia
taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba sasa
kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
2. Mheshimiwa Spika, awali
ya yote napenda kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa
kuliongoza kwa umahiri mkubwa Bunge hili la Bajeti la mwaka 2012/2013. Napenda
pia kuwapongeza Mheshimiwa Job Ndugai (Mb.), Naibu Spika na Waheshimiwa
Wenyeviti wanaokusaidia kuongoza Bunge hili kwa kazi nzuri
wanayoifanya.
3. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kwa uongozi wake mahiri wa Serikali ya Awamu ya Nne. Chini ya uongozi
wake Taifa letu limeendeleza utamaduni wetu wa kudumisha amani, utulivu
na mshikamano. Nawaomba Watanzania wote tuendelee kudumisha hali hiyo
ili kuimarisha umoja wetu ambao ni tunu isiyopatikana kwa bei yoyote.
4. Mheshimiwa Spika, niruhusu niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine wote walionitangulia kuwapongeza kwa dhati kabisa Waheshimiwa
Wabunge wapya, Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa na Mheshimiwa
Rais mwezi Mei 2012. Nawapongeza Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati
za Kudumu za Bunge waliochaguliwa kipindi hiki kutokana na mabadiliko
yaliyotokea kwenye nafasi mbalimbali humu Bungeni na ndani ya Serikali.
Nampongeza pia Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala, kwa
kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge.
5. Mheshimiwa Spika, kwa njia ya kipekee kabisa, niruhusu niwapongeze Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa na Bunge lako Tukufu kuiwakilisha Tanzania
kwenye Bunge la Afrika Mashariki. Wizara yangu kwa kuwa ndiyo
inayosimamia masuala yote ya mambo ya nje, nawaahidi Waheshimiwa Wabunge
ushirikiano wangu binafsi na ule wa Wizara nzima kwa kufanya kazi kwa
karibu na kushirikiana na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
6. Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru
pia Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.), Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa William A. Mgimwa (Mb.),
Waziri wa Fedha; pamoja na Mheshimiwa Stephen Masatu Wasira (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa
hotuba zao za kina ambazo zimetoa ufafanuzi na miongozo kwa masuala
mbalimbali muhimu ya Taifa letu kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kwa ujumla
wake, naomba kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote waliotangulia
kuwasilisha bajeti zao kwa kazi nzuri walizozifanya. Hotuba zao zote
zimefafanua kwa kina masuala ya uchumi, siasa na jamii yanayohusu nchi
yetu na hivyo kuigusa pia Wizara yangu kwa njia moja au nyingine.
7. Mheshimiwa Spika,
naomba nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati na za uongozi
mzima wa Wizara kwa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na
Usalama (NUU), chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Edward Ngoyai Lowassa (Mb.),
Mwenyekiti wa Kamati kwa ushauri wao mzuri ambao wamekuwa wakiutoa mara
kwa mara kwa Wizara yangu. Kamati hii imetoa mchango mkubwa sana
katika kuiwezesha Wizara kukabiliana na changamoto zinazoikabili katika
kutekeleza majukumu yake. Ninaamini ziara walizozifanya kwenye nchi
mbalimbali kutembelea Balozi zetu zimewapa fursa ya kujionea wenyewe na
kusikia kutoka kwa maafisa wetu changamoto mbalimbali zinazotukabili
kama Wizara. Aidha, kwa ujumla, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge
wote kwa michango yao wanayoitoa Bungeni katika kuishauri Serikali.
8. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani na pongezi maalum kwa Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
kwa ushirikiano anaonipa katika kutekeleza majukumu ya Wizara.
Vilevile, nawapongeza na kuwashukuru Bwana John M. Haule, Katibu Mkuu,
Mheshimiwa Balozi Rajabu H. Gamaha, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi,
Mabalozi na wafanyakazi wote kwa msaada mkubwa wanaonipa katika
kuiongoza Wizara hii. Pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali
katika kutekeleza majukumu yao, nawashukuru kwa kazi nzuri na ya kizalendo ya kutetea maslahi ya Taifa letu.
9. Mheshimiwa Spika, shukrani za pekee ziwaendee wananchi na viongozi wa Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Lindi na hasa wana-Mtama wote. Napenda pia nimshukuru mke wangu Mrs. Membe na watoto wangu kwa upendo na uvumilivu waliouonesha kwangu.
10. Mheshimiwa Spika,
kabla ya kuanza kueleza kwa kina kuhusu hotuba yangu, niruhusu niungane
na Viongozi wote, Wazanzibari na Watanzania kutoa pole kwa ndugu, jamaa
na marafiki wote waliopoteza ndugu zao kwenye ajali ya meli ya MV Skagit
iliyotokea Zanzibar. Kwa wale wote walioumia na wanaoendelea kujiuguza,
namwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu waweze kupona haraka.
11. Mheshimiwa Spika,
vilevile, natoa salamu za pole kwa wale Wabunge wote waliopatwa na
misiba ya wapendwa wao. Kwa wote, namwomba Mwenyezi Mungu awape faraja
na azilaze Roho za Marehemu mahali pema peponi. Amina.
12. Mheshimiwa Spika,
kwa ujumla, hali ya dunia kiuchumi, kisiasa na kijamii katika mwaka wa
fedha 2011/2012 imekuwa ya mashaka makubwa na hivyo kuathiri utulivu
katika nchi nyingi duniani. Hali hiyo imechochewa na mabadiliko ya
kisiasa, kiuchumi, kijamii na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo
mbalimbali duniani.
13. Mheshimiwa Spika, eneo la Ulaya limeathirika sana
kiuchumi kutokana na madeni pamoja na mdororo wa uchumi ulioikumba
dunia katika kipindi cha mwaka 2008. Hali hii pia iliathiri kwa kiasi
kikubwa sarafu ya Euro, uchumi wa nchi zilizo katika ukanda wa sarafu
hiyo ujulikanao kama “Eurozone”
pamoja na nchi ambazo zinafanya biashara na nchi za Umoja wa Ulaya.
Hali hiyo imechangia kwa kiwango kikubwa Viongozi katika baadhi ya nchi
hizo kama vile; Ufaransa, Ugiriki, Italia, Hispania na Ireland
kushindwa katika Chaguzi Kuu au kushinikizwa kujiuzulu. Kwa upande wa
Marekani nayo ilikumbwa na misukosuko ya uchumi iliyosababishwa pia na
mdororo wa uchumi wa mwaka 2008. Hata hivyo, uchumi wake umeanza
kutengemaa baada ya mdororo huo.
14. Mheshimiwa Spika, kutokana
na mdororo huo, nchi hizo zimelazimika kuchukua hatua kadhaa kunusuru
uchumi wao ikiwa ni pamoja na kubana matumizi, kukopa zaidi ili kuwekeza
katika sekta zenye kutoa ajira na kupunguza kutoa misaada kwa nchi
zinazoendelea ikiwemo Tanzania kulingana na ahadi zao za awali. Kuna
kila kiashiria kuwa uchumi wa Ulaya na Marekani hautapata utulivu kwa
muda mrefu na hivyo uwezo wao wa kutoa misaada kupungua kadiri siku
zinavyokwenda. Wizara na Balozi zetu za nje zinaendelea kufuatilia kwa
makini hali ya uchumi inavyoendelea duniani na kuishauri Serikali
kutekeleza mikakati ya kukabiliana na changamoto zitokanazo na hali hiyo
ili kuimarisha uchumi wa Taifa letu na kuondokana na utegemezi.
15. Mheshimiwa Spika, eneo la Mashariki ya Kati bado liko katika hali ya tahadhari. Nchini Syria hali imeendelea kuwa tete kutokana na
mapigano yanayoendelea nchini humo ambako waasi wanapigana dhidi ya
Serikali ya Rais Bashar al – Assad tangu Januari mwaka 2011 na tayari
wameshaingia kwenye Mji Mkuu wa Nchi hiyo. Umoja wa Mataifa na Jumuiya
ya Nchi za Kiarabu (Arab League) zikiongozwa na Msuluhishi wa Mgogoro
huo, Dkt. Kofi Annan wameshindwa hadi sasa kufanikisha kusitishwa kwa
mapigano. Aidha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limegawanyika
ambapo wajumbe wa kudumu wenye kura ya turufu wametofautiana juu ya
uamuzi wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Serikali ya Syria. Tanzania
inaunga mkono jitihada za Msuluhishi Kofi Annan na kuwaomba wadau wote
kutoingilia na kushinikiza matakwa yao nchini Syria na badala yake
kumuunga mkono Msuluhishi ili kumaliza mgogoro huo kwa njia ya amani.
16. Mheshimiwa Spika,
aidha, kuendelea kukua kwa uhasama baina ya Iran na nchi za Magharibi
kunaleta changamoto ya ustawi wa amani katika ukanda huo. Uhasama huo
unaletwa na hofu kuwa nchi ya Iran inarutubisha madini ya urani
yanayotumika kutengeneza silaha za nyuklia. Tayari, Iran imewekewa
vikwazo vya kiuchumi na Marekani ikishirikiana na nchi za Umoja wa
Ulaya. Iran
nayo imetishia kujibu mapigo kwa kufunga mlango wa Bahari ya Hormuz
ambao hupitisha asilimia ishirini 20 ya mafuta yote ulimwenguni. Iwapo
Iran itatekeleza uamuzi huo inaweza kuzusha vita ambayo italeta madhara
makubwa kwa uchumi wa dunia. Hali hii ya mtafaruku baina ya Iran na nchi
za Magharibi inaathiri pia mustakabali wa ukanda mzima wa Mashariki ya
Kati kwa kuwa Iran ina ushawishi mkubwa kwenye siasa za nchi nyingine
zenye machafuko kama vile Syria.
Kuendelea kwa migogoro na machafuko katika ukanda wa Mashariki ya Kati
kunaathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa dunia kwa sababu asilimia kubwa
ya mafuta yanayotumika duniani hutoka katika ukanda huo. Pamoja na
changamoto hizo, habari njema ni kwamba tayari Irani, Marekani, Nchi za
Ulaya pamoja na wadau wengine wameshakubaliana kurejea kwenye meza ya
mazungumzo na tayari mzunguko wa kwanza wa mazungumzo haya
umeshafanyika. Imani yetu kama nchi ni kwamba wahusika wote kwenye
mazungumzo hayo wataonesha utashi wa kweli wa kumaliza tatizo hilo kwa
njia ya mazungumzo na si vinginevyo.
17. Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa Mashariki ya Mbali hali ni tulivu ukiachilia majanga ya asili
yaliyozikumba nchi za Japan, Ufilipino na Thailand na kusababisha
athari za kijamii na kiuchumi kwa baadhi ya sekta, hususan viwanda na
makazi ya watu. Hali ya kiusalama katika Peninsula ya Korea
nayo imeonekana kutulia kidogo kufuatia mabadiliko ya uongozi nchini
Korea Kaskazini baada ya kifo cha Rais Kim Jong-il aliyekuwa Rais wa
Korea Kaskazini. Aidha, kwa upande wa Japan,
hali ya kiuchumi imeanza kuimarika hasa baada ya kukumbwa na tukio la
Tsunami la mwaka 2011 lililoathiri kwa kiasi kikubwa kinu cha nyuklia
cha Fukushima.
18. Mheshimiwa Spika, kama
ilivyo kwenye maeneo mengine duniani, Bara la Afrika nalo limeathiriwa
na hali ya mitikisiko ya aina mbalimbali duniani, ikiwemo ya kiuchumi,
kisiasa na kijamii. Maendeleo ya Bara hili yameendelea kukabiliwa na
changamoto za kiusalama, kisiasa, kiuchumi, kijamii, mabadiliko ya
tabianchi, vitisho vya ugaidi, uharamia wa baharini, kupanda kwa gharama
za bidhaa muhimu kama vile chakula,
matatizo ya nishati ya umeme na kukosekana kwa ajira. Pamoja na masuala
hayo ya jumla, yapo baadhi ya masuala ambayo yanaweza yakaipambanua hali
ya Barani Afrika kwa sasa, hasa katika kipindi hiki cha miezi sita
iliyopita. Aidha, kuna masuala yanayozigusa baadhi ya nchi kama inavyoelezwa hapa chini:
19. Mheshimiwa Spika,
suala kubwa lililotawala hali ya kidiplomasia Barani Afrika ndani ya
mwaka wa fedha 2011/2012 ni uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja
wa Afrika. Kama itakavyokumbukwa, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika
mwezi Januari, 2012 wakati wa Mkutano wa 18 wa Umoja wa Afrika wa
Wakuu wa Nchi na Serikali. Ushindani mkali ulizuka kati ya wagombea
wawili waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ambao ni Bw. Jean Ping wa Gabon,
Mwenyekiti wa Kamisheni aliyemaliza muda wake na Bibi Nkosazana
Dlamini-Zuma, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini. Mvutano huo
ulisababisha Wakuu wa Nchi kushindwa kumchagua Mwenyekiti mpya wa
Kamisheni hiyo baada ya wagombea wote wawili kushindwa kufikia theluthi
mbili za kura zinazohitajika kisheria.
20. Mheshimiwa Spika,
kutokana na kukosekana mshindi, Wakuu wa Nchi na Serikali waliamua
kuahirisha uchaguzi huo hadi kwenye mkutano wao wa 19 uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia,
mwezi Julai 2012. Katika uchaguzi huo, Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma,
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini, alifanikiwa kuibuka mshindi.
Hivyo, Mama Zuma anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Kamisheni hiyo.
Ushindi wa Bi. Nkosazana Zuma ni ushindi wetu pia kwa kuwa alikuwa ni
mgombea wa SADC na Tanzania ilishiriki kikamilifu katika kampeni zake.
21. Mheshimiwa Spika, hali
ya kisiasa nchini Misri ilishuhudia matokeo ya machafuko yaliyopelekea
kuangushwa kwa utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa Hosni
Mubarak. Baada ya utawala wa Mpito ulioongozwa na Jeshi la nchi hiyo,
hatimaye Chama chenye mlengo wa kushoto cha Udugu wa Kiislam (Muslim
Brotherhood) kimefanikiwa kushinda uchaguzi huru uliofanyika Juni, 2012
kupitia mgombea wake Mheshmiwa Dkt. Mohammed Mursi. Wizara
yangu itashirikiana na Serikali mpya na kuendeleza mahusiano mazuri
baina ya nchi zetu mbili ikizingatiwa kuwa Misri ni mdau muhimu katika
kufanikisha matumizi ya rasilimali za Bonde la Mto Nile kwa maslahi ya
pande zote husika.
22. Mheshimiwa Spika, ni vyema kutambua kuwa ingawa uchaguzi umefanyika bado hali ya kisiasa ni tete. Hii
ni kwa sababu licha ya kuwa Muslim Brotherhood wameshinda kwa kuwa na
Wabunge wengi Bungeni na kushika Ikulu, bado Jeshi la Misri linaendelea
kushika hatamu za uongozi. Jeshi limevunja Bunge na ndilo linalofanya maamuzi makubwa.
23. Mheshimiwa Spika,
ni matumaini yetu kwamba hali hiyo tete ya kisiasa itatengemaa na hali
kuwa nzuri. Tanzania itashirikiana na Serikali mpya ya Misri ili
kuendeleza na kudumisha mahusiano yetu ya kirafiki na ya kihistoria.
24. Mheshimiwa Spika, baada
ya aliyekuwa Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Qaddafi kuuawa na
Serikali yake kupinduliwa na wapinzani wa NTC, Libya ilikumbwa na
matatizo ya usalama. Mauaji ya Walibya weusi yaliendelea. Hakukuwa na Serikali madhubuti, hakukuwa na Bunge na wala hakukuwa na taasisi za Kidemokrasia.
25. Mheshimiwa Spika, Tanzania
tulilaani mauaji ya Kiongozi huyo na tulisema kuwa tungalitambua
Serikali ya NTC tu iwapo ingalikuwa na viongozi wa kuchaguliwa, Bunge,
Mahakama na uundwaji wa Serikali ya mpito ambayo itajumuisha wadau
kutoka vyama vyote vya siasa.
26. Mheshimiwa Spika, uchaguzi wa kwanza wa Kidemokrasia ulifanyika Libya mwezi Julai, 2012 kuchagua Wabunge 200. Waombaji 3,000 walijitokeza kugombea nafasi hizo. Pamoja
na matatizo yote ya kiusalama, wananchi milioni moja na laki nane
waliweza kuchagua Wabunge wao 200 na Bunge linategemewa kumchagua Rais
na Waziri Mkuu katika kipindi cha siku 30 baada ya uchaguzi. Zoezi
hilo limekamilika. Aidha, Bunge limechagua kutoka miongoni mwao Wabunge
60 wa kuunda Baraza la kuandika Katiba mpya, na Baraza hilo limepewa
siku 120 kuwakilisha mapendekezo ya Katiba kwenye Bunge lao. Mchakato
huo umeanza.
27. Mheshimiwa Spika,
uongozi wa Serikali ya Libya umekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Kikwete mjini Addis Ababa tarehe 15 Julai, 2012
na ukaeleza nia yake ya kutuma ujumbe Tanzania kuja kutoa taarifa ya
hali ya usalama na kisiasa na kufufua rasmi mahusiano ya Kibalozi na
Tanzania. Tunausubiri ujumbe huo na sisi sasa tumeridhika na mchakato wa kujenga demokrasia unaoendelea nchini Libya. Tanategemea
kuletewa hati za Balozi mpya hivi karibuni na tutazipokea ili tuweze
kurejesha huduma za Kibalozi kama ilivyokuwa mwanzo.
28. Mheshimiwa Spika,
hali ya kisiasa na kiusalama nchini Somalia kwa sasa inatia matumaini
ya kupatikana kwa amani kutokana na juhudi za Umoja wa Afrika pamoja na
washirika wake katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa muda mrefu wa nchi
hiyo. Serikali ya Mpito ya Somalia
inatarajiwa kumaliza muda wake mwezi huu Agosti, 2012 na tayari rasimu
ya Katiba kwa ajili ya Serikali mpya imeandaliwa na inatarajiwa kupitiwa
na Baraza la Katiba linalojumuisha Wazee kutoka Koo zote tarehe 20
Agosti 2012. Kupatikana kwa Serikali mpya ambayo uhalali wake utatokana
na wananchi wenyewe inatazamiwa kutoa fursa kwa Wasomali kujenga
mustakabali mpya wa taifa lao.
29. Mheshimiwa Spika,
hali ya usalama katika mji wa Mogadishu sasa ni ya kuridhisha kutokana
na jitihada za majeshi ya AMISOM na yale ya Kenya kudhibiti maeneo na
miji muhimu iliyokuwa ngome ya Al-Shabaab.
Pamoja na kuwa wamedhibitiwa, Al-Shabaab wameendelea kufanya matukio
machache nchini Kenya ikiwa ni njia ya kulipiza kisasi. Hali hiyo
imeleta hofu kwa watalii na wageni kutoka nje wanaotembelea ukanda wa
Afrika Mashariki. Serikali zetu zinashirikiana kwa karibu katika
kuimarisha usalama dhidi ya vitendo vya uharamia vya Al-Shabaab. Vivyo
hivyo, hali ya usalama katika pwani ya Bahari ya Hindi na Ghuba ya Aden
nayo inazidi kuimarika na matukio ya uharamia kupungua kutokana na
operesheni inayoendelea kati ya nchi za pwani ya Afrika Mashariki kwa
kushirikiana na Umoja wa Ulaya. Katika mwaka 2011/12 peke yake, Jeshi la
Wananchi liliweza kudhibiti matukio 27 ya uharamia. Tuungane
kulipongeza jeshi letu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda mipaka ya
nchi yetu. Tunachukua jitihada za makusudi kulisaidia jeshi letu kupata
vifaa madhubuti kwa ajili ya ulinzi wa pwani yetu ambayo ina utajiri
mkubwa wa gesi asilia dhidi ya maharamia hawa.
30. Mheshimiwa Spika, hali ya usalama mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ukanda wa Maziwa Makuu kwa ujumla nayo iko tete hata baada ya uchaguzi
wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulimalizika na Rais Joseph
Kabila kutangazwa mshindi dhidi ya mpinzani wake mkuu Bw. Etienne
Tshisekedi. Mapigano
yameripotiwa kutokea hivi karibuni tarehe 6 Julai, 2012 Kaskazini
Mashariki mwa DRC. Kikundi cha waasi kijulikanacho kama M23
kinachosemekana kinaongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda anayesakwa na
Jumuiya ya Kimataifa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita kujibu tuhuma mbele
ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kinadaiwa kuhusika na
mapigano hayo. Kikundi hicho kinasadikiwa kuyateka na kuyadhibiti
baadhi ya maeneo ya Mashariki ya DRC yakiwemo Rutshuru, Bunagana na
Kivu. Majeshi ya Umoja wa Mataifa yameingilia kati kwa kutoa ulinzi
katika mji wa Goma, na tarehe 25 Julai, 2012 yalilazimika kutumia silaha
kuwasambaratisha M23 kutoka kwenye maeneo wanayoyashikilia.
31. Mheshimiwa Spika, Wakuu
wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, katika kikao chao tarehe 14 Julai,
2012 waliuomba Umoja wa Mataifa kuongeza wanajeshi wa kulinda amani kwa
lengo la kudhibiti usalama wa mpaka kati ya DRC na Rwanda
ili kurejesha hali ya kuaminiana baina ya nchi hizi mbili. Vilevile,
walikubaliana kufufua mpango wa usuluhishi uliokuwa chini ya Mheshimiwa
Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania na Mheshimiwa Olesegum Obasanjo, Rais Mstaafu wa Nigeria. Serikali ya Tanzania
inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya kisiasa na kiusalama nchini
DRC kwa kuwa machafuko hayo yanatuathiri kiuchumi, kisiasa, kijamii na
kiusalama. Ni kutokana na hali hiyo, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho
Kikwete anahudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu
utakaofanyika Kampala nchini Uganda kesho tarehe 7 Agosti, 2012.
32. Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012, Wizara imetekeleza jukumu
la uratibu wa masuala ya ushirikiano wa kikanda kwa kuendelea kushiriki
kikamilifu katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya
ya Ushirikiano ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IOR-ARC) na
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Kwa kuwa eneo
la Jumuiya ya Afrika Mashariki limeelezewa vizuri na Waziri husika
kwenye hotuba ya bajeti yake, niruhusu nidurusu masuala machache yafuatayo:
33. Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Agosti, 2011 Tanzania iliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Kutokana
na uteuzi huo, Tanzania imeingia katika Kamati hiyo ya Utatu (Troika)
ambayo kwa sasa inaongozwa na nchi ya Afrika Kusini. Ifikapo tarehe 17 Agosti, 2012 Tanzania itatwaa rasmi Uenyekiti
wa Asasi hiyo muhimu ya SADC ambayo itaipa jukumu la kusimamia,
kufuatilia na kushiriki kwa kina katika masuala yote ya siasa, ulinzi na
usalama ya Nchi za SADC, hususan katika nchi za Madagascar na Zimbabwe
ambazo ziko kwenye agenda ya SADC Troika kwa sasa.
34. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kupata mgao kidogo sana
wa bajeti isiyokidhi mahitaji katika mwaka wa fedha 2011/2012. Katika
kipindi tajwa, Wizara yangu ilipata asilimia 44 tu ya Bajeti iliyoombwa. Bajeti ndogo tunayopewa imekuwa changamoto kubwa katika kutekeleza Diplomasia
ya Uchumi kwa kiwango kinachostahiki. Hata hivyo, pamoja na mapungufu
hayo, Wizara yangu kwa nafasi yake kama kiungo muhimu cha nchi yetu na
nchi za nje imeendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara, Idara na
Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na sekta binafsi kuhakikisha
kwamba nchi yetu inafaidika kwa kadri iwezekanavyo na fursa mbalimbali
zenye manufaa kwa nchi yetu katika sekta za uchumi na jamii. Juhudi zetu
katika kutafuta fursa hizo zilizingatia vipaumbele katika Mpango wa
Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/12 - 2015/16. Niruhusu
nitumie fursa hii kueleza kwa uchache mchango wa Wizara yangu kwenye
sekta mbalimbali katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo wa
Maendeleo wa Miaka Mitano.
35. Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa sekta ya nishati, Wizara yangu kupitia Ubalozi wetu nchini
China imeshirikiana bega kwa bega na Wizara ya Nishati na Madini pamoja
na Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata mkopo wa Dola
za Marekani bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi
asilia kutoka Mtwara hadi Dar es salaam. Kama ilivyokwishaelezwa na
Waziri wa Fedha hapa Bungeni, tayari mkataba wa kupata fedha hizo
umekwisainiwa na Mheshimiwa Philip Marmo, Balozi wetu nchini China kwa
niaba ya Serikali. Uzinduzi wa ujenzi wa Bomba hilo ulifanyika tarehe 21
Julai, 2012 Mkoani Mtwara. Ujenzi wa bomba hilo utaleta mapinduzi
makubwa sana
katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi. Bomba la zamani lilikuwa
dogo na lisilokidhi mahitaji ya kusafirisha kiasi kikubwa cha gesi
kwenda Dar es Salaam. Pindi ujenzi wa bomba hilo utakapokamilika fursa
nyingi za uchumi zitafunguka na kuimarika hasa zile zote zinazotumia
gesi.
36. Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu pia ilikuwa mstari wa mbele katika kuishawishi Tume ya Uhifadhi
Duniani (World Heritage Commission-WHC) na jumuiya ya kimataifa kukubali
kurekebisha mpaka wa Hifadhi ya Selous ili kuruhusu uchimbaji wa madini
ya urani kufanyika kusini mwa hifadhi hiyo. Juhudi zetu zimezaa
matunda ambapo mwezi Juni, 2012 WHC wameridhia hoja zetu, jambo ambalo
huwa si rahisi kufanywa na Tume hiyo. Ushindi huu ni kielelezo cha nguvu
ya ushawishi wetu na kuaminika kwetu duniani. Matarajio yetu ni kwamba
Kampuni ya Uranium One kutoka Urusi itaanza kazi ya utafiti na hatimaye
uchimbaji muda si mrefu mara baada ya kukamilisha taratibu zingine na
Wizara husika za Maliasili na Utalii na Wizara ya Nishati na Madini.
37. Mheshimiwa Spika, kwa
kutambua hofu za msingi juu ya usalama wa uchimbaji wa madini hayo,
Wizara yangu imetoa pia msukumo katika upatikanaji wa wataalam na
mafunzo na hivi karibuni Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na
Madini imekwenda Nchini Australia na Namibia kujifunza namna ya kuendesha miradi ya urani. Tanzania
itatumia nafasi yake ya Ujumbe wa Bodi ya Shirika la Atomiki Duniani
(IAEA) kupata kila aina ya utaalamu na uzoefu kuhakikisha kuwa uchimbaji
wa madini hayo unafuata taratibu na viwango vya kiusalama vinavyotolewa
na IAEA.
38. Mheshimiwa Spika, jitihada za Wizara yangu kuufufua mradi wa umeme wa Stieglers Gorge nazo
zinaanza kuzaa matumaini. Kufuatia jitihada za Wizara yangu, Mheshimiwa
Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu walifanya Ziara nchini Brazil ambapo agenda ya mradi wa Stieglers Gorge ilipewa kipaumbele kikuu. Kutokana na ziara hizo, Kampuni ya Brazil ya ODEBRECHT
na Shirika la RUBADA kwa upande wa Tanzania wameshasaini Makubaliano ya
Awali (MoU) kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme
ambao unakadiriwa utazalisha zaidi ya megawati 2,100 za umeme wa
uhakika na wa bei nafuu. Wizara yangu itaendelea kufuatilia ili
kuhakikisha Wataalam wanaotakiwa kuja tena nchini kwa ajili kufanya
mapitio ya taarifa ya environmental impact assessment (EIA) na upembuzi yakinifu wanafanya hivyo ili mradi huo uweze kuanza mara moja.
39. Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa sekta ya kilimo, Wizara yangu imeshirikiana kwa karibu na
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika katika kufanikisha upatikanaji wa
teknolojia ya umwagiliaji kutoka nchini India
chini ya makubaliano ya Mpango wa Maendeleo wa India-Afrika.
Makubaliano mahsusi haya ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili
yanayotokana na ziara ya Rais wa India
hapa nchini mapema mwezi Februari 2012. Vilevile, Wizara yangu
ilishiriki na kushuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Awali kati ya
Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Jain Irrigation ya India
mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kutekeleza kwa pamoja
miradi ya umwagiliaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Wizara yangu pia
imeendelea kuishawishi Serikali ya India
kutupatia mkopo kwa ajili ya awamu ya pili ya mradi wa Matrekta.
Matumaini yetu ni kwamba juhudi hizo zitazaa matunda katika mwaka huu wa
fedha.
40. Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu imeshiriki katika kufanikisha ushiriki wa nchi yetu
katika Mkutano wa nchi Tajiri na zenye Viwanda vikubwa duniani
zinazojulikana kama G8 uliyofanyika
nchini Marekani. Mkutano huo ulikuwa na mafanikio makubwa kwa sekta ya
kilimo nchini baada ya mataifa hayo kutoa ahadi ya Dola za Marekani milioni 890. Aidha, makampuni binafsi ya nchi hizo yaliahidi kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni 3 katika
sekta ya kilimo. Katika mwaka huu wa fedha, Wizara yangu itaelekeza
nguvu zake kuvutia wawekezaji kutoka nchi za Japan, Korea Kusini na
China
kuwekeza katika Ukanda wa Kusini wa SAGCOT na vilevile kuanzisha kanda
nyinginezo za kilimo magharibi, kaskazini na mashariki mwa nchi yetu.
41. Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa Sekta ya Miundombinu, Wizara yangu imeendelea kushirikiana na
Wizara ya Ujenzi katika kutafuta misaada na mikopo kwa ajili ya ujenzi
wa miundombinu. Katika mwaka wa fedha 2011/2012, Wizara yangu kupitia
Ubalozi wetu Japan,
iliweza kuishawishi Serikali ya Japan kugharamia upanuzi wa barabara
ya Gerezani na Mwenge-Morocco. Hivi sasa tunaendelea na juhudi za
kuwashawishi ndugu zetu wa Japan watusaidie kujenga barabara za juu
(Flyovers) maeneo ya Tazara. Wameonesha utayari wao kutusaidia.
Vilevile, Wizara yangu inaendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi
kupata wawekezaji wa ujenzi wa barabara ya njia sita ya kutoka Ubungo
hadi Chalinze chini ya mpango wa ushirikiano wa sekta binafsi na sekta
ya umma (PPP). Matumaini yetu ni kwamba ujenzi wa barabara hizi
utasaidia kupunguza tatizo sugu la msongamano wa magari jijini, Dar es
Salaam na yale yanayokwenda mikoani na nje ya nchi na hatimaye
kupunguza madhara ya kiuchumi yatokanayo na msongamano mkubwa wa magari.
42. Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa sekta ya maji, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya
Maji na Wizara ya Fedha tumeweza kuishawishi Serikali ya India kutupatia
mkopo wa Dola za Marekani milioni 178.25
kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji katika miji ya Dar es salaam na
Pwani. Hivi sasa mchakato wa kupata fedha hizo umefikia hatua za mwisho
na bila shaka inatarajiwa mapema mwezi ujao Mkataba utasainiwa na
utekelezaji wa mradi huo kuanza. Vilevile, Wizara yangu kwa kushirikiana
na Wizara ya Fedha, Ujenzi, Nishati na Maji za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imefanikisha upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 50 kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Uchumi ya Korea kwa ajili ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji Zanzibar.
43. Mheshimiwa Spika,
Wizara imeendelea na juhudi za kuchangia katika sekta ya ukuaji wa
viwanda. Kilicho dhahiri ni kuwa, kwa hali ya uchumi wetu kwa sasa,
viwanda vinavyohitajika haraka ni vile vya msingi ambavyo vinatumia
rasilimali za ndani, vinaongeza thamani na vinatoa ajira nyingi.
Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika mwaka huu wa fedha
tutapata wawekezaji wa viwanda vya kutengeneza nyuzi za nguo kutoka Japan na China.
Uwekezaji huu mkubwa sio tu utatengeneza ajira kwa wananchi wengi, bali
pia utawahakikishia wakulima wetu wa pamba soko la uhakika kwani
viwanda vyote hivi vikianza kufanya kazi, vitahitaji kiasi cha tani laki
mbili za pamba. Hivi sasa nchi yetu inazalisha tani laki moja tu. Hivyo
basi, ipo fursa kwa nchi yetu kuzalisha pamba kwa wingi zaidi kutokana
na kuwepo kwa soko la uhakika nchini. Aidha, uko uwezekano mkubwa kwa
Serikali ya Marekani kuendelea na Mpango wake wa AGOA ambapo bidhaa za
nguo kutoka Afrika ikiwemo Tanzania, zitaendelea kupewa upendeleo maalum.
44. Mheshimiwa Spika, katika kuwatafutia
ajira Watanzania nje, Wizara ikishirikiana na mamlaka husika za Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imekamilisha mchakato wa makubaliano ya kusaini mkataba wa ajira na nchi
ya Qatar. Kwa sasa, Wizara yangu inatarajia kupokea ujumbe kutoka Qatar
kuja hapa nchini kusaini mkataba huo ili Watanzania waweze kuchangamkia
fursa hizo nyingi za ajira wakati Qatar
ikijiandaa kuandaa Kombe la Dunia la mwaka 2022. Halikadhalika,
jitihada za Wizara yangu katika kuvutia misaada na uwekezaji katika
sekta za miundominu, zimechangia kuchochea uzalishaji wa ajira nyingi
nchini. Tunatambua changamoto ya ajira bado ni kubwa lakini tunaendelea
na jitihada hizi kwa kushirikiana na Sekta nyingine kadiri uwezo wetu wa
kibajeti utakavyoruhusu.
45. Mheshimiwa Spika,
mbali na kuendelea kutafuta fursa za mafunzo nje ya nchi, Wizara yangu
kwa kushirikiana na Bunge lako Tukufu ilisimama kidete kupigania
urejeshwaji wa fedha za ziada kiasi cha pauni za Uingereza milioni 29.5,
zilizojumuisha kiasi tulicholanguliwa na kile kilichotolewa mlungula
wakati wa ununuzi wa rada kutoka kampuni ya Kiingereza inayojihusisha na
uuzaji wa silaha (BAE). Kama
nilivyoahidi katika Bunge lako wakati wa kuwasilisha Kauli ya Serikali
na baadae wakati nikiwasilisha Bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka
2011/2012, fedha hizo zote zimerejeshwa Serikalini na sio kwenye Asasi
za Kijamii. Kwa pamoja, jitihada zetu zimewezesha kuipatia sekta ya
elimu shilingi bilioni 90 kama ambavyo Bunge hili limejulishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
46. Mheshimiwa Spika, sitakuwa
nimetenda haki nisipomshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa msimamo
wake thabiti na Mheshimiwa Spika kwa kuiunga mkono Serikali na kuteua
Kamati ya Wabunge ambayo imefanya kazi ya kutukuka kuhakikisha fedha
hizo zinarejeshwa Serikalini. Naomba nitambue mchango mahsusi wa
Waheshimiwa Wabunge wote. Aidha, niwashukuru pia Mhe. Balozi Peter
Kalaghe, timu yake na watumishi wa Wizara waliosimama kidete pamoja nasi
kwenye suala hili lenye maslahi kwa taifa. Nimejifunza kuwa imo ndani
yetu nguvu kubwa ya umoja pale tunapoweka kando maslahi yetu finyu ya
vyama na itikadi na kusimamia maslahi mapana ya Taifa. Hii ndio Tanzania
ninayoijua na kujivunia, Tanzania yenye umoja na Tanzania
yenye kuthubutu. Tumeonesha uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yetu na
historia itatupa tuzo njema na kulikumbuka Bunge hili kwa kazi hiyo
nzuri.
47. Mheshimiwa Spika,
lugha ya Kiswahili imekuwa ikitumika tangu mwaka 2004 katika shughuli
za Umoja wa Afrika na Serikali yetu imekuwa ikigharamia wakalimani wa
Kiswahili hadi mwaka 2008 ambapo Kamisheni ya Umoja wa Afrika ilichukua
jukumu hilo.
Serikali yetu inaendelea kushawishi nchi wanachama walau thelathini na
sita ambayo ni theluthi mbili kuridhia Itifaki ya Marekebisho ya Mkataba
wa Kuanzisha Umoja wa Afrika (Protocol on the Amendments to the
Constitutive Act of the African Union). Kuanza kutumika kwa Itifaki hiyo kutawezesha lugha ya Kiswahili kutumika katika shughuli za kila siku za Umoja wa Afrika.
48. Mheshimiwa Spika,
sambamba na juhudi hizo, mwezi Januari, 2012 Umoja wa Afrika umeanza
kufundisha lugha ya Kiswahili katika Kituo cha kufundishia Lugha cha
Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Tayari wamekwishajisajili wanafunzi 15
chini ya Wakufunzi wawili wa kujitolea kutoka Tanzania.
Naomba nitambue mchango wao wa dhati na kuwapongeza kwa uzalendo wao.
Mimi binafsi nilipata fursa ya kuwatembelea na kuwatia moyo mwezi
Januari, 2012 wakati nikihudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali
za Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.
Changamoto kubwa inayotukabili ni upatikanaji wa fedha za kuendesha
Kituo hicho na walimu wa kutosha wa kufundisha. Mpango wa Serikali ni
kutafuta fedha kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Utamaduni cha Kitanzania
jijini Addis Ababa
kwa lengo la kukuza utamaduni wetu na Lugha ya Kiswahili miongoni mwa
jamii ya Wanadiplomasia na Watumishi wa Umoja wa Afrika. Tukifanikiwa
katika hili tutakuwa tumetengeneza fursa za ajira kwa Wakufunzi wa
Kiswahili pamoja na kupanua wigo wa fursa kwa Watanzania kufanya kazi
katika Taasisi za Umoja wa Afrika.
49. Mheshimiwa Spika,
napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa ujenzi wa Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam,
umekamilika kwa Asilimia 95 na tunategemea kukabidhiwa mwezi Septemba
2012. Kituo hiki cha kisasa kinaweza kuhodhi Mikutano minne kwa mara
moja, yenye idadi ya watu 1,600. Kituo hiki kitakuwa na huduma nyingine
muhimu kama vile huduma za benki, afya, ukalimani na migahawa. Kituo kimejengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri wa Watu wa China.
Sanjari na Kituo hiki, pia Serikali hiyo imetoa msaada wa magari madogo
na mabasi yapatayo 75 ambayo tayari yapo nchini kwa ajili ya kutoa
huduma katika Kituo hicho. Kuanza kufanya kazi kwa Kituo hicho,
kutachochea ajira nyingi zaidi za moja kwa moja na nyingine zinatarajiwa
kutengenezwa katika sekta za huduma.
50. Mheshimiwa Spika,
kwa kuzingatia wajibu huu, Wizara imeshiriki kwenye majadiliano
mbalimbali yaliyopelekea uwekaji saini Makubaliano ya Mikataba
mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2011/2012 kama ifuatavyo:
1. Mkataba
wa mpaka wa Bahari kati ya Tanzania na Comoro, ambao uliosainiwa tarehe
05 Desemba, 2011 jijini Maputo – Msumbiji. Mkataba huu utahakikisha
kuimarika kwa usalama wa mpaka wa Bahari baina ya nchi hizi mbili;
2. Mkataba wa mpaka wa Bahari kati ya Tanzania na Msumbiji ambao ulisainiwa tarehe 05 Desemba, 2011 jijini Maputo – Msumbiji. Kama
ilivyo kwa Mkataba baina ya Tanzania na Visiwa vya Comoro, Mkataba huu
utahakikisha usalama wa mpaka wa bahari baina ya nchi hizi mbili
unaimarika;
3. Muhtasari
wa Makubaliano ya Mkutano wa Pili juu ya Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari
(EEZ) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Visiwa vya Comoro na
Serikali ya Ushelisheli, uliosainiwa tarehe 07 Septemba, 2011 huko Port
Louis, Mauritius. Utekelezaji wa makubaliano haya ni muhimu ili
kuwezesha nchi zote husika kunufaika na ukanda wa kiuchumi wa Bahari ya
Hindi;
4. Makubaliano kati ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd (BCEG) kuhusu ujenzi wa Mount Kilimanjaro International Convention Centre
ambayo yalisainiwa mwezi Agosti, 2011 mjini Arusha. Mkataba huu unatoa
fursa ya kujengwa kwa Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Jijini Arusha
ambao utaiingizia Serikali mapato na pia kuendelea kuitangaza Arusha na
Tanzania kwa ujumla kupitia Diplomasia ya Mikutano; na mwisho
5. Makubaliano ya Pamoja (MoU) kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na China Petroleum Technology and Development Corporation (CPTDC)
mwezi Machi, 2012 kufuatia ziara ya Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri
ya Watu wa China Mheshimiwa Li Jinzao hapa nchini ili kuendeleza eneo hilo.
51. Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu kupitia Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa -
New York, imekuwa ikiratibu na kushiriki katika utekelezaji wa Mradi wa
kuongeza eneo la Tanzania la Bahari nje ya Ukanda wa Kiuchumi. Wizara
ikishirikiana na Kamati ilioundwa kushughulikia suala hilo, imeendelea
kufanya mawasiliano na Taasisi za Umoja wa Mataifa zenye jukumu la
kupitia Maandiko ya Miradi kama hii ya nchi zote zilizofanikiwa kuongeza
eneo la Bahari. Andiko la Mradi la Tanzania
liliwasilishwa Umoja wa Mataifa mwezi Januari, 2012 na Mheshimiwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Aidha, mwezi Agosti,
2012 Timu ya wataalamu inatarajiwa kwenda kutetea Andiko hilo mbele ya “Commission on the Limits of the Continental Shelf” (CLCS),
inayoendelea na mkutano wake ulioanza tarehe 30 Julai, 2012 na
unaotarajiwa kumalizika tarehe 10 Agosti, 2012 huko New York. Wizara
imeendelea kushiriki katika maandalizi ili kufanikisha utetezi
unaotarajiwa.
52. Mheshimiwa Spika, Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPCs) ni nyenzo muhimu sana katika ufanikishaji wa utekelezaji wa diplomasia
ya uchumi. Ni katika Tume hizi mikataba ya msingi husainiwa ambayo
huweka mazingira kwa sekta binafsi kuweza kupata unafuu na fursa katika
nchi ambazo tuna Mikataba nazo. Kwa mfano, soko la tumbaku nchini China
ni kubwa zaidi kuliko lile la Marekani lakini wakulima wa Tanzania
wanashindwa kupenya katika soko hilo
kutokana na kukosekana kwa mikataba ya aina hii baina ya nchi zetu
mbili. Kutokana na ufinyu wa bajeti, tumeshindwa kutumia nyenzo hii
vizuri kufungua na kufufua fursa za ushirikiano. Kwa kutambua umuhimu
huo na kuzingatia ufinyu wa bajeti uliopo, tumedhamiria katika mwaka wa
fedha 2012/2013 kufanya mikutano ya JPC walau na nchi tatu kwa
kuzingatia vipaumbele vya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano
2011/2012 - 2015/2016.
53. Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa, asili
ya miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta nyingi nchini
kwa kushirikiana na washirika wetu wa maendeleo inatokana na Tume za
Pamoja za Kudumu za Ushirikiano. Katika mwaka wa fedha 2011/2012 Wizara
ilifanikisha makubaliano kuhusu uanzishwaji wa Tume ya Pamoja ya Kudumu
ya Ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini. Makubaliano hayo yalifikiwa mwezi
Julai, 2011 jijini Pretoria
– Afrika Kusini. Lengo la Makubaliano haya ni kuzidi kuimarisha
uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili katika nyanja
mbalimbali hasa za uchumi.
54. Mheshimiwa Spika, haya
niliyoyataja ni maeneo machache tu ambayo Wizara yangu imeyafanya
katika kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka
Mitano katika sekta za uchumi. Yako mengine mengi ambayo tumewezesha
kufanyika katika kila sekta nchini lakini kwa ufinyu wa muda siwezi
kuyasema yote kwa muda nilionao. Itoshe
tu kuongelea haya machache kwa leo. Ninaliahidi Bunge lako Tukufu
kwamba tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuwezesha
utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ya kwanza.
Zipo fursa nyingi za ushirikiano huko nje ya nchi ambazo nchi yetu
inaweza kunufaika nazo. Tumejidhatiti kunufaika na fursa zitokanazo na
China-Afrika Forum (FOCAC), TICAD V, EU-Africa, EBA, AGOA,
Turkey-Africa, SADC, NEPAD, Tume za Kudumu za Ushirikiano baina ya nchi
yetu na mataifa mengine. Tunachohitaji ni kuwezeshwa zaidi ili tufanye kazi hiyo kwa ufanisi zaidi.
55. Mheshimiwa Spika, bendera ya Tanzania imeendelea kupepea vyema katika medani za Kimataifa kutokana
na uongozi mahiri wa Waasisi wa Taifa hili na uongozi uliopo kufuatia
kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na Watanzania
katika Mashirika ya Kimataifa na Kikanda. Wizara
yangu imeendelea kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha Watanzania
wengi wanajiunga na kufanya kazi kwenye Mashirika ya Kimataifa. Aidha,
Tanzania imeendelea pia kugombania na kuchukuwa nafasi za uongozi kwenye
mashirika mbalimbali ya Kimataifa.
56. Mheshimiwa Spika, wakati
wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM)
uliofanyika Perth, Australia mwezi Oktoba 2011. Tanzania
ilichaguliwa kuingia kwenye Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa
Jumuiya ya Madola (Commonwealth Ministerial Action Group - CMAG) kwa
kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi 2013. CMAG ndiyo chombo chenye
jukumu la kusimamia misingi, sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Madola. Kikundi Kazi hicho kinaundwa na jumla ya nchi tisa kati ya nchi 54 za Jumuiya hiyo. Kuchaguliwa kwa Tanzania
kuingia kwenye Kikundi Kazi hicho kumezidi kudhihirisha imani ya
Jumuiya ya Kimataifa kwa nchi yetu. Mbali na kuleta sifa kubwa kwa Taifa
letu, nafasi hii inaipa
nchi yetu nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya Jumuiya ya Madola na pia
nafasi ya kuingiza na kusimamia maslahi yake kwenye Jumuiya hiyo.
57. Mheshimiwa Spika, napenda pia kumpongeza Dkt.
Agness L. Kijazi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA) kwa kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Shirika la
Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuanzia mwezi Juni, 2012 hadi mwaka 2015.
Nafasi hii ni muhimu kwani kati ya nchi 189 ambazo ni wanachama wa
Shirika la Hali ya Hewa Duniani, nchi 37 tu ndio wanaingia kwenye Baraza
Kuu la Shirika hilo. Dkt. Kijazi anakuwa ni mwanamke wa kwanza kutoka
Afrika Mashariki kuteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Shirika hilo.
58. Mheshimiwa Spika, Tanzania
kupitia raia wake Prof. Chris Maina Peter, ilichaguliwa kwa kishindo
kuwa Mjumbe kwa kipindi cha miaka mitano kwenye Kamisheni ya Sheria za
Kimataifa ya Umoja wa Mataifa katika uchaguzi wa wajumbe wa Kamisheni
hiyo uliofanyika mwezi Novemba, 2011 Mjini New York, Marekani. Prof. Maina ni Mtanzania wa pili kuiwakilisha Tanzania
kwenye Kamisheni hiyo, baada ya Mheshimiwa Balozi James L. Kateka
ambaye alikuwa Mjumbe kwenye Kamisheni hiyo kwa vipindi viwili vya miaka
mitano mitano (1997 - 2006). Balozi Kateka sasa ni Jaji katika Mahakama
ya Kimataifa ya Sheria za Bahari.
59. Mheshimiwa Spika, Majaji wawili Watanzania – Jaji William Hussein Sekule
na Jaji Joseph E. Chiondo Masanche nao walichaguliwa kuwa Majaji wa
Mahakama inayorithi shughuli za iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya
Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) katika uchaguzi uliofanyika New York, Marekani mwezi Desemba 2011.
60. Mheshimiwa Spika,
kupitia azimio namba 66/408 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwezi
Novemba, 2011 lilimthibitisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali wa Tanzania,
Bw. Ludovic Utouh pamoja na Ofisi yake kuwa kwenye Bodi ya Wakaguzi ya
Umoja wa Mataifa kuanzia Julai, 2012 kwa kipindi cha miaka sita.
Mafanikio haya yanatokana na umakini wa Wizara yangu kwa kufanya kampeni
za uhakika hadi kufanikisha kuchaguliwa.
61. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi
Septemba, 2011 Tanzania imekuwa mjumbe katika Bodi ya Magavana ya
Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) kwa kipindi cha 2011/2012.
Kuwemo kwenye Bodi hiyo, kunaipa nchi fursa ya kushiriki kwenye masuala
nyeti na muhimu kama vile kwenye majadiliano kuhusu mipango ya nyuklia
ya baadhi ya nchi. Bodi hiyo ina jukumu la kutathmini maombi ya nchi
zinazoomba uanachama na kuthibitisha viwango vya usalama. Aidha, Bodi
ndiyo inayomteua Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ambaye huthibitishwa na Mkutano
Mkuu wa IAEA. Hii ni fursa nzuri kwa nchi yetu hasa ikizingatiwa kwamba
Tanzania inayo malighafi ya urani.
62. Mheshimiwa Spika, niruhusu
nilitaarifu rasmi Bunge lako Tukufu kwamba Mtanzania mwenzetu, Dkt.
Asha-Rose Migiro, amemaliza kipindi chake kama Naibu Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa. Kwa
hakika Dkt. Migiro amefanya kazi nzuri na kubwa iliyotukuka katika
Umoja wa Mataifa. Ameiletea sifa nchi yetu na Bara la Afrika kwa ujumla
kutokana na kumsaidia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban ki
Moon. Kwa niaba ya Watanzania wote, ninamshukuru kwa kutuwakilisha
vizuri na ninampongeza sana
na kumkaribisha tena nyumbani ili aendelee kushirikiana na wananchi
wenzake katika ujenzi wa Taifa letu. Aidha, napenda pia, kupitia Bunge
lako Tukufu kumpongeza Dkt. Migiro kwa kuteuliwa tena kuwa Mwakilishi
Maalum wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Ugonjwa wa UKIMWI Barani
Afrika.
63. Mheshimiwa Spika,
vile vile, nchi yetu ilijipatia sifa kutokana na kazi nzuri aliyoifanya
Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula akiwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa
Jumuiya ya Nchi Wanachama wa Ukanda wa Maziwa Mkuu. Balozi Mulamula
aliratibu, aliisimamia na kuongoza Jumuiya hiyo kwa mafanikio makubwa
pamoja na changamoto nyingi zilizokuwepo katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Kutokana na kazi yake nzuri, ndio maana Mheshimiwa Rais amemteua sasa
kuwa Msaidizi wake Mwandamizi wa Masuala ya Kidiplomasia.
64. Mheshimiwa Spika,
tumekuwa tukishuhudia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na
kijamii duniani kote ambayo wakati mwingine yanahitaji nchi kuonesha
msimamo wake kwa baadhi ya masuala hayo. Moja ya sifa kubwa ambayo
Mwasisi wa Taifa hili Hayati Mwalimu Nyerere aliyotuachia ni kuweka
misimamo kwenye misingi tunayoiamini kama Taifa. Kutokana
na hali hiyo, Tanzania kama nchi huru imeweza kuwa na misimamo yake
kuhusiana na masuala hayo kama yanavyoelezewa hapa chini.
65. Mheshimiwa Spika, lipo tatizo la muda mrefu kati yetu na nchi jirani ya Malawi linalohusiana na mpaka kwenye Ziwa Nyasa. Tatizo
lenyewe ni kwamba Malawi wanadai kuwa Ziwa lote Kaskazini ya Msumbiji
kuelekea Ruvuma na Mbeya ni mali yao kwa mujibu wa Mkataba wa Heligoland
uliowekwa saini tarehe 1 Julai 1890.
66. Mheshimiwa Spika,
Tanzania kwa upande wetu tunasema kuwa mpaka wa kweli kati yetu na
Malawi unapita katikati ya Ziwa hivyo kufanya eneo lote la kaskazini
mashariki ya Ziwa kati ya Latitude digree 9° na digree 11° kuwa mali ya
Tanzania kwa mujibu wa Mkataba huo huo wa Heligoland (Ango-German
Agreement) wa mwaka 1890 ambao ulikubali kuwa kwa vile kuna maeneo ya
mpaka ambayo hayana mantiki, pande zinazohusika zikutane na kurekebisha
kwa kuunda “Border Commissions”. Aidha, tunazo ramani
ambazo Waingereza wenyewe (ambao wakati huo walikuwa wakitawala
Nyasaland na Tanganyika) walikubaliana kurekebisha na hivyo kusogeza
mpaka katikati kama ulivyo mpaka kati ya Malawi na Msumbiji.
67. Mheshimiwa Spika,
kutokana na tatizo hili, mwaka 2005 Marehemu Rais Bingu wa Mutharika,
alimwandikia Rais wa awamu ya tatu Mheshimiwa Mkapa akimtaka waunde
Kamati ya kuliangalia tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi. Awamu ya Nne ikaendeleza kwa kuunda Kamati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje kuliangalia tatizo na kulitolea mapendekezo. Kama
zilivyokutana mwaka 2010, mwaka 2012 zilikutana tena ili kuendeleza
mazungumzo ya mwaka 2010 na pia kujadili matukio ya kuonekana kwa ndege
ndogo ndogo za utafiti wa mafuta na gesi kwenye Ziwa Nyasa zikitafiti
hadi pwani ya Ziwa hilo upande wa Tanzania.
68. Mheshimiwa Spika,
baada ya majadiliano makubwa kati yetu na Malawi, Serikali yetu
iliwataka wenzetu wa Serikali ya Malawi pamoja na kampuni za utafiti au
uchimbaji kusitisha mara moja shughuli zote za utafiti hadi majadiliano
yatakapokamilika. Ni matumaini yetu kuwa wenzetu wa Malawi wametuelewa. Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa mgogoro huu mbele ya safari kutatuliwa na Msuluhishi badala ya sisi wenyewe.
69. Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili ya mgogoro bado iko mezani kwa majadiliano. Kufuatia maelekezo ya Marais wa
pande mbili, Mawaziri wa Mambo ya Nje na wataalamu wetu wa masuala ya
mipaka, ulinzi na usalama tulikutana Dar es Salaam tarehe 27 Julai, 2012
kujadili kwa kina mgogoro na kuupatia suluhu ya kudumu. Majadiliano
yanaendelea vizuri na tumekubaliana kuwa wakati tukiendelea na
mazungumzo, nchi zote zijiepushe na shughuli zozote kwenye Ziwa Nyasa
ambazo zinaweza kutafsiriwa kuathiri maslahi ya nchi mojawapo. Kwa
makubaliano haya, naomba niwatoe hofu wananchi wa mikoa ya Mbeya na
Ruvuma kuhusu hali ya usalama mpakani mwa nchi yetu na Malawi. Chini ya uongozi wa Serikali ya CCM, wananchi wa Tanzania
daima watakuwa salama dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho
la kiusalama. Tumefanya hivyo tokea uhuru na hatutachelea kufanya
vinginevyo wakati wote tukiwa madarakani. Hili limeelezewa katika Ibara
ya Nane, aya ya 191 na 192 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 -
2015.
70. Mheshimiwa Spika, Tanzania ina uhusiano mkubwa na wa kihistoria na Jamhuri ya Sahara Magharibi. Itakumbukwa kuwa nchi ya Sahara Magharibi inapakana na Morocco, Mauritania na Algeria ilikuwa ni koloni la Hispania. Wakoloni
hao waliondoka Sahara Magharibi mwaka 1975 na wakati wananchi
wanajiandaa kujitawala, ghafla nchi yao ikavamiwa na nchi jirani za
Mauritania na Morocco. Mauritania iliondoka na Morocco
ikaendelea kuikalia Sahara Magharibi tangu wakati huo yaani 1975 hadi
sasa. Wananchi wa Sahara Magharibi walianza kazi upya ya kudai uhuru wao
kutoka kwa jirani yao na Mwanachama wa OAU, Morocco. Mwaka 1976 Umoja
wa Afrika uliamua kuitambua Sahara Magharibi kama mwanachama wa OAU. Morocco ikajitoa kwenye Umoja huo. Kwa kuwa Tanzania
ilikuwa ndiyo Makao Makuu ya vyama vya Ukombozi Barani Afrika, kuanzia
mwaka 1963, ukombozi wa Sahara Magharibi ulikuwa ni moja ya agenda yetu
kuanzia wakati huo hadi sasa.
71. Mheshimiwa Spika, msimamo wa Tanzania kuhusu Sahara ya Magharibi, haujabadilika na upo pale pale. Tunataka
wananchi wa Sahara Magharibi waachwe waamue kupitia kura ya maoni
(referundum) iwapo wanataka kujitawala (independence) wenyewe au
wanataka kuwa chini ya Himaya ya utawala wa Morocco. Huo pia ndio msimamo wa AU na Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1992. Serikali
ya Morocco imekataa kura ya maoni (referendum) na badala yake wanataka
Sahara Magharibi iwe sehemu ya Himaya ya Morocco. Wamekataa kwa sababu wanajua kuwa wakikubali kura ya maoni kufanyika, wananchi wa Sahara Magharibi watataka kujitawala.
72. Mheshimiwa Spika, Tanzania inauomba Umoja wa Mataifa kuendelea na jitihada zake za usuluhishi na tunaitaka Serikali ya Morocco kubadilika. Tupo tayari kuwa na mahusiano na Morocco bila ya kuathiri msimamo wetu na Sahara Magharibi. Tunafanya hivyo kwa Israel na Palestina.
73. Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu imeendelea kuratibu ziara za Viongozi wa Kitaifa wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nje
ya nchi. Ziara hizo zimekuwa na mafanikio na faida kubwa kwa nchi yetu,
hasa
katika kulinda na kuendeleza maslahi ya kitaifa ya kiuchumi na kijamii,
kukuza mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbali mbali, Mashirika ya
Kimataifa na Kikanda, Kampuni za Kimataifa na hata watu binafsi.
74. Mheshimiwa Spika, ili
kuhakikisha kwamba ziara hizo zinaendelea kuwa na tija pamoja na
kupunguza gharama katika mazingira ya kiuchumi tuliyonayo, kama
alivyoelekeza Mheshimiwa Rais, Wizara yangu imeanza
kuchukua hatua mbalimbali kupunguza utegemezi wa ziara hizo pekee
katika kupata mafanikio mbalimbali, hususan ya kiuchumi. Miongoni mwa
mikakati hiyo ni:
1. Kupunguza ukubwa wa ujumbe katika misafara ya Viongozi Wakuu;
2. Kuwatumia
Wawakilishi, hususan Mawaziri katika safari mbalimbali hatua ambayo
inapunguza gharama kwani anaposafiri Waziri huongozana na wajumbe
wachache sana;
3. Kuelekeza
nguvu katika kuziimarisha Balozi zetu ikiwa ni pamoja na kufungua
Balozi Ndogo katika maeneo yenye maslahi ya kiuchumi kwa Taifa; na
4. Kutoa kipaumbele katika kufungua Ofisi za Wawakilishi wa Heshima katika maeneo muhimu ambayo Tanzania haina Uwakilishi.
75. Mheshimiwa Spika, katika
kudumisha mahusiano na nchi nyingine, nchi yetu imeendelea kutembelewa
na wageni mbalimbali katika ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali, Mawaziri
na Viongozi wengine wa Kimataifa. Katika diplomasia, kutembelewa na
wageni ni daraja muhimu la kukuza mahusiano na pia ni kielelezo cha sera
za nchi yako kukubalika na Mataifa mengine yakiwemo Mashirika ya
Kimataifa.
76. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
wa fedha uliopita wa 2011/2012 tulitembelewa na Marais kutoka Ivory
Coast, Somalia, Uganda, Liberia na Malawi. Vilevile, tulitembelewa na
Makamu wa Rais kutoka Burundi, Kenya, Zambia, Iran
na Afrika ya Kusini. Wageni wengine mashuhuri waliotembelea nchini ni
pamoja na Prince Charles wa Uingereza na mkewe Duchess of Cornwall
Camilla Parker, Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Donald Kaberuka na wengineo.
77. Mheshimiwa Spika, Tanzania
imepokea idadi kubwa ya mawaziri kutoka nchi mbalimbali duniani kama
vile China, Uingereza, Japan, Sweden, Finland, Afrika ya Kusini, Korea
ya Kusini, Korea ya Kaskazini, Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu. Wizara inaendelea kutekeleza mwongozo unaowataka viongozi wanaofanya ziara nchini Tanzania pia kutembelea Zanzibar.
78. Mheshimiwa Spika, katika mwaka fedha wa 2011/2012, Viongozi wafuatao walitembelea Zanzibar: Mwana
wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles na Mkewe Camilla; Mfalme wa
Ashanti wa Ghana; Waziri wa Uingereza wa Maendeleo ya Afrika; Waziri wa
Finland wa Maendeleo ya Afrika; Waziri wa Afya wa Finland; Waziri wa
Afya wa Marekani; na Waziri wa Afya wa Norway.
79. Mheshimiwa Spika, kama
ilivyo kwa Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali, Wizara yangu
imekumbwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake,
hususan kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Changamoto hizo kwa kiasi kikubwa
zinasababishwa na kuendelea kupungua kwa bajeti ya Wizara kila mwaka. Aidha, kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya
Dola ya Marekani ambayo hutumiwa na Balozi zetu nje nako kunasababisha
bajeti kuendelea kutokukidhi mahitaji. Ufinyu wa bajeti umesababisha
Wizara na Balozi zetu kushindwa kutekeleza kwa vitendo diplomasia ya
uchumi. Kuendelea kupewa bajeti ndogo kumesababisha, pamoja na matatizo
mengine, madeni makubwa, wafanyakazi kutolipwa stahili zao na uchakavu
wa magari na majengo. Aidha, ufinyu wa bajeti umechangia kwa kiasi
kikubwa kwa Wizara kushindwa kuwarejesha nyumbani watumishi waliomaliza
muda wao Balozini na kuwapeleka wengine kutoka Makao Makuu. Kama
nilivyosema hapo awali, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje,
Ulinzi na Usalam (NUU) imetembelea Balozi zetu mbalimbali na kujionea
hali halisi. Ninaamini Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati hiyo watakuwa
wasemaji wazuri wa matatizo yanayozikabili Balozi zetu kutokana na
ufinyu wa bajeti.
80. Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha changamoto hizo zinapungua, Wizara yangu imepanga
kuwa na majengo ya vitega uchumi katika baadhi ya Balozi zetu ili
kusaidia kuongeza mapato na kuokoa fedha ambazo zingetumika kulipia
pango katika maeneo hayo. Katika hatua nyingine, Wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha kuhusu uwezekano wa kutumia utaratibu wa mikopo ya nyumba (Mortgage Financing)
katika Balozi zetu badala ya utaratibu wa sasa ambao una gharama kubwa
kwa Serikali. Vile vile, Wizara yangu katika mwaka huu wa fedha imepanga
kuwasiliana na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ili
kuwaomba waruhusu Balozi zetu zitumie utaratibu wa “hire and purchase” kununua vifaa mbalimbali kama vile magari ya uwakilishi na hivyo, kupunguza gharama.
81. Mheshimiwa Spika, ninayo
kila sababu ya kuwapongeza wafanyakazi wa Wizara yangu walioko Wizarani
na Ubalozini kwa uvumilivu na kujitolea kwa moyo wao wote katika
mazingira haya magumu. Wafanyakazi wameendelea kutekeleza wajibu wao kwa
uaminifu na uadilifu mkubwa sana.
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama tumekuwa
tukiihusisha kwa karibu kuhusu changamoto hizi na wameshuhudia hali hii
kila walipopata fursa ya kutembelea Balozi zetu. Tunawashukuru kwa
kuielewa hali yetu halisi na kushirikiana nasi katika kushauri namna
bora ya kuondokana na changamoto hizo. Nasi tunauchukulia ushauri wao na
ule wa Kambi ya Upinzani kwa umakini mkubwa sana.
82. Mheshimiwa Spika,
napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteua Mabalozi –
kuiwakilisha nchi yetu huko Kenya, Misri, Msumbiji, Uganda, Oman,
Zambia, Italia, Ubelgiji na China. Vile vile, aliwateua Mwakilishi wa
Kudumu katika Umoja wa Mataifa na Naibu wake pamoja na Wakurugenzi tisa
katika Wizara yangu ambao wana hadhi ya Balozi.
83. Mheshimiwa Spika, hadi
sasa Wizara yangu ina jumla ya watumishi 430 ambapo kati yao 249 wapo
Makao Makuu ya Wizara, 18 wapo ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar na 163
wapo kwenye Balozi zetu. Kwa
kipindi cha Julai, 2011 hadi Juni, 2012 jumla ya watumishi 50
walihudhuria mafunzo ndani na nje ya nchi. Kati ya hao, 17 walihudhuria
mafunzo ya muda mrefu na watumishi 33 wamehudhuria mafunzo ya muda
mfupi.
84. Mheshimiwa Spika, kwa
kipindi hicho hicho, jumla ya watumishi 58 walipandishwa cheo baada ya
kutekeleza majukumu yao vizuri pamoja na kutimiza masharti ya Miundo ya
Utumishi inayosimamia kada zao. Vile
vile, watumishi 51 walithibitishwa kazini baada ya kumaliza muda wa
mwaka mmoja wa majaribio baada ya kuajiriwa, na watumishi wanne
walibadilishwa vyeo baada ya kujiendeleza na kupata sifa za kada husika.
85. Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu imeweka mkakati wa kuongeza idadi ya watumishi kutoka Zanzibar
katika kada ya Maafisa Mambo ya Nje kwa kuwapatia fursa Wanafunzi 18
kutoka Tanzania Visiwani kuingia kwenye Chuo chetu cha Diplomasia.
Dhamira ya Wizara ni kuona kwamba, pindi watakapomaliza na kufaulu
masomo hayo waweze kuajiriwa kwenye Wizara yangu kulingana na nafasi za
ajira mpya tutakazokuwa nazo.
TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA
86. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kukisaidia Chuo ili kiweze kutekeleza majukumu yake kama
yalivyo kwenye nia na madhumuni ya uanzishwaji wake. Lengo ni
kukiwezesha Chuo kuendelea kutoa mafunzo na kufanya utafiti katika
masuala ya diplomasia, uhusiano wa kimataifa, stratejia, usuluhishi wa
migogoro, ujenzi wa amani, kutoa ushauri na kuendesha mafunzo ya muda
mfupi. Lengo tarajiwa ni kukifanya Chuo kuwa taasisi bingwa ya elimu ya
juu na ushauri katika nyanja hizo pamoja na kushirikiana na Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika masuala ya utekelezaji
wa shughuli zake.
87. Mheshimiwa Spika, tatizo
la umiliki wa ardhi limemalizika baada ya Chuo kupatiwa Hati ya Umiliki
wa eneo lake. Kwa kuwa Chuo kinaendelea kupanuka ni wazi kuwa eneo la
sasa kwa Chuo haliwezi kukidhi mahitaji hayo. Hivyo, Serikali kupitia Wizara yangu imeendelea kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Hadi sasa eneo la ekari 1,000 limeshapatikana. Vile vile, tathmini ya
kulipa fidia ya ardhi imekwishafanyika ambapo Serikali inapaswa kulipa
shilingi bilioni 2.5 kwa
wananchi wa eneo la Buma lililopo Wilayani Bagamoyo na Wizara inaendelea
kufuatilia upatikanaji wa fedha hizo kutoka kwa mamlaka husika.
88. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Kituo kimeweza kukaribisha wastani wa mikutano 64 kwa mwaka. Kati
ya mikutano hii asilimia 30 ya mikutano ni ya kimataifa na asilimia 70
ni ya kitaifa. Idadi hiyo ya mikutano imeweza kuleta Arusha wageni
wanaokadiriwa kufikia 44,578 kila mwaka. Kwa
mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2011 Kituo kiliweza kuwa mwenyeji wa
mikutano ya kimataifa 15 na ya kitaifa 47 iliyoingiza nchini wageni
wanaokadiriwa kufikia 35,000.
89. Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kwa mara nyingine tena, Kituo kimeendelea kupata hati safi
ya hesabu zake zilizoandaliwa na kukaguliwa kwa wakati kwa kipindi
kilichoishia tarehe 30 Juni 2011. Kituo kilipata faida ghafi ya shilingi
milioni mia tano thelathini na moja, elfu mia sita na tano mia tatu na ishirini (531,605,320/=) na kinaendelea kufanya shughuli zake kwa ufanisi na bila kuwa tegemezi kwa Serikali Kuu. Katika
kipindi cha mwaka 2012/2013, Kituo kimepanga kuingiza mapato ya
shilingi bilioni tisa, milioni mia sita arobaini na tano, elfu mia tatu
hamsini na tisa na mia saba (9,645,359,700/=)
kutokana na vyanzo vyake mbalimbali vya mapato na baada ya kutoa
gharama za uendeshaji, Kituo kinategemea kupata ziada ghafi ya shilingi milioni miatano ishirini na tano, elfu mia moja hamsini na tisa, mia sita sitini na nne (525,159,664./=).
90. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kufuatilia kuhusiana na kujengwa kwa Kituo kipya cha mikutano mjini Arusha kitakachoitwa Mt. Kilimanjaro International Convention Centre (MK-ICC). Mradi huu ni moja ya miradi itakayofadhiliwa na Serikali ya Watu wa China kupitia benki yao
ya Exim. Napenda kuipongeza Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo, Menejimenti
na wafanyakazi wote wa AICC na pia kuwatakia mafanikio mema katika kazi
zilizo mbele yao.
91. Mheshimiwa Spika, kazi ya tathmini ya utawala bora hapa nchini imeendelea kufanyika kwa ufanisi mkubwa. Kwa kuwa Taarifa ya tathmini iliyokuwa imetayarishwa mwaka 2009 haikufanyiwa uhakiki kama
ilivyotarajiwa. taarifa hiyo ilihuishwa ili kurekebisha takwimu
mbalimbali zilizokuwa zimepitwa na wakati lakini pia kuakisi mabadiliko
ya kisiasa yaliyokuwa yametokea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
APRM Tanzania kwa kushauriana na Sekretarieti ya Afrika Kusini na
Wizara, iliandaa pia Taarifa mahsusi ya Zanzibar.
Hatua hii ilitokana na maoni ya mara kwa mara ya wadau wa Zanzibar hasa
Makatibu Wakuu na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa ingawa suala la
APRM ni la Muungano, ingekuwa ni busara ikaandaliwa taarifa mahsusi ya
Zanzibar kwa nia ya kurahisisha utekelezaji wa changamoto
zitakazobainishwa. Taarifa hiyo nayo ilikamilishwa na kuwa sehemu ya
Taarifa ya nchi iliyokuja kufanyiwa tathmini na uhakiki na Timu ya
Wataalamu wa kutoka nchi za Afrika tarehe 2 hadi 23 Machi 2012.
92. Mheshimiwa Spika, wataalam wa Country Review Mission
wapatao 20 waliwasili nchini mwezi Machi 2012. Wakiwa nchini walikutana
na Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Serikali ya Muungano, Makamu
wa Kwanza wa Rais (SMZ), Makamu wa Pili wa Rais (SMZ), Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri wa Katiba na Sheria
Zanzibar, Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Wawakilishi wa Serikali, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa,
Wabunge, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Jumuiya ya Wafanya Biashara,
Washirika wa Maendeleo pamoja na Asasi zisizo za Kiserikali ili kupata
maoni yao. Aidha, Wataalam hao, waligawanyika katika makundi mawili
tofauti walitembelea mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini Pemba, Mtwara,
Mbeya, Dodoma, Arusha, Kagera, Ruvuma na Kigoma.
93. Mheshimiwa Spika, katika
mikutano mbalimbali iliyofanyika masuala yafuatayo yalijitokeza ambapo
pamoja na kuwepo kwa amani na utulivu, maeneo mengine yaliyoonekana kuwa
ni tunu na yanayopaswa kuenziwa ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,
utaratibu wa kurithishana madaraka kwa amani kila baada ya uchaguzi
mkuu, Muafaka wa kisiasa Zanzibar na kazi nzuri inayofanywa kwa uhuru na
uwazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.
94. Mheshimiwa Spika, Tanzania
inatarajia kufanyiwa tahmini kwenye Kikao cha nchi wenza zinazoshiriki
katika mchakato Januari, 2013 badala ya Julai, 2012 kutokana na Timu
hiyo ya APRM kutokuweza kukamilisha taarifa yao
katika muda ambao ungetoa nafasi kwa Serikali yetu kutoa majibu na
kuyawasilisha kwenye Kikao cha APRM cha Tathmini cha Wakuu wa Nchi
kilichofanyika Julai, 2012 mjini Addis Ababa. Ninaipongeza Bodi ya Uendeshaji ya APRM kwa kazi nzuri walioifanyia nchi yetu.
95. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 Wizara yangu ilipangiwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni mia moja ishirini na tano, mia moja na mbili milioni na mia nane sabini na tano elfu (125,102,875,000/=). Kati ya fedha hizo shilingi bilioni themanini, mia sita na mbili milioni na mia nane sabini na tano elfu (80,602,875,000/=) ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni arobaini na nne na milioni mia tano (44,500,000,000/=)
ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Aidha, katika bajeti ya Matumizi
ya Kawaida ya Wizara (Recurrent Budget), shilingi bilioni sabini na
sita, mia tatu themanini na saba milioni na mia moja themanini na saba
elfu (76,387,187,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (OC) na bilioni nne, mia mbili kumi na tano milioni na mia sita themanini na nane elfu (4,215,688,000/=) ni kwa ajili ya mishahara.
96. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Balozi zake ilitegemea kukusanya kiasi cha shilingi bilioni kumi na nne, mia nane sabini na mbili milioni na mia nne tisini na mbili elfu (14,872,492,000/=). Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2012 kiasi cha shilingi bilioni kumi na tatu, mia nane hamsini na tatu milioni, mia nne arobaini na tisa elfu na mia tano hamsini na tisa (13,853,449,559/=)
ikiwa ni makusanyo ya maduhuli balozini na Makao Makuu. Kiasi hiki cha
fedha ni sawa na asilimia 93 ya makusanyo ya fedha zote za maduhuli
zilizokadiriwa kukusanywa balozini na Makao Makuu kwa mwaka wa fedha
2011/2012.
97. Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia tarehe 30 Juni, 2012 Wizara ilikuwa imepokea kutoka HAZINA
jumla ya shilingi bilioni mia moja na ishirini na tatu, milioni mia nane
themanini na nne elfu mia saba sabini na nane na mia saba themanini na
saba (123,884,778,787/=)
ikiwa ni pungufu ya asilimia 0.97 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida,
Mishahara, pamoja na bajeti ya Maendeleo. Kiasi cha shilingi bilioni
tisini na saba, milioni mia mbili arobaini na moja elfu mia mbili
thelathini na tisa, mia saba themanini na saba (97,241,239,787/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida pamoja na Mishahara ikionyesha ongezeko la asilimia 20.64 ya bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
98. Mheshimiwa Spika,
ongezeko hili limechangiwa na kuibuka kwa majukumu mbalimbali ya
kitaifa ambayo awali hayakupangiwa fedha kutokana na ufinyu wa bajeti
kama vile; Ujio wa Timu ya Ukaguzi kuhusu Mpango wa Kujitathmini Wenyewe
kuhusu Utawala Bora (APRM) kutoka Makao Makuu ya Taasisi hiyo, Mchakato
wa maandalizi pamoja na uzinduzi wa Majadiliano ya Ubia Nadhifu (Smart Partnership Dialogue), Ujumbe na ushiriki wa Tanzania katika Kikosi Kazi cha Kamati ya Mawaziri ya Jumuiya ya Madola (CommonWealth Ministerial Action Group – CMAG), Mchakato
wa ujumbe wa Tanzania katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya
Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika pamoja na Ujumbe wa Tanzania
katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.
99. Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa bajeti ya Maendeleo, Wizara hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2012
imepokea kutoka Hazina shilingi bilioni ishirini na sita, mia sita
arobaini na tatu milioni na mia tano thelathini na tisa elfu (26,643,539,000/=). Kiasi hiki ni sawa na asilimia 59.87 ya bajeti yote ya Maendeleo iliyotengwa kwa Wizara kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Ikumbukwe kuwa Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ilipunguzwa kwa kiasi cha shilingi 16,898,098,757/= kutokana na hali ya mapato ilivyodhihirika.
100. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Wizara itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kama yalivyoainishwa katika hotuba hii. Aidha, Wizara itaendelea kutekeleza malengo yake iliyojiwekea kulingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015. Msisitizo
utakuwa ushiriki wa Wizara katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano 2011/2012 – 2015/2016. Naomba kusisitiza na kukumbusha
Wizara nyingne kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
ni Wizara mtambuka na hivyo inahusika na ufanikishaji wa miradi mingi
inayotekelezwa na Wizara, Idara na Taasisi nyingine mbalimbali za
Serikali. Kama nilivyoeleza hapo awali, Wizara yangu ina nafasi kubwa
katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.
101. Mheshimiwa Spika, kama
sehemu ya kuendeleza na kuhimiza njia mbadala za kukabiliana na
changamoto zinazotokana na bajeti inayoendelea kupungua kila mwaka,
pamoja na mambo mengine, Wizara inatarajia kufaya mambo yafuatayo:
i. Kufungua Balozi Ndogo katika
miji ya Uturuki, Loss Angeles (LA), California, Lubumbashi na
Guangzhou; ambazo sanjari na kuendeshwa kwa gharama nafuu zinaweza
kukusanya maduhuli mengi kupitia utoaji wa viza na tozo, hivyo kuongeza
idadi ya watalii na kukuza biashara nje ya zile nchi tulizozoea
(traditional allies) zilizoko Ulaya ambazo uchumi wake unayumba kwa
sasa;
ii. Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano (JPC) -Wizara
inatarajia kuitisha mikutano ya Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano
angalau kwenye nchi tatu kwa lengo la kuzifufua tume hizo na kupanua
fursa za ushirikiano, hususan masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini;
iii. Watanzania Waishio Ughaibuni (Diaspora) - Nafurahi
kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa kufuatia Mheshimiwa Rais kuteua
Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora mapema Mei, 2012 Wizara yangu sasa ipo
katika mchakato wa kuandaa Sera na Mpango wa Kitaifa kuhusu masuala ya
Diaspora ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwahusisha Watanzania hao
katika kuchangia maendeleo ya nchi yao. Hatua hii muhimu itasaidia
kuainisha wigo wa kisera, ushiriki wa wadau na majukumu ya Wizara, Idara
na Taasisi nyingine katika kufanikisha ushirikishwaji wa Watanzania
waishio ughaibuni kuchangia katika maendeleo ya taifa. Ni azma ya Wizara
yangu kuona kuwa mchakato huu unakamilika mapema ili kutoa mwongozo kwa
wadau na kurahisisha uelewa wa pamoja kuhusu mikakati bora ya
kuwatambua na kuwashirikisha diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi
yao;
iv. Majukumu ya Kimataifa - Wizara imejipanga kutumia kikamilifu nafasi za Tanzania kimataifa katika kipindi hiki zikiwemo uenyekiti wa asasi ya SADC organ Troika na ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika kukuza taswira ya nchi yetu nje na kukuza ushirikiano wa Tanzania na nchi zilizoendelea ambazo ndizo zinafanya vizuri kiuchumi kwa sasa;
v. Utatuzi wa Migogoro na Uimarishaji wa Amani - Tanzania
imeendelea kuwa nchi ya kutumainiwa katika ulinzi na ujenzi amani
Barani Afrika. Kumejitokeza haja kubwa ya uzoefu wetu kutakiwa na nchi
nyingine katika utatuzi wa migogoro na ujenzi wa amani katika nchi
zinazotoka katika migogoro. Serikali imeamua kujikita katika kutumia
uzoefu wetu na sifa hii katika kupanua maslahi ya nchi yetu kwa kuitikia
fursa hizo. Tunajipanga kutumia Wanadiplomasia wetu wastaafu na waliopo
katika kutafuta suluhu ya migogoro. Lengo ni baadae kuanzisha taasisi
ya usuluhishi wa migogoro katika Chuo chetu cha Diplomasia. Uwepo wa
Taasisi hiyo nchini Tanzania itavuna mikutano mingi na hivyo kuingizia
nchi fedha za kigeni, kupanua sekta ya utalii na kutoa fursa ya kujenga
urafiki na kupanua maslahi yetu kwa nchi nyingi zaidi. Tutatumia fursa
zetu za kuwa Mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika na Uenyekiti
wa Asasi ya SADC kufanikisha azma hiyo; na
vi. Ulinzi wa Amani -
sambamba na mkakati huo, eneo la ulinzi wa amani (peacekeeping
operations) ni eneo jipya tunalotaka kulipa kipaumbele. Azma hiyo
inakwenda sambamba na uanzishwaji wa Chuo cha Ulinzi wa Amani
(Peacekeeping School) nchini kwa ushirikiano wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania na Jeshi la Canada. Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu
kuwa tayari Hati ya Awali ya Makubaliano (MoU) imesainiwa mwaka huu.
Kuanza kwa Chuo hicho kutatoa fursa kwa vijana wetu kujenga uwezo wa
kushiriki katika operesheni za Ulinzi wa Amani, vijana wetu wa jeshi
kupata uzoefu na mbinu mpya za kivita nje ya nchi, kuwezesha Watanzania
wa fani mbalimbali kupata ujuzi na utaalamu na kuweza kushiriki kwenye
operesheni za AU na UN (Civilian Peacekeeping Mission) ambako kwa sasa
ushiriki wetu ni mdogo kutokana na kukosa stadi za aina hii.
102. Mheshimiwa Spika, ili
kuweza kutekeleza kikamilifu kazi zilizotajwa hapo juu, Wizara yangu
imepangiwa kiasi cha shilingi bilioni tisini na nane, mia tatu
thelathini na tisa milioni na mia saba na saba elfu (98,339,707,000/=) kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni themanini na moja, milioni mia sita themanini na sita, mia tano na tatu elfu (81,686,503,000/=)
ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, shilingi bilioni kumi na sita, mia
sita hamsini na tatu milioni na mia mbili na nne elfu (16,653,204,000/)
ni kwa ajili ya bajeti ya Maendeleo. Aidha, jumla ya shilingi bilioni
sabini na sita, mia tano arobaini milioni na mia tano ishirini na moja
elfu (76,540,521,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na bilioni tano, mia moja arobaini na tano milioni na mia tisa themanini na mbili elfu (5,145,982,000/=) ni kwa ajili ya Mishahara.
103. Mheshimiwa Spika, katika
bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara; shilingi bilioni moja, mia
tano arobaini na tisa milioni na mia tisa ishirini na tano elfu (1,549,925,000/=)
ni kwa ajili ya mchakato wa APRM, shilingi bilioni moja, mia tano na
nne milioni, mia tano sabini na nne elfu na mia nne sabini na nane (1,504,574,478/=)
ni kwa ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na
shilingi bilioni mbili, mia tano ishirini na sita milioni, mia tisa
sabini na tatu elfu na mia nne sitini na mbili (2,526,973,462/=) ni kwa ajili ya fedha za Mshahara na Matumizi ya Kawaida ya Chuo cha Diplomasia.
104. Mheshimiwa Spika, aidha,
Wizara yangu, kupitia Balozi zake, inatarajia kukusanya kiasi cha
shilingi bilioni kumi na sita, milioni mia nane themanini na mbili elfu
mia mbili thelathini na moja, mia tatu na thelathini (16,882,231,330/=)
kama maduhuli ya Serikali. Kwa maana ya utekelezaji wa Bajeti, kiasi
hiki cha maduhuli tayari kimehesabiwa kama sehemu ya Matumizi ya Kawaida
ya Bajeti ya Wizara yangu.
105. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.