MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Tuesday, August 7, 2012

CUF YAONYA MGOGORO WA MALAWI, TZ

Salim Said
CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimeionya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania isije ikaiingiza nchi katika vita na Malawi badala yake itumie hekima na busara katika kutatua mgogoro huo.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Abdul Kambaya katika taarifa yake kwa vyombo vya habari nchini.
"Ni vyema serikali ikatumia hekima na busara za kidiplomasia kutatua mgogoro na Malawi kuliko kuiingiza katika hasara kubwa ya vita". 
Kambaya alisema kwa mujibu wa Onyo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe Agosti 06 mwaka huu Bungeni mjini Dodoma, nchi yetu inaapa kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote na kuzionya ndege zote za makampuni yanayofanya utafiti wa mafuta na gesi katika ziwa Nyasa kuacha mara moja kuruka kwenye anga la ziwa hilo, kwa upande wa Tanzania. 
"CUF tunakubaliana na Membe katika kulinda mipaka yetu kwa gharama yoyote iwapo kama Diplomasia na Busara zimetumika kwa nguvu zote na kushindikana, ndipo hapo nguvu zingine zozote ziweze kutumika".
 Kambaya alisema CUF inachelea Tanzania yenye amani na utulivu ambao umekuwa ni kijicho kwa majirani, kuingizwa kwenye vita vitakavyoathiri uchumi wa nchi.
Alisema CUF inasikitishwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ya kuchelewa kulipatia ufumbuzi suala hili la kugombania mpaka na Malawi ambapo lilianza muda mrefu tangu mwaka 1960.
Alifafanua kuwa suala hilo lililipuka tena kwenye miaka ya 1990, na mnamo mwaka 2005 Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi aliandika barua kwa Rais wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa, ambapo Kamati ya kufuatilia muafaka huo imekuja kuundwa 2010.
Kumekuwa na vita ya maneno baina ya Tanzania na Malawi kuhusu mpaka unaozigawa nchi hizo mbili katika ziwa Nyasa huku kila nchi ikidai ziwa hilo lipo ndani ya himaya yake.

No comments:

Post a Comment