Salim Said
SHIRIKA la Biashara la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (ZSTC) limeingia katika kashfa nzito baada ya watendaji wake kuuza tani kadhaa za karafuu chini ya bei tena kinyemela.
Hayo yalithibitishwa jana na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa SMZ Nassor Ahmed Mazurui alipokua akijibu hoja mbalimbali za wawakilishi wakati wa kupitia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo visiwani Zanzibar.
Mazurui aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo kuwa, Watendaji wa ZSTC walitumwa kwenda kufanya utafiti wa bei ya soko ya zao la karafuu katika soko la dunia kwa mwaka huu wa 2012/13.
Alifafanua kuwa kinyume chake watendaji hao wa ZSTC walikwenda kuuza karafuu kinyume cha taratibu na kanuni zinazoongoza uuzaji wa zao hilo ambalo ni mali ya serikali.
"Watendaji hawa hawakutumwa kwenda kutafuta soko wala kuuza karafuu, lakini walitumwa kwenda kutafuta bei ya karafuu kwa mwaka 2012/13" alisema Mazurui.
Alisema mara ya mwisho serikali iliuza karafuu kwa bei ya Dola za Marekani 12,500 kwa tani moja lakini cha kusikitisha wao wameuza karafuu chini ya bei kwa Dola 8,500 kwa kila tani.
Alisema serikali itakaa na kuangalia namna gani ya kufanya juu ya tukio hilo ambapo hatua za kinidhamu na kiutendaji zitachukuliwa dhidi ya watendaji hao.
"Hawa watendaji wamerejea nchini siku mbili tu zilizopita, hivyo tutakaa nao ili kupata maelezo yao na baadaye serikali itakaa na kuangalia namna ya kufanya juu ya tukio hilo, lakini kuna hatua za kinidhamu na kiutendaji ikibidi zitachukuliwa," alisema.
Mazurui alisema tayari fedha za mauzo hayo zimekwishaingia katika account ya Shirika hilo la serikali.
No comments:
Post a Comment