MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, July 22, 2009

CUF yawavaa JK, Pinda

Salim Said
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitoweza kujivua na lawama za kutokea kwa machafuko visiwani Zanzibar katika uchaguzi mkuu 2010, kwa sababu inaridhia vyombo vyake kutumiwa vibaya na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika maandalizi ya uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka CUF, SMZ chini ya uongozi wa Rais Amani Karume imekuwa ikivitumia vibaya vyombo vya dola vya serikali ya Muungano katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hususan uboreshaji wa daftari la wapigakura.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Salim Bimani ilisema, miongoni mwa vyombo hivyo ni Usalama wa Taifa na Polisi.

Kwa mujibu wa Bimani Usalama wa taifa ni miongoni mwa mambo ya Muungano na kwamba idara hiyo inasimamiwa moja kwa moja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

“Kwa mantiki hiyo, hakuna namna yoyote ambayo Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wanaweza kujivua na lawama za kutokea kwa vurugu kabla, wakati au baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka 2010,’ alisema Bimani

Alisema hiyo ni kwa sababu inaonesha wazi kuwa viongozi hao wanaridhia uvamizi wa vyombo hivyo vya dola katika kazi za ZEC au hawajali kile kinachofanywa na vyombo hivyo.

“Lolote kati ya hayo mawili linamaanisha kwamba wao ndiwo wanaopaswa kubeba dhima na lawama za hali ya juu kwa hali yoyote mbaya katika uchaguzi wa 2010 visiwani Zanzibar,” alisema Bimani.

Alisema, CUF inachukua fursa hiyo kuwakumbusha viongozi hao wakuu wa serikali ya Muungano kwamba, wao ndiwo wenye dhima ya kulinda usalama na haki zote za kikatiba za wananchi wa Tanzania wakiwamo na wa Zanzibar.

“Tunachukua nafasi hii tena na tena kuwakumbusha viongozi wakuu hawa wawili, wajue kama walikuwa hawajui kuwa wao ndiwo wenye jukumu la kulinda usalama na haki zote za kikatiba za wananchi wa Tanzania (bara na Zanzibar),” alisema Bimani.

Alisema, kisingizio kwamba Zanzibar ina sheria zake za uchaguzi si sababu ya wao kuviachia vyombo vya dola vilivyo chini ya mamlaka yao kuvunja haki za binadamu na wananchi kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa, suala la Zanzibar kuwa sheria zake si sababu ya msingi pia ya kudharau ukweli kwamba uchaguzi wa Zanzibar unavurugwa na vyombo vile vile ambavyo vilitarajiwa kuusimamia.

“Hili la kuwanyima wananchi haki ya kuandikishwa katika daftari la wapiga kura na kuweka vyombo vya dola ili kuhakikisha haki hiyo haipatikani ni katika mifano halisi ya ukiukwaji haki za binadamu,” alisema Bimani.

Alisema, wakati CUF inathamini nafasi ya vyombo vya dola, ikiwemo idara ya usalama wa taifa katika kuifanya nchi kuwa katika amani, umoja na mshikamano lakini chama chao hakikubaliani na dhana kwamba jukumu la Idara hiyo ni kuhakikisha kuwa wananchi wenye mawazo tafauti ya kisiasa na watawala hawana haki katika nchi yao.

Aidha Bimani alisema wamefadhaishwa na vitendo ya maafisa wa hao katika Wilaya ya Micheweni kuingilia kati utendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Alisema, tukio hilo linaonesha kwamba ZEC haiko huru na inafanya kazi zake kwa kufuata maagizo kutoka katika Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

“Vitendo hivi si tu kwamba vinathibitisha kauli yetu ya muda mrefu kwamba ZEC inaendesha uchaguzi kwa kufuata maagizo ya Idara ya Usalama wa Taifa, bali pia vinapigilia misumari mingine kwenye jeneza la kuizikia demokrasia ya Zanzibar,” alisema Bimani na kuongeza:

“Kila mara tumekuwa tukisema kwamba vyombo vya dola ndivyo vinavyosimamia na kuendesha uchaguzi wowote unaofanyika Zanzibar, huku ZEC ikiwa kama ni alama tu ya kuwepo kwa chombo huru kinachoendesha shughuli za uchaguzi.”

Alisema, kwa mujibu wa taarifa walizozikusanya kutoka katika vituo vya uboreshaji wa daftari hilo vya Wingwi Mapofu, Mgogoni, Kinyasini, Finya na Konde zinaonesha kwamba vyombo vya dola vimekuwa vikishiriki kikamilifu katika kutoa maelekezo kwa watendaji wa ZEC.

“Miongoni mwa maelekezo hayo ni pamoja na kuwazuia masheha wa Shehia kuzungumza na waandishi wa habari ambao huwa wanataka kujua usahihi wa madai yanayotolewa dhidi ya masheha hao,” alisema Bimani.

Katika uchaguzi wa 2001 CUF ilipinga matokeo ya urais Zanzibar na wananchi kuingia barabarani jambo ambalo lilisababisha vifo vya askari mmoja na raia zaidi ya 30.