Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Mamlaka
ya Usafiri wa Baharini Zanzibar imezifutia rasmi hati ya kufanya kazi
Meli ya Mv.Kalama, Mv.Seagul na Mv.Sepideh kutokana na meli hizo
kutokukidhi hali ya usalama wa abiria katika meli hizo.
Aidha
meli hizo zimepewa muda wa mwezi mmoja kuanzia leo kuhakikisha
zimeondoka katika maeneo ya Zanzibar kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa
dhidi ya wamiliki wa Meli hizo.
Kauli
hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri wa Baharini
Zanzibar Abdullah Husein Kombo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari Afisini kwake kuhusu hali ya usafiri wa baharini na usalama
Zanzibar.
Amesema
Mamlaka hiyo imefanya tathmini na uhakiki wa kutosha na kujiridhisha
kuwa Meli hizo hazifai kufanya kazi katika maeneo ya Zanzibar jambo
ambalo limepelekea kuchukua hatua za kufuta hati za kufanyia kazi meli
hizo.
Amefahamisha
kuwa sababu kuu zilizopelekea Mamlaka kufanya maamuzi hayo ni pamoja na
uchakavu,umri wa meli hizo kuwa mrefu na kupata matatizo mara kwa mara
katika safari zao.
Kombo
amefahamisha kuwa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri na Bandari Zanzibar ya
mwaka 2006 kifungu cha 17.1 inampa mamlaka Msajili wa Meli kuifuta meli
yoyote ambayo itakuwa haikidhi usalama wa abiria.
Kufuatia
sheria hiyo Kombo amesema watawataka wamiliki wa Meli hizo kuzirudisha
hati za kufanyia kazi meli hizo ili waende kutafuta sehemu nyengine za
usajili kinyume na maeneo ya Zanzibar.
Akizungumzia
Meli ya Mv.Serengeti Kombo amesema wamelazimika kuiagiza meli hiyo
kupunguza idadi ya abiria kutoka watu 800 hadi 350 na tani za mizigo
kutoka 100 hadi 50 hadi pale ambapo watajiridhisha kutokana na hali ya meli hiyo ilivyo.
Aidha
amegusia kuwa Kampuni ya Bakhresa italeta Meli kubwa ya abiria
itakayofanya kazi zake Zanzibar ambapo pia Serikali ya Mapinduzi nayo
iko mbioni kuhakikisha wanaleta meli inayokidhi mahitaji ya wananchi wa
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment