MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Sunday, June 14, 2009

CUF yawatimua maafisa watatu kwa usaliti chamani

Salim Said

CHAMA Cha Wananchi (CUF), kimewatimua maafisa wake watatu wa uchaguzi kwa tuhuma za kukisaliti chama hicho katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Busanda.

Uamuzi huo uliofikiwa katika kikao cha Baraza Kuu kilichomalizika jana jijini Dar es Salaam baada ya wajumbe kuridhika kuwa moja ya sababu za CUF kushindwa katika uchaguzi huo uliompa ubunge mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni usaliti huo uliofanywa na maafisa wake.

Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, Baraza limefikia uamuzi huo kulinda maslahi ya chamasema, baraza kuu liliamua kuchukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha na makosa ya watu hao, ili kulinda maslahi ya chama chao.

Aliwataja maafisa hao kuwa ni Husein Mmasi aliyekuwa msimamizi wa shughuli zote za kuandaa mawakala katika uchaguzi huo, Katibu wa Tume ya Uchaguzi ya CUF Maole Kuchilingulo na Juma Wandwi, aliyekuwa mjumbe wa tume ya uchaguzi wa chama hicho.

Alisema mbali na uamuzi huo wa kuwavua madaraka, Baraza limetoa onyo kali kwa maafisa hao na kuweka wazi kuwa hakitovumilia vitendo vya aina hiyo wala kusita kuwaadhibu viongozi na watendaji wa chama kwa uzembe au hujuma.

Akielezea kwa undani tukio hilo, Profesa Lipumba alisema siku tatu kabla ya uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitangaza kuwafuta mawakala wa wa CUF, kwa kuwa majina yao hayakupangwa kwa mujibu wa vituo vya kupigia kura, kama sheria ya uchaguzi inavyotaka.

“Baraza kuu limeridhika kwamba kuzuiwa kwa mawakala wetu kulitokana na hujuma ya afisa wa ndani ya chama, kwa kutotekeleza kwa makusudi masharti hayo ya kisheria,” alisema profesa Lipumba.

Pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Wilfred Lwakatare ameamua kuachia ngazi nafasi zote za uongozi ndani ya Chama hicho kwa kile kilichoelezwa kuwa, anataka kurudi Jimboni kwake Bukoba kwa ajili ya kuimarisha chama chao.

Profesa Lipumba alithibitisha kupokea barua ya maombi ya kuachia ngazi kwa Lwakatare wakati wa kikao cha Baraza hilo, kilichoanza Juni 8 hadi 9 mwaka huu, akitaka kurudi jimboni kwake kuimarisha chama.

“Chama chetu ni cha demokrasia na katika demokrasia huwezi kumkataza mtu kujiuzulu, lakini hatujamjibu barua yake. Lwakatare tulikuwa naye na kushirikiana naye kwa mambo mingi na pia tutaendelea kushirikiana, ila kwa sasa ameamua kuwa mwanachama wa kawaida tu,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema, Lwakatare hajawahi kutuhumiwa na kashfa ya aina yoyote ndani ya chama na wala hajashinikizwa na mtu yoyote kujiuzulu, ila ameamua mwenyewe kujiuzulu na sisi kama Baraza kuu la uongozi hatuwezi kumzuiya kujiuzulu.

Aidha Profesa Lipumba alisema, CUF imeandaa operesheni maalumu kwa ajili ya uzinduzi na kuitangaza dira ya mabadiliko (vision for changes) ya chama chao ijulikanayo kwa jina la ‘Operesheni Zinduka’ itakayoanza Julai mosi mwaka huu.

“Operesheni hii itaongozwa na viongozi wa CUF na itatembea katika kanda zote saba za chama chetu, zikiwamo tano za Tanzania bara na mbili za Zanzibar kwa ajili ya kuwazindua wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu na ule wa taifa mwakani,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema katika hatua ya awali operesheni hiyo itanzia katika kanda ya Ziwa na kanda ya Dar es Salaam Julai mosi mwaka huu.

Wakati huohuo Profesa Lipumba aliwataka waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Mwinyi na Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Devis Mwamunyange, kuwajibika kwa kujiuzulu mara moja kufuatia uzembe wa mamlaka wanazoziongoza, uliosababisha milipuko ya mabomu Aprili 29 mwaka huu na kusababisha maafa makubwa kwa wananchi.

“Baraza kuu linalaani vikali ubaguzi wa dhahiri uliofanywa na unaondelea kufanywa kwa misingi ya kisiasa katika uhakiki na ugawaji wa misaada kwa waathirika wa milipuko hiyo,” alisema.

Alifafanua kuwa, baraza kuu la uongozi la CUF linalaani vikali matamshi ya dharau nay a kejeli yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Willim Lukuvi, ya kuwataka wananchi wa Mbagala kuzoeya milipuko ya mabomu na kuichukulia kama sehemu ya maisha kama wananchi wa Kipawa walivyozoeya sauti za ndege zinazoruka mara kwa mara katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

“Matamshi hayo yanaonesha dharau ya hali ya juu kwa wananchi walioathirika na vitendo vilivyosababishwa na uzembe na kutowajibika kwa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM),” alisema Profesa Lipumba.

Aliwata Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Machano Othman Said na Mkurugenzi wa Bandari ya Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe, kuwajibika kwa kujiuzulu mara moja kutokana na uzembe wa mamlaka wanazoziongoza uliosababisha vifo vya wananchi na hasara ya mali baada ya Meli ya MV Fatih kuzama ikiwa bandarini.

“Baraza linasikitishwa na uzembe uliofanywa na watumishi wa bandari ya Zanzibar kiasi cha Meli kuzama ikiwa bandarini nakupoteza maisha ya wananchi ambayo yangeweza kuokolewa,” alisema Lipumba na kusisitiza.

“Baraza kuu la CUF linazitaka serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar kuunda tume huru zikiwashirikisha wajumbe wa kambi ya upinzani Bungeni na katika baraza la wawakilishi wa Zanzibar kuchunguza chanzo cha milipuko na kuzama kwa meli ya MV Fatih na baadaye kutoa ripoti kwa wananchi.”

Kikao cha baraza kuu la uongozi la CUF kilimalizika juzi baada ya wajumbe kupitisha maazimio mbali mbali ya kiutendaji na kuhimiza uwajibikaji kwa serikali ya SMZ nay a Muungano.

No comments:

Post a Comment