MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Tuesday, June 9, 2009

Tani 3.8 za dawa zilizopita muda wa matumizi zateketezwa Dar

Salim Said

MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), imeteketeza tani 3.8 za dawa za Viuavijasumu (antibiotics) jamii ya ‘Pencillin’, Unga wa Sindano ya Benzathine Pencillin kutoka China, zenye thamani ya 62.6 milioni baada ya kusadikiwa kutokidhi viwango vya ubora.

Dawa hizo zilikamatwa katika maduka mbalimbali ya dawa na makazi ya mfanyabiashara mmoja wa kichina, anayefahamika kwa jina la Du Juu Zhe yaliyopo Kariakoo Jijini Dar es Salaam, kufuatia msako mkali uliofanywa na maofisa wa TFDA na Jeshi la Polisi, Machi 22 mwaka huu, baada ya kumtilia shaka.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Magreth Ndomondo, Afisa Uhusiano wa Mamlaka hyo, Gaudensia Simwanza, alisema walimuhisi Zhe kuwa anatunza dawa katika jengo lisilo na usajili wa TFDA kwa ajili ya utunzaji wa dawa, jambo ambalo ni kinyume na Sheria Nambari 1 ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya 2003.

“Muhusika anatambuliwa na TFDA kama muingizaji wa dawa husika nchini kutoka kiwanda kilichosajiliwa cha China, lakini katika msako huu tulikamata boksi 54 zilizoisha muda wake,” alisema Simwanza.

Alisema, dawa hizo toleo nambari 0602630 na 0602631, ambazo muda wake wa matumizi ulikwishapita tangu Febuari mwaka huu, zilikuwa zimesajiliwa na TFDA kwa nambari TAN 05,208J0H SH1, ambapo katika kila katuni ilikuwa na chupa 600.

“Kutokana na mazingira ya uhifadhi wa dawa hizo kutokidhi viwango, TFDA ilifuatilia jinsi dawa hizo zilivyosambazwa na kufanikiwa kuzuiya jumla ya boksi 173 zenye uzito wa tani 3.8 na thamani ya 62,640,000,” alisema Simwanza na kuongeza:

“Tulisitisha usambazaji na matumizi yake hadi hapo tutakapojiridhisha na ubora wa dawa hizo, lakini baada ya kufanya uchunguzi wa kimaabara kwa matoleo yote mawili, tulibaini kuwa hazikutimiza viwango na hivyo tukahikisha dawa hizo zinaondoka sokoni haraka ili ziteketezwe.”

Alisema, baada ya uamuzi huo walifanya utaratibu wa kuziteketeza dawa hizo na jana wakaamua kuziteketeza katika Dampo la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam lililopo Puga Kinyamwezi.

“Leo (jana) tunateketeza dawa hizi baada ya kuhakikisha kuwa utaratibu umefuatwa ikiwa ni pamoja na vipimo na mmiliki kujiridhisha,” alisema Simwanza.

Uteketezwaji wa dawa hizo ulifanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye silaha, mgambo wa Manispaa ya Temeke, TFDA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mei 26 mwaka huu, TFDA iliteketeza tani 34 za maziwa ya unga aina ya Golden Bell-Instant Full Cream kutoka China yaliyokuwa na thamani ya sh150 milioni, ambayo yalichanganywa na Kemikali aina ya ‘Melamine’ ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.

Kwa mujibu wa Sheria nambari moja ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003, mmiliki anapaswa kugharamia gharama zote za uteketezaji wa bidhaa zitakazogundulika kuwa chini ya ubora.


No comments:

Post a Comment