Salim Said
MUFTI wa Tanzania sheikh Issa Shaban Simba, amemfukuza kazi Katibu wa Baraza Kuu la Waislaam Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Arusha sheikh Ally Juma Mzee kufuatia tuhuma mbalimbali za ubadhirifu wa mali zinazomkabili.
Sheikh Mzee alitenguliwa katika nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Bakwata taifa Mei mwaka huu na kuteuliwa kuwa Katibu wa baraza hilo Mkoa wa Arusha kabla ya kufukuzwa kazi.
Mabadiliko hayo ya uongozi Mkoa wa Arusha yamefanyika wakati Mufti Simba akiwa nchini Uturuki kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Bakwata sheikh Suleiman Lolila, aliwaarifu waislaam nchini kote kuhusu mabadiliko ya uongozi wa Bakwata Mkoa wa Arusha.
“Tunapenda kuwaarifu waislaam nchini kote mabadiliko ya uongozi wa Bakwata mkoani Arusha, ambapo Katibu wa baraza mkoa huo, sheikh Ally Juma Mzee amefukuzwa kazi na nafasi yake inachukuliwa na ustadh Abdulkarim Jonjo,” alisema sheikh Lolila na kuongeza:
“Tunawaomba waislaam nchini kote watoe ushirikiano wa hali na mali kwa Jonjo, ili tuweze kufanikisha kusogeza mbele uislaam.”
Kwa mujibu wa sheikh Lolila, sheikh Mzee kwa sasa anabakia kuwa muumini wa kawaida wa dini ya kiislaam, badala ya kushika nafasi yoyote ya uongozi wa baraza.
Aidha, sheikh Lolila alisema Mufti Simba bado yuko Ankara Uturukia katika hospitali Bingwa akiendelea na uchunguzi wa afya yake na kwamba anaendelea vizuri.
“Na hivi karibuni anakusudia kukutana na viongozi wa serikali ya nchi hiyo pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi za kiislaam za Uturuki, kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya waislaam wa Tanzania likiwamo la elimu,” alisema sheikh Lolila.
Kabla ya sheikh Mzee kufukuzwa kazi Masheikh na waumini mkoani Arusha, walishampinga Mzee, kuendelea kuongoza baraza hilo kwa madai kuwa hana sifa.
Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Arusha, Mahmoud Salum, alisema katika tamko lao mara baada ya kikao kilichofanyika katika Msikiti wa Ngarenaro Arusha kuwa, kwa kauli moja wanaunga mkono mapendekezo na uamuzi wa Halmashauri ya Ulamaa Mkoa wa Arusha kumfukuza ustadhi Mzee.
''Tuhuma zilizomkabili ustadhi Mzee ni nzito, hivyo haturidhishwi na utendaji wake na pia kupewa jukumu kubwa la Katibu Mkuu wa Bakwata kwani, hana sifa stahiki,'' alisema Sheikh Salum.
Aidha Mwananchi imebaini kuwa ustadhi Mzee anakabiliwa na tuhuma za kutumia mapato ya msikiti huo na kusababisha hasara kwa baraza.
No comments:
Post a Comment