Salim Said na Neema Materu
SIKU moja baada ya Baraza Kuu la Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kuwatimua maofisa watatu wa uchaguzi, aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa chama hicho,Wilfred Lwakatare, amesema mamuzi hayo ndiyo yaliyomfanya kuwasilisha barua ya kuachia ngazi nyadhifa zake zote ndani ya chama.
Juzi Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba, alitangaza, kuwatimua Maole Kuchilingulo, aliyekuwa Katibu wa Tume ya Uchaguzi ya CUF, Hussein Mmasi na Juma Wandwi wajumbe, baada ya kubainika kuwa walikihujumu chama chao katika uchaguzi mdogo wa Busanda.
Lwakatare ambaye alishawahi kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini, alimewasilisha barua ya kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya chama hicho na jana alithibitisha habari hizo.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam, alisema amefikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho.
“Ni kweli nimewasilisha barua hiyo, kwa sababu sikuridhishwa na uamuzi wa vikao vya Baraza kuu wa kuwatimua maAfisa watatu wa uchaguzi wa chama chetu,” alisema Lwakatare.
“Nimeona maamuzi ya baraza hilo si ya mustakbali mzuri ndani ya chama chetu,” alisema.
Kauli hiyo imekuja huku kukiwa na taarifa kuwa, kigogo huyo wa CUF ana mpango wa kukihama chama hicho na kuhamia Chadema.
Lwakatare, alikiri kusikia uvumi huo.
“Hata mimi nasikia hivyo hivyo lakini hakuna mtu rasmi aliyeniambia taarifa hizo. Mimi sina uwezo wa kuzungumzia hilo kwa sababu uamuzi wa hilo wanao wananchi na si mimi,” alisema Lwakatare.
No comments:
Post a Comment