MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, October 7, 2009

Hamad amvaa JK

Salim Said na Levina Chengula
KATIBU mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameihusisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vurugu zinazoendelea Zanzibar katika zoezi la kuboresha daftari la kudumu la wapigakura, akidai ni mpango wa kumuandalia mgombea urais wa CCM visiwani humo mazingira ya ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwakani.


CUF imekuwa mpinzani mkubwa wa chama hicho tawala visiwani humo tangu kuruhusiwa kwa vyama vingi, kiasi cha kufanya matokeo ya uchaguzi wa rais wa visiwa hivyo kujawa na utata na mshindi, ambaye amekuwa akitokea CCM, kushinda kwa tofauti ndogo ya kura.

Lakini CUF imeeleza kuwa Serikali ya Muundano sasa inafanya njama ili mgombea wa chama hicho tawala aibuke na ushindi mkubwa zaidi ili kukimaliza nguvu chama hicho cha upinzani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Hamad alisema serikali ya Muungano inabariki vurugu hizo ili itekeleze nia yake ya kumuwezesha mgombea wake wa kiti cha urais wa visiwa hivyo kupata asilimia 70 ya kura katika uchaguzi mkuu ujao.

“...Lakini kipindi hiki tumepata taarifa za uhakika kutoka vyanzo vya kuaminika kwamba mikakati miovu ya kulivuruga daftari la wapiga kura Zanzibar inaendeshwa na kusimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya viongozi wakuu wa Serikali hiyo na vyombo vilivyo chini yake,“ alisema Hamad.

“Taarifa hizo zinaonyesha kwamba ni kutokana na mikakati hiyo hata maagizo yaliyotolewa hadharani na viongozi wa Zanzibar, akiwemo Rais Amani Karume kwamba Wazanzibari wote wenye sifa za kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi wapatiwe vitambulisho hivyo na kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hayakutekelezwa na vyombo vinavyoshughulikia suala hilo, yaani wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, Idara ya Usajili wa Wazanzibari Wakaazi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC),“ alisema.

“Matukio yote yanayotokea kisiwani Pemba na Unguja ni mkakati uliopangwa ili kumhakikishia ushindi wa asilimia 70 mtu wao ambaye wameshamuandaa.”


Kwa mujibu wa Hamad, ambaye alikuwa waziri kiongozi wa Zanzibar, serikali ya Muungano imeagiza kukiukwa maelekezo ya taratibu za zoezi hilo ili kupunguza kwa madri itakavyowezekana idadi ya Wazanzibari wenye na pia kuwaingiza wengine wasio Wazanzibari.

Alisema hayo yanafanyika ili CCM ijihakikishie ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwakani visiwani humo na kwamba matokeo yameshapangwa.

Alisema kwa upande wa Zanzibar mkakati huo unaungwa mkono na kuratibiwa na baadhi ya viongozi wa SMZ wenye malengo ya kugombea urais, ambao wamepewa tamaa na viongozi wa Serikali ya Muungano kwamba wana nafasi nzuri ya kupitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM.

“Tunazo taarifa za kutosha za hata wakuu wa mikoa na wilaya wa Zanzibar waliyoandaliwa kutekeleza mkakati huu muovu kufikia hatua ya kudharau hata maagizo ya SMZ kwa madai kwamba wanachokifanya kimeagizwa na Serikali kuu ya Muungano,” alisema Hamad.

Kwa mujibu wa Hamad, hadi sasa mkakati huo umefanikisha kuwakata zaidi ya watu 11,000 katika majimbo matatu ya Konde, Mgogoni na Micheweni Kisiwani Pemba na wengine 6,000 katika Jimbo la Magogoni, Unguja.

“Hali hii inatisha na iwapo itakamilishwa katika majimbo yote 50 ya Zanzibar kwa wastani wa kukatwa watu 3,500 kwa kila jimbo, itasababisha Wazanzibari wasiopungua 175,000 kunyimwa haki ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2010,” alisema.

“Huu ni uhalifu na uporaji mkubwa wa haki ya Wazanzibari ya kuchagua na kuwaweka madarakani viongozi wanaowataka, uliopangwa kutekelezwa na viongozi wa juu wa Muungano. Lakini uhalifu na uporaji huu hauwezi kukubalika hata kidogo kwa Wazanzibari.”
Zanzibar ina takriban watu milioni moja.


Alisema kuhusika kwa Serikali ya Muungano katika mkakati huo kunathibitishwa na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa bungeni mjini Dodoma kwamba uandikishaji wa wapiga kura Zanzibar ni halali na unafanywa kwa mujibu wa sheria licha ya wakazi wengi kunyimwa haki zao.

“Inasikitisha zaidi kuona kwamba Serikali ya Muungano sasa imejiingiza kichwa kichwa katika kuvuruga daftari la wapigakura kwa malengo ya kulinda maslahi yake maovu visiwani na dhidi ya demokrasia,” alifafanua Hamad.

Alikumbusha kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa bungeni Disemba 30 mwaka 2005 kwamba anasononeshwa na mpasuko wa kisiasa Zanzibar na kuahidi kuupatia ufumbuzi wa kudumu mpasuko huo haraka, akisema hakuwa na nia hiyo.

“Hatukujua kwamba dhamira yake halisi ya kuupatia ufumbuzi mpasuko huo ni kuvuruga daftari la wapigakura na uchaguzi ili chama na mgombea wake wa urais Zanzibar aonekane anakubalika,” alisema Hamad.

Alisema tayari wameshawaeleza Wazanzibari kutokubali kunyimwa haki zao na kuwataka wasimame kidete kudai haki zao kwa njia za amani bila ya kufanya vurugu.

“Hivi sasa sio Pemba tu, hata Unguja jana (juzi) nasikia wamewafungia ndani wafanyakazi wa Idara ya Uandikishaji Vitambulisho vya Ukaazi. Lakini kwa nini serikali iwafikishe hapo wananchi; kwa nini chaguzi zisiwe huru na haki; kwa nini tusiandae mkakati wa kufanya chaguzi huru na haki,” alihoji Hamad.

Hamad aliziomba kumuiya ya kimataifa kuingilia kati mikakati hiyo kwa lengo la kuinusuru Zanzibar na Tanzania kwa ujumla dhidi ya hatari ya kutokea janga alilodai linaandaliwa na serikali ya Rais Kikwete.

Hivi karibuni kumetokea matukio yanayoashiria machafuko ya kisiasa Zanzibar baada ya kuanza kwa awamu ya kwanza ya uboreshaji wa daftari la wapigakura ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2010.

Baadhi ya matukio hayo ni kumwagiwa tindikali kwa sheha wa Ole, Mussa Ali; kukataliwa baadhi ya wananchi kujiandikisha katika daftari; kususiwa kwa daftari; nyumba za viongozi kulipuliwa kwa mabomu na kukamatwa kwa watu wakihusishwa na vurugu zilizosababisha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kusitisha kazi hiyo kwa muda usiojulikana.

No comments:

Post a Comment