Salim Said
KAMBI ya upinzani kwenye Baraza la Wawakilishi imewapongeza wananchi wa jimbo la Ole kwa ujasiri wao katika kutetea haki zao uliosababisha zoezi la uandikishaji wapiga kura kwenye daftari la kudumu, kusitishwa.
Kambi hiyo inayoundwa na wajumbe wa CUF, imesema wananchi wa Ole ndio walioichachafya ZEC na kusababisha usitishwaji wa zoezi la uandikishaji.
Kambi hiyo pia imeilaumu Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ikidai zilihusika kuhujumu haki za kiraia na wananchi kisiwani Pemba.
Msimamo huo umo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana baada ya kumalizika kwa kikao cha pamoja cha wawakilishi wote wa CUF kilichofanyika juzi kwenye jimbo la Wawi wilayani Chake Chake, Pemba.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na mwenyekiti wa kambi hiyo, Abubakar Khamis Bakar, wawakilishi wanawaunga mkono wananchi wa jimbo la Ole kwa ukakamavu na ujasiri wa kuhakikisha kwamba haki yao ya kuwa wapigakura inapatikana.
“Msimamo wa kambi ya upinzani ndani ya Baraza la Wawakilishi ni kuwaunga mkono wananchi wote waliosimama kidete kutetea haki zao, hasa wale wa jimbo la Ole,” inaeleza taarifa hiyo ya Khamis ambaye pia ni mwakilishi wa jimbo la Mgogoni.
Siku chache zilizopita, maelfu ya wananchi katika shehia za Kiuyu Minungwini, Mjini Kiuyu, Mchangamdogo, Shumba ya Vyamboni na Sizini walijikusanya kwenye vituo vya uandikishaji wakiitaka ZEC iwaandikishe watu wote wenye sifa ya kuwa wapiga kura, vinginevyo tume hiyo isiandikishe mtu hata mmoja.
Wananchi hao hawakuwa na vitambulisho vya ukaazi wa Zanzibar, ambavyo ZEC inavitambua kama kielelezo pekee cha kumuwezesha mtu kuandikishwa kuwa mpigakura.
Wananchi hao, waliokuwa wakiimba nyimbo za kuhamasishana, walidai kwamba kuandikishwa kuwa wapigakura ni haki yao ya kikatiba, msimamo ambao umeungwa mkono na watunga sheria wa Baraza la Wawakilishi kutoka kambi ya Upinzani.
“Madai ya wananchi ni halali kisheria. ZEC inajaribu kutumia sheria Namba 12 ya 2002 ambayo katika kifungu chake cha kwanza (b) inazungumzia kuwa moja ya sifa za kutoweza kujiandikisha ni kutokuwa na kitambulisho cha Uzanzibari. Lakini kifungu (a) kinasema kuwa mtu anaweza kuandikishwa ikiwa ametimiza masharti ya kifungu cha 7 (2) cha Katiba ya Zanzibar, ambacho kabisa hakiweki kitambulisho cha ukaazi kwa kigezo cha kujiandikisha,” alisema Khamis.
“Mle mnatajwa kitambulisho cha umri au uraia au uandikishwaji kuwa mpigakura. Kwa hivyo, hati yoyote ile ambayo ingeliweza kuthibitisha moja kati ya hayo ingetosha kumpatia mtu haki yake ya kupiga kura. ZEC inapolazimisha kuwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi tu ndicho kitumike inakwenda kinyume na katiba na hilo wananchi wanalielewa.”
Khamis alisema hiyo ndiyo sababu iliyowasukuma wananchi kusema kama ni kuandikishwa, waandikishwe wote kwa mujibu wa katiba au asiandikishwe hata mmoja, kutokana na kuhisi kuwa serikali haina nia ya kuwaandikisha.
Alisema kambi yake inasimama pamoja na wakaazi wote wa jimbo la Ole na kuwataka wananchi wa maeneo mengine ya Zanzibar kuiga mfano wa wenzao kama serikali haitafanya marekebisho ambayo aliyataja kuwa ni kuondoa sherti la kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi au kuwapa Wazanzibari wote wenye sifa vitambulisho hivyo kabla ya kuanza tena zoezi hilo.
“Hapa ni moja kati ya mawili: aidha serikali iiagize ZEC kufuata ule uamuzi wa makamishna wa tume hiyo kwamba kithibitisho chochote cha ukaazi na uzawa kitumike kumruhusu mtu kuandikishwa au isitishe zoezi la uandikishaji mpaka kila mtu mwenye sifa awe amepata kitambulisho chake cha ukaazi. Hakuna njia ya mkato katika hili,” alisema Said Ali ambaye ni msemaji wa upinzani kuhusu fedha na uchumi kwenye Baraza la Wawakilishi.
Said alisema ukweli ni kuwa serikali imekuwa ikitumia hila, udanganyifu na ghilba nyingi ili kuhakikisha kuwa wakazi wengi wa kisiwa cha Pemba, ambacho ni ngome ya upinzani dhidi ya serikali, hawaandikishwi kuwa wapigakura, na hivyo kupunguza nguvu za upinzani nchini.
Said alionyesha barua zilizoandikwa mwezi Juni na Julai mwaka huu kwa hati za mkono kutoka kwa Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha kwenda kwa watendaji, akijnga hoja kuwa kiongozi huyo alishatoa agizo kwa watendaji wa chini yake kuhakikisha kuwa kila mtu anapatiwa kitambulisho.
Hata hivyo, masheha ambao ndio watendaji wa chini wa serikali wanasema kwamba hawajapewa fomu zinazowawezesha watu kupata vitambulisho hivyo.
Hivi karibuni kuliripotiwa kwamba masheha wa maeneo kadhaa kisiwani Pemba wamekuwa wakikataa kuwapatia wananchi fomu za kudai vitambulisho vya Uzanzibari Mkaazi kwa madai kwamba watu hao hawana vyeti vya kuzaliwa.
Lakini hata watu hao walipokwenda mahakamani kudai hati za viapo ili kupata vyeti hivyo, nako walikataliwa kupewa hati hizo.
Katika kile kinachoonekana kama ni kuwepo kwa usumbufu wa makusudi kwa wananchi, masheha wamekuwa wakikataa hata kutoa fomu za kuwasaidia wakazi wao kutoa taarifa za kupotelewa kwa mali zao katika vituo vya polisi.
Mfumo wa utawala wa Zanzibar unawapa masheha, ambao ni ngazi ya chini kabisa ya utawala, madaraka makubwa ya kuamua hatima ya wakaazi wa maeneo yao katika masuala mbalimbali yakiwemo haki za kiraia kama uchaguzi.
Wakilishi hao pia walilaani vikali vitendo walivyoviita vya kuingilia mamlaka za taasisi huru vinavyofanywa na mkuu wa mkoa wa Kaskazini Pemba , Dadi Faki Dadi.
Baadhi ya vitendo hivyo ni pamoja na, kufanya kikao cha pamoja kati ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa na mahakimu wa mkoa wake na kuwakataza mahakimu hao wasitoe hati za viapo kwa watu wanaokwenda kuomba hati hizo kwa ajili ya kuthibitisha uzawa wao.
No comments:
Post a Comment