Mohamed Ghassan, Pemba na Salim Said
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Husein Mwinyi amesema Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) halitakiwi kufanya shughuli zozote za ulinzi katika maeneo ya vituo vya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura hadi hapo mamlaka za kiraia zitakapoliomba rasmi kufanya kazi hiyo.
Dk Hussein Mwinyi ametoa kauli hiyo katika uwanja wa ndege wa Karume kisiwani Pemba muda mfupi baada ya kuwasili na ujumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanya ziara ya siku moja kisiwani Pemba.
"Sisi kama wasimamizi wa JWTZ, kwa kawaida mpaka mamlaka za kiraia zitakapotuomba rasmi msaada wetu kama utahitajika ndipo huwa tunafanya kazi hiyo, lakini kwa sasa tumekuja kwa safari ya kawada tu kutembelea vikosi vya Jeshi," alisema Dk Hussein Mwinyi.
Dk Mwinyi alisema wao kama viongozi wa Wizara zilizo chini ya kamati hiyo ya bunge ya ulinzi na usalama wanatakiwa kuwa pamoja na kamati hiyo katika maeneo yote wanayotembelea na kukagua vikosi vya JWTZ, Jeshi la Polisi, Uhamiaji pamoja na kuangalia majukumu ya ulinzi na usalama katika kisiwa cha Pemba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo Wilson Masilingi alisema kamati yake imesikitishwa na matukio yaliyojitokeza katika zoezi la uandikishaji ikiwemo kumwagiwa tindikali mmoja wa viongozi (Sheha) hali ambayo ni tishio la uvunjifu wa amani.
Alisema kamati hiyo inawaomba Wazanzibari upande wa Pemba watoe ushirikiano kwa Serikali hasa baada ya kufanya mazngumzo na Rais Aman Abeid Karume ambaye aliihakikishia kamati hiyo kuwa kila mtu atapata haki ya kuandikishwa ili aweze kupiga kura.
Miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo waliowasili jana Pemba ni Jackson Makweta, Athuman Ngwilizi, Masoud Abdllah Salim, Feteh Mgeni, Beutrice Shelukindo, Khalifa Suleiman, Saleh Farah na John Shibuda.
Taarifa za kuwasili kwa kamati hiyo ya bunge zilipokelewa kwa hisia tofauti huku wananchi wengi wakiamini kuwa ziara hiyo ililenga suala zima la uandikishaji hasa baada ya tukio la askari wa vikosi vya SMZ kufyatua risasi katika kituo cha Mchanga mdogo muda mfupi baada ya tume ya uchaguzi kufunga vituo vya uandikishaji.
Wakati huo huo Mbunge wa viti maalum jimbo la Wete (CUF) Riziki Omar Juma alisema, wananchi walijitokeza kwa wingi katika vituo vya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura jana, lakini walikuta vituo hivyo vikiwa vimefungwa.
Alisema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilisimamisha zoezi hilo juzi baada ya kutokea kwa vurugu baina ya wananchi na vyombo vya dola.
Alifafanua kuwa, ZEC haikuwatangazia wananchi kwamba zoezi hilo limesitishwa na hivyo kusababisha wananchi hao kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kujiandikishia.
“Sisi tulifika vituoni majira ya saa 3:00 asubuhi na kuwakuta wananchi wengi vituoni, lakini tuliwaomba wananchi watawanyike na kwenda kufanya shughuli zao kwa sababu ZEC imesitisha uandikishaji,” alisema Juma ambaye pia ni Katibu wa CUF wilaya ya Wete.
Katika hatua nyingine Mbunge Juma alisema, vijana Ali Bakari Hassan na Khamis Ali Ali walioshambuliwa na askari wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) walifikishwa mahakamani jana wakikabiliwa na makosa ya Uzembe, Ukorofi na kuzuiya gari la msafara wa askari waliokuwa wakienda kumpeleka Sheha.
“Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 11 mwaka huu na washitakiwa wamerudishwa rumande baada ya kukataliwa kupewa dhamana,” alisema Juma.
Aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuhakikisha kwamba wanatumia nafasi hiyo ya kusitishwa kwa zoezi la uandikishaji kuwapatia wananchi haki yao, ambayo wananyimwa kutokana na kisingizio cha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (Zan ID).
“Haki tunanyimwa kwa kisingizio cha Zan ID na chanzo cha kupatia kitambulisho hicho ni masheha ambao ni kikwazo kikubwa, wanaweka vipingamizi vya kila namna ilimradi kuwakwamisha na kuwakatisha tamaa wananchi,” alisema Juma.
No comments:
Post a Comment