MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Tuesday, February 9, 2010

Membe: Ama zao ama zetu waliohusika rada

Salim Said

SAKATA la kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi nchini, limeingia katika sura mpya baada ya serikali kuahidi lazima iwashughulikie watuhumiwa wote waliohusika katika kashfa hiyo, ili kulinda heshma ya nchi katika sura ya kimataifa.

Hivi karibuni kampuni ya BAE Systems inayodaiwa kumlipa dalali zaidi ya Sh12 bilioni kwa kufanikisha kwake serikali ya Tanzania kununua rada ya kijeshi ya Plessey Commander Fighter Control System kwa Sh 40 bilioni, imekiri makosa na kuahidi kurudisha fedha kwa serikali ya Tanzania.

Wiki iliyopita BAE System ilikiri kufanya makosa kwa kulipa rushwa katika mkataba wa kuiuzia serikali ya Tanzania rada hiyo ya kijeshi, chini ya Sheria ya Mikataba ya Makampuni ya mwaka 1985.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC), mjini Dodoma jana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema lazima serikali isafishe wale wote waliohusika na kashfa hiyo kwa kulinda heshma ya nchi.

Alisema kashfa ya sakata la rada imefikia katika ukingo wake, baada ya BAE System kukiri makosa na kukubali kujisafisha kutokana na makosa hayo.

“BAE imejisafisha, imekiri makosa na imekubali kujisafisha na ule ndio uaminifu, wanakwenda wanafanya uchunguzi, wanagundua udhaifu, wanakiri makosa na wanajisafisha,” alisema Membe.

Membe alifafanua kuwa baada ya BAE System kukubali kujisafisha kwa kuirudishia Tanzania "chenji" yake, kazi kubwa iliyobaki ni kwa serikali kuhakikisha inawashughulikia wahusika.

Alisema, “…..lakini la pili ambalo sihitaji ushauri wala utaalamu kulisemea, ni kwamba safari hii ya sakata la rada imefikia ukingoni, wenzetu wameshajisafisha na sisi hatuna budi kujisafisha katika sura ya dunia,”.

“Kwa hiyo sasa shughuli ni kwetu sisi, mimi nina uhakika kabisa zile nchi zilizoguswa na kashfa hii zitachukuliwa kutoka pale, ili zisafishwe na sisi Watanzania sasa lazima tujiweke sawa tujisafishe katika sura ya kimataifa, yaani katika ngazi ya kimataifa ya nchi zinazoheshimika katika utawala bora,” alisisitiza Membe.

Membe alifafanua kuwa, “Lazima tulifikishe suala hili katika hitimisho lake, yani lazima tujisafishe, tukae vizuri ili tuonekane kwamba mashimo yote ya rushwa yamefukiwa na kama kuna mtu yeyote amehusika katika kashfa hii, hiki ndicho kipindi ambacho, utawala bora wa Tanzania unatakiwa kuimarishwa.”

Membe alisistiza kuwa suala la rada nchini halitopita hivihivi bila ya kuchukuliwa hatua za kisheria ili Tanzania ijionyeshe katika sura ya dunia kwamba inawajibika.

“Suala hili halitoisha hivihivi kwa sababu tumesemwa sana na lazima tujionyeshe katika serikali za dunia na katika uhusiano wa kimataifa kwamba na sisi tuko ‘responsive’ (tunawajibika) kwa maana tunajibu mapigo,” alisema Membe na kusisitiza;

“Kama hili limetokea na tumepata ushahidi, lazima tusafishane humu ndani kwa heshima ya nchi,”.

Juzi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Sofia Simba alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa hadi sasa hakuna taarifa rasmi ambayo serikali imepokea kuhusu sakata la kashfa ya rada, isipokuwa wamekuwa wakisoma katika magazeti na katika mitandao ya kimataifa.

Hata hivyo, aliahidi kuwa, watakaohusika katika kashfa hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Katika moja ya ziara zake nchini Uingereza, Rais Jakaya Kikwete aliambia Serikali ya Wingereza kwamba kama kuna fedha imezidi katika ununuzi wa rada anaomba chenji yao.

Membe alisema jana kuwa, hatimaye sasa chenji hiyo inarudi na kwa maana hiyo Tanzania imeula kwa kurudishiwa fedha hiyo takribani paundi 28 milioni kwani miradi mingi itafanikiwa.

“Tanzania tumeula na tunasema Alhamdulillaahi, nilisema na narudia tena kwa vile tunarudishiwa chenji yetu tumeula, miradi yetu itakwenda vizuri, kilimo kwanza kitakwenda vizuri, elimu yetu itakwenda vizuri na masuala mengine yatakwenda vizuri,” alisema Membe.

Wanaotuhumiwa na kashfa ya rada ni Mwanasheria Mkuu wa wakati huo Andrew Chenge, Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Dk Idrisa Rashid na dalali mwenye asili ya Asia, Saileth Vithlani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni mtu alioongoza wanaharakati katika kufichua sakata la ununuzi wa rada na ndege ya rais tangu wakati wa rais Mkapa, alisema anashangazwa na kigugumizi cha serikali kuchangamkia fedha hizo.

“Nastaajabu sana ufisadi ndani ya nchi hii, nyinyi mmetapeliwa na taarifa zimo katika vyombo vya habari vya uhakika, lakini waziri anaulizwa anasema serikali haijapata taarifa rasmi, si ufuatilie,” alihoji Lipumba.

Alisema kigugumizi cha serikali kwenda kudai fedha hizo kinakuwapo kwa sababu, waliohusika na kashfa hiyo wapo madarakani na hivyo wanaogopa kuwajibika.

No comments:

Post a Comment