MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Tuesday, February 9, 2010

Fataki atinga bungeni

Salim Said

MBUNGE wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti jana alizua kicheko kwa wabunge wenzake baada ya kuitaka serikali kuliangalia upya jina la watu wanaowapachika mimba wanafunzi la Fataki, kwa madai kuwa jina hilo ni la babu yake.

Kimiti ambaye ni mmoja kati ya wabunge waliokaa bungeni kwa muda mrefu na mwenye umri mkubwa, alitangaza kuachana na ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa ubunge, urais na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Kimiti alimuomba Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza kuliangalia upya jina hilo kwa sababu huwa anaumia akisikia wanaitwa watu wanaowapachika mimba wanafunzi kwa kuwa ni jina la babu yake.

“Mheshimiwa Spika naomba serikali iliangalie upya jina la Fataki kwa watu hao kwa sababu ni jina la babu yangu,” alisema Kimiti bila ya kufafanua.

Kimiti hakufafanua iwapo babu yake anatumia jina hilo kama la utani au iwapo ni jina lake halisi alilopewa na wazazi wake.

Baada ya mbunge Kimiti kutoa hoja hiyo, Spika wa Bunge Samuel Sitta alihoji kwa utani iwapo babu yake alikuwa Fataki kweli au la.

“Lakini Mheshimiwa Kimiti hakutufafanulia iwapo babu yake alikuwa Fataki kweli au vipi,” alisema Spika Sitta huku wabunge wengine wakiangua kicheko.

Akijibu suala hilo, Mahiza alisema wizara yake itawatafutia jina jingine waharibifu hao ili kuepukana na kumkwaza mbunge Kimiti.

“Mheshimiwa Spika tutawatafutia jina jingine mafataki wa elimu nchini,” alijibu kwa ufupi Mahiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya alikiri kuwa jina hilo linaweza kuleta maumivu makali ikiwa ni jina halisi la mtu fulani katika jamii.

“Kwa kweli ikiwa ni jina halisi la mtu ni kweli linaweza kuleta maumivu makali, lakini hii ni changamoto kubwa katika sanaa zetu kuangalia kwanza kama majina tunayoyatumia hayataumiza baadhi ya watu,” alisema Nkya.

“Kwa kweli hata kama ni baba yangu au baba yako ndugu mwandishi usingefurahi kutokana na maana ya jina lile, ungejisikia vibaya hata mimi pia kama ni baba yangu ningejisikia vibaya.”

Hata hivyo, Nkya alisema ni vigumu kwa sasa kulifuta jina hilo katika nyoyo za watu kwa kuwa limeleta athari kubwa na kwamba lina maslahi ya umma.

“Kwa vile jina hili lina maslahi ya umma na limeleta athari sana katika sekta ya elimu, mheshimiwa Kimiti angejaribu kumuelewesha babu yake aone kama vile yeye ni msanii anatumia jina hilo, lakini sio sifa yake kwa sababu kitaaluma na kimaadili huwezi kumnusuru mtu mmoja kwa kuwaumiza wengi,” alisema Nkya.

Fataki ni tangazo lililobuniwa na wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kitengo cha kuzuia Ukimwi.

No comments:

Post a Comment