Salim Said
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemshukia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapnduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete kwamba, ziara yake jijini Dar es Salaam ililenga kujipigia kampeni na kwamba ni matumizi mabaya ya madaraka ya umma.
Rais Kikwete alifanya ziara ya siku tatu jijini hapa, ambapo wachambuzi wa mambo wameihusisha na kampeni zake za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010 huku akitarajiwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM.
Mkurugenzi wa Siasa wa CUF Mbarallah Maharagande, alisema CUF inasikitishwa na matumizi mabaya ya madaraka yaliyofanywa na Rais katika ziara zake zilizofanyika wiki iliyopita.
Maharagande alisema mwenyekiti huyo wa CCM alitumia ziara hiyo ya kichama kutoa ahadi mbali mbali za kiserikali huku baadhi ya wakati akitoa kauli za kutishia kuwawajibisha watendaji wa Serikali, ili kujisafishia njia.
“Katika ziara hiyo, pamoja na kuongozana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam William Lukuvi, ambapo si sahihi kabisa katika ziara za kichama lakini, Kikwete alitumia ziara hiyo ya kichama kutoa ahadi mbalimbali za kiserikali, huku akitoa kauli za kutishia kuwawajibisha watendaji wa Serikali, ili kujisafishia njia,” alisema Maharagande.
Alisema CUF inalaani vikali ziara hiyo ambayo alidai ni matumizi mabaya ya madaraka, kwa kutumia nafasi ambazo ni za kuchaguliwa kwa kura za wananchi wenye itikadi tofauti na wasio na itikadi kwa maslahi ya CCM.
“CUF tunawaomba watanzania kuwa makini na viongozi wa Serikali ambao ni wasanii hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi ambapo, hujitokeza kwa ahadi zisizotekelezeka ambazo, ni kiini macho kwa nia ya kuwalaghai watananzania,” alisema Maharagande.
Wakati huohuo Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa CUF, Ashura Mustafa alisema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kwamba, chama chake hakikushangazwa na matokeo mabovu ya kidato cha nne katika shule za sekondari za Kata mkoani Dar es Salaam.
“Haya ni matokeo ya mipango na sera mbovu za CCM na serikali yake kwa kurejesha tena mfumo wa ualimu pasipo na elimu (UPE) katika ngazi ya Sekondari,” alisema katika taarifa yake.
Alisema pamoja na wadau wengi wa elimu nchini, kupigia kelele kuhusu madhara ya shule za sekondari za kata, lakini serikali ya CCM imekaidi na kudai kuwa ni mchakato bila ya kujua kuwa wanafunzi wa shule hizo hawasimami kusoma wanaenda sambamba na shule nyingine zenye ubora wa waalimu na vifaa vya kisasa.
“Pia wanaotunga mitihani hawajali kuwa shule za kata ziko katika mchakato na hazina maabara, maktaba na zina waalimu waliopata mafunzo ya wiki tatu na pia hawakufanya vizuri katika mitihani yao ya kumaliza kidato cha sita,” alisema Mustafa.
“CUF inaitaka serikali ya CCM kuacha kuwahadaa watanzania katika sekta ya elimu ili, kutimiza malengo yao ya kupigiwa kura katika chaguzi mbalimbali kwa kuwajengea shule za kata ambazo, hazina mwelekeo wa kutoa elimu bora kwa watoto masikini wa kitanzania,” alisema.
No comments:
Post a Comment