MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Sunday, May 31, 2009

Urithi mweusi wa Bushi

Kipindi cha miaka minane ya utawala wa Rais George W. Bush wa Marekani pamoja na wenzake wa mrengo wa wahafidhina mambo-leo kinaelekea ukingoni katika hali ambayo ulimwengu unaachwa na kumbukumbu chungu ya utawala na siasa zao mbovu katika Ikulu ya White House.

Kwa kuzingatia madhara ya siasa hizo ambazo zimewaletea wanadamu machungu mengi, ulimwengu kamwe hausikitishwi na kuondoka kwao madarakani bali unaridhishwa na jambo hilo ambalo bila shaka litapunguza mivutano na vita katika pembe mbalimbali za dunia.

Tarehe nne Novemba mwaka huu wa 2008, Wamarekani walishiriki katika uchaguzi muhimu ambao uliomwondoa madarakani Rais Bush na kumfungulia Barack Obama mlango wa utawala kupitia uchaguzi huo uliomshirikisha mgombea huyo wa chama cha Democrat na John McCain wa chama tawala cha Republican.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kupita miezi 20 ya kampeni kali za uchaguzi ambazo ziligharimu mabilioni ya dola za Wamarekani na kushuhudia mijadala mitatu muhimu kati ya wagombea hao.

Mbali na kampeni hizo ambazo zimepelekea kuchaguliwa Barak Obama kuwa rais wa kwanza mweusi na wa 44 katika orodha ya marais wa Marekani, lakini Wamarekani na walimwengu bado wanaathirika na madhara ya siasa mbovu za ubabe, upande mmoja na za umwagaji damu za Rais Bush pamoja na watenda jinai wenzake wa mrengo wa wahafidhina mambo-leo katika Ikulu ya White House.

Bila shaka machungu yanayowasibu walimwengu hivi sasa kutokana na siasa hizo yataendelea kushuhudiwa kwa miaka mingi ijayo.

Katika mazungumzo yake ya hivi karibuni alipokutana na shakhsia kadhaa wa kisiasa na kidini mjini Tehran, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alisisitiza kwamba ukweli mchungu unaoshuhudiwa hii leo katika pembe mbalimbali za dunia, vikiwemo vita, majanga ya njaa na ukiukwaji wa haki za binadamuu, yote hayo yanatokana na dhulma ikiwemo ya uchu wa madaraka na tamaa ya watawala.

Kwa msingi huo alisema, katika kila juhudi zinazofanywa kwa lengo la kutatua matatizo yanayoukabili ulimwengu, nara za uadilifu na mapambano dhidi ya dhulma zinapasa kuchukuliwa kuwa muhimili na nguzo muhimu.

Alisema kuwa mazungumzo na kubadilishana mawazo ni jambo zuri na la dharura na kusisitiza kuwa, jambo hilo lina nafasi muhimu katika kuleta maelewano kati ya mataifa na serikali mbalimbali. Ameongeza kwamba licha ya hayo, lakini jambo hilo pekee halitoshi kufutilia mbali sifa mbaya za madola ya kibabe na dhalimu ulimwengu wala kutatua masaibu yanayoikumba jamii ya mwanadamu, bali mambo mengine yanapasa kutiliwa maanani kuhusiana na suala hilo.

Ayatullah Khamenei aliongeza kwamba, uonevu na dhulma ndicho chanzo cha historia ya masaibu na matatizo yanayoikumba jamii ya mwanadamu. Huku akiashiria mauaji ya kinyama ambayo yamekuwa yakifanywa na Marekani pamoja pamoja na nchi nyingine za Magharibi dhidi ya watu wa Iraq, Afghanistan na Palestina, Ayatullah Khamanei aliuliza swali hili kuwa je, mauaji hayo yanatokea kutokana na kutokuwepo maelewano na kutofahamiana vyema pande mbili hizi au yanatokana na tamaa, ubabe na dhulma ya madola makubwa? Hata kama migogoro inayoendelea nchini Afghnaistan, Iraq, Palestina na mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini na ule unaogharimu fedha nyingi wa Iran, mpango uliofeli eti wa Mashariki ya Kati Kuu na mivutano iliyopo kati ya Marekani na China na vilevile Russia inaweza kuchukuliwa kuwa miongoni mwa mifano ya wazi ya kufeli kwa siasa mbovu za Marekani ulimwenguni, lakini rais huyo anayeondoka madarakani anakabiliwa na matatizo mengine chungu nzima ndani ya Marekani yenyewe.


Mfano wa wazi zaidi wa matatizo hayo yanayowakabili Wamarekani hivi sasa kutokana na siasa mbovu za rais wao, ni mgogoro wa kifedha unaoendelea hivi sasa nchini humo.

Si tu kwamba mgogoro huo umewakumba Wamarekani peke yao bali na ulimwengu mzima kwa ujumla, kutokana na kuwa mifumo ya kiuchumi ya nchi nyingi ulimwenguni inafungamana na mfumo wa kifedha na kiuchumi wa Marekani. Uchumi wa nchi hiyo ndio mkubwa zaidi duniani.

Kufeli kwa siasa za Bush ndani na nje ya mipaka ya nchi hiyo hakujafumbiwa macho na Wamarekani bali siasa hizo mbovu na za kupenda vita, na hasa kuhusiana na Iraq na Afghanistan, zimekabiliwa na radiamali kali ya Wamarekani wa kawaida na vilevile wasomi na wanafikra wa masuala ya kisiasa wa nchi hiyo.

Katika maafikiano yasiyo ya kawaida ya kimitazamo, mara hii wasomi wengi wa Marekani wamekubaliana kwamba urithi wa pekee ulioachwa na Bush na wahafidhina wenzake mambo-leo, ambao wameeneza siasa za uchokozi, uharibifu, vita na umwagaji damu kote ulimwenguni unaoana kikamilifu na maana ya ibara 'urithi mweusi.'

Huku akisema kuwa mshindi wa uchaguzi wa Marekani hatapata fursa nzuri ya kutulia na kupumzika, Chas Freeman, mkuu wa kamati ya Marekani inayoshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati anaamini kuwa, ili kubadili sura mbaya na nyeusi ya Marekani iliyoharibika duniani kutokana na siasa mbovu za Rais Bush, rais wa baadaye wa Marekani atahitaji kufanya jitihada maradufu ili kupunguza chuki na hasira iliyoenea duniani dhidi ya nchi hiyo kutokana na siasa mbovu za Bush.

Kwa mujibu wa Freeman, rais wa baadaye wa Marekani anapasa kufungua ukurasa mpya katika siasa za nje za Marekani kwa ajili ya kuwakinaisha walimwengu kwamba serikali mpya ya nchi hiyo inaheshimu sheria za kimataifa na kwamba iko tayari kurekebisha siasa nyeusi na mbovu zilizotekelezwa na Bush kuhusiana na kashfa za jela za Abu Ghuraib na Guantanamo na vilevile kurekebisha siasa hizo zilizotumika na serikali inayoondoka madarakani kwa shabaha ya kumwaga damu za watu wasio na hatia katika nchi za Iraq na Afghanistan.

Katika ripoti ya hivi karibuni kwenye mtandao wake, harakati inayopinga vita ya Anti-War iliashiria rekodi mbovu ya siasa za uingiliaji na uchokozi za serikali ya Bush dhidi ya nchi nyingine na kusema kuwa rais huyo ndiye aliyetengwa na kuchukiwa zaidi katika historia ya marais wa Marekani. Laurence Wool, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sheria cha Massachusetts nchini Marekani pia anasema kuwa Bush na serikali yake wanapasa kufikishwa mbele ya vyombo vya mahakama kuhusiana na jinai walizofanya na kuchukuliwa hatua za kisheria hata kama itakuwa na maana ya kupewa adhabu ya kifo kama watapatikana kuwa na hatia.

Francis Fukoyama, mwananadharia wa Marekani na ambaye hivi karibuni alijitenga na mrengo wa Wazayuni na Wakristo wenye misimamo ya kupindukia nchini humo pia hivi karibuni aliandika kitabu ambapo alisema kuwa, udiplomasia wa kikaoboy wa Marekani ulikuwa unaelekea ukingoni na kuituhumu serikali ya Bush kwamba imetumia vibaya madaraka.

Joseph Nay, mkuu wa zamani wa Halmashauri ya Habari za Kitaifa ya Marekani vilevile hivi karibuni aliwalinganisha marais wa Marekani na kusema kuwa Bush ndiye rais mbaya na anayechukiwa zaidi katika historia ya marais wa Marekani katika kipindi cha karne mmoja iliyopita. Amesema, katika kipindi cha utawala wake, serikali ya Bush imekuwa ikitajwa ulimwenguni kuwa serikali inayochukiwa ziadi na mataifa.

Paul Findlay, mbunge wa zamani wa Marekani katika Congress ya nchi hiyo kwa tiketi ya chama cha Republican aliandika makala ya kielimu katika gazeti la Lebanon la Daily Star ambapo alisema kwamba, serikali ya Bush ilifanya makosa makubwa na ya kipumbavu ambayo yamehatarisha usalama wa Marekani.

Seneta Joe Biden, Makamu wa Rais wa baadaye katika serikali ya Obama alisema katika mjadala wake wa televisheni wa hivi karibuni na Sara Palin ambaye alikuwa mgombea mwenza wa John McCain kwamba, hali mbaya inayotawala hivi sasa nchini Marekani inatokana na siasa mbovu za Bush.

Akizungumza hivi karibuni na televisheni ya CNN, Nancy Pelosi Spika wa Congress ya Marekani alimwita Bush kuwa msindwa mkuu na halisi wa siasa zake na kuongeza kuwa amepoteza shakhsia na itibari yake mbele ya Wamarekani, yakiwemo masuala yanayohusiana na uchumi, vita na nishati.

Katika kampeni zake za uchaguzi kabla ya kushindwa na mwenzake, Barrack Obama katika kinyang'anyiro cha kuwania urais wa Marekani, Seneta Hillary Clinton aliashiria kufeli kwa siasa za Bush katika kipindi cha miaka minane ya utawala wake nchini Marekani na kusema kuwa hatua za lazima zilipasa kuchukuliwa ili kukomesha siasa zake za kikaoboy na hivyo kupunguza madhara ya siasa hizo kwa taifa la Marekani.

Bush ambaye alijiita kuwa Kaoboy alipoingia madarakani nchini Marekani, amepitisha miaka hiyo mieusi kwa kutekeleza siasa hatari za umwagaji damu katika maeneo mengi ya dunia. Ubovu wa siasa hizo ulianza kuonekana wazi pale alipoanza kupinga wazi, na kwa mshangao wa wengi katika upeo wa kimataifa, juhudi za kimataifa za kulinda mazingira na kukabiliana na uchafuzi wa hali ya hewa duniani.

Kwa kisingizio cha kulinda viwanda vya Marekani, Bush alipinga vikali na akakataa kutia saini mkataba wa kulinda mazingira wa Kyoto Japan. Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo, hatua hiyo imeongeza matatizo ya mazingira pamoja na kiwango cha joto duniani. Kipindi hiki cheusi cha utawala wa Bush ambacho kinamalizika kwa mgogoro wa fedha na uchumi, kinaelekea ukingoni katika hali ambayo walimwengu wanatamani kimalizike haraka ili waweze kupumzika kutokana na matatizo pamoja na mikasa kilichoandamana nayo.

Kipindi hicho mbali na kuandamana na mikasa mikubwa ikiwemo ya fedha na uchumi pamoja na uharibifu wa mazingira, kimekuwa na machungu mengine mengi ambayo yalisababishwa na siasa mbovu za Bush, vikiwemo vita vya Afghanistan ambavyo vilitekelezwa dhidi ya makundi ya Taliban na al-Qaida kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Ni wazi kuwa vita hivyo havikuwa na natija nyingine isipokuwa kuwafaidi magaidi na kuwaletea machungu zaidi wananchi wa Afghanistan.

Hii leo, licha ya kuwepo kwa wingi askari-jeshi wa Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi Nato, katika ardhi ya Afghanistan na kwa uongozi wa Marekani, matatizo ya Waafghani yamekithiri na ulanguzi wa madawa ya kulevya umeongezeka maradufu. Si tu kwamba wafuasi wa makundi ya Taliban na al-Qaida wanajiimarisha zaidi, bali kwa mshangao na aibu kubwa, watawala wa kisiasa na kijeshi wa Marekani hivi sasa wanadai kwamba makundi hayo yanayochukuliwa kuwa ni ya kigaidi hayawezi kutokomezwa kwa njia za kijeshi bali, yanapaswa kushirikishwa katika mazungumzo ya amani na pia katika uendeshaji wa serikali kwa kupewa nyadhifa muhimu za wizara katika serikali hiyo!

Matamshi ya hivi karibuni ya Robert Gates, Waziri wa Ulinzi na vilevile, Condoleezza Rice, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani juu ya ulazima wa kushirikishwa serikalini makundi ya Taliban na al-Qaida na ushauri wao kwa serikali ya Hamid Karzai kuwa anapasa kuanzisha mazungumzo na makundi hayo ya kigaidi, ni ishara na tathmini kwamba njia za kijeshi dhidi ya makundi hayo hazina tena athari na kwamba njia bora ni kufanywa mazungumzo na magaidi. Kufeli kwa nadharia ya Marekani ya kutekeleza vita kwa ajili ya kuzuia mashambulio, nadharia ambayo ilitumiwa na serikali ya Bush kwa lengo la kuanzisha vita dhidi ya Iraq na kupitia propaganda chafu na kubwa za mtambo wa propaganda wa vyombo vya habari vya Marekani, hii leo ni jambo ambalo liko wazi kwa kila mtu kulishuhudia duniani.

Hadi leo Wamarekani wameshindwa kuthibitisha madai yao kwamba Iraq ilikuwa na mpango wa kutengeneza silaha za maangamizi ya umati za nyuklia na kemikali na vilevile kwamba ilikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mtandao wa al-Qaida, visingizio viwili vilivyotumiwa na serikali ya Bush kuanzisha hujuma kali ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo. Kisingizio kingine kilichotolewa dhidi ya serikali ya Dikteta Saddam Hussein ni kuwa ilihusika kwa njia moja au nyingine katika mashambulio ya Septemba 11 katika miji ya New York na Washington.

Hii leo Wamarekani wameshindwa kabisa kurudisha amani na utulivu nchini Iraq na ili kuondokana na jinamizi linalowaandama kutokana na siasa zao bovu katika nchi hiyo, wanajaribu kuepuka mashinikizo yanayotolewa dhidi yao kimataifa na ndani ya Marekani yenyewe kuhusiana na jambo hilo kwa kujaribu kuwatupia wengine lawama za machafuko yanayoendelea nchini humo.

Wanajaribu kupunguza mashinikizo hayo kwa kudai kwamba nchi jirani ndizo zinazochochea machafuko katika ardhi ya Iraq au kuwashinikiza viongozi wa Iraq watie saini mkataba wa amani na serikali ya Washington ili jambo hilo liwape mwanya wa kupumua, wakidhani kwamba kuendelea kubaki kwao nchini Iraq kwa muda zaidi huenda kukawapa fursa ya kutatua matatizo ya usalama ya nchi hiyo na wakati huohuo kuwapa fursa ya kupora utajiri wa Iraq na kutekeleza malengo yao mengine haramu nchini humo.

Ni wazi kuwa hii leo siasa za upande mmoja za Marekani zimefeli kabisa na wala serikali ya Marekani haiwezi kudai kwamba Iraq ni nchi yenye uthabiti na iliyosimama kwenye misingi ya demokrasia ya kuagizwa kutoka nje. Hatua ya watawala wa nchi hiyo ya kuomba msaada wa mashirika na jumuiya za kimataifa ziingilie kati baada ya kushindwa siasa zake za upande mmoja, ni dalili ya wazi inayothibitisha kwamba jumuiya hizo sio ubao wa sataranji unaotumiwa daima na watawala wa Marekani kama muhuri wa kupitisha na kuunga mkono siasa zao za kibabe na kijuba duniani.

Mfano mwingine wa wazi wa watawala wa Marekani kutumia nguvu zao za kijeshi kama wenzo wa kufikia malengo yao haramu duniani ni mashinikizo yao dhidi ya Ethiopia kwa lengo la kupelekwa askari jeshi wake katika ardhi ya Somalia mwaka 2006. Jambo hilo kwa hakika halijakuwa na natija nyingine isipokuwa mauaji, wizi, uporaji na utumiaji mabavu dhidi ya raia wasio na hatia. Mkono mbovu wa watawala hao wapenda vita pia unaonekana wazi katika mauaji na machafuko yanayoendelea hivi sasa katika mpaka wa Pakistan na jirani yake Afghanistan, nchi ambayo imekuwa ikihesabiwa kuwa mshirika wa kwanza wa Washington katika vita vinavyodaiwa kuwa ni vya kupambana na ugaidi wa kimataifa.

Hii ni katika hali ambayo mzozo ambao unachukuliwa kuwa mkubwa zaidi katika Mashariki ya Kati, yaani suala la Palestina, ni nembo ya faili jeusi la serikali mbalimbali za Marekani na hasa utawala wa miaka minane wa Bush. Faili hilo limefumbiwa macho na kunyamaziwa kimya na Wamarekani kana kwamba halina umuhimu wowote kwao.

Miaka minane ya Bush imepita bila ya kutekelezwa ahadi za uongo za utawala huo za kusaidia kuunda serikali ya taifa huru la Palestina. Badala yake utawala huo umekuwa ukiunga mkono waziwazi jinai zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia wala ulinzi. Kwa masikitiko makubwa, uungaji mkono na himaya ya serikali ya Washington kwa jinai za utawala huo zimeupelekea kumea pembe na kupata kiburi zaidi cha kuendelea kutekeleza jinai zake hizo dhidi ya watoto, wanawake, wazee na vijana wa Kipalestina huku ulimwengu mzima ukiwa umenyamaza kimya na kutochukua hatua yoyote ya maana kwa ajili ya kukabiliana na jinai za utawala huo.

Kufanywa mazungumzo yasiyo na natija, uungaji mkono mkubwa na usio na masharti wa serikali ya Washington kwa utawala haramu wa Israel pamoja na kupuuza haki za Wapalestina imekuwa moja ya nguzo muhimu za serikali ya Bush katika kipindi cha miaka minane iliyopita. Hii ni katika hali ambayo mzingiro wa kidhulma wa chakula, madawa na misaada ya dharura kwa Wapalestina umeimarishwa zaidi dhidi ya Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza. Mifano hii ni moja ya ukweli mchungu unaotawala hii leo ulimwenguni, mifano ambayo matokeo yake yanapasa kuwa funzo kwa watu wanaofuata kibubusa siasa za Marekani. Hatima ya Parviz Musharraf wa Pakistan ni mfano mzuri wa ukweli huo.

Siasa za Bush zilipata pigo jingine kubwa kwa kufichuliwa njama za serikali yake za kuzusha mgogoro wa kifedha na kiuchumi duniani. Mara hii mfumo wa kiuchumi wa Marekani umepata pigo kubwa na hata kumpelekea Bush mwenyewe kuomba msaada kutoka kwa jamii ya kimataifa ili kuiokoa nchi hiyo katika siku za mwisho za serikali yake. Kwa bahati mbaya, madhara ya mgogoro huo wa kiuchumi yamezipata pia nchi masikini ambazo zinalazimika kulipa gharama ya mgogoro huo wa Marekani.

Hata hivyo, inatarajiwa kuwa mgogoro huo wa kiuchumi na kifedha utakuwa na matokeo mazuri kwa Bush, wahafidhina mambo-leo na rais wa baadaye wa Marekani kwa kuwakumbusha kwamba wanapasa kuondoa vichwani mwao fikra kwamba wao ndio viongozi wa ulimwengu. Wakati huohuo wanapasa kutambua kwamba siasa za mabavu na kujichukulia maamuzi ya upande mmoja hazitawafikisha popote na kwamba wanawajibika kukubali na kutambua rasmi ukweli wa kuwepo nguvu za nchi nyingine duniani na hasa zile za nchi za Kiislamu.

Kwa vyovyote vile kipindi cha miaka minane ya utawala wa wahafidhina mambo-leo nchini Marekani kimemalizika na kuanza kipindi kilichojaa changamoto muhimu kwa watawala wa baadaye wa chama cha Democrat. Ulimwengu unasubiri kuona iwapo watawala hao watabadili siasa mbovu za uchokozi, ubabe na ujuba zilizotekelezwa na wenzao Warepublican au wataamua kuendelea na siasa hizo na hivyo kuvuruga zaidi amani na utulivu wa ulimwengu.

No comments:

Post a Comment