Salim Said
MAREKANI imesisitiza kuwa itatekeleza ahadi yake ya kuipatia Tanzania fedha kwa ajili ya miradi ya changamoto za Milenia (MCC) licha ya uchumi wake kutikisika.
Hayo yalielezwa juzi na rais Jakaya Kikwete alipokuwa akifungua harambee ya kuchangisha fedha za Mfuko wa Elimu mkoa wa Rukwa, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Jambo la faraja kwetu ni kuwa miradi ya MCC haijaathirika na matatizo ya mtikisiko wa uchumi wa dunia nchini Marekani, wala mabadiliko ya serikali ya nchi hiyo,” alisema Rais Kikwete na kusisitiza:
“Marekani imenihakikishia kuwa fedha ya miradi hiyo bado ipo, imetengwa na iko salama. Vilevile serikali ya rais Barrack Obama, inaunga mkono mpango wa MCC na miradi yake hapa nchini, na ile yote iliyoamuliwa na rais mstaafu George Bush.”
Aidha alifafanua, fedha za barabara za ndani ya mkoa wa Rukwa zipo kupitia misaada ya Benki ya Dunia, kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya kilomita 230 kutoka Sumbawanga hadi Mpanda.
Alizitaja barabara nyingine kuwa ni pamoja na ile ya Chala-Katongoro kilomita 87, Kilyamatunda-Muze kilomita 148 na upanuzi wa bandari ya Kusanga katika ziwa Tanganyika unaofanywa na mamlaka ya bandari.
“Nataka kuwahakikishia kuwa ni dhamira ya serikali kuchukua hatua za dhati kukabiliana ya barabara yanayoukabili mkoa wa Rukwa,” alisema rais Kikwete.
Kuhusu maendeleo ya elimu Rais Kikwete, alisema hivi sasa kata zote 2,556 nchini zina sekondari yake na kwamba nyingine zina sekondari zaidi ya moja.
“Matkeo yake ni kuongezeka kwa vijana wa kike na kiume wanaoingia sekondari kutoka 180,239 mwaka 2005 hadi 432,000 mwaka 2008,” alisema rais.
Hata hivyo alisema, maendeleo makubwa nay a haraka katika sekta ya elimu nchini yana changamoto za kupata walimu bora, maabara, vitabu na nyumba za walimu.
“Tumejipanga vyema kukabiliana na changamoto zote hizo. Nyongeza kubwa ya bajeti ya elimu ni ushahidi tosha wa kutambua wajibu wetu,” alithibitisha.
No comments:
Post a Comment