MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Sunday, May 31, 2009

Mahakama yatetea uamuzi wa mjane kurudishwa kwenye nyumba alimofukuzwa

Ellen Manyangu na Salim Said

MAHAKAMA ya Ardhi Wilaya ya Kinondoni imetupilia mbali ombi la wakili wa mlalamikaji katika shauri la kutaka mahakama hiyo ifute agizo la mjane Shamsa Nassor wa Kiluvya kurudishwa katika nyumba alimohamishwa.

Mwenyekiti Joseph Kaare alitoa uamuzi huo jana alipokuwa akisoma hukumu ya maombi hayo yaliyowasilishwa na mlalamikaji Abdalah Malik kupitia wakili wake kutoka kampuni ya uwakili ya Rutabingwa.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo yakiambatanishwa na nakala mbalimbali za hukumu zilizotolewa na mahakama za ngazi tofauti kuhusu kesi hiyo.

Nakala hizo, ambazo ni kutoka katika ngazi ya Mahakama ya mwanzo Magomeni, mahakama ya Wilaya Kinondoni na Mahakama Kuu ya Tanzania (High Court).

Kaare alithibitisha kuwa, nakala za hukumu za kesi ziliwasilishwa mahakamani hapo na wakili Rutabingwa hazihusiani na kesi ya ardhi aliyopeleka Shamsa Nassor.

Alisema, nyumba na eneo ambalo Rutabingwa aliwasilisha nyaraka zake ni la marehemu Zuwena Salum (mama mkwe wa Shamsa) ambayo msimamizi wake ni Mohammed Markbel na sio ya marehemu mume wa mjane huyo Salum Aklan.

“Amri yangu ya kumrudisha nyumbani mwake Shamsa, ambayo Rutabingwa alinitaka kuitengua haihusiani na mali zote za Zuwena wala maamuzi yoyote ya mahakama,” alisema Kaare katika hukumu ya kukataa ombi hilo na kusisitiza:

“Amri yangu ilikuwa ya kumrudisha mlalamikaji katika nyumba ya marehemu mume wake Salum Aklan, ambayo Shamsa na Alhaj Mohammed walichaguliwa kusimamia eneo na mali hiyo na mahakama ya mwanzo Kinondoni, ambapo namba ya kesi ilikuwa 55 ya mwaka 2008.”

Katika hukumu yake ambayo nakala imepatikana Kaare alisema, kwa maamuzi hayo nyumba iliyokuwa na mgogoro anayoishi mlalamikaji (Shamsa) ni ya marehemu mume wake Salum Aklan na maamuzi hayo hayajawahi kutofautishwa na maamuzi mingine yoyote.

Kwa upande wake Wakili wa Malik alikataa kuzungumza na mwandishi wa Mwananchi kwa madai kuwa hana muda.

“Sina muda wa kuzungumza na wewe kama unataka njoo ofisini,” alisema Rutabingwa ambaye pia Mwananchi ilimshuhudia akizungumza na waandishi wa baadhi ya vyombo vya habari nje ya mahakama hiyo ya Ardhi.

Baada ya hapo, Mwandishi wa habari hii alimpigia simu Malik ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Maji ya Cool Blue, Tembo Blox na Safari Kargo ili kuzungumzia kutupiliwa mbali kwa ombi lake.

“Sitaki kuzungumza katika simu, nifate ofisini, kwanza ulishindwa kunifata ofisini ukaandika uongo mtupu,” alisema Malik na kukata simu.

Hata hivyo baada ya dakika 10, Malik aliamua kumpigia simu mwandishi na kumueleza kwamba yeye hana kesi na Shamsa na kudai kuwa, mwenye kesi ni Shamsa na msimamizi wa mirathi ambaye hakumtaja jina lake.

“Usiniandike mimi sina kesi na Shamsa mwenye kesi na Shamsa ni msimamizi wa mirathi,” alijitetea Malik na kukata simu bila ya kumruhusu mwandishi kuzungumza.

Hata hivyo alipoulizwa Mohammed Markbel ambaye ni msimamizi wa mirathi ya marehemu Zuwena iwapo ana kesi na Shamsa au la, alikanusha kwa madai kuwa kesi zote zilishatolewa hukumu mahakamani.

“Mimi sina kesi na Shamsa ila tatizo lilikuwa baada ya kuteuliwa mimi kuwa msimamizi wa mirathi ya Zuwena Salum, Shamsa alikataa lakini alishindwa kwa sababu nilichaguliwa na watu watatu na yeye pekee ndiye alikataa,” alisema Markbel.

No comments:

Post a Comment