MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Sunday, May 31, 2009

Serikali kupunguza gharama za mawasiliano

Salim Said

SERIKALI inafikiria kuangalia upya mfumo wake wa gharama za kodi kwa vyombo vya mawasiliano, ili kuwianisha gharama za mawasiliano kwa nchi zote tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, uamuzi huo unakuja kutokana na gharama za mawasiliano nchini kuwa juu kuliko nchi nyingine.

Hatua hiyo ni katika juhudi za serikali ya Tanzania kutaka kupunguza gharama za mawasiliano nchini ili kuwianisha gharama zake za mawasiliano na zile za nchi tano za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla, mara baada ya kufungua siku ya pili ya mkutano wa kuwianisha kanuni na sera za mawasiliano ya posta na simu, kwa nchi za Afrika Mashariki, uliomalizika jana, jijini Dar es Salaam.

Profesa Msolla alisema, gharama za mawasiliano nchini ziko juu zaidi kuliko nchi zote za Afrika Mashariki na Kati na kwamba tatizo ni mfumo wa kodi wa Tanzania kwa vyombo vya mawasiliano.

“Gharama za mawasiliano tanzania ziko juu kuliko nchi nyingine kwa sababu ya mfumo wa gharama za kodi kwa vyombo vya mawasiliano,” alisema Msolla.

Hata hivyo alisema, serikali ina mpango wa kuangalia upya mfumo huo wa kodi kwa ajili ya kuwianisha viwango vya gharama za mawasiliano miongoni mwa nchi zote tano za Jumuiya ya Afrika ya ashariki.

“Serikali inaandaa utaratibu wa kuangalia upya mfumo wake wa kodi hasa kwa vyombo vya mawasiliano ili viwango vya gharama za bidhaa hii viweze kufanana miongoni mwa nchi washiriki wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki,” alithibitisha Msolla.

Alisisitiza kuwa mawasiliano ni moja ya bidhaa katika soko la pamoja la Afrika ya Mashariki kwa hiyo lazima gharama zilingane kwa watumiaji wote wa mijini na vijijini.

Aidha alifafanua kuwa mkutano wa 16 wa wadhibiti na watoa huduma ya mawasiliano wa ukanda wa Afrika ya Mashariki pia ulijadili ujenzi wa mundombinu ya uhakika ya mawasiliano ili bidhaa hiyo iweze kuwafikia watu wote wa mijini na vijijini.

Aidha priofesa Msolla alisema, katika kufanikisha shirikisho la Afrika ya Mashariki lazima maudhui ya vyombo vya mawasiliano na lugha zifanane ili kulinda utamaduni wa watu wake.

“Sisi tuna lugha zetu na mila na utamaduni wetu, kwa hiyo maudhui ya vyombo vyetu vya mawasiliano lazima yange katika kulinda na kuendeleza utamaduni wetu,” alisema Msolla na kusisitiza:

“Tusiwe tunaiga na kufuata mila na tamaduni za watu, tunacho Kiswahili chetu basi tukitumie kwa manufaa ya watu wetu.”

Kwa upande wake Mshauri wa Sheria wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Rwanda, Lamin Jabir alisema, serikali ya nchi yake inajitahidi kutoa ruzuku kwa watoa huduma za mawasiliano ili kuwapa nafuu watumiaji.

“Serikali yetu inajitahidi kutoa ruzuku kwa watoa huduma ya mawasiliano ili mtumiaji aweze kumudu kwa urahisi,” alisema Jabir na kusisitiza:

“Lakini pia sera, sheria na kanuni zetu ni nzuri kabisa kwa watumiaji na watoa huduma.”

No comments:

Post a Comment