MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Sunday, May 31, 2009

Mamlaka zakutana kujadili sera,kanuni

Salim Said

MAMLAKA za Mawasiliano za nchi tano za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, zimekutana na watoa huduma za mawasiliano jijini Dar es Salaam kuoanisha sera, sheria na kanuni za mawasiliano katika nchi hizo.

Mamlaka hizo zilikutana jana katika semina iliyojali umuhimu wa kuharakisha uundaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki.
Tayari baadhi ya asasi za shirikisho hilo zimekwishaundwa.

Akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Dk. Naomi Katunzi, alisema katika mjadala wa kuunda soko la pamoja baina ya nchi hizo, suala la mawasiliano lilijitokeza.

“Kwa hiyo leo tupo hapa kwa ajili ya ‘kuoanisha sera, sheria na kanuni za mawasiliano miongoni mwa nchi washiriki,” alisema Dk. Katunzi na kuongeza:

“Mawasiliano na biashara ni vitu vinavyotegemeana kwa karibu, huwezi kufanya biashara na kufanikiwa bila ya kuwa na mawasiliano mazuri yanayohusisha wafanyabiashara, walaji na wadhibiti,” alisema.

Hata hivyo shirikisho hilo, linaonekana kuwa na kikwazo ambapo nchi za Kenya na Uganda zinagombania kisiwa cha utalii cha Migingo.

Katibu mkuu huyo alisema, Tanzania itakuwa kitovu cha mawasiliano kupitia Mkonga wake wa taifa wa mawasiliano na kwamba nchi hizo jirani zitaomba kuunganishwa katika mkonga huo kupitia Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Profesa John Nkoma, alisema mkutano huo pia unawakutanisha wadhibiti na watoa huduma za mawasiliano kutoka nchi hizo.

Alisema, moja ya lengo la semina hiyo ni kujadiliana nao kuhusu namna ya kupunguza gharama za mawasiliano kwa watumiaji.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya Kanuni, Posta na Mwasiliano) Charles Njoroge wa Kenya, alisema jumuiya yake imekuwa vikikutana mara kwa mara, kujaribu kuweka utaratibu na mfumo wa mawasiliano unaofanana baina ya nchi husika.

“Tutajitahidi kuwasiliana na watoa huduma ili kuhakikisha kuwa gharama za mawasiliano katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki zinakuwa rahisi zaidi,” alisema Njoroge ambaye pia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya.

No comments:

Post a Comment