MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Thursday, August 16, 2012

TRA WAPATA SCANNER MPYA TANGA

TANGA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Tawi la Tanga imepata mashine mpya ya kisasa yenye uwezo wa kutambua bidhaa zilizohifadhiwa ndani ya makontena (Scarner) na kuiwezesha mamlaka hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi na haraka.
Meneja wa Mamlaka hiyo Mkoani Tanga Nyonge Mahanyu, amesema mashine hiyo itakuwa mkombozi kwa wafanyabiashara wa mkoa huo kwa kuwa itaondosha kero za wafanyabiashara kucheleweshewa shehena zao katika Bandari ya Tanga.
Mahanyu amesema awali wafanyabiashara wa Tanga walikuwa wakilalamikia kucheleweshwa kwa ukaguzi wa mizigo yao bandarini hapo jambo lililokuwa likitishia uhai wa bandari kongwe ya mkoa wa Tanga.
Amesema baada ya ujio wa mashine hiyo utaweka mvuto kwa wafanyabiashara wengi kwa kuwa wataweza kushusha shehena zao kwa wakati na bila ya usumbufu.
Mahanyu amefafanua kuwa mashine hiyo ina uwezo wa kukagua kontena moja kwa dakika tatu tu jambo ambalo litaiwezesha TRA kukagua makontena mengi ndani ya muda mfupi na hivyo kukusanya kodi nyingi tofauti na ilivyo sasa.
Kwa upande wake mtaalamu wa Scana Mhandisi Julias Joseph, amesema mashine hiyo ambayo ina uwezo mkubwa wa kukagua na kutambua shehena zilizomo ndani ya makontena itakuwa kimbilio la wafanyabiashara kushusha bidhaa zao katika bandari ya Tanga.
Kutokuwapo kwa ufanisi katika utoaji wa huduma katika Bandari ya mkoa wa Tanga kumesababisha wafanyabiashara wengi nchini kuikimbia bandari hiyo na kuamua kushushia mizigo yao katika bandari za Mombasa, Zanzibar na Dar es Salaaa.

No comments:

Post a Comment