ZANZIBAR
Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimesema wanafunzi wote
wanaomaliza masomo yao na ambao hawatakamilisha malipo ya ada hadi
Agosti 22 mwaka huu hawataruhusiwa kufanya mitihani yao ya muhula wa
pili kwa mwaka 2011/2012.
SUZA
inatarajia kuanza mitihani yake ya muhula wa pili ya kufunga mwaka
wasomo kuanzia Agosti 22 mwaka huu chuoni hapo.
Onyo
hilo limetolewa na Makamu Mkuu wa SUZA Professa Idriss Ahmad Rai
mbele ya waandishi wa habari muda mfupi baada ya kikao cha pamoja
kati ya uongozi wa chuo na serikali ya wanafunzi kwenye Makao Makuu
ya chuo hicho Vuga, mjini Unguja.
Profesa
Rai amesema onyo hilo halitawahusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa
pili ambao wameruhusiwa kufanya mitihani baada ya kujaza mkataba
maalum baina ya mwanafunzi binafsi na chuo.
Profesa
Rai amesema mkataba huo utawalazimisha wanafunzi hao kulipa
malimbikizo ya ada wanayodaiwa kabla ya kuanza muhula mpya wa masomo
unaotarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu na kwamba watakaoshindwa kulipa
hawataruhusiwa kuanza masomo katika muhula huo.
Hata
hivyo amesema wanafunzi watakaoshindwa kuanza mitihani Agosti 22
mwaka watapewa nafasi ya kufanya mitihani wakati wa mitihani ya
marejeo (supplementary examination) lakini kwa upande wao utakuwa
ndio mtihani wa kawaida iwapo watakamilisha malipo ya madeni yao.
Professa
Rai amesema SUZA imeamua kufanya uwamuzi huo mzito kutokana na
wanafunzi wengi kushindwa kulipa ada zao na hivi sasa wanawadai kiasi
cha shilingi 270 milioni.
Amesema
lengo la chuo siyo kuwakomoa wanafunzi lakini ni njia ya kuhakikisha
wanapata fedha ambazo ni muhimu katika kukiendeleza chuo hicho pamoja
na ruzuku inayotolewa na Serikali.
Ameongeza
kuwa wanaelewa ugumu wa maisha unaowakabili wanafunzi wengi hasa
katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani na kuelekea sikukuu ya
IDD-EL-FITRI lakini alidai hakuna njia ya mkato ya kupata mapato ya
kuendesha chuo hicho.
No comments:
Post a Comment