MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Monday, May 25, 2009

DC akiri vyama vya upinzani kuimarika

Salim Said

MKUU wa Wilaya ya Makete mkoani Iringa, Hawa Ng’humbi amewataka viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kujipanga vizuri, ili kuhakikisha wanapata ushindi mkubwa katika chaguzi za serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu, kwa kuwa upinzani umekuwa mkubwa sasa.

Akizungumza mara baada ya kutawazwa kuwa Mlezi Mkuu wa Jumuiya hiyo, kata ya Mabibo jijini Dar es Salaam jana, Ng’humbi alisema matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu ndiyo utakaotoa taswira ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 nchini kote.

“Tujipange vizuri katika uchaguzi za serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka, ili kujenga mazingira ya CCM kutwaa tena dola mwakani katika uchaguzi mkuu na pia kuzuia jimbo la Ubungo lisichukuliwe na upinzani” alisema Ng’humbi.

Ng’humbi ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro kabla ya kuhamishiwa Makete, alisema upinzani kwa sasa ni mkubwa na kila chama cha upinzani kinajaribu kujiimarisha ili kuhakikisha kwamba kinashika dola.

“Ndugu zangu mimi ni mchapa kazi mzuri, nitahakikisha kwamba tunashirikiana katika kuhakikisha tunashinda uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu katika kata yetu na taifa kwa ujumla,” aliahidi Ng’humbi.

Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo kata ya Mabibo Bononi Mlowe aliwataka, wanajumuiya kutokubali kurubuniwa kwa fedha na kuchaguwa wafadhili badala ya viongozi.

Alisema, watanzania wamekuwa wakichagua viongozi kwa miaka mingi lakini viongozi hao hawawajali wapiga kura wao na badala yake wanaamua kutajirisha matumbo yao.

Alisema katika awamu yake, atahakikisha kuwa anawashawishi viongozi wa jumuiya hiyo kutafuta kazi nyingine kwa ajili ya kupata fedha na kuifanya kazi ya uongozi kuwa huduma badala ya biashara.

“Wakipata kazi nyingine ya kutafutia fedha watakuwa waaminifu katika mali za chama na ada za watoto wetu, hii itatusaidia kunyanyua maendeleo na kuimarisha Chama chetu,” alisema Mlowe.

No comments:

Post a Comment