Mwandishi Wetu
MUFTI wa Tanzania sheikh Issa Shaban Simba ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislaam Tanzania (Bakwata) ustadhi Ally Juma Mzee na kumteua sheikh Suleiman Said kukaimu nafasi hiyo.
Mabadiliko hayo yamefanyika kimya kimya bila ya kutangazwa kabla ya Mufti Simba kusafiri kuelekea nchini Uturuki, ambako ameenda kufanya uchunguzi wa kawaida wa afya yake.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema kwamba, Mufti amechukua hatua hiyo kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa mali za Bakwata zinazomkabili aliyekuwa Kaibu Mkuu wake ustadhi Mzee.
Utenguzi huo unafanyika wakati uchaguzi mkuu wa baraza hilo unaendelea kufanyika katika ngazi mbalimbali kuanzia Msikiti hadi taifa.
Kabla ya Mufti kufanya utenguzi huo Masheikh na waumini mkoani Arusha, walishampinga ustadhi Mzee, kuendelea kuongoza baraza hilo kwa madai kuwa hana sifa.
Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Arusha, Mahmoud Salum, alisema katika tamko lao mara baada ya kikao kilichofanyika katika Msikiti wa Ngarenaro Arusha kuwa, kwa kauli moja wanaunga mkono mapendekezo na uamuzi wa Halmashauri ya Ulamaa Mkoa wa Arusha kumfukuza ustadhi Mzee.
''Tuhuma zilizomkabili ustadhi Mzee ni nzito, hivyo haturidhishwi na utendaji wake na pia kupewa jukumu kubwa la Katibu Mkuu wa Bakwata kwani, hana sifa stahiki,'' alisema Sheikh Salum.
Aidha, Bakwata Mkoa huo ilitoa onyo kali Mei 21 mwaka huu kwa ustadhi Mzee, ambaye sasa ni katibu wa Bakwata mkoa kwa madai anawarubuni waumini ili kuibua upya mgogoro wa kidini ambao walishaupatia ufumbuzi.
Aidha Mwananchi imebaini kuwa ustadhi Mzee anakabiliwa na tuhuma za kutumia mapato ya msikiti huo na kusababisha hasara kwa baraza.
Pamoja na uamuzi huo mzito wa Mufti bado baadhi wa maafisa wa ngazi za juu wa Bakwata hawajaridhika na wanasema licha ya Mufti kutengua uteuzi wa ustadhi Mzee na kumteua kuwa Katibu wa Mkoa wa Arusha wa baraza hilo, ni kwamba bado hajatatua tatizo.
“Tatizo la mwenzetu ni kubwa kwa sababu anakabiliwa na tuhuma za ufisadi lakini Mufti analichukulia suala kijujuu jambo ambalo ni hatari na linaweza kuligawa Bakwata,” alisema Afisa mmoja na kuongeza:
“Kwa nini waumini ambao unawaongoza wakukatae? Lazima kutakuwa na matatizo tu unachaguliwa kuwa katibu wa Mkoa wa Bakwata halafu unafukuza viongozi na kuchagua unaoona watafanyakazi kukulinda unapofanya maovu yako. Hata ukatibu wa msikiti unautaka wewe.”
“Mufti ni bora akaunda tume huru kwanza kuchunguza tuhuma za ustadhi mzee na siyo kulichukulia suala hili zito juu juu,” alisema.
Uchunguzi unaonesha kuwa Msikiti Mkuu wa mkoa wa Arusha una vitega uchumi vingi vikiwamo milango mingi ya maduka ambayo inakodishwa kwa wafanyabiashara na kuliingizia mapato Baraza.
“Sio siri bwana, mwenzetu anakabiliwa pia na tuhuma za kuuza viwanja vya Wakfu vya Bakwata, lazima watu wakukatae kwa hali hiyo,” alisema Afisa mwengine na kusisitiza:
“Mufti bado hajatatua tatizo kwa sababu ustadhi Mzee anakabiliwa na tuhuma za ufisadi Arusha na waumini wa mkoa huo wameshamkataa, halafu unamrudisha tena kuwa katibu wa mkoa, haingii akilini.”
No comments:
Post a Comment