MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Monday, May 25, 2009

HRLC Yalaani kupigwa Trafiki

Salim Said

KITUO cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu nchini (HRLC) kimelani vikali kitendo cha askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kumsambulia kwa kumpiga askari wa usalama barabarani, Sajenti Thomas Mayapila akiwa kazini.

Askari hao wa JWTZ walifanya kitendo hicho, mapema wiki hii baada ya kushuka katika gari lao na kumshambulia Mayapila wakidai kuwa, aliwachelewesha kuvuka katika makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma Ubungo jijini Dar es Salaam, walipokuwa katika msafara wao kuelekea Mbagala.

Akizungumza na Mwananchi Jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kituo hicho, Francis Kiwanga alisema, wanalaani vikali kitendo hicho kwa kuwa ni kinyume na sheria, haki za binadamu na uraia.

“Tunalani vikali kitendo cha askari wa JWTZ kumsambulia kwa kumpiga askari wa usalama barabarani akiwa kazini, kwa sababu ni kinyume cha sheria, haki za binadamu na haki za uraia,” alisema Kiwanga.

Kiwanga aliitaka serikali kuchukua hatua kali za kisheria na kinidhamu kwa wote waliohusika katika kitendo hicho kibaya haraka iwezekanavyo, ili iwe fundisho kwa wengine wenye kiburi cha namna hiyo.

“Tunaiomba serikali ichukuwe kwa haraka sana hatua kali za kisheria na kinidhamu kwa wote waliohusika katika kumshambulia askari mwenzao, ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema Kiwanga.

Alifafanua kuwa, askari wa JWTZ nchini wanajiona kuwa wako juu ya sheria na kwamba wanaweza kufanya lolote na kwa wakati wowote, jambo ambalo si kweli hata kidogo.

Alisema, kiburi cha askari wa JWTZ kinatokana na elimu ndogo ya uraia na ya haki za binadamu waliyonayo.

“Tunawaomba wakuu wa vikosi vya JWTZ watengeneze mazingara ya kuwapatia mafunzo ya elimu ya uraia na haki za binadamu askari wao kwa sababu inaoneka elimu yao ni ndogo sana,” alisema.

Alisema, kupitia utaratibu huo wataweza kupunguza kiburi cha wanajeshi na kuwafanya wananchi wa Tanzania kusalimika na kiburi hicho.

Matukio ya askari wa JWTZ kuwashambilia askari wa usalama barabarani na raia wa kawaida yamekuwa yakitokea mara kwa mara nchini, jambo ambalo limekuwa likisababisha madhara makubwa kwa wanaoshambuliwa.

No comments:

Post a Comment