Salim Sai
MTANDAO wa asasi za kiraia nchini, FemaAct, jana umeeleza kuwa dola ya Tanzania imetekwa na kundi la mafisadi.
Tamko hilo, lilosainiwa na viongozi kutoka asasi 14 za kiraia na lililowakilisha asasi 50 wanachama wa mtandao huo, lilisomwa na msemaji wa FemAct, Buberwa Kaiza mbele ya waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) yaliyo Mabibo jijini Dar es Salaam.
Kaiza, ambaye anatoka taasisi ya Fordia, alisema wameamua kutoa tamko hilo kali kwa kuwa wameguswa na kuchukizwa na mwenendo wa kushughulikia matukio ya ufisadi na ukwapuaji wa mali za umma nchini, ambao unaendelea kushamiri nchini.
“Kushamiri kwa ufisadi kunabainisha jambo moja kubwa na lenye kutia shaka. Ni kwamba dola ya Tanzania tayari imetekwa na mafisadi,” alisema Bubelwa.
“Tumetathmini kwa muda mrefu na kubaini kuwa kushamiri kwa ufisadi nchini kunasababishwa na kutekwa kwa dola, sera ya uchumi wa soko holela, kutokuwepo kwa misingi endelevu ya utawala bora, ulafi wa madaraka na ubinafsi wa viongozi.”
Pia alisema kitendo cha wananchi kutodai uwajibikaji; kuendelea kutumika kwa baadhi ya sheria za kikoloni; katiba iliyopitwa na wakati na serikali kulea kundi la ‘wateule’ wasioguswa na sheria, ni ushahidi tosha wa kutekwa nyara kwa dola ya Tanzania na mafisadi wachache.
“Ushahidi mwingine wa dola kutekwa na mafisadi ni serikali na bunge kutumikia maslahi ya watu wachache; kutawala kwa rushwa kubwa; kulegalega kwa dola katika kuwachukulia hatua za haraka za kinidhamu na kisheria watuhumiwa wa ufisadi; kucheleweshwa kwa kesi za wakubwa za tuhuma za ufisadi na sheria kutumikia wachache,” alisema Bubelwa.
Bubelwa alifafanua kuwa kushamiri kwa ufisadi na sera za uchumi wa soko holela nchini kumesababisha madhara makubwa kwa Watanzania masikini.
Alisema madhara hayo pia yanasababishwa na hali ya serikali kukosa msimamo thabiti katika kutetea maslahi ya taifa.
Alisema madhara mengine ni kuyumba kwa uchumi wa taifa; utumishi wa umma kugeuzwa daraja la kujipatia utajiri; mgawanyo mbovu wa mapato ambao umesababisha pengo kubwa la kipato; kuongezeka kwa ufukara; kuporomoka kwa ubora wa huduma za jamii na ukosefu wa ajira.
Awali Bubelwa alianisha baadhi ya kashfa za ufisadi zilizotikisa nchi kuwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la minara pacha ya Benki Kuu (BoT), wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), mikataba ya madini ya Buzwagi, Kiwira, Kagoda, Tangold, Meremeta ununuzi wa vifaa vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kufilisika kwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), ununuzi wa rada na ndege ya Rais.
No comments:
Post a Comment