MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, May 27, 2009

Mjane ahamishwa 'kinyama Kiluvya

Salim Said
KAMPUNI ya Yono Auction Mart imeihamisha kwa nguvu familia ya Shamsa Nassor katika nyumba yake iliyopo Kiluvya Mtaa wa Gogoni, Kinondoni jijini Dar es Salaam na kasababisha hasara ya mali na kujeruhi.

Nymba hiyo ambayo ni mali ya marehemu mume wa Shamsa aitwae Salim Aklan, ilivamiwa jana na kampuni hiyo kwa madai kuwa wamepewa amri na mahakama ya mwanzo Magomeni ya kuwahamisha huku kukiwa hakuna notisi.

Akizungumza na Mwananchi mara baada ya tukio hilo lililotokea mapema asubuhi ya jana Shamsa alisema, kundi la watu zaidi ya 30 walivamia nyumba yake na kumtoa kwa nguvu yeye na watoto wake na kumsababishia hasara ya mali na majeraha ya mwili.

“Walikuja na mjumbe wa shina, wakaniambia kuwa wametumwa na mahakama, nikawaomba kabla ya kuanza kunitoa tukae chini kwanza kwa sababu wao wana nyaraka na mimi ninazo, halafu sina notisi, ndipo waliponisukuma na kuanza kuvunja vitu na kuviburuza nje,” alisimulia Shamsa huku akibubujikwa na machozi na kuongeza:

“Nilipoona hivyo nikachukua gari ili niende polisi kituo cha Kiluvya Gogoni kutoa taarifa na wakati gari liko katika mwendo wakaniwekea mtungi uliokuwa na bustani kwenye tairi na gari ilikakosa mwelekeo na kugonga mti na baadae kupinduka huku ndani nikiwa na mwanangu wa msichana.”

Alisema kutokana na ajali hiyo, wamepata majeraha yeye na mwanawe ambapo baadae alipiga simu kituo cha polisi Ostabey ambapo askari wa usalama barabarani walifika katika eneo hilo kupima ajali hiyo.

“Dhabu zangu zote zenye thamani ya 15 milioni sizioni, wameniibia saa ya aina ya Rado, fedha taslimu 5.9 milioni, wamenivunjia vitu vya jikoni, vitu vya samani na vitabu na madaftari ya shule ya watoto wangu,” alilalamika Shamsa.

Shamsa alidai kuwa, tukio hilo lilishinikizwa na shemgi yake aitwae Abdallah Malik kwa madi kuwa anataka kurithi mali hiyo kwa nguvu.

Alipoulizwa Malik kuhusiana na tukio hilo alijibu kwa jeuri na kutoa vitisho kwa mwandishi.

“Ahaa! Kama ni mwandishi andika unachojua na ukiandika vibaya likikuripukia utajijua, maana mimi nitakuchukulia hatua na wala sitokuachia,” alisema Malik na kuongeza:

“Andika tu wewe kama huyo unayemsikiliza (Shamsa) ni Bibi yako lakini litakalokufika utajua mwenyewe eneo hili lipo chini ya mahakama. Askari asiingie mtu humu, sawa.”

Mara baada ya kumalizika kazi ya kumuhamisha mama huyo, Malik alileta askari wa Kampuni ya Ulinzi ya General (General Guard) na kuwapa kazi hiyo licha ya kudai kuwa eneo hilo lipo chini ya mahakama ya Mwanzo ya Magomeni jijini Dar es Salaam.

Mkaguzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Peter Yohana alithibitisha kuletwa hapo na Malik kwa kazi moja tu ya kuhakikisha kuwa haingii mtu ndani ya eneo hilo hata mama huyo aliyehamishwa au mtoto wake.

“Sisi tumeletwa leo (jana) asubuhi na Malik na ametutaka asiingie mtu na hata wewe kama si mwandishi usingeingia humu. Ametuthibitishia kuwa eneo hili lipo chini ya mahakama na vitu vya yule mama vyote vipo nje ya geti kule,” alisema Yohana.

Kwa upande wake mjumbe wa shina la Gogoni Kiluvya mama Mramba alisema yeye hakuwa na taarifa ya kazi hiyo na alikwenda kugongewa asubuhi wakati akichoma vitumbua vyake ili kuwasindikiza wafanyakazi wa Yono.

“Mimi nilipoona vuru nikakimbia polisi na nilipofika sijakuta hata askari mmoja nikaamua kwenda kuendelea kuchoma vitumbua vyangu kwa kuwa ndio kazi ninayoitegemea na biashara ni asubuhi,” alisema mama Mramba.

Hata hivyo Polisi Wilaya ya kipolisi Kimara ilisema haina taarifa za hamishahamisha hiyo na kwamba kitaratibu shughuli kama hizo hutakiwa kusimamiwa na polisi kwa ajili ya amani na uslama.

“Mimi sina taarifa ya tukio hilo wala sina taarifa ya amri ya mahakama kuhusu kuhamishwa kwa watu hao lakini wewe nenda mahakamani ili ujue kama ‘order’ amri ya mahakama ilitoka au la,” alisema Mkuu wa kituo cha polisi Mbezi J.K Ndaki.

No comments:

Post a Comment