MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Wednesday, May 27, 2009

TFDA yateketeza tani 34 za Maziwa hatari kutoka China

Salim Said
HATIMAYE Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imeteketeza tani 34 za maziwa ya unga aina ya Golden Bell-Instant Full Cream kutoka nchini China yenye thamani ya sh150 milioni, ambayo yamechanganywa na Kemikali aina ya ‘Melamine’.

Uteketezaji wa maziwa hayo, ulifanyika jana chini ya uangalizi mkali wa polisi wenye silaha katika Dampo la Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam eneo la Pugu Kinyamwezi.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya uteketezaji huo, Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula wa TFDA Raymond Wigenge alisema, Maziwa hayo yalikamatwa Septemba mwaka jana lakini yalichelewa kuteketezwa kutokana na taratibu za kimaabara baina ya mmiliki na TFDA.

Alisema, taarifa za kuwepo kwa maziwa yaliyochanganywa kemikali ya ‘Melamine’ walizipata kutoka kwa Mtandao wa Mamlaka za Udhibiti wa Usalama wa Vyakula Duniani (Inforsan) na walipofanya uchunguzi waligundua kuwapo kwa maziwa hayo nchini.

“Hatua ya kwanza baada ya kupata taarifa hiyo tulisitisha uingizaji na pili tulifanya ukaguzi nchini kote na kukamata tani nyingi za maziwa hayo. Tatu tulipeleka ‘sampo’ vigezo katika maabara za Afrika ya Kusini na za TFDA kwa ajili ya vipimo,” alisema Wigenge na kuongeza:

“Tulichukua aina 94 za bidhaa nyengine za maziwa zilizomo ndani ya soko nchini kwa ajili ya vipimo, lakini hatukubaini maziwa yaliyochanganywa ‘melamine’ zaidi ya huyo mtu mmoja ambaye alikuwa anaingiza kihalali.”

Alifafanua kuwa, Mmiliki wa maziwa hayo ambaye ni Kampuni ya Vin Mart Ltd hakuridhika na vipimo hivyo na alitaka kupelekwa vigezo vya maziwa hayo katika maabara za Ubeligiji na Ufaransa, ambako pia matokeo yake yalilingana na ya TFDA na ya Afrika ya Kusini.

“Leo ndio tumeamua kuyateketeza baada ya mmiliki kujiridhisha na vipimo vilivyofanywa katika maabara nne zikiwa ni ya TFDA, Afrika ya Kusini, Ufaransa na Ubeligiji ambako majibu yalilingana,” alisema Wigenge.

Alisema, mmiliki huyo hakuwa na kosa, kwa sababu maziwa hayo yaliingizwa kemikali hiyo kiwandani nchini China, ikiwa ni mbinu ya kuongeza virubitisho vya Protini kutokana na tabia ya wafugaji wa nchi hiyo kuweka maji katika maziwa baada ya kuyakamua.

“Kama mmiliki atataka kudai fidia kutoka kwa kampuni iliyotengeneza maziwa haya, sisi tunaweza kutoa ushirikiano kwa kuthibitisha kuwa tuliyaharibu kwa kuwa yalikuwa na kemikali yenye madhara kwa afya ya binadamu,” alisema Wigenge.

Hata hivyo Wigenge alithibitisha kuwa, mmiliki wa maziwa hayo hana kosa kwa sababu kemikali ya ‘melamine’ ambayo inasababisha ugonjwa wa figo hasa kwa watoto haikuwa kigezo cha kupima ubora wa maziwa hapo awali.

Uteketezaji huo ulifanyika chini ushuhuda wa maafisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), TFDA, Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC), polisi, na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.

Afisa Mkuu wa Forodha kutoka TRA Tmeke Peles Mwaipopo alisema, wao kazi yao ni kushuhudia tu na kuthibitisha kwamba uteketezaji umefanyika na si vyenginevyo.

“Baada ya hapa tutaandika ripoti kwa ajili ya kuiwasilisha kwa wakuu wetu kama kumbukumbu ili siku yoyote mmiliki akilalamika tunatoa ushahidi kuwa kitendo hicho kilifanyika,” alisema Mwaipopo.

Kwa mujibu wa sheria anayekamatwa na bidhaa bandia hupaswa kugharamia hasara yote ya uteketezaji wa bidhaa hiyo ikiwa ni pamoja na usafiri, posho za maofisa na wabebaji.

No comments:

Post a Comment