MARASHI

PLAN YOUR WORK AND WORK ON YOUR PLAN BUT, WHEN YOU FAIL TO PLAN, YOU PLAN TO FAIL

Thursday, June 25, 2009

Chadema kumpokea Lwakatare Bukoba Mjini leo

Salim Said
ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Tanzania Bara Wilfred Lwakatare, ametangaza rasmi kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na leo anatarajiwa kupokelewa rasmi na wanachama wa chama hicho mjini Bukoba.


Baada ya kupokelewa leo, kesho Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe atampa kadi chama hicho katika hafla maalumu, itakayofanyika katika Jimbo la Biharamulo Magharibi, kabla ya kuanza kupanda majukwani kumnadi mgombea wa chama hicho katika kinyang'anyiro cha ubunge.

Lwakatare ambaye alishika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara kwa zaidi ya miaka 10, alitangaza hayo jana baada ya kupata ushauri kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki zake.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu akiwa wilayani Bukoba, Lwakatare alisema:“Mimi ni Chadema kuanzia jana (juzi) saa 1:30 usiku, nyinyi mko nyuma sana kwa sababu taarifa hizi zimefika Ujerumani nyinyi Dar es Salam hamjapata!”

Lwakatare alitangaza kujiondoa CUF kupitia mahojiano yake ya moja kwa moja na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani juzi saa 1:30 usiku.

Alisema uamuzi huo aliuchukua baada ya kufanya kikao na familia yake, mzazi wake na wanachama wake 284, na kuwaeleza mkasa uliomfika, wanachama 282 walimwambia aende Chadema na kwamba wanachama wawili tu walimtaka aende Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Mzazi wangu ameniambia niende Chadema, familia pia imeniambia hivyo hivyo wanachama 282 katika kikao waliniambia ‘nenda chadema’ isipokuwa wawili walioniambia ‘nenda CCM’ kwa hiyo wengi wameshinda,” alisema Lwakatare.


Pamoja na uamuzi huo, Lwakatare aliwataka viongozi wa CUF kujifunza kwa kupitia vitabu yake kuanzia namba moja hadi tatu ambavyo amewatumia ili kurekebisha chama chao kwa kuwa si chama chake.

Alisema bado anaamini kuwa ukombozi wa Watanzania ni vyama vyote kuungana ili kujenga nguvu moja ya mapambano na CCM, na kwamba bila hivyo CCM itaendelea kutawala nchini.

“Licha ya kujiunga na Chadema niko tayari kushirikiana na CUF kwa lengo la kuunganisha nguvu ya upinzani kuing’oa CCM,” alisisitiza Lwakatare.

Naye Mwenyekiti wa CUF taifa Profesa Ibrahim Lipumba alisema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa kwa kuwa Lwakatare alikuwa mjumbe katika Baraza Kuu la Uongozi la chama na mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa.

“Tunasikitika sana kwa sababu alikuwa kiongozi wetu na tulikuwa naye muda mrefu. Tulifanya mabadiliko ili kumpa muda wa kuimarisha chama lakini ameamua kufanya uamuzi huo, tunasikitika sana.

“Licha ya jitihada zangu za kuzungumza naye sana na kumsihi ameamua hivyo, mimi nilidhani tumeshaelewana na kuyamaliza kumbe ilikuwa bado. Lakini kukosa unaibu si sababu ya kuhama chama,” alisema Profesa Lipumba.

Lwakatare aliwahi kuwa mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini na Mwenyekiti wa Kambi ya upinzani Bungeni kupitia tiketi ya CUF na hatimaye sasa ameamu kujiunga na Chadema baada ya kuangushwa Machi mwaka huu katika nafasi yake ya unaibu Katibu Mkuu.

Wakati huohuo, aliyekuwa naibu katika mkuu wa chama cha wananchi CUF Alfred Rwakatare kesho anatarajia kujiunga rasmi na chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema na kukabidhiwa kadi ya uanachama na mwenyekiti wa taifa wa chama hicho Freeman Mbowe.

Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi wa oparesheni na uchaguzi wa Chadema John Mrema alisema kuwa Rwakatare ataingia rasmi Chadema ijumaa na kukabidhi kadi ya uanachama katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanjwa wa Uhuru mjini Bukoba.

Mrema alisema mara baada ya Kukabidhiwa kadi hiyo na kuwa mwanachama rasmi Rwakatare atawasili jumamosi Biharaulo magharibi kwa ajili kusaidia kampeni za kumnadi mgombea wa chadema Dk. Grevas Mbassa pamoja na viopngozi wengine wa Chadema.

Aliwataja viongozi hao kuwa ni pamoja na Dk. slaa, Philimoni Ndesambulo pamoja na Zitto Kabwe ambao baada ya zoezi hilo nao pia wataingia Biharamulo kwa ajili ya kusaidia kampeni za chama chao.

Wednesday, June 24, 2009

Profesa Lipumba aiponda bajeti ya 2009/10




Salim Said
JUNI 18 mwaka huu Watanzania wameshuhudia wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiipitisha kwa kishindo bajeti ya serikali ya Sh9.5 trilioni kwa mwaka 2009/10, baada ya wabunge 221 wa chama hicho kuipigia kura za ndio.

Katika kazi ya kupitisha bajeti hiyo, jumla ya wabunge 33 wa kambi ya upinzani kati ya wabunge wote 318 wa bunge la Tanzania, waliipinga bila ya mafanikio kwa kupiga kura za sio, kutokana na idadi yao kuzidiwa na wale wa CCM waliopiga kura za ndio.

Bajeti hiyo ambayo awali ilipata upinzania mkubwa kwa wabunge wa CCM kabla ya kufika bungeni, lakini kilichotokea ni kwa ujasiri wa wabunge hao haukuthubutu kujitokeza bungeni jambo ambalo baadhi ya wachambuzi wamesema ni unafiki.

Wadau mbalimbali wa masuala ya kiuchumi nchini waliipokea kwa mitazamo tofauti bajeti hiyo na kutoa maoni yao wakiamini kuwa serikali huenda ikayatumia katika kuirekebisha bajeti hiyo.
Mchambuzi nguli, wa masuala ya kiuchumi nchini Profesa Ibrahim Lipumba anaiponda bajeti hiyo kwa madai kuwa, ni tegemezi na haiwezi kumfikisha popote mtanzania wa kawaida.

Anasema, bajeti hiyo haikuzingatia misingi muhimu ya bajeti na hivyo haiwezi kuitwa bajeti bora na iliyokamilika.

Anasema bajeti hiyo, ina upungufu mwingi na haiwezi kabisa kupambana na matatizo ya umasikini yanayomkabili Mtanzania wa kawaida, kwa sababu haikuzingatia misingi muhimu ya bajeti.

“Bajeti hii bado ni tegemezi iliyojaa kasoro na wala hawiezi kumfikisha popote mtanzania wa kawaida katika kumuondeshea matatizo ya umasikini wa kipato,” anasema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anasema, bajeti iliyokamilika inapaswa kujumuisha mapato yote na matumizi ya serikali bila ya kujali taratibu maalum za kuendesha baadhi ya miradi au programu.

“Kwa ujumla mapato na matmizi yote lazima yapangwe na kuainishwa katika bajeti bila ya kujali chanzo cha mapato, hii itabainisha iwapo kuna uhusiano wa karibu kati ya mapato na wanaonufaika na matumizi ya mapato hayo, kwa sababu hoja ya mapato husika kulipia matumizi ya huduma inakubalika,” anasema Profesa Lipumba.

Anasema, utayarishaji wa bajeti lazima uzingatie malengo ya uchumi mpana, ukuaji wa pato la taifa, mfumko wa bei, akiba ya fedha za kigeni na thamani ya sarafu ya nchi husika.

“Bajeti bora lazima matumizi yake yagawiwe kulingana na malengo ya sera ya maendeleo ya taifa kwa sababu jambo linaloathiri sera, utayarishaji na utekelezaji wa bajeti ni uanzishwaji wa sera na utamkaji wa ahadi zisizoendana na vipaumbele vilivyotumika kuandaa bajeti,” anasema Profesa Lipumba.

Anafafanua kwamba, pia bajeti lazima ilenge kujenga mazingira mazuri ya utekelezaji mzuri wa bajeti ya serikali.

Anasema, kwa kuwa bajeti ni kioo cha sera za serikali, ni lazima iwe na uhusiano wa karibu na sera hizo ili kuratibu vizuri uanzishwaji wa sera na kushirikisha umma katika utungaji wake.

Anasema, bajeti lazima iweze kupitia na kutathmini mafanikio na mapungufu ya sera za maendeleo ya taifa na kuchambua kwa kina mahitaji ya fedha na rasilimali nyingine za taifa, ili kuhakikisha bajeti inashika hatamu katika mapato na matumizi ya serikali.

“Maandalizi ya bajeti lazima yazingatie hali halisi ya uchumi ili kuweza kukadiria kwa usahihi mapato na kuyatambua matumizi yake yote ya lazima,” anafafanua Profesa Lipumba.

Anasema, bajeti ya mwaka huu ni ya kisanii kwa sababu haikuzingatia sera za maendeleo ya taifa ikiwamo ya Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umasikini (Mkukuta), Dira ya Maendeleo ya 2025, Ilani ya CCM na Mpango Maalum wa Kurahisisha Maendeleo (Tiger Plan 2020).

Anasema, mpango wa kunusuru uchumi wa nchi umetengewa sh1.7 trilioni na rais Jakaya Kikwete, ambaye amesema fedha hizo zimeingizwa katika bajeti ya serikali, lakini bajeti haijaainisha waziwazi mpango huo na matumizi ya fedha hizo.

Anailaumu serikali, kwa kukusudia kukopa kiasi hicho cha sh1.7 trilioni kwa riba kubwa ili kukopesha kwa wafanyabiashara kwa riba ndogo.

“Hivi wewe unakopa fedha kwa riba ya asilimia 11 au zaidi, halafu unamkopesha mfanyabiashara kwa riba ya asilimia 2, hizo ni akili kweli? Tutasema wewe uko makini kweli au una lengo zuri kwa wananchi wako,” anahoji profesa Lipumba.

Anasema, kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) umebaini kuwa mabenki ya kigeni yaliyopo nchini yanakula njama ya kuhakikisha kuwa yanapata faida kubwa na kwa haraka ili kununua amana za serikali.

“Benki Kuu ya Tanzania (BoT) haina mamlaka ya kupanga riba kwa wateja wa benki za biashara. Tusipokuwa makini mikopo ya serikali itawanufaisha wenye mabenki na kuwadidimiza wafanyabiashara wetu wadogo na wa kati,” anatoa angalizo.

Anasema, benki zinawalipa riba ndogo wanaoweka akiba zao kwa wastani wa asilimia 2.7 wakati yanatoa mikopo kwa riba ya wastani wa asilimia 16.1 huku kukikosekana benki inayofanya jitihada za kutosha kutoa motisha na kukusanya akiba za watanzania.

“Serikali imeweka mikakati na mfumo gani wa kiutawala ili kuhakikisha Benki ya Rasilimali (TIB) haitoi mikopo kisiasa na fedha za walipa kodi zilizoweka kama mitaji katika benki hiyo hazipotei,” anahoji Profesa Lipumba.

Anasema, ili kunusuru hilo, utawala wa benki hiyo unahitaji kuimarishwa, kwa kuteua watendaji makini na Bodi ya Wakurugenzi iteuliwe bila ya kujali hisia za kichama ili iwe na mamlaka ya kusimamia watendaji wake na kutotoa mikopo kisiasa na kifisadi.

Profesa Lipumba anasema, kaulimbiu ya ‘Kilimo Kwanza’ ni msemo wa kisiasa na kwamba imepita mingi lakini katika utendaji hakuna mabadiliko kwa kuwa mgao wa fedha katika sekta hiyo hauna tofauti na ule wa mwaka jana katika bajeti.

“Bajeti ya mwaka jana ilitenga sh513 bilioni sawa na asilimia 7.1 na hii ya mwaka huu imetenga sh666 bilioni sawa na asilimia 7.0 ya bajeti yote. Je tofauti iko wapi, ni usanii tu wa kisiasa katika utendaji,” anasema Profesa Lipumba.

“Mara Kilimo Kwanza, Kilimo ni Uti wa Mgongo, Siasa ni Kilimo, Utu ni Kilimo yote ni misamiati tu ya kuwababaisha watanzania.”

Anasema, ili kuhakikisha umasikini unapungua vijijini kilimo kinapaswa kukuwa kwa wastani wa asilimia 6 hadi 8, kwa mwaka katika kipindi cha mpito kwani wakulima wadogo ndiyo tegemeo la kilimo cha Tanzania, lakini hawajasaidiwa vya kutosha kuboresha kilimo chao.

Anaitaka serikali kufuta misamaha ya kodi kwa viongozi wa juu wa serikali na wabunge na kuhakikisha kuwa wanalipa kodi ili kuondoa matabaka kati yao na wanaowaongoza.

“Mapato mingi ya serikali yanapotea kupitia misamaha holela ya kodi. Viongozi wana misamaha mingi ya kodi ikiwa ni pamoja nay a kuingiza vitu vyao binafsi nchini,” anasema Profesa Lipumba.

Kwa upande wake Msomi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam Dk. Benson Bana anatofautiana na Profesa Lipumba kuhusu bajeti hiyo akisema kwamba, ni nzuri na imezingatia vipaumbele muhimu kwa maisha ya Mtanzania.

“Profesa Lipumba, ni mchumi nguli, tunamuamini na tunamuheshimu kweli, lakini profesa huyu ni mwanasiasa, hivyo nilitegemea ataipinga, na kama angeipongeza au kuikubali ningemshangaa sana, hasa ukizingatia nafasi yake,” anasema Dk. Bana.

Anasema, “Namuheshimu sana lakini naweza kumkosoa Profesa kwa hili, bajeti yetu imezingatia sana misingi ya bajeti ina uhusiano na sera zote za maendeleo ya taifa na imeainisha mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa bajeti, kwa sababu hata mimi nimechambua.”

Anasema bajeti kwa kawaida inatenga fungu maalum kwa ajili ya vipaumbele vyake kwa kuzingatia umuhimu, mahitaji na uwezo wa mapato ya taifa na sio kupanga bajeti kubwa hadi kuvuka kiwango cha mapato yako, itakuwa haitekelezeki.

Lakini Dk Bana anasema, bajeti hiyo imeandaliwa na wataalamu wa fedha na uchumi nchini ambao ni wanafunzi wa Profesa Lipumba.

CUF yaanza kuweweseka kwa Lwakatare

Salim Said
SIKU chache baada ya Willfred Lwakatare kuvua nyadhifa zake zote na kurudi jimboni kwake, CUF imeanza kudhibiti nyendo zake baada ya kumzuia kufanya mikutano ya hadhara.


Mkurugenzi wa habari na uenezi wa CUF, Ashura Mustafa aliiambia Mwananchi jana kuwa chama hicho kimesambaza barua katika wilaya na matawi yake yote nchini kuwaagiza watendaji wake wamdhibiti Lwakatare ili asifanye mikutano kwa mgongo wa chama.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Lwakatare, ambaye amekuwa akiripotiwa kuhutubia mikutano ya hadhara akiuliza watu ahamie chama gani, haruhusiwi kufanya mkutano wowote isipokuwa kwa idhini ya makao makuu.

Nafasi ya Lwakatare, ambaye aliondolewa katika kutetea nafasi yake ya naibu katibu mkuu baada ya kuuishikilia kwa karibu miaka 10, ilichukuliwa na Joram Bashange. Kwa upande wa Zanzibar, nafasi hiyo inashikiliwa na Juma Duni Haji.

Kitendo hicho kilimfanya aandike barua ya kujivua nyadhifa zote kwenye chama hicho na kubaki na mwanachama wa kawaida.

Jana Ashura aliliambia gazeti hili kuwa pamoja na chama kusambaza barua hizo za kumzuia Lwakatare kufanya mikutano, pia kinakusudia kutoa tamko zito dhidi ya mbunge huyo wa zamani wa Bukoba Mjini.

Alisema anachofanya Lwakatare si kuimarisha chama kama alivyodai kwenye barua yake kwa mwenyekiti alipotaka kujiuluzu bali kukivuruga katika kipindi hiki cha kukaribia chaguzi za kitaifa.

“Ni kweli tumewaandikia wenyeviti wa chama katika kata na wilaya zote Tanzania Bara na hasa Kanda ya Ziwa kuwataka kuwataka wamzuie Lwakatare kufanya mikutano ya kukivuruga chama kwa kuwalisha sumu wa wananchi akitumia jina la CUF,” alisema Mustafa.

“Tumewaagiza kama atataka kufanya mkutano wowote kwa jina la CUF asiruhusiwe, badala yake waripoti makao makuu, halafu tutaangalia lengo la mkutano huo. Tukijiridhika tunaweza kuruhusu lakini bila hivyo asifanye.”

Alisema Lwakatare sasa hana mamlaka kikatiba kufanya mkutano wowote kwa jina la CUF kwa sababu si kiongozi tena wa chama bali mwanachama wa kawaida.

“Kwa vile ameamua kujivua nyadhifa zake zote ndani ya chama na chama kimeridhia, hana tena mamlaka ya kuitisha mikutano ya wanachama; uwe wa hadhara au wa ndani,” alisema Mustafa.

Mwishoni mwa wiki iliyopita mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alimsihi Lwakatare kutoharibu chama baada ya kujiengua katika nyadhifa zake.

Habari za ndani zinasema kuwa tayari viongozi wakuu wa chama hicho- Prof Lipumba, katibu mkuu Seif Sharif Hamad na makamu mwenyekiti Machano Khamis- wamekutana kujadili namna ya kukihami chama na kile kilichoelezwa kuwa mkakati wa Lwakatare kutaka kukichafua.

Inadaiwa kuwa katika kikao hicho, Machano, ambaye alifanya ziara fupi Kanda ya Ziwa baada ya Lwakatare kujiuzulu, alieleza mambo aliyoyaona wilayani Bukoba kuhusu maendeleo ya chama chao.

Akizungumzia uamuzi huo wa CYF, Lwakatare aliiambia Mwananchi kuwa hana taarifa ya agizo hilo kwa kuwa anaamini halijafika wilayani kwake Bukoba mjini.

“Huku hili agizo au barua halijafika na ikifika tutaijadili kuona kitu gani cha kufanya kuweza kufanya kazi yangu ya kuimarisha chama,” alisema Lwakatare jana.

“Mimi bado ni mwanachama wa CUF na nilisema kwamba uamuzi wa kujiunga na chama chochote upo mikononi mwa familia yangu, wananchi na viongozi wangu wa CUF,” alisema Lwakatare alipozungumza kwa njia ya simu akiwa Bukoba.

'Kutogusa Meremeta ni kukiuka utawala bora'

Salim Said
UAMUZI wa Serikali kuzuia kujadiliwa kwa kampuni ya Meremeta Gold Mine umeelezwa kuwa ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, wanaharakati na wanasiasa wameeleza.


Kwa mara nyingine, serikali juzi ililieleza Bunge kuwa masuala yanayohusu kampuni ya Meremeta hayawezi kujadiliwa kwenye chombo hicho cha wawakilishi wa wananchi kwa kuwa yanahusu usalama wa nchi na Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari alitoa tamko hilo akirejea kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa Bungeni mwaka jana kuwa suala hilo haliwezi kujadiliwa na kuwataka Wabunge waheshimu kauli hiyo ya mtendaji mkuu wa serikali.

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, ambaye aliuliza swali la msingi, alipotaka kueleza kuwa anachohoji ni wizi, spika wa Bunge, Samuel Sitta alimkatisha na kumwambia kuwa walishakubaliana katika kikao cha kamati ya maadili ya viongozi kuwa suala la Meremeta lisijadiliwe hadharani kwa sababu za kiusalama.

Jana mratibu wa masuala ya utawala bora wa Mtandao wa Mashirika ya Wanaharakati (FemAct) ambao unaunganisha taasisi 50, Buberwa Kaiza alisema jana kuwa kitendo hicho kinajenga taswira kuwa dola inashabikia ufisadi.


Alisema katika nchi yoyote inayofuata misingi ya utawala bora, hakuna jambo linalopaswa kuendeshwa kwa usiri hasa jambo hilo linapohusu wizi wa mali ya umma na kwamba kuzuia Meremeta kujadiliwa hadharani ni kukiuka kanuni hizo.

“Katika utawala bora hakuna siri na matumizi ya fedha za umma yanapaswa kuwekwa hadharani,” alisema Kaiza.

Alisema ni jambo la kushangaza kuona bunge ambalo ni sehemu pekee ya haki ya kuzungumza na kujadili masuala ya maendeleo ya nchi, hasa matumizi ya fedha za umma linazuiwa kujadili kampuni hiyo ya Meremeta kwa kigezo cha ulinzi na usalama wa taifa.

Kaiza, ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la Fordia, alisema: "Hii ni ishara ya nchi kutekwa na mafisadi kwa sababu serikali imeamua kuwatetea kwa nguvu zote watu wachache ambao wanatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma."

Kauli ya Buberwa iliungwa na mkono na katibu mkuu wa chama cha NCCR- Mageuzi, Samwel Ruhuza aliyetaka kampuni hiyo ijadiliwe kwa sababu imetuhumiwa kwa ufisadi ambao hauna uhusiano na usalama wa taifa.

Ruhuza alisema licha ya kuwa suala la Meremeta linahusisha usalama wa taifa, serikali inatakiwa kutambua kuwa kampuni hiyo inahusika na ubadhilifu wa fedha za walipakodi.

“Hivi mfanyakazi wa usalama wa taifa akiiba hataulizwa wala kushtakiwa," alihoji Ruhuza
"Suala la msingi hapa ni ubadhilifu... hayo ya usalama yasijadiliwe, lakini hili la ubadhilifu lazima liongelewe.”


Kwa mujibu wa Ruhuza, inaeleweka kuwa fedha nyingi za walipakodi zilitolewa na kupelekwa Meremeta, hivyo serikali haina sababu za kuzuia suala hilo kujadiliwa hadharani kwa kuwa linawahusu wananchi.

“Mimi sina haki ya kujua kama jirani yangu anamiliki bunduki au la lakini ikitokea mtoto wangu amekutwa ameuawa nje ya nyumba ya jirani yangu, hapo lazima niulize ili nipate ufafanuzi na maelezo sahihi juu ya kifo hicho sasa suala hili ndio mfano halisi wa hii kampuni ya Meremeta.”

Kauli hiyo ya serikali imekuja wakati Bunge likiwa limemuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), kuikagua Meremeta pamoja na Mwananchi, ambayo imeelezwa kuwa iko katika mchakato wa kufilisiwa na kwamba itajadiliwa baada ya kumalizika kwa zoezi hilo.

Inadaiwa kuwa wanahisa wa Meremeta, ambayo ilipewa kiasi cha Sh155 bilioni na Benki Kuu (BoT) katika mazingira yanayoonyesha kuwepo kwa ufisadinatuhumiwa, ni kampuni ya Trienex ya Afrika Kusini ambayo inamiliki asilimia 50 na Hazina (50%).

Wanahisa wengine wa kampuni hiyo inayodaiwa kuwa ilianzishwa jijini London, ni London Law Secretary Services. Ilidaiwa Bungeni kuwa kampuni ya Tangold ndiyo iliyorithi mali za Meremeta baada ya kampuni hiyo kuwa mufilisi.

Sunday, June 21, 2009

Dk. Bana aishauri Serikali


Salim Said
PAMOJA na Serikali kutengua uamuzi wa kufuta misamaha ya kodi kwa Taasisi na Mashirika ya Dini juzi, Msomi na Mchambuzi mashuhuri wa masuala ya kisiasa na uchumi Dk. Benson Bana, ameitaka serikali kuunda Tume Huru ya Wataalam kuchunguza matumizi ya misamaha hiyo kwa miaka mitano iliyopita katika kila dini na dhehebu nchini.


Alisema utitiri wa taasisi hizo unatishia amani ya pato la taifa na kusababisha baadhi yao kuitumia vibaya misamaha hiyo kwa maslahi yao binafsi jambo ambalo linaingizia hasara serikali, ambapo inatumia asilimia 30 ya mapato yake kila mwaka kugharamia misamaha hiyo.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum Ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana alisema, serikali imekuwa laini sana kwa kuwa inatoa misamaha lakini inashindwa kuisimamia.

“Serikali imekuwa laini sana, huwezi kutoa msamaha wa kodi halafu ukaachia huru bila ya kusimamia ni uzembe. Kwa hiyo lazima serikali iunde tume huru ya wataalamu kuchunguza matumizi ya misamaha kwa miaka mitano iliyopita,” alisema Dk Bana na kuongeza:

“Uchunguzi lazima ufanyike kwa dini zote na madhehebu yote na taasisi zitakazogundulika kutumia vibaya misamaha hiyo, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake. Huwezi kuwa na gari tatu halafu unaingiza tairi 400 kutoka nje ya nchi.”

Dk Bana ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam alifafanua, zamani Tanzania ilikuwa na dini nne tu lakini kwa sasa ina dini zaidi ya 100 na kila siku zinaendelea kuchepua kama uyoga.

“Zamani tulikuwa na dini ya kisslaam, Katoliki, Protestant na Hindu lakini sasa utashanga utitiri wa dini umekuwa mkubwa lazima serikali idhibiti hali hii, iache ulegelege. Kila mtu anaanzisha kanisa kwa maslahi yake wenzetu waislaam wamejitahidi,” alifafanua Dk Bana.

Aidha aliitaka serikali, kuangalia gharama za huduma zinazotiolewa na taasisi za dini kwa madai kuwa wanatoa huduma kwa gharama kubwa wakati wanapata misamaha ya kodi.

“Ndio! lazima serikali iangalie gharama wanazotoza ni kubwa ukilinganisha na huduma zao halafu wanapata misamaha ya kodi wanapoingiza vitu nchini,” alisema.

Alisema, misamaha ya kodi iwe katika vifaa na magari yanayoendana na mazingira halisi ya maisha ya watanzania na isiwe vya kifahari.

“Kwa maisha ya kitanzania haiwezekani kwamba Kanisa Bakwata linaingiza magari aina ya Landcruiser VX kwa kila kiongozi wake au hata kwa sheikh wa Mkowa, unaweza kuingiza VX ya baba Askofu au ya Mufti lakini sio kila kiongozi,” alisema Dk Bana.

Kwa upande wake Afisa habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), David Kafulila alisema, kutenguliwa kwa uamuzi wa kufutwa kwa msamaha wa kodi kwa taasisi za dini nchini kumetokana na maamuzi mabovu ya serikali.


Alisema, Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo alisema hawezi kufuta misamaha ya kodi kwa makampuni ya madini hadi hapo watakapokaa na makampuni hayo na kukubaliana lakini kwa mashirika ya dini ilifuta bila ya makubaliano na viongozi wa dini.

“Kutokana na uzembe huo, viongozi wa dini hawakubaliana na uamuzi huo na hatimaye serikali imetengua uamuzi wake. Huku ni kutokuwa makini kwa serikali inapofanya maamuzi yake,” alisema Kafulila.

Aliitaka serikali kuweka wazi mahali itakapopata fedha za kufidia au kugharamia misamaha ya kodi kwa taasisi za dini kwa kuwa haikuwamo katika bajeti na bajeti imepitishwa bila ya marekebisho katika kipengele hicho.

Lwakatare awashukia viongozi wa CUF

Salim Said
ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania bara, Wilfred Lwakatare amewashushia tuhuma nzito baadhi ya viongozi wa wa Chama hicho akidai kuwa jina lake liliachwa kwenye uteuzi wa kutetea nafasi yake kwa fitina na majungu yaliyojaa CUF.

Alisema, hiyo ndiyo sababu kuu iliyomfanya aandike barua ya kujiuzulu nafasi zote katika chama hicho na kubaki kama mwanachama wa kawaida.

Rwakatare alitoa shutuma hizo kupitia mtandao wa Bidii, ambapo alidai maelezo hayo ndiyo aliyoyawasilisha katika kikao cha Baraza Kuu la Taifa la CUF kilichofanyika tarehe 09/06/2009.

Alisema licha ya chama hicho kuyumbishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), pia kuna baadhi ya wanachama na viongozi wenye tabia mbaya ya majungu na fitina dhidi ya wenzao.

Akieleza alisema maelezo ya Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba kwamba uteuzi aliofanya katika nafasi hiyo bara na Zanzibar ulizingatia kifungu na 68,(l)(i) cha katiba ya Chama sio sahihi, jambo ambalo Lwakatare alisema si kweli.

“Majina hayo yaliteliwa kwa kusikiliza majungu, fitina, njama za unafiki, roho mbaya, uchoyo na mtimanyongo wa baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho,” alisema Lwakatare.

Lwakatare alimtuhumu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar ambaye pia ni Mkurugenzi wa Chumi na Fedha Juma Duni Haji kuwa anampikia majungu na ndiye aliyesababisha jina lake kuachwa.

Hata hivyo akijibu tuhuma hizo Duni alisema CUF haina kawaida ya kujibizana na viongozi wake walioacha au kuachwa kupitia vyombo vya habari.

“Sisi CUF hatuna kawaida ya kujibizana na viongozi tuliokuwa nao katika chama na baada ya kujitoa au kuachia ngazi nyadhifa zao kupitia vyombo vya habari,” alisema Duni.

Hata hivyo juhudi za kumtafua profesa Lipumba na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho Ashura Mustafa ambaye alituhumiwa na Lwakatare kwa madai ya kumpakazia kuwa aliangushwa katika unaibu kwa sababu uwezo wake kiutendaji umedidimia (amefulia), hazikufanikiwa.

Matokeo ya wanafunzi wa LST yawa mabovu

Salim Said
MATOKEO ya wanafunzi Chuo cha Sheria yameonyesha kuwa watahiniwa 178 sawa na asilimia 61.1 ya wanafunzi 288, wameshindwa mtihani.

Matokeo hayo ambayo yamebandikwa katika kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani yameonyesha kuwa wanafunzi waliofaulu mtihani huo ni 35 Hayo ni matokeo ya kwanza kwa wanafunzi wa chuo hicho ambao mtihani wao ulifanyika Juni mwaka huu.

Chuo hicho, ambacho ni sehemu ya chuo kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) pia kina ofisi zake Ubungo jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa matokeo hayo, jumla ya wanafunzi 178 sawa na asilimia 61.8 wanatakiwa kurudia mtihani wa baadhi ya kozi huku wanafunzi 45 sawa na asilimia 15.6 wameshindwa kabisa.

Wanafunzi 24 kati ya wanafunzi hao 288 ambao ni sawa na asilimia 8.3 waliahirisha kutokana na sababu mbalimbali ambazo hazikutajwa katika ubao huo, huku wengine sita wakiwa wameekewa mapengo.

Matokeo yalionyesha kwamba, watahiniwa waliofaulu zaidi katika mitihani ni wawili ambao wamepata wastani wa pointi (GPA) 2.5 kila mmoja.

Watahiniwa hao walifuatiwa na wenzao wawili waliopata wastani wa pointi (GPA) 2.4 kila mmoja na kufuatiwa na wengine wawili waliopata wastani wa pointi 2.3 kila mmoja. Watahiniwa waliobakia walipata kati ya wastani wa pointi 0.0 hadi 2.3 ambao ndio wingi.

Hata hivyo Mwananchi ilifika katika ofisi za Chuo hicho zilipo katika Jengo la Ubungo Plaza lakini hakukua na muhusika wa kutoa maelezo juu ya matokeo hayo mabovu ya wanafunzi wake katika mitihani.

Juhudi za Mwananchi kutafuta maoni ya utawala wa chuo hicho hazikuishia hapa, ambapo pia ilitembelea tovuti ya chuo hicho kwa ajili ya kutafuta namba za simu ili kufanya mawasiliano lakini pia hazikufaniwa baada ya kukosekana katika tovuti fiyo ya www.lst.ac.tz.

Mwananchi haikuweza kufahamu mara moja sababu za wanafunzi hao kuanguka kama hivyo katika mitihani yao. Hata hivyo juhudi za kuwatafuta wahusika wa chuo hicho ili kufafanua sababu za kuanguka kwa wanafunzi wao zitaendelea leo.