Salim Said
UAMUZI wa Serikali kuzuia kujadiliwa kwa kampuni ya Meremeta Gold Mine umeelezwa kuwa ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, wanaharakati na wanasiasa wameeleza.
Kwa mara nyingine, serikali juzi ililieleza Bunge kuwa masuala yanayohusu kampuni ya Meremeta hayawezi kujadiliwa kwenye chombo hicho cha wawakilishi wa wananchi kwa kuwa yanahusu usalama wa nchi na Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari alitoa tamko hilo akirejea kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa Bungeni mwaka jana kuwa suala hilo haliwezi kujadiliwa na kuwataka Wabunge waheshimu kauli hiyo ya mtendaji mkuu wa serikali.
Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, ambaye aliuliza swali la msingi, alipotaka kueleza kuwa anachohoji ni wizi, spika wa Bunge, Samuel Sitta alimkatisha na kumwambia kuwa walishakubaliana katika kikao cha kamati ya maadili ya viongozi kuwa suala la Meremeta lisijadiliwe hadharani kwa sababu za kiusalama.
Jana mratibu wa masuala ya utawala bora wa Mtandao wa Mashirika ya Wanaharakati (FemAct) ambao unaunganisha taasisi 50, Buberwa Kaiza alisema jana kuwa kitendo hicho kinajenga taswira kuwa dola inashabikia ufisadi.
Alisema katika nchi yoyote inayofuata misingi ya utawala bora, hakuna jambo linalopaswa kuendeshwa kwa usiri hasa jambo hilo linapohusu wizi wa mali ya umma na kwamba kuzuia Meremeta kujadiliwa hadharani ni kukiuka kanuni hizo.
“Katika utawala bora hakuna siri na matumizi ya fedha za umma yanapaswa kuwekwa hadharani,” alisema Kaiza.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona bunge ambalo ni sehemu pekee ya haki ya kuzungumza na kujadili masuala ya maendeleo ya nchi, hasa matumizi ya fedha za umma linazuiwa kujadili kampuni hiyo ya Meremeta kwa kigezo cha ulinzi na usalama wa taifa.
Kaiza, ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la Fordia, alisema: "Hii ni ishara ya nchi kutekwa na mafisadi kwa sababu serikali imeamua kuwatetea kwa nguvu zote watu wachache ambao wanatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma."
Kauli ya Buberwa iliungwa na mkono na katibu mkuu wa chama cha NCCR- Mageuzi, Samwel Ruhuza aliyetaka kampuni hiyo ijadiliwe kwa sababu imetuhumiwa kwa ufisadi ambao hauna uhusiano na usalama wa taifa.
Ruhuza alisema licha ya kuwa suala la Meremeta linahusisha usalama wa taifa, serikali inatakiwa kutambua kuwa kampuni hiyo inahusika na ubadhilifu wa fedha za walipakodi.
“Hivi mfanyakazi wa usalama wa taifa akiiba hataulizwa wala kushtakiwa," alihoji Ruhuza
"Suala la msingi hapa ni ubadhilifu... hayo ya usalama yasijadiliwe, lakini hili la ubadhilifu lazima liongelewe.”
Kwa mujibu wa Ruhuza, inaeleweka kuwa fedha nyingi za walipakodi zilitolewa na kupelekwa Meremeta, hivyo serikali haina sababu za kuzuia suala hilo kujadiliwa hadharani kwa kuwa linawahusu wananchi.
“Mimi sina haki ya kujua kama jirani yangu anamiliki bunduki au la lakini ikitokea mtoto wangu amekutwa ameuawa nje ya nyumba ya jirani yangu, hapo lazima niulize ili nipate ufafanuzi na maelezo sahihi juu ya kifo hicho sasa suala hili ndio mfano halisi wa hii kampuni ya Meremeta.”
Kauli hiyo ya serikali imekuja wakati Bunge likiwa limemuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), kuikagua Meremeta pamoja na Mwananchi, ambayo imeelezwa kuwa iko katika mchakato wa kufilisiwa na kwamba itajadiliwa baada ya kumalizika kwa zoezi hilo.
Inadaiwa kuwa wanahisa wa Meremeta, ambayo ilipewa kiasi cha Sh155 bilioni na Benki Kuu (BoT) katika mazingira yanayoonyesha kuwepo kwa ufisadinatuhumiwa, ni kampuni ya Trienex ya Afrika Kusini ambayo inamiliki asilimia 50 na Hazina (50%).
Wanahisa wengine wa kampuni hiyo inayodaiwa kuwa ilianzishwa jijini London, ni London Law Secretary Services. Ilidaiwa Bungeni kuwa kampuni ya Tangold ndiyo iliyorithi mali za Meremeta baada ya kampuni hiyo kuwa mufilisi.
No comments:
Post a Comment